Tafuta

Vatican News
FTafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka: Umoja, mshikamano na mafungano na Kristo Yesu kwani ndiye Mzabibu wa kweli na wengine ni matawi yanayochota nguvu za kiroho kutoka kwake! FTafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka: Umoja, mshikamano na mafungano na Kristo Yesu kwani ndiye Mzabibu wa kweli na wengine ni matawi yanayochota nguvu za kiroho kutoka kwake! 

Neno la Mungu Jumapili V ya Pasaka: Choteni Nguvu Kwa Yesu

Leo tunaalikwa kutafakari kuhusu: Umoja, Mshikamano na Mafungamano yetu na Kristo Yesu, kwani Yeye ndiye Mzabibu wa kweli na wengine sisi ni “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” ni matawi yanayochota nguvu zake za kiroho kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma kama kielelezo cha imani na upendo. Mvinyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kanisa likiwa limezamisha mizizi yake katika upendo wa Kristo Yesu linaweza kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anasema “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lolote… mtatupwa nje kama tawi na kunyauka”. Kristo Yesu ni chemchemi ya nguvu ya maisha ya kiroho, kumbe, huu ni mwaliko wa kushikamana na kufungamana na Kristo Yesu katika maisha na wito wa kila mmoja wetu. Na kwa utangulizi huu, ninapenda kuchukua fursa hii kukualika ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Pasaka. Leo tunaalikwa kutafakari kuhusu: Umoja, Mshikamano na Mafungamano yetu na Kristo Yesu, kwani Yeye ndiye Mzabibu wa kweli na wengine sisi ni “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” ni matawi yanayochota nguvu zake za kiroho kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma kama kielelezo cha imani na upendo. Kimsingi upendo wa dhati unajionesha katika matendo mema. Mtakatifu Stefano Shahidi ni chachu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa.

Katika Liturujia, ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa fumbo wa Yesu Kristo, yaani Kanisa na Kichwa na viungo vyake. Hiki ni kielelezo kingine kinachotolewa na Mtakatifu Paulo, Mtume ili kuelezea mafungamano kati ya mwamini na Kristo Yesu. Katika hili Mtakatifu Paulo anakaza kusema, tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika. Rej. Rum. 11:16. Hii inatokana la pendo la Mungu ambalo limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi waja wake. Kukaa ndani ya Kristo ili hatimaye, kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, kuna haja kwa Wakristo kuhakikisha kwamba wanatekeleza kikamilifu ahadi zao za Ubatizo. Ahadi za Ubatizo zinamwezesha mwamini kukataa ubaya, kwa kukataa vishawishi, dhambi na nafasi zake, lakini zaidi ni kumkataa Shetani, Ibilisi na mambo yake yote pamoja na fahari zake zote!

Hatua ya pili ili kushikamana na kufungamana na Kristo Yesu ni kukiri na kushuhudia imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu: aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu ni Mlango wa huruma ya Mungu na kwa njia yake watu: wanaonja upendo wa Mungu anayefariji, anayetakasa, anayesamehe na hatimaye, kuwapatia waamini wake matumaini. Kristo Yesu ni Mlango wa wokovu wa watu wake na Yeye ndiye wokovu wenyewe. Kumbe, basi, Ubatizo unakuwa ni mwanzo mpya wa ujenzi wa mafungamano na mshikamano na Kristo Yesu, Mzabibu wa kweli. Na kwa njia hii, waamini wanakuwa ni watu wake Kristo Yesu, yaani “Wakristo”. Kumbe, Wakristo wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wakiwa wanakimbia huruma na upendo wake wa milele kama ilivyokuwa kwa yule Mwana mpotevu na Baba Mwenyewe huruma. Uaminifu na udumifu katika mahusiano na mafungamano haya ni muhimu sana. Kukaa ndani ya Kristo maana yake, ni kuendelea kukaa katika huruma na upendo wake wa daima kwa njia ya: Sala kama kielelezo cha majadiliano baina ya watu wawili wapendanao.

Ni mwaliko wa kushiriki kikamilifu “Actuosa participatio”, kwa uadilifu, Ibada na Uchaji wa Mungu maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yaani Sakramenti za Kanisa. Lakini kwa namna ya pekee kabisa: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayomkirimia mwamini chakula cha maisha yake ya kiroho kwa kutambua kwamba, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanahimizwa: Kuadhimisha, Kuabudu na Kutafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wajichotee huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Ili kuweza kukaa ndani ya Kristo Yesu ili hatimaye kuzaa mtunda yanayokusudiwa, kuna haja pia ya kumwilisha: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anatukuzwa na mwanadamu anatakatifuzwa. Kukaa ndani ya Kristo Yesu ni kushika Amri na Maagizo yake.

Ni kuubeba Msalaba kwa imani, matumaini na mapendo na kuanza kumfuasa Kristo Yesu katika Njia yake ya Msalaba. Kwa njia hii waamini wataweza kukua na hatimaye, kushuhudia ukomavu wao wa imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kukaa ndani ya Kristo ni kuambata mambo msingi katika maisha kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya Kikristo. Waamini wajitahidi kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na Maskini kama sehemu ya mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Kumbe, jitihada zetu za kutafuta na kutaka kujenga misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli zianze na kupata kibali chake kutoka kwa Kristo Yesu, maana pasipo Kristo Yesu, wafuasi wake “hawawezi kufua dafu”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya Kanisa kuwa na mashuhuda wanaothubutu kuendelea kusali na kusamahe, kama mfano bora wa kuigwa. Kati ya watu walioombewa na Stefano alipokuwa anapigwa kwa mawe alikuwepo pia kijana Sauli aliyeona na kushuhudia vyema kuuawa kwake. Lakini baadaye kwa njia ya neema ya Mungu, Sauli akatubu na kumwongokea Mungu, akageuka kuwa ni Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Huyu ndiye mmisionari aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia.

Mtakatifu Paulo alizaliwa upya kwa neema ya Mungu na kwa njia ya ushuhuda wa msamaha wa Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi, kiasi kwamba, amekuwa ni mbegu ya toba na wongofu wake mwenyewe, uliomwezesha kukaa ndani ya Kristo na kuzaa matunda ya kuenea kwa Habari Nje ma ya Wokovu. Haikuwa rahisi hata kidogo kwa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo kumkubali na kumpokea Mtume Paulo na kuwa miongoni mwao kwa sababu ya historia na matendo yake ya ukatili dhidi ya wafuasi wa Kristo! Ushuhuda wa Mtume Barnaba na faraja ya Roho Mtakatifu ililiwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa akabahatika kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yake, chachu ya uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto mashiko. Hii ni changamoto ya kuendelea kudumisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake kwa kujenga, kudumisha na kulea dhamiri nyofu, ili kuweza kumpenda Mungu na jirani.

Liturujia J5 ya Pasaka
30 April 2021, 15:18