Tafuta

Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Salam zake za Pasaka kwa mwaka 2021 amekazia: Umuhimu wa watanzania kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa na weledi. Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Salam zake za Pasaka kwa mwaka 2021 amekazia: Umuhimu wa watanzania kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa na weledi. 

Salam za Pasaka kutoka kwa Makamu wa Rais Dr. Philip Mpango

Makamu wa Rais anawataka Watanzania wajenge utamaduni wa kufanya kazi kwa uaminifu, bidi na weledi, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza. Watawa wasali kweli kweli, wafanyabiashara wafanye kazi kwa uadilifu, ukweli na uwazi. Watumishi wa umma wafufuke na kuanza kujielekeza katika mchakato wa ujenzi wa uadilifu, waachane na umauti na uzembe kazini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesikitishwa na taarifa ya kifo cha Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe, kilichotokea tarehe 6 Aprili 2021 katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu zaidi. Rais Samia anasema, Askofu Maluma alikuwa ni mtu mwema, mpenda maendeleo na aliyekuwa tayari kushirikiana na Serikali wakati wote. Ametumia fursa hii kutoka salam zake za rambirambi kwa waamini wa Kanisa Katoliki pamoja na watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Njombe na wote walioguswa na msiba huu. Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kadiri ya Maandiko Matakatifu ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni, mwanadamu amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kustahilishwa kuitwa mwana wa Mungu.

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, tarehe 4 Aprili 2021, Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshiriki Ibada ya Misa Takatifu. Akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma, baada ya Misa Takatifu akapata nafasi ya kusalimiana na watu wa Mungu nchini Tanzania. Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango, amewakumbusha waamini kwamba, kwa muda wa siku arobaini, waamini walifunga na kusali; wakatafakari Neno la Mungu na hatimaye, kulinafsisha katika uhalisia wa maisha yao kama sehemu muhimu sana ya maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka. Ametumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwafikisha katika siku hii adhimu kwani wengi walitamani kuifikia akiwemo Hayati Dr. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano nchini Tanzania. Amesema, kazi ambayo Mwenyezi Mungu amependa kwa neema yake akabidhiwe Dr. Philip Mpango ya kuwa ni Makamu wa Rais ni ngumu.

Mbele yake kuna watanzania milioni 60, kwa umaskini anaouona na kwa wanyonge wengi wanaonekana ni kazi ngumu sana. Dr. Mpango amechukua nafasi hii, kuwaomba watanzania, kumkumbuka na kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili aweze kutembea katika njia ambazo Mwenyezi Mungu anapenda kwa ajili ya watu wake wa Tanzania. Na pia kwa Serikali nzima, akiwemo hata yeye Dr. Philip Mpango, mtumishi wao mkosefu. Wamwombee sana na hasa kupitia kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria Msimamizi wa Tanzania, ili awe Makamu wa Rais mwaminifu, anayesimamia haki za wanyonge na wote wanaodhulumiwa nchini Tanzania. Watanzania waendelee kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kama njia sahihi ya kumuenzi Hayati Dr. John Joseph Pombe Magufuli. Watanzania wajenge utamaduni wa kufanya kazi kwa uaminifu, bidi na weledi, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza. Watawa wasali kweli kweli, wafanyabiashara wafanye kazi kwa uadilifu, ukweli na uwazi. Watumishi wa umma wafufuke na kuanza kujielekeza katika mchakato wa ujenzi wa uadilifu, waachane na umauti na uzembe kazini.

Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA imekuwa ikishtumiwa kwa kuwawekea wananchi viwango vikubwa vya kodi, kiasi cha kuwafanya wafanyabiashara wengi kushindwa kulipa. Na huo ndio mwanzo kwa wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kuanza kukwepa kodi au kutafuta njia za mkato kwa kutoa rushwa. Kumbe, kuna haja ya kujenda jukwaa la majadiliano kati ya TRA na wafanyabiashara, ili waone fahari kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi yao. Mkakati huu unahitaji pia walipa kodi “kupigwa msasa” kuhusu umuhimu wa kulipa kodi. Dr. Philip Mpango katika salam zake za Pasaka kwa watu wa Mungu nchini Tanzania, ameitaka TRA kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kufanya kazi zao kwa haki na uhuru kamili na kamwe wasinyanyaswe. Serikali inahitaji kodi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote. Zoezi hili lifanyike bila ya kuwanyanyasa wafanyabiashara kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu za kulipa kodi nchini Tanzania Lakini kwa wafanyabiashara wasio waaminifu wahakikishe kwamba, wanamrudishia Kaisari yale yaliyo ya Kaisari.

Dr. Philip Isdor Nzabhayanga Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametumia nafasi hii, kuwasilisha salam za Pasaka kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anawasalimia watanzania wote na anawatakia sherehe njema ya Pasaka. Watanzania washerehekehe kwa amani, waendelee kuiombea Tanzania ili iweze kuneemeka zaidi ya hapa ambapo Hayati Dr. John Pombe Magufuli amewafikisha na kuwaachia ili kuendeleza kazi zake njema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Serikali inapenda kuwahakikishia watanzania kwamba, amani itaendelea kutawala, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ambao ni msingi muhimu wa Katiba ya Tanzania utaendelea kuzingatiwa. Watanzania waendelee kufanya kazi ili kuijenga nchi yao.

Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 8 Novemba 1984, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka unaojulikana kama “Tot Tantaeque” yaani “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Hili ni ombi lililotolewa kwa wakati huo na Askofu Anthony Peter Mayalla aliyekuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Alimwomba Mtakatifu Yohane Paulo II, ili Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili aweze kuwa msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia familia ya Mungu nafasi ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhuru. Kwani Tanzania ilipata uhuru wake, siku moja tu, baada ya kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania kunako mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezeshe watanzania kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwaombea Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu. Mtakatifu Yohane XXIII aliwaombea watanzania upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila, utaifa usiokuwa na tija ili watanzania wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanzania na majirani zake; viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele!

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Mkewe Mama Jenisia Mpango, Jumatatu ya Pasaka tarehe 5 Aprili 2021 wamewatembelea watoto, wazee pamoja na watu wenye mahitaji maalum katika Kituo cha Huruma cha Watawa wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, Hombolo, Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania kwa ajili ya kuwafariji na kusherehekea nao Pasaka ya Bwana! Amewapatia chakula, vinywaji na fedha taslimu kwa ajili ya mahitaji muhimu kwa Kituo hiki ambacho ni alama ya Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii. Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema, aliyethubutu kumwilisha Injili katika huduma ya mapendo kwa Mungu na jirani. Akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wagonjwa, maskini na watoto yatima; huduma iliyorutubishwa kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Salam za Pasaka

 

 

 

07 April 2021, 14:07