Tafuta

Vatican News
Shemasi Mtarajiwa Achiles Narcis Charukula kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma Tanzania anasema, chimbuko la wito wake ni unadhifu wa Mafrateri, Sala na Sadaka ya Misa takatifu Parokiani kwake. Shemasi Mtarajiwa Achiles Narcis Charukula kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma Tanzania anasema, chimbuko la wito wake ni unadhifu wa Mafrateri, Sala na Sadaka ya Misa takatifu Parokiani kwake. 

Achiles N. Charukula Shemasi Mtarajiwa toka Kigoma! Wito Wake!

Frt. Achiles Narcis Charukula ni kati ya Mafrateri 29 wanaotarajiwa kupewa Daraja ya Ushemasi, Mei Mosi, 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kardinali Luis A. G. Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ndiye atakayeongoza Ibadaa ya Misa takatifu. Kati ya Majandokasisi 29, kati yao 11 wanatoka Afrika. Unadhifu na Sala Mvuto wa Wito wake!

Na Frt. Achiles N Charukula, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, - Roma

Daraja Takatifu ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo Yesu kwa Mitume wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati; hivyo hii ni Sakramenti ya huduma ya kitume nayo ina ngazi kuu tatu: yaani: Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Mapadre kwa mamlaka wanayokabidhiwa na Mama Kanisa wanakuwa ni wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma yanayotekelezwa katika maeneo yao. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hutenda kwa nafsi ya Kristo Yesu na kutangaza Fumbo lake; huyaunganisha maombi ya waamini na Sadaka ya Kristo Yesu Msalabani inayoadhimishwa kila siku katika Ibada ya Misa Takatifu. Ni daraja inalowataka kujenga na kuimarisha umoja kati yao kama Mapadre pamoja na Askofu wao. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo kwa kupewa chapa isiyofutika na hivyo kufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi na Mhudumu wa wote. Shemasi ni msaidizi mkuu wa Askofu na Mapadre katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; Ni wahudumu wa Neno la Mungu na matendo ya huruma yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Frt. Achiles Narcis Charukula ni kati ya Mafrateri 29 wanaotarajiwa kupewa Daraja ya Ushemasi, Mei Mosi, 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ndiye atakayeongoza Ibada hii ya Misa takatifu. Kati ya Majandokasisi 29, kati yao 11 wanatoka Barani Afrika. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, iliyoadhimishwa Jumapili, tarehe 25 Aprili 2021, ulinogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021.

Naitwa Frt. Achiles Narcis CHARUKULA. Nilizaliwa tarehe 2 Mei 1990 katika Kigango cha Mtakatifu Luka, Makere, Parokia ya Makere jimboni Kigoma, Tanzania. Mimi ni mzaliwa wa kwanza kati ya watoto tisa. Nilihitimu elimu ya kidato cha sita mwaka 2012 katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo, Jimbo Katoliki la Kigoma. Masomo hayo yalitanguliwa na elimu ya kidato cha nne niliyoipata katika shule ya sekondari Makere (2006-2009), na kabla ha yapo, elimu ya shule ya msingi ambayo nayo niliipata katika shule ya msingi Makere (1999-2005). Kwa sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya uzamili ya Sheria za Kanisa katika Chuo kikuu cha Kipapa Urbaniana, Roma. Ikumbukwe kuwa nimeanza masomo haya baada ya kuhitimu masomo ya taalimungu hapohapo chuoni Urbaniana mwaka 2019, ambayo nayo yalitanguliwa na masomo na malezi ya falsafa niliyochota kutoka katika Seminari kuu ya Mtakatifu Anthony wa Padua -Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba.

Wito: Safari yangu ya wito ilianza katika uchanga wangu nilipokuwa katika kikundi cha watoto watumikiaji Altareni na kikundi cha Utoto Mtakatifu wa Yesu. Hakika ni katika kipindi hicho ambapo nilipenda sana kuwa padre katika maisha yangu. Nilivutwa na maisha ya mapadre waliokuwa wakihudumia parokiani kwetu Makere na kutamani kufahamu zaidi ni hatua zipi zinazoweza kumfikisha kijana kuwa padre. Aidha nilivutwa na unadhifu wa mafrateli waliokuwa wakija kuhudumu parokiani kwetu wakati wa likizo zao, mmoja wao akiwa ni Gambera wa sasa wa seminari ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo, (Pd. Patrick Tarcisius Mahinja). Hii si kwamba nimesahau masifu ya asubuhi yaliyokuwa yakisaliwa na mapadri na masista baada ya misa parokiani hapo. Ni dhahiri kwamba katika malezi nimejifunza kuwa maisha ya wenye daraja takatifu ni zaidi ya viashiria nilivyo viona mwanzoni. Ni utumishi kwa Mungu na kwa Kanisa lake bila kujibakiza, kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo aliye kuhani milele.

Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, licha ya kufaulu vema mtihani wa kujiunga na seminari ndogo na kuchaguliwa, sikuweza kwenda na badala yake nilijiunga na shule ya Sekondari ya Kata iliyotajwa hapo juu. Hata hivyo hii haikuzima kiu yangu ya kuwa Kasisi wa Kanisa Katoliki. Nilipiga moyo konde, ndoto yangu mtimani nikaihifadhi. Katika hili shukrani nyingi kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na wito, lakini pia kwa mapadre waliohudumu parokiani Makere ambao, si tu walinitia moyo kwa maneno na namna zao za maisha, bali pia walinielekeza na kunisaidia kujiunga na Seminari ndogo ya Iterambogo, kwa kidato cha tano na sita ambako huko wito wangu ulichanua zaidi. Katika muktadha wa maandalizi ya kupokea daraja takatifu ya Ushemasi, nimechagua maneno ya Mtakatifu Tomaso mtume “Bwana Wangu na Mungu Wangu” Yn. 20:28 si tu kwa sababu tuko katika kipindi cha Pasaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, bali pia ni namna yangu ya kukiri Imani yangu kwa Yesu Kristo mfufuka, ambayo pia ni imani yetu Wakatoliki, Imani ya Kanisa ambayo twajivunia kuikiri na kuishuhudia.

Aidha ni katika kuustajabia: ukuu na huruma ya Mungu katika safari yangu ya wito, kwa wema wake mwingi alionionyesha. Ninamshukuru nikikiri imani yangu kwake nikisema “Bwana Wangu na Mungu Wangu”. Ninamstaajabia Mungu nikitambua wazi kabisa kwamba, si kwa haki yangu ninaitwa kumtumikia Mungu katika Sakramenti ya daraja takatifu, bali ni kwa upendo na huruma yake kuu. Ndipo hapo ninapoungana na Mzaburi kusema “Ndiwe Mungu wangu nami nitakushukuru, ndiwe Mungu wangu, nami nita kutukuza”. Zab. 118:28. Ninapomshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na wito, Nawashukuru wazazi wangu Mzee Narcis Charukula na Mama Felista Paulo Mapengo kwa kushiriki kazi ya uumbaji na hivyo mimi nikazaliwa na kulelewa vyema, pamoja na hao nawashukuru wadogo zangu wote kwa kushiriki vema malezi yangu. Natambua na kushukuru mamlaka ya Kanisa jimboni Kigoma, na hivi namshukuru sana Baba Askofu Joseph Roman MLOLA, Askofu wa jimbo katoliki Kigoma na waandamizi wake wote kwa malezi, misaada ya hali na mali na kwa kukubali kwake kunipokea kati ya Waklero jimboni Kigoma mara tu nitakapopokea Daraja takatifu ya Ushemasi hapo 01.05.2021, kwa msaada wa Mungu.

Shukrani hizo zinamwendea pia Baba Askofu mkuu Paul Runangaza RUZOKA wa jimbo kuu katoliki Tabora, aliyenipokea katika nyumba ya malezi akiwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Kigoma mwaka 2013. Nawashukuru mapadre na watawa jimboni Kigoma na seminari zote nilizopitia, Iterambogo, Ntungamo, Bukoba na hapa Urbaniana kwa namna ambavyo kila mmoja amegusa maisha yangu. Ni ngumu kusahau mchango wa waseminaristi wenzangu, wema wa WAWATA jimboni Kigoma, watanzania walioko Roma, taifa lote la Mungu na wote wenye mapenzi mema.

SHEMASI ACHILES CHARUKULA
30 April 2021, 16:11