Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Kuinuliwa kwa Kristo Yesu juu ya Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Kuinuliwa kwa Kristo Yesu juu ya Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake. 

Tafakari Jumapili IV Kwaresima: Yesu Kristo Juu ya Msalaba!

Ni Yesu mwenyewe atainuliwa pale juu Msalabani na kila amwaminiye basi atapata maisha ya uzima wa milele. Na ndio mwaliko wa Kipindi cha Kwaresima, kubaki chini ya Msalaba wake Yesu Kristo kwa kutafakari kwa imani, upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu wadhambi. Dhambi ni ishara ya sumu kali inayotuondolea maisha ya umilele, maisha ya urafiki na Mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Ni mwinjili Yohane pekee kati ya Wainjili wote wanne, anayemzungumzia Nikodemo. Ni mtu wa makamo na  aliyeheshimika kati ya mafarisayo na yawezekana alikuwa mmoja kati ya wakuu wa “Sinedrio” yaani baraza la wazee, leo akitumia fursa ya wakati wa giza na ukimya wa usiku kwenda kwa Yesu Kristo kwa mazungumzo. Ikumbukwe kuwa marabi au walimu wa dini ya kiyahudi walitumia sana nyakati za usiku kwa sala na hata kwa kufanya katekesi kwa wanafunzi wao kwa maswala mazito na magumu yaliyoshindikana kueleweka nyakati za mchana. Ni wakati wa usiku pia marabi walijifunza zaidi Maandiko Matakatifu. Ni wazi kama sababu ya pili, Nikodemo alijiiba saa na mida hiyo ili asiweze kuonekana na Mafarisayo wenzake kuwa naye anamwamini Yesu wa Nazareti kuwa Rabi na Nabii. Nikodemo anatafuta mwanga na ukweli kutoka kwa Rabi huyu kijana kutoka Nazareti. Mwinjili Yohane pamoja na kutuonesha akiwa katika mjadala na Yesu wa Nazareti ila hatuelezi zaidi juu ya nini hatima ya Nikodemo baada ya kupokea katekesi hii muhimu juu ya kuzaliwa katika roho au ubatizo na imani kwa Yesu Kristo aliye mkombozi wa ulimwengu kwa kuinuliwa pale juu Msalabani.

Je, Mzee Nikodemo aliondoka akiamini au alibaki na kutoamini katika Yesu Kristo? Ni swali tafakarishi katika Dominika ya leo. Nikodemo anatajwa tena katika Maandiko Matakatifu wakati wa mjadala mzito wa kutaka kumuua Yesu uliofanyika na wakuu wa makuhani.  Ni Nikodemo anayewakumbusha wakuu wa makuhani haki ya msingi ya kumhoji Yesu Kristo kabla ya kumhukumu kifo. Na ndipo mmoja wa makuhani anajibu kuwa katika Maandiko hakuna Nabii anayetoka Galilaya. Rejea Yohane 7:51-52. Nikodemo akiwa katika Baraza la wazee na wakuu wa makuhani anajaribu kutetea haki ya kusikilizwa na hata ya kuokoa maisha ya Yesu wa Nazareti. Nitatumia kila mara Jina la Yesu wa Nazareti kila mara ninaporejea mzee Nikodemo kwa makusudi mazima ya kuonesha kwake Yesu ni Rabi kijana kutoka Galilaya ya Nazareti maana hilo halikuwa na mashaka kwake na wakuu wengine wa Kiyahudi, ila kuwa ni Kristo hapo tunabaki na swali la kutafakari.

Nikodemo ataonekana tena wakati wa maziko ya Yesu Kristo, pale Kalvario pamoja na Yusufu wa Arimateya wakimvika sanda Yesu na kumzika kaburini. Rejea Yohane 19:39-40 Hivyo ni kwa ufupi tu tunaweza kupata picha pamoja hatuelezwi wazi wazi na Mwinjili juu ya hatima ya mazungumzo yake na Yesu Kristo, yafaa kuona mtazamo na mwelekeo wake kwa Mwalimu na Nabii kutoka Galilaya ya Nazareti. Nazareti ni kijiji katika mkoa wa Galilaya, ulioko Kaskazini mwa Nchi ile ya Palestina/Israeli. Sehemu ya kwanza ya Injili ya leo, Yesu Kristo anajaribu kunukuu picha ya tukio lililotokea wakati Wanawaisraeli walipokuwa jangwani kuelekea nchi ya ahadi.  Wakiwa jangwani wengi wa Wanawaisraeili waliumwa na nyoka wenye sumu kali, hivyo Musa alimlilia Mungu na ndipo alipopokea maagizo ya kutengeneza nyoka wa shaba ili kila anayeumwa na nyoka amwangalie yule nyoka wa shaba naye atapona. Rejea Hesabu 21:4-9 Hata katika hekalu la Yerusalemu kuliwekwa pia huyu Nyoka wa shaba aliyesadikiwa kuwa ndiye aliyefanywa na Musa kuwanusuru walioumwa na nyoka wakiwa jangwani.

Labda ni ngumu kusema kwa hakika kile kilichojiri wakati wa tukio hili la nyoka wa sumu kali katika Kitabu cha Kutoka, ila yatosha kuelewa kuwa Wanawaisraeli waliponywa siyo kwa kumwangalia nyoka wa shaba bali kwa kunyanyua mioyo yao na kumwangalia Mungu mwenye huruma, ni Mwenyezi Mungu aliyewaalika kumgeukia na kumkimbilia katika nyakati za shida na taabu. Ni Mungu mwenyewe anayewaponya na sumu kali ya nyoka wale wa jangwani. Rejea Hekima 16:7. Ni katika muktadha wa leo ambapo dunia nzima tunalazimika kupiga magoti na kumlilia Mwenyezi Mungu ili atulinde na kutukinga dhidi ya janga la UVIKO19, ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha Korona. Ni katika mahangaiko na taabu, kila mmoja wetu anaalikwa kuunyanyua moyo wake kwa Mungu aliye Baba na Muumba wetu. Ni katika mazingira haya basi, na Yesu Kristo anatumia mfano huo wa picha kueleza kile kitakachotokea na kujiri kwake mwenyewe. Ni Yesu mwenyewe atainuliwa pale juu Msalabani na kila amwaminiye basi atapata maisha ya uzima wa milele.

Na ndio mwaliko wa Kipindi cha Kwaresima, kubaki chini ya Msalaba wake Yesu Kristo kwa kutafakari kwa imani, upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu wadhambi. Dhambi ni ishara ya sumu kali inayotuondolea maisha ya umilele, maisha ya urafiki na Mungu. Dawa ya kweli ni msalaba wake Kristo, ni hapo juu msalabani tunapatanishwa na Mungu, tunapewa tena hadhi ile ya kuwa wana wa Mungu ambayo tunaipoteza kila mara tunapoishi mbali na Mungu. Kuwa mbali na Mungu ni kukosa uzima na uhai ndani mwetu. Mzee Nikodemo si tu alipata ugumu kuelewa juu ya kuzaliwa kutoka juu mara ya pili ila pia hata fundisho hili la kuinuliwa juu Mwana wa mtu. Mzee Nikodemo alibaki na mshangao mkubwa juu ya mafundisho yake Nabii kijana Yesu wa Nazareti. Labda kwetu leo ni baada ya tukio la kifo na ufufuko wake ndio tunaamini juu ya mafundisho yake Yesu wa Nazareti, na bado wapo wengi hata katika nyakati zetu si tu wanakosa kuamini ila wanaona inakwenda kinyume na sheria asilia za kimaumbile!

Msalaba kwetu tuaminio katika mateso, kifo na ufufuko wake Yesu Kristo ni ishara ya upendo wa Mungu kwetu, ni ishara ya ushindi dhidi ya sumu kali inayotuondolea urafiki na Muumba wetu, ni ishara ya imani yetu juu ya maisha mapya katika Yesu Kristo. Ni pale juu Msalabani, utumwa wetu ulimalizika. Ni pale juu Msalabani Yesu Kristo anatutangazia kuwa mtu mpya ni yule anayetoa maisha yake kwa upendo na hiari yake kwa ajili ya rafiki zake, mtumwa kwa upendo wa ndugu zake, mtumwa wa upendo! Leo hii sumu kali ndio matendo yale kinyume na upendo ule kwa Mungu na kwa jirani: ni ubinafsi, chuki, majivuno, kiburi, wivu, dharau, masengenyo, tamaa mbaya, uchu wa mali, madaraka na kutaka hata kwa nguvu kutawala wengine na mengine mengi tunayoweza kuyaorodhesha, ila yote haya yanaponywa kwa kunyanyua mioyo yetu na kumwangalia Yesu Kristo pale juu msalabani. Mwinjili Yohana anatabiri juu ya ile siku ambapo watu wote watamwinulia macho na kumtazama nao wataokolewa. Rejea Yohane 19:37. Ni hapo juu Msalabani tunauona na kuuonja upendo na huruma ya Mungu kwetu wanadamu.

Sehemu ya pili ya Injili ya Dominika ya leo, ni ujumbe wa kitaalimungu juu ya utume wa Yesu Kristo. Yohane 3: 16-21.  Ni katika sehemu hii ya Injili kwa mara ya kwanza linatumika neno la Kigiriki αγαπειν (agapein yaani kupenda), wengi tumezoa neno Agape, likimaanisha upendo usio na masharti, ni upendo usiojitafuta wala kujibakisha. Ni neno linalotumika katika Kigiriki cha Agano Jipya na hivyo halipo katika Kigiriki cha kale au Classical Greek. Hivyo ni kwa ujio wake Yesu Kristo anatufunulia upendo kamili usio na mawaa wala kujitafuta. This is simply pure and unconditional love! Kwa jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, ni jinsi ya kujitoa sadaka pale msalabani ili kila amwaminie apate uzima wa milele. Yesu Kristo, pia anajitanabaisha kuwa ametumwa na Baba yake sio kuhukumu ulimwengu bali ulimwengu upate kuokolewa kwa njia yake. Yesu Kristo amekuja kutupatanisha na Mungu Baba, kuturejeshea tena urafiki ule na Muumba wetu kabla ya dhambi kuingia ulimwenguni. Ujio wake ulimwenguni kama walivyopenda kusema mababa wa Kanisa, ni ili mwanadamu apate kufanana na Mungu, ni Mungu anayejimwilisha anakubali kufanyika mwanadamu ili mwanadamu apate kufanyika pia mwana wa Mungu. Hivyo ujio wake ni Habari Njema kwa kila mmoja wetu.

Mwinjili Yohane anazungumzia juu ya hukumu ya sasa tofauti na Mwinjili Matayo katika sura ile ya 25 inayozungumzia juu ya hukumu siku ya mwisho. Kwa kweli wainjili hawa wawili wanatumia picha tofauti ila hawapingani kimantiki wala kiujumbe, kwani ni mwanadamu anafanya maamuzi yake akiwa huru kuchagua nuru au kuchagua giza. Maamuzi na uchaguzi huo ndio tuufanyao kila dakika na sekunde ya maisha yetu. Ni sisi wenyewe tunajihukumu na kuharibu maisha yetu kwa kufanya maamuzi mabaya sasa, ni mwaliko wa kuacha njia zetu mbaya na kumrudia Mwenyezi Mungu. Hukumu yetu tunaifanya sisi wenyewe katika maisha yetu ya sasa. Tuchague nuru na tuachane na matendo ya giza. Hukumu ile ya siku ya mwisho ni matokeo ya maisha yangu na yako kwa sasa. Ni leo inaamua juu ya kesho yetu, hukumu yetu ni jinsi tunavyoishi maisha yetu leo. Ni pale juu msalabani kwenye kiti cha hukumu ya Mungu, ni kwa kifo chake sisi unaokolewa, ni mwaliko wa kuitikia upendo wa Mungu kwetu kwa kubadili maisha yetu na kuanza maisha mapya katika Kristo Yesu.

Ni mwaliko leo tuchague nuru na kutembea na nuru hiyo, ni kumchagua Yesu Kristo katika maisha yetu ili tupate uzima wa milele. Hakika sio Mwenyezi Mungu anayeangamiza maisha yetu milele yote bali ni mimi na wewe tunayaangamiza maisha yetu kwa kufanya maamuzi mabaya. Kwaresma ni kipindi cha neema kwani kinatualika kufanya toba na kubadili njia zetu nasi tupate uzima wa milele. Hatuna budi kukumbuka na kuimba pamoja na Mzaburi sura ile ya 136 ya kuwa huruma yake ni ya milele! Ni upendo wake wa milele kwa ulimwengu na kutokana na upendo na huruma hiyo ameuumba ulimwengu. Ni mwaliko wa kuitikia upendo wa Mungu kwani tukimpenda Mungu kweli hakika tutaishi. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.

10 March 2021, 14:05