Tafuta

 EKOLOJIA FUNGAMANI EKOLOJIA FUNGAMANI 

Amecea inajiandaa na mkutano wake 2022 kuhusu ekolojia fungamani

Katika maandalizi ya Mkutano wa AMECEA 2022 utakaofanyika nchini Tanzania,mada iliyochaguliwa ni Ekolojia Fungamani ambapo waratibu wa kitaifa wa Caritas na Tume ya haki na amani wa Mabaraza ya maaskofu wamezindua utafiti kuhusu matokeo ya Waraka wa Laudato si’ utakaofanyika katika nchi zote wanachama wa Amecea.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mkutano wa mwaka wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki (AMECEA) utakaofanyika mnamo 2022 utajikita kwenye mada ya Ekoloja na utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja. Ni mkutano unaowashirikisha maaskofu wa Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan, Tanzania, Uganda na Zambia. Mkutano wa mwaka ujao utafanyika nchini Tanzania. Katika matazamio ya mkutano huo, waratibu wa kitaifa wa Caritas na Tume za Haki na amani, wamezindua utafiti juu ya matokeo ya Waraka wa “Laudato sì” kuhusu maendeleo endelevu na fungamani, Afrika Mashariki. Utafiti huo unakusudia kuandaa mwongozo wa kuhamasisha jumuiya za Wakatoliki mahalia, kuhusu mambo yaliyomo kwenye Waraka wa Papa Francisko.

Kwa mujibu wa maelezo zaidi kutoka kwa Padre Paul Mung’athia Igweta, mratibu wa Kitengo cha uhamasishaji wa Maendeleo Fungamani ya binadamu (Pihd), amethibitisha kuwa timu ambayo itafanya utafiti itaingiliana na watu kutoka nchi mbali mbali za Kanda, ili kuelewa ni kitu gani wanajua kuhusu waraka wa “Laudato si”, nini wanafikiria juu yake na nini kimefanywa au kinahitajika kufanywa ili kutekeleza mapendekezo yake. Njia iliyochaguliwa ni kuona, kujadili na kutenda kulingana na matokeo ya utafiti. Kwa maana hiyo Waratibu wa Haki na Amani watatathmini uchapishaji wa mwongozo wa katekesi na muhtasari rahisi wa “Laudato Sì”.

Timu hiyo tayari imeunda zana muhimu za kufanyia utafiti huo ambazo sasa zinachunguzwa na waratibu, maaskofu na makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu. Wazo pia ni kuwashirikisha wanatalimungu ili utafiti uweze kuwa na msimamo wa kichungaji zaidi. Kwa kuongezea, tafsiri yao kwa lugha nyingine zinazozungumzwa katika kanda zao zimepangwa, pamoja na Kiamhariki kinachozungumzwa nchini Ethiopia, Kiswahili na Chichewa, lugha inayotumiwa hasa Malawi, lakini pia katika nchi ya Zambia, Msumbiji na Zimbabwe.

Kikao cha hivi karibuni kilichofanyika kwa njia ya mtandao kiligundua maandalizi ya uchunguzi, hasa mafunzo kwa watakaohoji na maswali kadhaa ambayo yatawasilishwa kwa wahojiwa, pamoja na Jumuiya Ndogo za Kikristo (SCC), vijana na hata watoto. Mkutano huo uliangazia umuhimu wa kukuza uelewa pia wa maoni ya umma ya Kiafrika juu ya uharaka wa uongofu wa mazingira, hasa juu ya ulinzi wa bioanuwai, unyonyaji endelevu wa maliasili na juu ya umuhimu wa kuhakikisha maji na hewa safi kwa wote katika wakati muhimu na kwa mustakabali wa ubinadamu ambao una hatari ya kujiangamiza. Ikumbukwe kwamba mkutano wa mwisho wa Amecea ulifanyika mnamo Julai 2018 huko Addis Ababa, Ethiopia, kwa kuoongozwa na kaulimbiu: “Utofauti wa kupendeza, utu sawa na umoja wa amani katika Mungu” ambapo ulizungumzia mizozo inayoendelea ya kikabila na kidini katika kanda za Afrika mashariki.

16 May 2021, 13:46