Tafuta

Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe amefariki dunia tarehe 6 Aprili 2021 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam. Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe amefariki dunia tarehe 6 Aprili 2021 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam. 

Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe Amefariki Dunia!

Hayati Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe alizaliwa tarehe 12 Desemba 1955 huko Lukani. Tarehe 17 Novemba 1985 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kunako tarehe 8 Juni 2002, akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe na kuwekwa wakfu tarehe 1 Septemba 2002. Na tarehe 6 Aprili 2021, Oktava ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, akafariki dunia! Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linasikitika kutangaza kifo cha Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe, Tanzania kilichotokea saa 6:40 usiku wa tarehe 6 Aprili 2021 katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu zaidi. Mipango ya mazishi inaendelea kufanyika, ikikamilika, familia ya Mungu nchini Tanzania itapewa taarifa rasmi. Haya yamethitishwa na Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita, ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Hayati Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe alizaliwa tarehe 12 Desemba 1955 huko Lukani. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Novemba 1985 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Njombe. Kunako tarehe 8 Juni 2002 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 1 Septemba 2002 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Na tarehe 6 Aprili 2021 katika maadhimisho ya Oktava ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, akafariki dunia, ili kwenda kupumzika katika usingizi wa amani, huku akiwa na tumaini la Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele.

Hayati Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe amefariki dunia, akiwa amewahudumia watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Njombe kama Padre kwa muda wa miaka 35. Kama Askofu mahalia, amewafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 18, sasa astahilishwe na Hakimu mwenye haki, kuyaona katika ukamilifu wake, Mafumbo ya Kanisa aliyokuwa anayaadhimisha katika maisha yake, Apumzike Kwa Amani. Amina!

Tanzia: Askofu Maluma

 

06 April 2021, 13:34