Tafuta

Vatican News
Frt. Edwin Jerome Lyanga wa Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasimulia historia fupi ya wito wake. Malezi na makuzi ya kifamilia! Frt. Edwin Jerome Lyanga wa Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasimulia historia fupi ya wito wake. Malezi na makuzi ya kifamilia! 

Historia Fupi ya Shemasi Mteule Edwin Jerome Lyanga, Ifakara

Wito wangu ulianza nikiwa mdogo sana baada ya kuvutika na Padre aliyekuwa anaimba Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, Ijumaa kuu. Mawazo yangu yalinituma kuwa vile alikuwa ni Yesu mwenyewe aliyekuwa anajibu maswali kwa kuimba vizuri. Baada ya kuelekezwa na babu yangu kuwa alikuwa ni mtu wa kawaida tena yeyote yule angeweza kuimba vile, nikatamani kuwa Padre.

Na Frt. Edwin Jerome Lyanga, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma.

Jandokasisi Edwin Jerome Lyanga, wa Jimbo la Ifakara, Tanzania ni kati ya Mafrateri 29 wanaotarajiwa kupewa Daraja ya Ushemasi, Mei Mosi, 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ndiye atakayeongoza Ibada hii ya Misa takatifu. Kati ya Majandokasisi 29, kati yao 11 wanatoka Barani Afrika. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, iliyoadhimishwa Jumapili, tarehe 25 Aprili 2021, ulinogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021. Frater Edwin Jerome Lyanga anasimulia historia fupi ya maisha na wito wake.

Jina langu ni Frt. Edwin Jerome Lyanga, wa Jimbo la Ifakara, Tanzania, nimezaliwa katika Parokia ya Ifakara, Jimbo Katoliki la Ifakara. Nimesomea shule ya msingi Kiyongwile, baada ya hapo nikajiunga na seminari, mwaka mmoja wa pre-form one katika Seminari ya Mtakatifu Patriki Sofi 2005, na Seminari ndogo ya Mtakatifu Francisko, Kasita iliyopo Jimbo la Mahenge kati ya mwaka 2006-2012 kwa elimu ya sekondari. Nimesoma Falsafa na mwaka mmoja wa taalimungu Katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augostino, Peramiho, Jimbo kuu la Songea, kati ya mwaka 2012-2016. Jimbo lilinituma kumalizia masomo ya taalimungu Roma na sasa namalizia masomo yangu ya shahada ya uzamili taalimungu ya Maandiko Matakatifu, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Wito wangu ulianza nikiwa mdogo sana baada ya kuvutika na Padre aliyekuwa anaimba mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, Ijumaa kuu. Mawazo yangu yalinituma kuwa vile alikuwa ni Yesu mwenyewe aliyekuwa anajibu maswali kwa kuimba vizuri. Baada ya kuelekezwa na babu yangu kuwa alikuwa ni mtu wa kawaida tena yeyote yule angeweza kuimba vile baada ya kupitia malezi maalumu mpaka kufikia hatua ile nami nikawaka tamaa na nia ya kusimama pale mbele siku moja na kuimba kama Yesu.

Katika malezi ya upadre nimekuja kujua lengo hasa la maisha yangu ya wito, kutolea maisha yangu kwa ajili ya Kristo na watu wake, hamna jambo lililonipa nguvu, faraja na furaha kama kujua kama siku moja nitaweza kutumia nguvu na vipaji vyangu kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kwa utumishi wa huduma kwa watu wake. Kwa namna ya pekee, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu anayenipitisha katika mapito yote ambayo ni hatua muhimu katika malezi yangu, namwomba anifungue macho zaidi niweze kuona kile ambacho anataka nichote katika kila hatua ninayopitia. Namshukuru Mungu kwa kunivumilia nami niwe kati ya wale wanaojongea Altare yake maana mara zote naonja ukuu wa huruma na upendo wake wa kibaba ambao najua sina chochote cha pekee kustahili yote hayo. Pili, napenda kumshukuru Askofu na Jimbo langu kwa misaada yote ya hali, mali na malezi kwani baada ya wazazi wangu najivunia kuwa katika jumuia hii yenye kujali, Mwenyezi Mungu awabariki wote; Askofu wangu Mhashamu Salutaris Melchior Libena na waandamizi wake wote, Mkurugenzi wetu wa Miito na paroko wangu na hata aliyekuwa paroko wangu kipindi naanza safari hii na mapadre wote wa Jimbo Katoliki la Ifakara na Mahenge.

Tatu, napenda kuwashukuru walezi wangu wote kuanzia Seminari ndogo, Seminari kuu Peramiho na hata jumuiya nzima ya Urbaniano bila kuisahau Jumuiya ya watanzania hapa Roma; nilikuwa kama udongo mikononi mwa wafinyanzi, nao kwa uvumilivu na upendo mkubwa wamenisaidia kuwa hivi nilivyo, kujitambua na kumtambua Mungu ninayetaka kumtumikia, Kanisa lake na watu wake na hasa kwa mafundisho yao yote. Nne napenda kuwashukuru walelewa wenzangu waseminari wa Jimbo Katoliki la Ifakara, waseminari na marafiki wote nilio nao na wale waliobadilisha njia, natambua mchango wao katika kuwa kwangu hivi nilivyo. Na mwishoni napenda kuishukuru familia yangu, wadau wote na ndugu zangu wanaonisindikiza kwa sala zao na maneno yao ya kutia moyo huku wakisubiria kwa hamu kama vile nia yangu ni wito wetu wote, Mungu awabariki sana; wote wanaoishi na kwa waliotangulia Mungu awapumzishe katika amani yake, hasa baba yangu Mpendwa Jerome Lyanga, baba zangu wakubwa na wadogo bila kumsahau marehemu babu yangu mpendwa Mzee Lyanga ambaye pamoja na bibi yangu walinifunza kwa vitendo kuwa Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana kama kielelezo cha udugu wa kibinadamu.

Shemasi Edwin Lyanga

 

29 April 2021, 16:31