Tafuta

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: Ujumbe wa Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2021: Nguvu na Ujasiri wa kupambana na changamoto mamboleo! Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: Ujumbe wa Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2021: Nguvu na Ujasiri wa kupambana na changamoto mamboleo! 

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Ujumbe wa Pasaka 2021: Ujasiri

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika ujumbe wake kwa Pasaka ya Mwaka 2021 linasema kwamba, Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu linaadhimishwa wakati ambapo ulimwengu bado umegubikwa na maambukizi makubwa ya janga la UVIKO-19. Watu, familia na mataifa mengi yanakabiliwa na hali ngumu sana katika kipindi cha miaka miwili sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo ambayo jamii ya kwanza ya Wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi wa Mapokeo; wakaithibitisha kwa njia ya Maandiko Matakatifu kutoka Agano Jipya. Wakristo wa kwanza wakaihubiri imani hii kama sehemu muhimu ya Fumbo la Pasaka sanjari na Fumbo la Msalaba. Kristo amefufuka kutoka wafu. Kwa kifo chake ameshinda mauti, wafu amewapa uzima. Rej. KKK. 638. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika ujumbe wake kwa Pasaka ya Mwaka 2021 linasema kwamba, Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu linaadhimishwa wakati ambapo ulimwengu bado umegubikwa na maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Watu, familia na mataifa mengi yanakabiliwa na hali ngumu sana katika kipindi cha miaka miwili sasa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linakiri kwamba, watu wengi wana hofu juu ya hatima ya maisha yao kwa siku za usoni. Watu wengi wanaendelea kufungiwa majumbani kama sehemu ya kudhibiti maambukizi mapya ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna wagonjwa ambao wamepondeka moyo na kukata tamaa ya maisha. Kuna familia hata katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka, wanaomboleza vifo vya ndugu zao waliofariki dunia kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 au kutokana na sababu nyingine, lakini kuna majonzi kwenye familia. Gonjwa hili hatari limepelekea hata maadhimisho ya Juma kuu na hatimaye, Sherehe ya Pasaka kuadhimishwa katika hali ya kimya kikuu pasi na shamrashamra zilizozoeleka katika kipindi hiki. Waamini wengi wameadhimisha Mafumbo ya Wokovu kwa njia ya luninga na mitandao ya kijamii na kukutana na Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao! Licha ya yote haya yanayoendelea kutokea sehemu mbalimbali za dunia, lakini ujumbe wa Pasaka unabaki ukiwa umesimama imara bila ya kutikisika! Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Rej. Ebr. 13:8.

Fumbo la Pasaka linawakumbusha na kuwatia shime waamini kwamba, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu Mfufuka anaendelea kuwapenda waja wake na kutegemeza ulimwengu wote, ili kushinda kifo kwa njia ya Injili ya uhai; kuondoa hofu kwa kuwa na matumaini. Kaburi ni wazi, Kristo Yesu amefufuka kweli kweli, Aleluiya! Huu ni ujumbe ambao katika historia ya maisha ya mwanadamu, umekuwa ni chachu ya ujasiri, nguvu na hamasa ya kukabiliana na Fumbo la kifo, dhuluma na nyanyaso, ili hatimaye, kumkomboa mwanadamu kutoka katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, hofu na mashaka. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC linapenda kuwahakikishia Wakristo na watu wote wa Mungu kwamba, liko pamoja nao kwa sala na sadaka zake hasa katika kipindi hiki cha mapambano mazito dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Waamini waendelee kuimarisha imani na matumaini yao kwa Kristo Mfufuka na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anayewajalia ushindi katika mapambano yao! Ujumbe wa Pasaka kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni umetiwa mkwaju na Mheshimiwa Profesa Dr. Loan Sauca, Katibu mtendaji, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC.

Baraza la Makanisa WCC

 

03 April 2021, 17:53