Tafuta

Vatican News
Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Hiki ni kielele cha maadhimisho ya Fumbo la Ukombozi wa mwanadamu kutoka dhambini. Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Hiki ni kielele cha maadhimisho ya Fumbo la Ukombozi wa mwanadamu kutoka dhambini.  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Juma Kuu: Kesha la Jumamosi Kuu: Hofu ya Kifo!

Katika mkesha huu wa Pasaka ambao kadiri ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa ndio Mama wa kesha zote za Kanisa, Mama Kanisa leo anakazia umuhimu wa Neno la Mungu na hivyo kupendekeza masomo tisa, ikiwa saba kutoka Agano la Kale na mawili kutoka Agano Jipya. Ni mwaliko wa kutembea katika matumaini, imani na mapendo ya Kristo Mfufuka na Mshindi!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Katika mkesha huu wa Pasaka ambao kadiri ya Mtakatifu Augustino ndio mama wa kesha zote za Kanisa, Mama Kanisa leo anakazia umuhimu wa Neno la Mungu na hivyo kupendekeza masomo tisa, ikiwa saba kutoka Agano la Kale na mawili kutoka Agano Jipya. Katika tafakuri yetu yatosha kama kawaida kuchukua somo la Injili na kujikita hapo. Ila ni vema kuchukua muda binafsi na kusoma kwanza nyumbani kwa tafakuri ili kuweza kuutajirisha mkesha huu kwa Neno la Mungu lenye kueleza historia nzima ya wokovu wa mwanadamu kutoka kuumbwa kwa ulimwengu mpaka siku hii kuu ya ufufuko wake Mwokozi wetu. Ufufuko ni uumbaji mpya, ni mwanzo wa maisha mapya kwa kila mfuasi wake Kristo Mfufuka. Mwanadamu tangu mwanzo amebaki na swali la msingi juu ya kwa nini kifo? Kifo kinaleta uchungu na mahangaiko ya nafsi, kila mara mwanadamu anapotafakari kuwa lazima atakufa. Kwa nini maisha yetu yana mwisho hapa duniani? Ni Mungu ametuadaa kwa kutuumba na kutupa maisha ya muda mfupi tu hapa duniani? Kwa nini tunakufa, kwa nini kifo? Ni swali la haki ambalo nawaalika japo kulitafakari pamoja katika mkesha huu mama wa kesha zote za Kanisa.

Mwanadamu amejaribu kutoa majibu ya fumbo la kifo. Katika Maandiko ya kale ya watu wa Mashariki ya mbali Gilgameshi anajaribu kumjibu rafiki yake Akidu kuwa miungu walipomuumba mwanadamu wakabaki nayo wenyewe ile roho ya kutokufa hivyo mwanadamu ameumbwa bila roho idumuyo milele; Mfalme Suleimani naye anajaribu kuona siku zake mwanadamu juu ya uso wa nchi ni kama kivuli kinachotoweka mara moja, hivyo hakuna matumaini katika maisha. Muhubiri naye anaona maisha ya duniani ni ubatili mtupu ni sawa na maisha ya wanyama kwani wote tunakufa. Ni Mzaburi anayejaribu kutualika kuwa swali juu ya kifo hatuwezi kupata jibu lake kwa kutegemea akili zetu au falsafa za kibinadamu bali ni katika kuutafakari upendo wa Mungu kwa mwanadamu, Mungu anamuumba mwanadamu kwa sababu anampenda. Katika zaburi ya 16, tunaona kuwa Mungu hawezi kumwacha mpendwa wake aangamie sheol, kule kuzimu, kwenye shimo la umauti bali atabaki naye milele. Ni mzaburi anatupa japo mwanga wa matumaini pale anapotualika kuutafakari upendo wa Mungu.

Jioni ya Ijumaa Kuu, baada ya maziko yake Yesu Kristo, waliokuwepo pale Mlimani Kalvari akina Yusufu wa Arimateya na akina Nikodemo na hata wale wanawake waliokuwa wamesimama kwa mbali, walirejea majumbani kwao wakiona kuwa sasa kila kitu kumhusu Yesu kimefika tamati, kimefika mwisho. Kila kitu kumhusu Yesu kimesimama, hakuna tena matumaini. Walirejea katika nyumba zao kwa ajili ya mlo wa jioni wa Pasaka bila matumaini yeyote. Simulizi za juu ya ufufuko wake Yesu Kristo kadiri ya wainjili wote wanne tunaona zinatofautiana. Ni vyema tangu mwanzo kuelewa kuwa lengo na shabaha ya waandishi wote wanne ilikuwa sio kutoa kila aina ya taarifa juu ya nini kilichojiri kwa hakika katika tukio lile, badala yake wanatumia ishara mbali mbali ili kutoa Katekesi juu ya kweli hii ya imani, “Kerygma” ya ufufuko. Mwinjili Marko anaeleza kuwa wanawake waliona kijana mle kaburini; Mwinjili Luka anasema juu ya watu wawili;Mwinjili Matayo anaeleza juu ya ishara za tetemeko na hofu kuu. Msomaji wa Injili hana budi kutoishia katika lugha za ishara wanazotumia waandishi hawa bali kwenda mbele zaidi na kuona ni ujumbe gani walikuwa wanataka kuufikisha kwa msomaji.

Ni vema kwa leo tubaki kutafakari Injili ya mkesha huu kama ilivyoandikwa na Marko ili tuweze kuelewa hasa ishara alizozitumia na katekesi nyuma yake. Marko anatueleza kuwa wanawake walienda kaburini mapema asubuhi ile siku baada ya Sabato wakiwa na mafuta yale ili kuupaka mwili wake Yesu. Wanaenda na mafuta yale yenye harufu nzuri, ni nini maana yake? Tunabaki na maswali zaidi kuliko majibu maana wanawake hawa walijua kwa hakika kuwa tayari kaburi lilikuwa limefungwa na hawakuwa na uwezo wa kuliondoa lile jiwe, hivyo ya nini basi mafuta yale? Jiwe lile lilikuwa ni ishara wazi kuwa kifo kinatutenganisha kati ya ulimwengu wa walio hai na ule wa wafu. Kufikiri kuwa walikuwa na matumaini kuupatia tena uzima mwili wa Yesu kwa jinsi alivyoteswa na hata kuchomwa mkuki pale juu Msalabani ilikuwa si lengo na shabaha ya hawa wanawake. Kadiri ya Wainjili Mathayo na Yohane ilikuwa ni desturi kufika kaburini kwa siku tatu za mwanzo kwa kutembelea kaburi ili kujiridhisha kwamba ni kweli yule mtu amekufa kweli kweli. Ni mwendelezo pia wa maombolezo kama ilivyo katika baadhi ya desturi zetu za kiafrika, kufika kaburini na kulia au kuomboleza kwa siku 40 baada ya maziko.

Juu ya ufufuko ni wachache walikuwa wanaamini, ni Mafarisayo walioamini juu ya ufufuko na wengi walikuwa wanawacheka na kuwashangaa kwa kuamini katika ufufuko. Pia Yesu alizungumza mara kadhaa juu ya ufufuko wake na hakueleweka hata na Mitume wake. Hivyo hatuwezi kusema kwa hakika kuwa wanawake wale walifika kaburini wakitegemea ufufuko. Mwinjili anasisitiza kuwa ilikuwa alfajiri na giza bado. Alfajiri ni wakati ambapo siku mpya inaanza, hivyo giza linapungua kama sio kutoweka na matumaini mapya yanaanza. Ni mwanzo mpya, ni nuru inayochipuka na kuangaza uso wa nchi. Ni mwanzo wa matumaini mapya. Nani atatuondolea jiwe? Ni swali zuri kabisa la hawa wanawake wanaofika kaburini mapema asubuhi. Wanainua macho yao juu na kuona kuwa jiwe limeondolewa. Naomba tuzingatie kitendo cha wao KUINUA MACHO YAO JUU, ni katika kumtumainia Mungu pekee na si kwa nguvu za kibinadamu kuweza kushinda nguvu za umauti, na ndio wanaona jiwe limeondolewa. Mpaka muda ule walikuwa wakitazama chini kwa maana ya kutegemea mantiki na akili na nguvu za kibinadamu ambazo daima ni sawa na lile jiwe kubwa linalotenga ulimwengu wa wafu na ule wa walio hai.

Fumbo la kifo haliwezi kupata majawabu yake kwa kutegemea akili za kibinadamu au sayansi au teknolojia au utaalamu au ujuzi wa aina yeyote pasipo kumwangalia Mungu pekee aliye asili na hatima ya maisha ya mwanadamu. Wanaingia ndani ya kaburi na kumwona kijana ameketi. Kijana hapa ni lugha ya ishara kama tulivyotafari Dominika ile ya Matawi, yule kijana aliyekuwa anamfuata Yesu na kukimbia na kuacha shuka lake na kubaki uchi. Neno kijana kwa kigiriki ni νεανισκον (neaniskon); katika ulimwengu mpya hakuna tena kifo, hakuna uzee yote ni mapya, ni sawa na ujana unaodumu milele. “Waswahili wanasema eti uzee unaishia Chalinze”. Ni kama ambavyo kila mmoja wetu anatamani siku zake za ujana na ndivyo ilivyo maisha katika ulimwengu mpya. Maisha ya ufufuko ni ujana usio na mwisho maana hakuna muda tena. Hakuna jana wala kesho, yote ni sasa tu. Ni leo ya daima, ndio umilele! Kinyume chake wanawake wale wanaogopa. Neno la Kigiriki likimaanisha woga na hofu hii ni εκστασις (ecstasis), ni muunganiko wa maneno mawili yaani εκ na στασις. (ek na stasis).

Najaribu kuyaeleza kwa tafsiri yangu na si sisisi, yakimaanisha kutoka msimamo au mtuwamo. Ni hali ya kuachana na kusimama na kuanza maisha tena. Ni kuwa katika mwendo sasa. Ni baada ya ile Ijumaa Kuu ambapo kila kitu kilionekana kuwa kimesimama na sasa maisha yanaanza upya na kusonga mbele. Ni hali hii inawakuta sio kwa maana hasi bali chanya, uoga wao ni baada ya kuelewa ujumbe wa Pasaka. Kila mmoja wetu anayeelewa ujumbe wa Pasaka anakuwa katika hali hii ya ecstasis, ile furaha ya ndani na shauku ya kutaka kushirikisha wengine uliyoyaona na kuyashahudia. Ni hofu chanya, ni hofu ya furaha kwani wamepata kuelewa juu ya fumbo la ufufuko. Ufufuko unatutoa katika mkwamo au hali ile ya kukosa nguvu ya kusonga mbele na hivyo kutoka na kuanza maisha mapya! Ufufuko ni uumbaji mpya, ni mwanzo wa maisha mapya! Ndio ujumbe wa Pasaka, tunaalikwa nasi kama tumeelewa maana yake kuwa wenye furaha hata kati ya nyakati ngumu tusizozielewa sawa sawa. Na ndio wanawake wale wanaopokea utume wa kwenda kuwaalika mitume waende Galilaya. Yesu Kristo amefufuka, ni mzima, hayupo kaburini ambapo maisha yanasimama bali ni mzima na anatualika mimi na wewe kurudi Galilaya.

Pasaka ni wito na mwaliko wa uinjilishaji, ni mwaliko wa kila mmoja wetu kutokubaki katika hali ya awali bali kuachana nayo na hivyo kutoka na kupeleka Habari Njema ya Wokovu kwa wengine, kifo kimeshindwa kwa njia ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo! Kurudi tena katika safari yake nzima ya wokovu aliyoanza tangu kule Galilaya mpaka Yerusalemu. Ni kurudi katika Maandiko Matakatifu na kutafakari upya upendo wake wa Kimungu, ni kurudi katika Injili. Ni kutembea naye kuanzia Galilaya na kumsikiliza kwa makini Yesu anayeongea nasi katika nafasi mbali mbali. Ni mwaliko wa kuanza upya maisha yetu kwa kushika Neno lake analotuhubiria kila siku. Pasaka ni mwaliko wa maisha mapya, ni maisha bila hofu, ni maisha pamoja na mfufuka. Ni maisha ya mwanga na furaha pamoja na Yesu Kristo Mfufuka. Na ndio adhimisho la mkesha huu tumeanza na liturjia ya mwanga, Yesu Kristo mfufuka anaondoa giza la maisha ya dhambi kwa kutushirikisha masakramenti yake, neema zake za kimungu kwa wanakanisa, ni maisha ya kuongozwa na Neno la Mungu na ndio maana usiku huu tunaalikwa kusikiliza Neno la Mungu, mintarafu historia ya wokovu wetu.

Ni kubaki kijana kwa maana ni kushiriki maisha ya umilele, maisha ya Kimungu, maisha ya mwanga. Ni maisha mapya. Ni maisha ya utakatifu. Hatuna budi kumwomba Mungu neema na baraka zake ili Kristo afufuke nasi kwa maana ya kuanza maisha mapya ya furaha na urafiki na Mungu na mwanadamu. Tusali pia kwa ajili ya amani na umoja wa Taifa letu Tanzania, ili tudumu kuwa Taifa la mwanga wa matumaini; Taifa linalokuwa ni la watanzania wote na sio kikundi cha watu wachache wanaojimilikisha nchi kwa vigezo fulani fulani tu vya ujanja wa kisiasa. Tuwaombee viongozi wetu ili wawe na roho ya uongozi wa kweli wakijua nchi si mali yao bali wamewekwa madarakani na watanzania kwa kuchaguliwa na si kujiweka wenyewe hivyo hawana budi kuwaheshimu watanzania wote na kutenda kwa haki. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viwe kweli kwa ajili ya kuwalinda watanzania wote bila kujali itikadi zao na kamwe visitumike kwa masilahi ya wanasiasa wachache. Vyombo vyetu vya haki kama mahakama navyo visikubali kutumiwa kwa masilahi ya kisiasa ila vibaki kulinda haki na kweli ya watanzania wote bila ubaguzi wa aina yeyote.

Ni mwaliko wangu ili kama Taifa tuweze kubaki Taifa lenye haki kwa kila mmoja wetu. Hiyo iwe sala yetu kwa ajili ya ustawi wa Taifa zima maana hakuna amani kama hakuna haki. Pasaka iwe nafasi ya kutufanya tena kusafiri kwa pamoja bila kujali tofauti zetu za kisiasa na kiitikadi, sote tunawajibika kwani Mama yetu ni mmoja, yaani, Tanzania, tuunganike sote kwa ajili ya ustawi wa huyu mama yetu sote. Tuwaombee viongozi wetu ili wakubali kuongozwa na tunu msingi za Injili na sio akili zao tu, maana akili zetu za kibinadamu haziwezi kamwe kuondoa jiwe la upofu na matumaini ya kweli mpaka pale tutakapoinua macho yetu juu na kumtumaini Mungu kwa kila jambo. Amani ya Kristo mfufuka ilete amani, matumaini na furaha ya kweli kwa kila mmoja wetu! Amani na furaha ya Kristo Mfufuka ikawe juu ya kila mmoja wetu, kila familia, jumuiya, kigango, parokia na taifa letu na ulimwengu mzima! Pasaka njema kwa kila mmoja wetu. Kristo amefufuka kweli kweli Aleluiya Aleluiya!

02 April 2021, 16:32