Tafuta

Vatican News
Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe aliyefariki dunia tarehe 6 Aprili 2021 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam atazikwa tarehe 13 Aprili 2021 Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe aliyefariki dunia tarehe 6 Aprili 2021 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam atazikwa tarehe 13 Aprili 2021 

Hayati Askofu Alfred Maluma: 12 Desemba 1955 - 6 Aprili 2021

Kanisa Katoliki Tanzania, Jumatatu tarehe 12 Aprili 2021 saa 1:00 asubuhi litaanza safari ya kumsindikiza Hayati Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki la Njombe kwenye safari yake ya mwisho hapa duniani, ili kumweka mikononi mwa Kristo Yesu kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa la Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Kurasini, DSM.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanafundisha kwamba, Sakramenti zote, na hasa zile za kuingizwa katika Ukristo, zina kama lengo, Pasaka ya mwisho ya mtoto wa Mungu, ile ambayo kwa kifo inamwingiza katika uzima wa Ufalme wa Mungu. Sasa kinatimilizika kile alichokisadiki katika imani na katika matumaini: “Nangojea ufufuko wa wafu na uzima wa ulimwengu ujao.” Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka la Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani yake mna tumaini moja la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo “huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Bwana. Kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo. Yaani: “kufanana” kamili na “sura ya Mwana” kulikotolewa kwa mpango wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa Mungu, uliotangulizwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu hata kama ana lazima bado ya kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi. Rej. KKK 1681-1683.

Kanisa Katoliki nchini Tanzania, Jumatatu tarehe 12 Aprili 2021 saa 1:00 asubuhi litaanza safari ya kumsindikiza Hayati Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki la Njombe kwenye safari yake ya mwisho hapa duniani. Lengo ni kumweka mikononi mwa Kristo Yesu kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa la Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Kurasini, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Baada ya Ibada ya Misa Takatifu mwili wa Hayati Askofu Alfred Leonhard Maluma utasafirishwa kwa ndege hadi Njombe. Kutakuwa na mkesha wa Ibada na Sala kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Askofu Maluma. Jumanne tarehe 13 Aprili 2021, Kanisa litamtolea Mwenyezi Mungu Ibada ya Misa Takatifu katika Kristo Yesu, Askofu Maluma, mtoto wa neema yake, na katika imani, litaikabidhi ardhi mbegu ya mwili utakaofufuliwa katika utukufu. Hiki ni kipindi kigumu cha maombolezo, yanayopaswa kufanyika kwa imani na matumaini juu ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele!

Itakumbukwa kwamba, Hayati Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe alizaliwa tarehe 12 Desemba 1955 huko Lukani. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Novemba 1985 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Njombe. Kunako tarehe 8 Juni 2002 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 1 Septemba 2002 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Na tarehe 6 Aprili 2021 katika maadhimisho ya Oktava ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, akafariki dunia kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) tayari kwenda kupumzika katika usingizi wa amani, huku akiwa na tumaini la Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Hayati Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe amefariki dunia, akiwa amewahudumia watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Njombe kama Padre kwa muda wa miaka 35. Kama Askofu mahalia, amewafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 18, sasa astahilishwe na Hakimu mwenye haki, kuyaona katika ukamilifu wake, Mafumbo ya Kanisa aliyokuwa anayaadhimisha katika maisha yake, Apumzike Kwa Amani. Amina!

Hayati Askofu Maluma

 

09 April 2021, 15:15