Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amewapongeza viongozi wanawake waliobahatika kupata nyadhifa za uongozi wa ngazi ya juu serikalini: Waendelee kuwa: waaminifu, waadilifu na wachapa kazi. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amewapongeza viongozi wanawake waliobahatika kupata nyadhifa za uongozi wa ngazi ya juu serikalini: Waendelee kuwa: waaminifu, waadilifu na wachapa kazi.  (AFP or licensors)

Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya Awapongeza Viongozi Wakuu Wanawake Tanzania

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, amempongeza na kumwombea heri, baraka na afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu nchini Tanzania. Amewataka wanawake wote waliobahatika kupata nyadhifa za juu kuwa: wachamungu, waaminifu na wachapakazi.

Na Ndahani Lugunya, - Dodoma, Tanzania.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania, amempongeza na kumwombea heri, baraka na afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu nchini Tanzania. Amesema hayo wakati akitoa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska-Kiwanja cha Ndege Jimboni Dodoma hivi karibuni. Katika mahubiri yake Askofu mkuu Kinyaiya amesema kuwa Watanzania wana imani kubwa na Uongozi wa Mh.Samia Suluhu Hassan katika kusimamia miradi mbalimbali ya kimkakati iliyoachwa  na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na ile atakayo ianzisha chini ya uongozi wake. “Kwa namna ya pekee nimwongelee huyu Mama ambae Afrika Mashariki ni wa kwanza kabisa kuwa Rais mwanamke Mheshimiwa sana Mama Samia Suluhu Hassan kwa kweli ni Mama na ni Mama kwelikweli, Mama wa uhakika,Mama mwenye busara, Mama aliyetulia, Mama anaejiamini na simba kwelikweli hivyo tumwombee  sana Mama yetu,” amesema Askofu mkuu Kinyaiya. Hata hivyo amewaombea pia akina Mama wote walioshika nafasi za juu serikali, ili waongeze jitihada zaidi katika utendaji wao wa kazi, huku akitolea mfano wa Mh.Waziri Jenista Mhagama.

“Pamoja naye naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza akina Mama wote na hasa pia wenye nafasi za juu katika uongozi Serikalini na ambao wameonesha imani kubwa sana kwa Mungu, kwa namna ya pekee Dada yetu Mh. Jenista Mhagama maana yake wengine wakishapata madaraka kusali tena Kanisani wanaona wataonekana kama wapo chini na mawazo mengine kama hayo lakini huyu mama huwa anakuja kila wakati. Pamoja nae nawapongeza akina mama wote ambao wameonesha umahiri wa hali ya juu sana, kuna akina Ummy Mwalimu, Anjelina Mabula,Doroth Gwajima, akina Mama Tunu Pinda  na wote akina mama ambao kweli ni wanawake wa nguvu,” amepongeza Askofu Mkuu Kinyaiya. Sanjari na hao amewapongeza akina Mama wote ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla kwa tunu yao ya utendaji wa haraka waliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Ametolea mfano wa mwanamke Maria Magdalena shuhuda wa Kwanza aliyekwenda Kaburini kushudia ufufuko wa Kristo Yesu Mfufuka, alivyofanya uharaka wa kusambaza habari hizo za ufufuko wa Yesu kwa wanafunzi wake. Amesema tunu nyingine walizonazo akina Mama ambazo Yesu aliziona kwao ni tunu ya uaminifu, uthamini na upendo, hivyo amewaomba akina Mama wote kuwa waaminifu katika kuuishi ukristo wao na hata katika maisha ya kawaida ndani ya jamii.

“Sisi akina Mama na zile tunu ambazo Mungu ametupa na kuziona ndani yetu na kuziheshimu tuone zinakwendakwendaje, mojawapo ni ile ya uaminifu nawapongezeni kwa hilo lakini ninawaombea na kuwakumbusha mwendelee kuwa waaminifu kwanza kwa Mungu kwa kuishi Imani ya Kikristu nawaombeni sana akina mama muendelee kuwa mstari wa mbele muendelee kuwa kweli ni nguzo imara,” amesema Askofu mkuu Kinyaiya. Hata hivyo katika tunu ya uaminifu Askofu mkuu Kinyaiya amewataka akina Mama wote kuwa waaminifu katika familia zao, uaminifu katika uwajibikaji wa majukumu mbalimbali ndani ya Kanisa na jamii, sanjari na kuwa wawajibikaji katika semina na mafungo mbalimbali kuanzia Jumuiya hadi Taifa. “Naomba uaminifu wenu na upendo wenu uendelee kukua siku kwa siku katika familia zenu na kwa waume zenu na kwa watoto wenu,naomba muendelee kuwa waaminifu  katika wajibu wenu wowote ule mnaoufanya haijalishi unafanya kazi gani uwe mama wa nyumbani,uwe umeajiriwa,uwe mfanyabiashara,uwe nani naomba na hili tulifanye kwa uaminifu na upendo. Nalisema hivi kwa sababu vijana wanaoibukia sasa hivi na naona kuna vijana wengi na wasichana wengi wanapenda sana kupata mshahara wa hela nyingi lakini kazi kidogo sana akitegea akiweza kupata hela bila kufanyakazi anajisifu kweli anasema nimemuweza nimekusanya za bure.

Sasa vijana popote pale mlipo nchini Tanzania tunu yenu iwe ni uaminfu naomba hilo lionekane katika utendaji wenu wa kila siku, lakini pia niombe tuendelee kujiongeza unajua Viongozi wetu wa WAWATA iwe ni Dekania au Parokia au Jimbo au Taifa wakati mwingine huwa wanapanga semina, hija na mafungo naomba tuwe tunakwenda akina Mama na tuwajibike akina Mama,” amesema Askofu mkuu Kinyaiya. Katika hatua nyingine Askofu Kinyaiya amesema kuwa, suala la mirathi bado ni changamoto katika familia nyingi, na baadhi ya familia na koo kukumbatia mila na tamaduni zinazowabagua akina Mama. “Halafu suala zima la mirathi tatizo kweli kwa baadhi ya familia bado ni tatizo najua sheria iko wazi lakini bado kuna wanaume vichwa ngumu kweli Mama akifiwa wanachofikiria ndugu ni kuja kuchukua kila kitu wewe mjane wewe utajijua na watoto wako hawajali, sisi wanaume tunaanza kusema mali ya ndugu yetu hiyo ni tabia mbaya sana. Halafu pia akina Baba wanaotoa urithi kwa watoto wao wa kike ni wachache sana yaani anapofikiria urithi anajua ni watoto wa kiume tu! Ukisoma Wagalatia 3:28 Paulo Mtume anasema Mungu kaumba wanaume na wanawake sawa hakuna cha huyu hakuna cha yule wote sawa wote ni watoto wa Mungu na wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,” amesema Askofu mkuu Kinyaiya.

 

04 May 2021, 14:44