Tafuta

2021.03.11 Mwaka maalumu wa 'Amoris laetitia' 2021-2022 2021.03.11 Mwaka maalumu wa 'Amoris laetitia' 2021-2022 

Ufilipino:mwaka wa Amoris Laetitia:Familia ni shule ya kwanza ya uinjilishaji

“Familia kwa utashi wa Mungu ni ya kwanza kuwa shule ya mafunzo,mahali ambamo wazazi ndiyo makatekesta wa kwanza wa watoto wao na shule ya kwanza ya uinjilishaji,mahali ambamo wajumbe wote wanajifunza kushirikishana na wengine neema na mwanga wa Kristo”.Ni kutoka katika barua ya kichungaji ya Baraza la Maaskofu wa Ufilipino katika fursa ya kuanza rasmi mwaka wa 'Familia Amoris Laetitia'.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Baraza la Maaskofu nchini Ufilipino (Cbcp) wameandika barua yao ya Kichungaji iliyotiwa sahini na Rais wa Baraza hilo, Askofu Mkuu Romulo Valles wa Davao, iliyochapishwa tarehe 19 Machi  katika fursa ya ufunguzi rasmi wa mwaka Maalum wa “Famiglia Amoris Laetitia”. Hii ni kutokana na matashi  ya Papa Francisko aliyotoa mwishoni mwa mwaka 2020, ikiwa ni katika fursa ya kuwakilisha maadhimisho ya miaka 5 tangu kutangazwa kwa Wosia wake wa Kitume baada ya Sinodi kuhusu “Upendo ndani ya Familia” ambalo ni tunda la Sinodi mbili,  ya kwanza  maalum mnamo 2014 na Sinodi ya 2015 iliyojikita katika mada hiyo hiyo.  Katika barua yao ya kichungaji, Maaskofu wa Ufilipino wanaandika kuwa “Familia ni kwa utashi wa Mungu na kuwa shule ya kwanza ya mafunzo, mahali ambamo wazazi wanakuwa makatekesta wa kwanza wa watoto wao na shule ya kwanza ya uinjilishaji, mahali ambamo wajumbe wote wanajifunza kushirikishana na wengine neema na mwanga wa Kristo”. Katika mantiki ya janga la Covid-19 ambayo inaendelea kuvuruga maisha yetu, ni matarajio ya maaskofu wa Ufilipino na kwamba familia ambayo shukrani kwa neema ya imani ya kikristo, wanaweza kuishi na kufurahia taifa huru, ambalo linalisha uzalendo wa maisha na katika upendo.

Maaskofu hata hivyo, wanazingatia muktadha wa mwaka wa Familia Amoris Laetitia ambao unakwenda sambamba na maadhimisho yao ya miaka 500 tangu kufika ukristo katika taifa hilo.  Ni tukio ambao linaweka mwanga umuhimu kwa walei katika unjilishaji. Katika waraka huo Baraza la Maaskofu Ufilipino, wanakumbuhsa kwamba katika Nchi,  Kerygma yaani Tangazo  lilipokelewa kwa mara ya kwanza kutoka kwa mlei mmoja aliyekuwa baharia Ferdinando Magellano ambaye, mnamo 1521, aliinjilisha watu wa asili ya nchi hiyo, akiwafundisha kuwa Mungu aliumba mbingu na dunia na akwapatia amri ya kuwaheshimu baba na mama. Viongozi  hao wamekumbuka pia shughuli nyingi zilizofanywa na Kanisa la Ufilipino mnamo 2016 hadi leo hii kusaidia na kuhimiza kazi ya walei na familia: kwa mfano, kujenga mitandao ya kichungaji ili kuleta Injili katika ngazi zote za jamii na Kanisa, hasa katika maeneo ye pembezoni mwa maisha; kuanzisha tena kozi za maandalizi ya ndoa za Kikristo kwa mtazamo wa upendo wenye matunda na hali ya kiroho ya muungano; kufungamanisha zaidi na kuunganisha mashirika ya kifamilia ndani ya miundo ya jimbo ili parokia ziweze kuwa familia ya kifamilia; Na tena, Maaskofu wa Ufilipino wamejikita katika utunzaji wao wa kichungaji kwa kuwasindikiza wahanga wa unyanyasaji wa nyumbani na unyanyasaji mwingine, walevi wa dawa za kulevya, wahamiaji na familia zao.

Kiini  cha shughuli za viongozi hao  ni  katika uwanja wa utume wa vijana ambapo wanasema pia ni muhimu, kuwasaidia ili kugundua hadhi na uzuri wa ndoa. Kanisa la Manila, wanasisitiza katika Barua ya Kichungaji kuwa  halikusimama hata wakati wa janga la Covid-19 na limeendelea kutembea, kusaidia na kusindikiza maisha ya familia kupitia njia mpya za ubunifu, kama vile kozi za mtandaoni na ushauri. Kwa namna ya pekee maaskofu wamethamini wakati huo huo ushiriki hai wa walei ambao wametetea familia katika mashtaka mbele ya serikali. Katika suala hilo, wanakumbusha kwamba Baraza la Maaskofu (CBCP) limempatia  heshima wakili Bi Maria Concepcion S. Noche kwa kufanikiwa kusaidia kuondolewa kwa vifungu visivyo vya katiba vya sheria ya afya ya uzazi. Lakini kwa malengo haya yote yaliyofanikiwa, sasa mengine yameongezwa, wanabainisha ili kuweza kutimizwa katika kipindi cha Mwaka huu maalum wa Familia ya Amoris Laetitia. Kwa mujibu wa Maaskofu wanaonesha matano: kushirikisha kwa upana zaidi yaliyomo kwenye Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, (Amoris laetitia) kwa sababu familia inayogundua na kupata furaha ya kuwa na zawadi, na ya kuwa zawadi kwa Kanisa na jamii, inaweza kuwa nuru katika giza la ulimwengu. Na ulimwengu leo hakika unahitaji nuru hii!”.

Pili, ni  kutangaza kwamba sakramenti ya ndoa ni zawadi na ndani yake ina nguvu ya kubadilisha katika upendo wa mwanadamu. Na tena: ”kuruhusu familia kuwa mawakala hai wa familia ya kitume”; “kuhamasisha na kukuza ufahamu kwa  vijana juu ya umuhimu wa malezi katika ukweli wa mapenzi na katika zawadi ya  nafsi zao  na hatimaye, “kupanua utume wa familia shukrani kwa njia pana inayojumuisha wenzi wa ndoa, watoto, vijana, wazee na hali ya udhaifu wa familia”. Baraza la Maaskofu wa Ufilipino (CBCP) aidha wamekumbusha katika barua yao ya kichungaji njia kumi na mbili ambazo  Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linapendekeza kusindikiza familia ambazo ni: kuimarisha mipango ya kichungaji ya matayarisho ya ndoa na ratiba mpya za katekisimu pia zilizokabidhiwa kwa wenzi wa ndoa ambao, pamoja na wachungaji, wanakuwa marafiki wa kusafiri kwa wenzi wa ndoa na wenzi wapya; kukuza huduma ya kichungaji ya kuwasindikiza wenzi, kupitia mikutano ya mafunzo na nyakati zilizowekwa kwa ajili ya sala,  maombi na  maendeleo ya kiroho; kuandaa mikutano ya wazazi juu ya elimu ya watoto na changamoto za sasa; kuhamasisha mikutano ya tafakari juu ya uzuri na changamoto za maisha ya familia, pia kuunda mitandao ya pamoja ya kichungaji na familia ambayo inaweza kusindikiza wale walio na shida.

Baraza la kipapa la Walei, Familia na Maisha pia linashauri kuboresha usindikizwaji  wa wanandoa walio katika shida ili kuwafundisha katika mtazamo wa uthabiti ambao unawasaidia kukua katika upendo; kufikiria kwa upya malezi ya wahudumu wa kichungaji, seminarini na makuhani, ili waweze kushirikiana kwa tija na familia; kuanzisha tena wito wa kimisionari katika familia;  kukuza na kuandaa mipango ya utunzaji wa kichungaji kwa wazee, ili kushinda utamaduni wa kutumia na kutupa; kuamsha shauku ya vijana na kuongeza uwezo wao wa kujitoa kikamilifu kwa ajili ya maadili mazuri. Hatimaye wanatoa maelekezo matatuo ya tatu za mwisho yanayohusu maandalizi ya Mkutano wa 10 wa Familia Ulimwenguni utakaofanyika mnamo  Juni 2022 jijini Roma; kusindikiza  na kufanya mang’amuzi ya  familia zilizojeruhiwa na kujikita kwa kina  katika parokia na katika jumuiya, kuhusu Waraka wa Amoris Laetitia wenyewe. Barua ya kichungaji ya Baraza la Maaskofu  CBCP inahitimisha, kwa maana hiyo na maombi kwa Familia Takatifu ya Nazareti.

21 March 2021, 16:54