Tafuta

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Tafakari ya Neno la Mungu: Ushuhuda wa imani kutoka katika Jumuiya ya kwanza ya Wakristo; Amani zawadi ya Kristo Mfufuka na Madonda Mtakatifu chemchemi ya huruma ya Mungu Jumapili ya Huruma ya Mungu: Tafakari ya Neno la Mungu: Ushuhuda wa imani kutoka katika Jumuiya ya kwanza ya Wakristo; Amani zawadi ya Kristo Mfufuka na Madonda Mtakatifu chemchemi ya huruma ya Mungu 

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Madonda Matakatifu ya Yesu!

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Jumuiya ya kwanza ya Wakristo walivyomshuhudia Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya maisha adili yaliyosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Pili ni zawadi ya amani kutoka kwa Kristo Mfufuka. Tatu ni Madonda Matakatifu ya Yesu, ufunuo wa chemchemi ya upendo, huruma, msamana na imani thabiti kutoka kwa waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika Kipindi hiki cha Pasaka ya Bwana, Mama Kanisa anaendelea kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ninapenda kuchukua fursa hii, kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika kipindi hiki cha Liturujia ya Neno la Mungu, leo ikiwa ni Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka inayojulikana kama “Domenica in albis”. Hii ni Jumapili ya Huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kinga na kimbilio la maskini na wadhambi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili waweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Huruma ya Mungu inazidi uelewa, maarifa na ufahamu wa akili ya binadamu.

Katika tafakari hii, ningependa kujielekeza zaidi katika maisha ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo waliomshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya maisha yao adili yaliyosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Pili ni zawadi ya amani kutoka kwa Kristo Mfufuka. Tatu ni Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, ufunuo wa chemchemi ya upendo, huruma, msamana na imani thabiti kutoka kwa waamini. Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 4:32-35) linaonesha jinsi Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walivyoshuhudia na kutangaza imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu uliofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo, kiasi kwamba, wote walikuwa na “moyo mmoja na roho moja”. Kila mtu akapata mahitaji yake msingi kutoka katika Jumuiya ya waamini. Hivi ndivyo udugu wa umoja, upendo na mshikamano ulivyotangazwa na kushuhudiwa na Wakristo wa Kanisa la mwanzo, kielelezo cha furaha ya Pasaka ya Bwana.

Imani kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, ni chimbuko la upendo kwa Mungu na jirani na ni sehemu ya utekelezaji wa Amri za Mungu. Hivi ndivyo anavyokazia Mtume Yohane katika Waraka wake wa kwanza kwa watu wote 5:1-6. Ujumbe huu ni sehemu ya katekesi kwa ajili ya wakatekumeni wanaoifia dhambi na kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu”. Mwinjili Yohane anasema, “siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi, akaja Yesu akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu”. Rej. Yon. 20:19-31. Amani ni zawadi ya kwanza ya Kristo Mfufuka kwa Mitume wake waliokuwa wamepepetwa “kama ngano”, wakajaribiwa kiasi cha kupondeka na kufa moyo kutokana na Kashfa ya Msalaba. Amani ya Kristo Mfufuka inaweza kudumu katika moyo wa mwanadamu, ikiwa kama, atashika Amri za Mungu na kuzimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Amani ya kweli ni kiungo na daraja linalowaunganisha waamini na Mwenyezi Mungu.

Ulimwengu mamboleo umesheheni hofu na wasi wasi ya vita, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; vita na mipasuko ya kijamii sanjari na athari za maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Changamoto kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya amani, ujumbe uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Kanisa linahamasishwa kuwa ni chombo cha Injili amani inayojikita katika ushuhuda wa mchakato wa uponyaji na upatanisho kati ya watu wa Mataifa na kazi ya uumbaji. Amani anasema, Mtakatifu Paulo VI ni jina jingine la maendeleo fungamani ya binadamu. Maandalizi ya Jumapili ya Huruma ya Mungu yalianza Ijumaa Kuu kwa Novena ya Huruma ya Mungu. Kristo Yesu ni yule yule, jana, leo na hata milele na kwamba, nyakati zote ni zake.  Ndiye yule aliyeteswa, akafa na sasa amefufuka kwa wafu. Katika mwili wake mtukufu anabeba Madonda Matakatifu, chemchemi ya: imani, huruma, mapendo na matumaini yanayoganga, kuponya na kutakasa madonda ya mwanadamu.

Huu ni muda wa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano unaokita mizizi yake katika matumaini, yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Kristo Yesu awe ni matumaini kwa maskini, watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni uso wa huruma ya Mungu, muhtasari wa imani ya Kanisa ambayo imefunuliwa naye kwa njia ya: mafundisho, matendo na nafsi yake. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Kusamehe makosa ni kielelezo dhahiri cha upendo wenye huruma. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa mwanadamu. Anajisikia kuwajibika, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuwaona watoto wake wakiwa wamesheheni furaha na amani tele.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ibada ya Upatanisho ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia huruma, upendo na amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, waamini wanakirimiwa tena maisha mapya baada ya kuanguka dhambini na kupoteza ile neema ya utakaso waliyopokea wakati walipokuwa wanapokea Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya upatanisho, Kanisa linazidi kukua na kupanuka, kwa kumfuasa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu asiyekuwa na mawaa. Huu ni mwaliko wa kujitakasa kwa kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu kuzungumza kutoka katika undani wa maisha ya watu, ili kweli wakleri waendelee kuwa ni vyombo vya huruma na upatanisho kati ya Mungu na watu wake. Mtakatifu Toma, Mtume kwa kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, akatubu, akaongoka na kuwa Shuhuda wa Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Fumbo la Huruma ya Mungu limekaziwa sana na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Francisko akaliwekea mikakati ya kichungaji, kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji!

Kila mwamini anaweza kukutana na Kristo Yesu Mfufuka kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Unaweza kukutana na Yesu katika historia ya maisha yako ya kila siku. Kashfa ya imani ya Mtakatifu Toma imekuwa ni kielelezo cha ufunuo wa imani, upendo, huruma na uaminifu wa Mungu.

Liturujia Huruma ya Mungu
09 April 2021, 15:35