Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tano ya Kipindi cha Pasaka: Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli na Baba yake ndiye mkulima na wafuasi wake ni matawi yanayopaswa kukaa ndani mwake ili kuzaa matunda ya utakatifu wa maisha. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tano ya Kipindi cha Pasaka: Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli na Baba yake ndiye mkulima na wafuasi wake ni matawi yanayopaswa kukaa ndani mwake ili kuzaa matunda ya utakatifu wa maisha. 

Tafakari Jumapili ya 5 Pasaka: Kristo Yesu Ni Mzabibu wa Kweli!

Mimi ni mzabibu wa kweli na Baba yangu ni mkulima, ndiyo maneno anayoanza nayo Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya Dominika ya leo. Ndio kusema Yesu anajitambulisha kuwa mzabibu na matawi yake ndio jumuiya ya wabatizwa, jumuiya ya wale wote wanaoamua kuunganisha na kuyafananisha maisha yao na Kristo Mfufuka, ndio Kanisa lake. Umoja na mshikamano ni muhimu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani ya Kristo Mfufuka iwe daima nanyi! Katika Maandiko Matakatifu, taifa la Israeli lilitambulishwa na kufananishwa kama shamba la mizabibu lenye rutuba hasa pale lilipobaki aminifu kwa Mungu; lakini kila mara walipokuwa mbali na Mungu, hapo lilifananishwa na ardhi au shamba lililokosa rutuba nzuri, na hivyo kushindwa kutoa zabibu nzuri, na hata kushindwa kutoa mvinyo mzuri wa kufurahisha moyo wa mwanadamu. Divai ni kinywaji kilichotokana na zabibu nzuri kama tunavyoona katika tafakuri yetu ya leo, ni ishara ya furaha. Zaburi 104:15 “divai ya kumchangamsha…” Somo la Injili ya leo linatuonesha badala yake kuwa shamba la mizabibu, na hata miti ya mizabibu sio tena Taifa la Israeli bali ni Yesu Kristo Mwenyewe, ambaye kwa njia ya sadaka yake ya upendo pale msalabani, sisi sote tunakombolewa, na hata kuunganishwa pamoja naye katika shamba lake la mizabibu. Ni mwanzo wa uumbaji mpya kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ni kwa tendo hilo la Wokovu, nasi tunaalikwa kuwa sehemu ya huu mti wa mizabibu, yaani Kristo Mfufuka, kwa kulishika Neno lake na kuishi maisha yetu kadiri ya Neno hilo. Rejea Yohane 15:2-4.

Ni kwa njia ya kujishikamanisha naye, tunakuwa nasi matawi yenye kuweza kuzaa matunda mema. Mtakatifu Francisko wa Sale alipenda kusema, tawi linalojishikamanisha na shina linatoa matunda sio kwa uwezo wake peke yake bali kwa njia na msaada wa shina lenyewe; hivyo hata nasi sasa, matendo yetu mema hayatokani na juhudi au bidii zetu peke yetu bali ni kutokana na kuunganika kwetu na Kristo. Ni kwa msaada wa neema zake nasi tunaweza kuzaa matunda mema. Ni siku na kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, nasi tunaunganishwa na shina, yaani Fumbo la Pasaka la Kristo, ndio kufa na kufufuka naye, tunapata hadhi na maisha ya kuwa nasi wana wa Mungu na warithi wa uzima wa milele pamoja na Mwana pekee wa Mungu, Kristo Mfufuka. Ni kwa kuunganika na Kristo hapo nasi tunajaliwa neema ya kuishi maisha ya neema, maisha ya urafiki na Mungu na wengine. Pasaka ni kipindi cha neema kuweza kuutafakari tena Ubatizo wetu, ndio kusema muunganiko wetu na tendo la ukombozi wetu, yaani mateso, kifo na ufufuko. Ni kipindi cha kuangalia tena ahadi zetu tulizoweka siku ile ya Ubatizo wetu, ahadi ya kuwa waaminifu daima kwa Mungu na kuacha yale yote yanayotutenga naye, yanayotufanya kukosa kuzaa matunda mema katika maisha yetu.

Nchi ile ya ahadi si tu ilikuwa inatiririka maziwa na asali bali pia mizabibu na mizeituni, na hivyo kila familia ya Kiyahudi pembeni ya nyumba zao walipanda mizeituni na matawi yake kutoa kivuli safi wakati wa kiangazi. 1 Wafalme 5:5 Ni kutoka matunda ya mizabibu waliweza pia kupata matunda, lakini sana kwa ajili ya kutengeneza divai nzuri na tamu.  Mzabibu na shamba la mizabibu ni ishara za furaha na sherehe, na zinatumika mara nyingi katika Maandiko Matakatifu zikimaanisha baraka zake Mungu kwa taifa lake. Hata Yesu Kristo naye aliyelelewa na kukulia katika mazingira hayo na ndio maana naye anatumia lugha ya wakulima inayoakisi maisha ya kawaida ya watu wake. Kama tulivyotangulia kuona hapo juu kuwa ili kuelewa vema lugha ya picha inayotumika katika somo la Injili ya leo, ni vema pia kukumbuka kuwa daima shamba la mizabibu la Bwana katika Agano la Kale ni Taifa la Israeli. Hosea 9:10 “Mwenyezi Mungu asema: Nilipowakuta Waisraeli walikuwa kama zabibu jangwani.” Isaya 27:2-5 “Siku hiyo, Mwenyezi Mungu atasema hivi: Imbeni utenzi wa shamba langu zuri la mizabibu!

Mimi, Mwenyezi Mungu, ni mkulima wake; nalimwagilia maji kila wakati. Ninalilinda usiku na mchana, lisije likaharibiwa na mtu yeyote. Silikasirikii tena shamba hili; kama miiba na mbigili ingelilivamia, mimi ningepambana nayo na kuichoma moto. Maadui wa watu wangu wakitaka ulinzi wangu, basi, na wafanye amani nami; naam, wafanye amani nami.” Hivyo tunaona manabii wakiimba na kulitambulisha taifa lile teule kama shamba la mizabibu la Mungu mwenyewe. Ni kwa kuunganika na Mungu mwenyewe, taifa lile linakuwa na hakika ya kuzaa matunda mazuri, na kinyume chake ni kuangamia kwake. Taifa la Israeli kama anavyotuonesha Nabii Isaya, lilikuwa ni shamba la mizabibu lilipandwa kwenye ardhi nzuri na yenye rutuba juu ya kilima, lakini walipomuasi na kuwa mbali na Mungu basi nalo likakoma kutoa zabibu nzuri na badala yake kuzaa zabibu chungu. Isaya 5:1-4 “…Ni kitu gani nilichokosa kulifanyia shamba langu? Na nilipotazamia lizae zabibu nzuri, mbona basi, likazaa zabibu chungu?” Nabii Yeremia 2:21 pia anatuonesha juu ya ukengeufu wa taifa lile la Israeli; “Lakini mimi nilikupanda kama mzabibu mteule, mzabibu wenye afya na wa mbegu safi; mbona basi umeharibika, ukageuka kuwa mzabibu mwitu?”

Ni katika mazingira haya ya kuwa mbali kwa uasi na ukengeufu, Mwenyezi Mungu analiondolea taifa lile sifa ya kuwa shamba lake zuri la mizabibu na lenye kuzaa matunda mazuri. Hivyo usalama na kuzaa kwake matunda mema, haitokani na kitu kingine chochote, bali uaminifu na muunganiko wake na Mungu mwenyewe. Isaya 5:5-7 “Na sasa nitawaambieni nitakavyolifanya hilo shamba langu. Nitauondoa ua wake, nalo litaharibiwa. Nitaubomoa ukuta wake, nalo litakanyagwakanyagwa. Nitaliacha liharibiwe kabisa, mizabibu yake haitapogolewa wala kupaliliwa. Litaota mbigili na miiba. Tena nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. Naam! Shamba la mizabibu la Mwenyezi Mungu wa majeshi ni jumuiya ya Waisraeli, na mizabibu mizuri ni watu wa Yuda. Yeye alitazamia watende haki, badala yake wakafanya mauaji; alitazamia uadilifu, badala yake wakasababisha kilio!” Pamoja na Taifa lile teule kushindwa kuwa aminifu kwa Mungu bado tunaona Mwenyezi Mungu hakati tamaa wala kuwaacha watu wake, kwani Yeye daima anabaki kuwa ni mwaminifu. Waroma 11:29 “Maana Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo.” Na hivyo kutoka shina lile la kale lilishindwa kuzaa matunda mazuri, Mwenyezi Mungu anachipusha shina jipya na zuri katika siku ile ya Pasaka, na ndio mzabibu wa kweli, yaani Yesu Kristo Mfufuka. Na Taifa lake teule sasa ndio Kanisa lake.

Mimi ni mzabibu wa kweli na Baba yangu ni mkulima, ndiyo maneno anayoanza nayo Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya Dominika ya leo. Anajitambulisha kwa lugha ya picha kama mzabibu tena wa kweli. Yeye ni mzabibu kwa maana ya mti wenye kubeba matawi na wafuasi wake ni matawi ya huo mti wa mzabibu, na Baba yake ndiye mkulima. Ndio kusema Yesu anajitambulisha kuwa mzabibu na matawi yake ndio jumuiya ya wabatizwa, jumuiya ya wale wote wanaoamua kuunganisha na kuyafananisha maisha yao na Kristo Mfufuka, ndio Kanisa lake. Ni Yesu kama mti wa mzabibu anayetoa uzima na kuwezesha matawi kuzaa matunda, kwani tawi likibaki peke yake haliwezi kuzaa matunda na badala yake unyauka na kuchomwa moto. Ila tawi linalobaki katika mti ndilo linalochipua na kuzaa matunda. Mtakatifu Agustino alipenda kutumia msemo wa Kilatini; “Aut vitis aut ignis”, ukiwa na maana; “Aidha mzabibu au moto”, salama na hakika ya maisha yetu ni katika kuwa na muunganiko wa shina yaani mzabibu, yaani Yesu Kristo Mfufuka na kinyume chake ni kuangamia na kuyapoteza maisha yetu.

Kwa desturi mkulima aliwajibika kulitunza na hasa kukata matawi yasiyofaa pamoja na vichipukizi vilivyokuwa dhaifu kwa mwaka mara mbili. Wakati wa majira ya baridi mkulima alipaswa kuondoa matawi yale yasiyohitajika na wakati wa mwezi wa nane pia kuondoa vichipukizi vilivyoonekana dhaifu. Labda mfano huu usipoeleweka vema unaweza kutupa picha potofu ya Mungu aliye Baba Mwema na Mwingi wa Huruma kwa wanawe. Ni vema ieleweke kuwa nia na shabaha haswa ni matunzo kutoka kwa mkulima, na ndivyo Mwenyezi Mungu daima analitunza na kulilinda kundi lake, Kanisa lake na kila mmoja wetu ili maisha yetu yaweze kuzaa matunda yaliyo mema. Ni vema kutambua nafasi ya Mungu mwenyewe katika kuishi imani yetu. Kila mmoja wetu anayo madhaifu yake au mambo yanayomzuia katika kuzaa matunda mema katika maisha yake, ni haya yasiyofaa Mwenyezi Mungu anataka kuyaondoa na kuyatupa nje yetu ili tubaki wenye kuzaa matunda mema. Zaidi Yesu Kristo anatualika kubaki ndani mwake. Neno “KUBAKI” au “KUISHI”, kwa Kigiriki ‘’μενειν’’ (menein), neno hili Mwinjili Yohana analitumia pale mwanzoni wanafunzi wa Yohana walipotaka kufahamu wapi Yesu Kristo anaishi na wakabaki naye. Kubaki hapa halina maana ya sehemu au mahali fulani bali ni kuingia katika mahusiano ya upendo ya ndani kabisa.

Ni kubaki moyoni na rohoni na akilini. Hivyo Yesu Kristo anatualika nasi kubaki naye kwa maana ya kubaki katika nafsi na mioyo yetu na akili zetu. Ni kumbeba katika nafsi zetu. Ni kuishi ndani yake naye aishi ndani mwetu, ni kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa, ni kuruhusu maisha yetu yatawaliwe na kuongozwa naye, ni kutokukubali kufikiri au kutenda lolote bila neema na maongozi yake. Na ndio pia tumesikia kutoka somo letu la pili la leo kutoka Waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa watu wote. “Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.” Kitenzi tunachokisikia hapa, yaani, kukaa = kubaki = kuishi; kikimaanisha mauhisiano ya ndani kabisa, kujifungamanisha kwa uaminifu wote. Na hakika ni mwaliko wa sisi kujifungamanisha na Mungu sio kwa sababu sisi tulikuwa wa kwanza au tunachukua nafasi ya kwanza kumwendea Mungu bali kwa ni yeye kwa upendo wake usio na kipimo wala mfano amekuwa wa kwanza kutaka mahusiano nasi wanadamu. Na kuunganika naye kama anavyotuonesha Mtume Yohane ni katika kushika amri zake, yaani, kumpenda Mungu na jirani.

Na ndio somo letu la Injili ya leo, kama mojawapo ya wosia wa Yesu kwa wanafunzi wake kabla ya fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake. Ni Yesu anayetualika kuwa na mahusiano ya pekee naye, akiwa mzabibu wa kweli nasi tukiwa matawi yake. Matawi hayawezi kuzaa matunda yakiwa nje ya shina, maana tawi nje ya shina linasinyaa na kunyauka. Na ndio hakika ya maisha yetu ya kiroho, ni katika kujifungamanisha na kujishikamanisha naye. Yesu leo anajitanabaisha sio tu kama mzabibu kama anaongeza kivumishi pale “wa kweli”, likiwa na maana kuwa kuna mzabibu usio wa kweli na ndio malimwengu, yale yote yanayokwenda kinyume na Neno na mpango wa Mungu, ni kujishikamanisha na yale yote yanayotuweka mbali na Kristo, maisha yasiyozaa matunda mema bali zabibu chungu, ndio dhambi na hatimaye mauti. Maisha ya kila mfuasi wake Kristo Mfufuka hayana budi kuwa kama tawi lenye kujishikamanisha na mzabibu wa kweli, na Kristo mwenyewe, ili kuzaa matunda mema maisha yetu kama matawi hayana budi kutunzwa kwa kukatwa kila mwaka, ndio kutoa yale yote yanayotukwamisha katika kuzaa matunda mema na mazuri, kutoa kila aina ya kilema cha kiroho ili maisha yetu yaweze kumuakisi kweli Kristo aliye mzabibu wa kweli, maisha yetu hayana budi kutoa daima matunda mema, matunda yatokanayo na neema na baraka zake Kristo Mfufuka.

Ni kwa njia ya Neno lake lenye makali kuwili kama tusomavyo kutoka Waraka kwa Waebrania nasi tunaongozwa na kuelekezwa njia ya kweli iletayo uzima wa kimungu. Utukufu wa Mungu unaonekana kwa utayari wetu wa kuitikia upendo wake wa milele kwa kila mmoja wetu. Kama vile mzabibu hautoi matunda mema kwa ajili yake wenyewe ndivyo nasi tunavyoalikuwa kutoa zabibu nzuri ya upendo kwa Mungu na kwa jirani. Maisha ya mfuasi wa Kristo daima ni baraka kwa wale wote wanaomzunguka, ni maisha yanayotoa sifa kwa Mungu, maisha yetu yanapaswa kuwabariki wengine ili hatimaye waweze kumsifu Mungu kwa uwepo wetu. Nawatakia tafakuri na Dominika njema.

28 April 2021, 16:23