Tafuta

2020.05.01 sherehe za mashahidi wa Uganda 2020.05.01 sherehe za mashahidi wa Uganda  

Askofu Mkuu Lwanga wa Kampala alifariki dunia Jumamosi Kuu

Askofu Mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo Kuu Katoliki Kampala aliyekuwa na umri wa miaka 68 alifariki dunia.Ijumaa Kuu aliudhuria Njia ya Msalaba ya kiekumene katika Kanisa Kuu la Kianglikani.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Baraza la maaskofu wa Uganda wamesikitishwa na kifo cha ghafla cha aliye kuwa mmoja wa Baraza la Maaskofu aliyekutwa amekufa chumbani mwake asubuhi ya Jumamosi Kuu Takatifu, tarehe 3 Aprili 2021, Askofu Mkuu Cyprian Kizito Lwanga aliyekuwa na umri wa miaka 68. Askofu Mkuu alikuwa ameudhuria hata Njia ya Msalaba ya Kiekumene, jioni Ijumaa Kuu Takatifu tarehe 2 Aprili 2021. Kwa maana hiyo mnamo tarehe 3 Aprili 2021 Baraza la Maaskofu kwa njia ya msemaji wake alisema kwamba “mmoja wa washiriki wa Baraza ametoa pole kwa Wakleri, watawa na waamini wa Jimbo kuu la Kampala, na Kanisa Katoliki nchini Uganda. Askofu Mkuu Kizito Lwanga alikuwa ameshiriki Ijumaa kuu katika Njia ya Msalaba ya kila mwaka ya Kanisa la Namirembe, Kanisa kuu la Kinglikani la Kampala.

 “Yesu alikufa kwa ajili yako, alikufa kwa ajili yangu, alikufa kwa ajili ya wanadamu wote. Ninatawakia ufanisi mzuri wa Njia ya Msalaba”, Askofu Mkuu Lwanga alisema mwanzoni mwa Njia ya Msalaba tarehe 2 Aprili. Askofu Mkuu Stephen Kaziimba wa kianglikani wa Uganda, alitoa maoni kwamba “jana tu, tulitembea Njia ya Msalaba pamoja, na ni mshtuko kwetu sote. Sauti yake ya wazi ya Injili ya kutetea maskini na wanyanyaswaji, kujitolea kwake kwa umoja wa Kikristo, na haki kwa wote tutamkosa sana.”

Marehemu Askofu Mkuu Lwanga alizaliwa mnamo 1953, na aliwekwa wakfu kuwa kikuhani wa Jimbo kuu la Kampala mnamo 1978. Aliteuliwa kuwa Askofu wa Kasana-Luweero mnamo 1996, wakati Jimbo lilipoinuliwa kuwa Jimbo kuu la Kampala, yeye aliwekwa wakfu kuwa askofu mnamo tarehe 1 Machi 1997. Na mnamo 2006 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Kampala.

Katika sherehe za kuadhimisha Siku ya Wafia dini nchini Uganda mwezi Juni mwaka jana, askofu mkuu marehemu aliwataka watu wa Mungu wawe chini ya uangalizi wake wa kichungaji kufuata mfano wa mashahidi wa Uganda kwa nia ya kuimarisha imani yao ndani ya familia zao katikati ya janga la virusi vya corona. “Ni wakati wetu kuimarisha Kanisa la nyumbani kwa kufuata mfano wa mashahidi wa Kanisa la kwanza na kwa kufanya hivyo, kuwa imara katika imani, Askofu Mkuu Lwanga alisema hayo mnamo tarehe 3 Juni 2020, katika sikukuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake mashahidi.

Askofu Mkuu Lwanga aliendelea kuhamasisha wanafamilia kumiliki na kusoma Biblia kila siku, akisema, “Kwa bahati nzuri, kwetu sisi Wakatoliki, kila siku ya mwaka kuna masomo ambayo tunaalikwa kutafakari. Na masomo hayo yote yanatualika kujipyaisha.  Basi tujitahidi kuyasoma na kuzitafakari kama familia." Kabla ya ugonjwa huo kuenea nchini Uganda, alikuwa amekazia kupokea Komunyo Takatifu mkononi, na akasisitiza tena kwamba wale “wanaoishi katika  ndoa ambazo hazihjabarikiwa hawawezi kupokea Komunyo Takatifu.

06 April 2021, 16:17