Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili III ya Kipindi cha Kwaresima: Ukuu wa Fumbo la Msalaba na Amri za Mungu zinazofunga Agano la Kale kati ya Mungu na Waisraeli. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili III ya Kipindi cha Kwaresima: Ukuu wa Fumbo la Msalaba na Amri za Mungu zinazofunga Agano la Kale kati ya Mungu na Waisraeli.  (AFP or licensors)

Tafakari Jumapili 3 Kwaresima: Ukuu wa Msalaba; Amri za Mungu!

Kiini cha Agano hilo ni wema wa Mungu. Wema unaotafsiriwa pia kama upendo au huruma ya Mungu. Wema ambao tunaweza kusema umemfanya Mungu “akae meza moja” na watu wake. Amri hizi anazozitoa sasa, sio kiini cha Agano bali zenyewe anazitoa ili ziwasaidie watu wake wabaki katika Agano naye. Hii ndiyo maana Biblia haiziiti Amri bali Maneno ya Mungu. Ukuu wa Msalaba!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Katika kipindi cha leo tunayaangalia masomo ya dominika ya 3 ya Kwaresima. Tutatoa ufafanuzi ili kuyaelewa yanatuambia nini na kisha kupata tafakari fupi ya kutuongoza katika kuuishi ujumbe wake. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Kutoka 20:1-17) Somo la kwanza linaeleza tukio la Mungu kutoa Amri Kumi, maarufu kama Amri Kumi za Mungu. Amri hizi Mungu alizitoa kwa taifa lake teule mlimani Sinai, wakati taifa hilo likiwa njiani kuelekea katika nchi ya ahadi. Kuzielewa Amri hizi ni vuzuri turudi katika wito wa Abrahamu. Wakati Mungu anamwita Abrahamu kutoka katika nchi yake aende pale ambapo Mungu mwenyewe atakayomuonesha (Rej Mwa 12:1-4), alimpa pia ahadi. Na ahadi zenyewe ni tatu: alimwahidi kumjalia uzao mwingi, aliahidi kumpatia nchi hiyo ya ahadi na tatu kwake Abrahamu na kwa uzao wake aliahidi kuwa Mungu wao na wao watakuwa watu wake (Rej. Mwa 17:3-8). Mpaka hatua hii, uzao wa Abrahamu ulikuwa umekuwa mkubwa hadi ukawa tishio kwa Wamisri; nchi ya ahadi ndio walikuwa wanaiendea na sasa walikuwa wako njiani ila ile ahadi kuwa Mungu atakuwa Mungu wao na wao watakuwa watu wake ilikuwa bado haijakamilika.

Ni tukio hili la leo, la Mungu kuwapa Waisraeli Amri Kumi ndio linakamilisha ahadi hiyo. Linaikamilisha kwa sababu kwa tukio hilo, Mungu anaingia Agano na watu wake. Ni hapa ndipo linafanyika linaloitwa Agano la Kale. Mungu hatangazi tu kuwa sasa mimi ni Mungu wenu na ninyi ni watu wangu, hapana. Anafanya hivyo kwa kujifunga katika Agano na hao anaotaka awe Mungu kwao na wao wawe watu wake. Kiini cha Agano hilo ni wema wa Mungu. Wema unaotafsiriwa pia kama upendo au huruma ya Mungu. Wema ambao tunaweza kusema umemfanya Mungu “akae meza moja” na watu wake. Amri hizi anazozitoa sasa, sio kiini cha Agano bali zenyewe anazitoa ili ziwasaidie watu wake wabaki katika Agano naye. Hii ndiyo maana Biblia haiziiti Amri bali Maneno ya Mungu. Sio kwamba neno amri sio sahihi bali neno hilo halitoshi, halifiki pale kilipo kiini cha Agano yaani wema wa Mungu. Kumbe Mungu anazitoa amri hizi kama wigo ambamo ndani yake anawahifadhi watu wake katika wema wake. Ni wigo wa kulinda mahusiano. Mahusiano kati yao na Mungu (amri ya 1-3) na pia mahusiano yao kati yao (amri ya 4-10).

Somo la Pili (1Kor 1:22-25) Somo la Pili linatuletea fundisho la Mtume Paulo kuhusu Taalimungu ya Msalaba. Katika somo hili Mtume Paulo anafundisha kuwa Msalaba wa Kristo ni Kristo mwenyewe, ni nguvu ya Mungu na ni Hekima ya Mungu. Kama vile katika Agano la Kale Mungu alivyoshuka akaingia katika mahusiano na mwanadamu kwa njia ya Agano na amri zake, vivyo hivyo katika Kristo. Katika Agano Jipya Mungu amependa sasa kukikamilisha kile alichokianza. Kwani kwa njia ya Kristo, kwa njia ya kifo chake Msalabani Mungu amemletea mwanadamu ukombozi.  Pamoja na yote hayo aliyofanya Mungu, Wayahudi bado wanatafuta ishara na Wayunani bado wanatafuta hekima. Wayahudi wanatafuta ishara kwa kisingizio cha kuona kikwazo katika kifo cha Kristo. Na kikwazo hicho wanakiona kwa sababu katika Maandiko mtu aliyeangikwa Msalabani amelaaniwa (rej. Kumb 21:23). Kwa sababu hiyo walisema hawawezi kumwamini Kristo kama mwokozi wao kwa sababu yeye amekufa kifo cha Msalaba. Wayunani wao waliona ni upuuzi. Kifo cha Msalaba ilikuwa ni adhabu waliyopewa wanyang’anyi, majambazi sugu na wale wote waliokuwa hatari kwa utawala wa dola ya Kirumi. Ilikuwa ni adhabu kali, ya aibu na ilitolewa iwe fundisho kwa wengine.

Sasa elimu yao ya falsafa waliyokuwa nayo, Wayunani hawakuamini kabisa kuwa aliyekufa kifo cha namna hiyo ndio wanatakiwa wampokee kama Mwokozi wao. Mtume Paulo katika somo hili anawakemea Wakorintho (Wayahudi kwa Wayunani) dhidi ya kutumia vipawa alivyowajalia Mungu katika kumpinga Mungu mwenyewe. Ufunuo na Hekima vyote ni vipawa vya Mwenyezi Mungu. Ni Mungu aliyejifunua katika Maandiko Matakatifu na ni yeye aliyewajalia wanadamu hekima. Kitabu chenyewe cha Hekima kinafundisha kuwa kumcha Bwana ndio chanzo cha hekima (Hek 7:25). Alichokiona Mtume Paulo kwa Wakorinto ni kuwa vipaji hivi Mungu aliwajalia makundi haya yote mawili ili wavitumie vema viwaongoze kufika kwa Kristo kama ukamilifu wake. Anayeyatumia vizuri Maandiko yatamuongoza kumwamini Kristo na kumpokea kama mwokozi wa maisha yake. Hali kadhalika anayetumia Hekima na elimu. Akiitumia vizuri alivyokusudia Mungu, itamwongoza kumwamini Kristo na kumpokea kama mwokozi wa maisha yake.

Injili (Yoh 2:13-25). Somo la Injili ya dominika hii ya 3 ya Kwaresima linahusu utakaso wa Hekalu. Yesu anaingia Hekaluni kipindi ambacho sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa inakaribia. Humo akakuta Hekalu limekuwa kama soko kwa sababu walikuwa wanauza humo wanyama na ndege bila shaka kwa ajili ya kutolea sadaka wakati wa sherehe na walikuwamo pia wanaobadilisha fedha. Yesu akapindua meza zao akawafukuza wote. Tukio hili limeelezwa katika Injili zote nne. Mwinjili Yohane anapolielezea katika Injili yake, analihusisha na sherehe ya Pasaka ya Wayahudi na ile Pasaka ya Wakristo. Tunafahamu kuwa Pasaka ya Wayahudi ilikuwa ni sherehe ya kukumbuka kuokolewa kwao kutoka utumwani Misri na Pasaka yetu wakristo ni adhimisho la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo. Mwinjili Yohane analihusisha tukio hili na Pasaka ya Wayahudi kwa kuwa anaonesha lilitokea wakati watu wanaiandaa sherehe hiyo. Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu. Na anaihusisha na Pasaka ya Wakristo pale Yesu anapojibu na kusema “livunjeni hekalu hili nami katika siku tatu nitalisimamisha”. Na hapo hapo Yohane anaongeza kusema “Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake”. Ni mwili wake utakaovunjwa, yaani kuuwawa, lakini yeye kwa umungu wake atafufuka baada ya siku tatu.

Anachokifanya Yesu ni kama tendo la kinabii. Na kwa tendo hilo analenga kuwaambia kuwa siku zinakuja ambapo ukombozi wanaousherekea katika Pasaka hautakuwa ule wa kutoka Misri bali utakuwa ni ule ambao Pasaka yake unauleta. Yaani ule wokovu anaouleta kwa ulimwengu mzima kwa Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Kwa upande mwingine pia anapowaambia livunjeni hekalu hili anamaanisha kuwa katika Pasaka yake Hekalu halitahitajika. Hapa inabidi tukue pia kuwa dhana ya Hekalu ni tofauti kabisa na dhana ya Kanisa kama tunavyoelewa sasa. Kwa Wayahudi Hekalu lilikuwa ni sehemu pekee ambapo Mungu yupo. Kwa Wayahudi Mungu alikuwa na makao yake mbinguni. Kwa duniani makao yake yalikuwa ndani ya Hekalu. Na Hekalu hilo lilikuwa ni moja tu. Ukitaka kukutana na Mungu ni lazima uende Hekaluni. Yesu anapodokeza kuhusu kuvunjwa Hekalu anadokeza kuwa katika Pasaka yake, watu hawatakutana tena na Mungu Hekaluni bali watakutana na Mungu kwa njia yake. Kristo ndio namna mpya ya watu kukutana na Mungu. Yeye mwenyewe alisema “anayeniona mimi amemuona Baba” (Yoh 14:9)

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tumeyasikia masomo ya dominika hii ya 3 ya Kwaresima na tumepata ufafanuzi wake. Ninawaalika katika dominika hii tuingie katika tafakari kuhusu mahusiano yetu. Mahusiano tuliyonayo na Mwenyezi Mungu lakini pia mahusiano tuliyonayo sisi kwa sisi. Tutumie kipindi hiki cha Kwaresima kuboresha mahusiano hayo ili tuendelee kubaki katika wema, upendo na huruma ya Mungu. Tuchote kutoka kwa Kristo nguvu ya kuanza upya pale ambapo mahusiano hayo yamelegalega. Na kama anavyotukumbusha Baba Mtakatifu Francisko, Sakramenti ya Upatanisho, toba na Maungamo ni mahala pa msingi sana pa kuanzia kwa yule anayetaka kujenga upya mahusiano na kupata tumaini jipya la kusonga mbele.

Liturujia j3 Kwaresima

 

06 March 2021, 16:27