Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. 

Tafakari Jumapili IV Kwaresima: Msalaba: Huruma na Upendo

Kifo cha Kristo Msalabani kimefungua njia ya wokovu kwa ulimwengu mzima. Wokovu huu ni nuru iliyokuja kumwangazia mwanadamu aishiye katika giza. Ni mwanadamu huyu anayealikwa kwa njia ya imani aipokee nuru na kuanza maisha ya matendo mema. Imani ni mwanga unaomsaidia mtu kupiga hatua kumwendea Kristo ili kuanza naye njia mpya ya maisha, njia ya wokovu. Imani!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Tupo leo katika dominika ya 4 ya Kwaresima. Hii ni dominika ambayo kadiri ya mapokeo hufahamika kama dominika ya furaha (Laetare). Ni furaha ya kufika nusu ya safari ya mfungo wa Kwaresima na ni furaha inayodokeza ile furaha kubwa zaidi inayotazamiwa, furaha ya kuadhimisha Ufufuko wa Bwana. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (2Nyakati 36:14-16, 19-23). Vitabu viwili vya Mambo ya Nyakati tunaweza kuviita kuwa ni vitabu vinavyoandika upya historia ya Waisraeli. Hii haina maana kuwa vitabu hivi vinakosoa au kurekebisha mahala fulani katika yale ambayo yamekwisha elezwa na vitabu vilivyotangulia, hapana. Vitabu hivi vinakuja kuyaangalia matukio hayo katika ujumla wake. Vinaunganisha matukio yaliyotokea katika nyakati mbalimbali za kihistoria ili yule anayesoma sasa aweze kuona yanavyohusiana. Msomaji aweze kwa mfano kuona kuwa tukio hili lilileta baadaye madhara haya au tukio hili ni matokeo ya tukio fulani la nyuma n.k. Lakini sio hilo tu, vitabu hivi vya Mambo ya Nyakati havielezi tu matukio bali vinayapima kwa namna yalivyoendana na Agano la Mungu au yalivyolikiuka.

Somo la kwanza la leo linahusu tukio moja kubwa sana katika historia ya Waisraeli. Nalo ni tukio la kubomolewa kwa mji wa Yerusalemu pamoja na hekalu lake, tukio lililoenda sambamba na waisraeli hao hao kuchukuliwa kutoka nchi yao na kupelekwa utumwa katika nchi ya Babeli. Kitabu cha Pili cha Mambo ya Nyakati kinapoelezwa tukio hili la kusikitisha na lililoacha doa katika historia ya waisraeli lilianza pale ambapo waisraeli walimweka Mungu kando, wakaacha kulishika Agano. Tunasikia somo linasema mfalme, makuhani na watu walimkosea Mungu na waliinajisi nyumba ya Bwana. Na hata Mungu kwa huruma yake alipowatumia manabii wawakumbushe kumrudia, wao hawakuwasikiliza na tena waliwadhihaki wajumbe hao wa Mungu na wakayadharau maneno yao. Matokeo yakawa ndio hayo: kuharibiwa mji wa Yerusalemu, kubomolewa hekalu na wao kukaa utumwani kwa mkuda wa miaka 70. Somo hili linaletwa kwetu leo ili kukazia umuhimu wa toba na wongofu wa ndani. Tunaona kuwa endapo waisraeli wangesikia sauti ya wajumbe wa Mungu, wangekuwa tayari kufanya toba na kumrudia Mungu basi hawangefikia huko katika uharibifu mkubwa namna hiyo. Tunaalikwa tutumie vema huruma na upole wa Mungu ili kumrudia kwa toba na wongofu wa ndani.

Somo la pili (Ef 2, 4-10). Kwa jinsi hiyo hiyo ambavyo somo la kwanza limetupa mwaliko wa kuitumia vema huruma na wema wa Mungu ili tumrudie, Mtume Paulo katika somo la pili anatufundisha kuwa tumeokolewa kwa neema. Ni vizuri tukalielewa vema fundisho hili la Mtakatifu Paulo kwa sababu kuna tafsiri isiyo ya kikatoliki inayobadilisha kabisa taalimungu ya Mtakatifu Paulo. Tafsiri hiyo ina inaona katika fundisho hili la Mtakatifu Paulo uwiano wa imani na matendo katika ukombozi. Na moja kwa moja imani inapewa kipaumbele kiasi ambacho inaelezwa kuwa mtu akishaamini tu na kumpokea Kristo basi inatosha, atakuwa ameokolewa. Kwa jinsi hii matendo yake yatafunikwa na imani yake kubwa. Mtakatifu Paulo lakini anachokieleza ni tofauti. Yeye anaanza kuangalia kile alichofanya Kristo. Kujitoa kuteswa, kusulubiwa hadi kufa Msalabani kwa ajili ya wanadamu.

Sasa tendo hilo la Kristo ambalo ndio limewafungulia wanadamu wote mlango wa wokovu, ukililinganisha na hali aliyokuwa nayo mwanadamu kabla ya Kristo, hali ya dhambi ile ya tangu Adamu, ni hapo unaona kuwa ni neema tu ya Mungu iliyofanya hayo yote ili kumkomboa mwanadamu. Mwanadamu katika hali hiyo ni kama alikuwa amekufa, ni neema iliyomrudisha katika uzima. Sasa kutoka katika ukombozi huo wa Kristo, ili mwanadamu apokee matunda yake anahitaji imani. Na hii imani ni maisha ndani ya Kristo tofauti na yale maisha ya awali nje ya Kristo. Haupo hapa ukinzani kati ya imani na matendo wala haupo uwiano kuwa kipi kitangulie au kipi ni muhimu zaidi kati ya imani na matendo. Na hii ndiyo tafsiri Katoliki ya fundisho hili la Mt. Paulo kuwa tumekombolewa kwa neema.

Somo la Injili (Yoh. 3,14-21). Somo la Injili pia linajikita kueleza tukio la Yesu kufa Msalabani. Mwinjili Yohane analifananisha tukio hili na tukio lile la nyoka wa shaba wakati wa Musa. Wakati huo Mungu alimwambia Musa atengeneze nyoka wa shaba ili kila atakeumwa na nyoka, amtazame huyo nyoka wa shaba apone. Injili inatuonesha kuwa kile alichokifanya Mungu zamani hizo kwa njia ya mfano, sasa anakikamilisha kwa njia ya Kristo. Kristo Msalabani ni zaidi ya nyoka wa shaba. Yeye anawapa uzima wa milele wote wanaomwangalia kwa jicho la imani. Hapa pia tunaona unaelezwa uhusiano kati ya Msalaba wa Kristo, wokovu na imani. Kifo cha Kristo Msalabani kimefungua njia ya wokovu kwa ulimwengu mzima. Wokovu huu ni nuru iliyokuja kumuangazia mwanadamu aishiye katika giza. Ni mwanadamu huyu anayealikwa kwa njia ya imani aipokee nuru na kuanza maisha ya matendo mema ili asiingie katika hukumu. Hapa imani inaelezwa kama mwanga unaomsaidia mtu kuona yuko wapi na hapo hapo inamsukuma kupiga hatua kumwendea Kristo ili kuanza naye njia mpya ya maisha, njia ya wokovu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, upendo wa Mungu kwa wanadamu ni mkubwa mno. Ni kwa upendo Mungu alimuumba mwanadamu, ni kwa upendo amemkomboa kwa njia ya Kristo na ni kwa upendo anaendelea kumualika mwanadamu aishi katika muungano naye. Masomo ya dominika hii ya nne ya Kwaresima yametuoensha namna mbalimbali ambazo Mungu ameudhihirisha upendo wake huu kwa mwanadamu na kwa ulimwengu mzima. Kwa njia ya ujumbe huu, hata leo Mungu anatukumbusha kuwa Yeye yupo na upendo wake kwetu haujakoma. Uwepo huu wa Mungu katika maisha yetu unajionesha kwa namna mbalimbali. Na tukiketi chini na kutafakari hatua mbalimbali za maisha ambazo tumezipitia au ambazo tunazipitia tutamuona. Yupo na upendo wake upo.

Jibu la upendo ni upendo. Yeye Mungu aliyetupenda sisi kwanza, anatualika na sisi tumpende. Tuoneshe upendo kwake.  Masomo ya leo yametuonesha matokeo ya kutokumpenda Mungu, ndiyo kuishi nje ya Mungu. Somo la kwanza limeeleza hali hiyo kama ni kumkufuru Mungu na ni kukiuka Agano naye. Na matokeo yake yakawa kubomolewa kwa mji wa Yerusalemu na waisraeli kupelekwa utumwani. Injili yenyewe inamfananisha asiye na upendo kwa Mungu kama yule ambaye nuru imekuja kwake lakini yeye akapenda kubaki katika giza, akapenda giza kuliko nuru. Na matokeo yake ni kuwa anaingia hukumuni. Haya yanaelezwa si ili kutujaza hofu. Yanaelezwa kutupa mwanga ili kwa uhuru kamili tuchague maisha ndani ya upendo wa Mungu, tuiishi imani yetu vema na imani hiyo itufikishe katika wokovu.

Liturujia J4 Kwaresima

 

12 March 2021, 15:40