Tafuta

2021.03.02 Sr. mmoja alipiga magoti mbele ya polisi nchini Myanmar. 2021.03.02 Sr. mmoja alipiga magoti mbele ya polisi nchini Myanmar. 

Myanmar:Mapinduzi ya kijeshi.Mshikamano wa maaskofu wa Marekani

Maaskofu nchini Marekani wanaonesaha mshikamano na Baraza la Maaskofu nchini Myanmar kutokana na wakati mgumu wanaopitia raia.Na ujasiri wa Sista Ann Nu Thawng aliyepiga magoti kusali huku akiwaombe Polisi wasiwadhuru waandamanaji nchini Myanmar.Picha yake imetanda katika mitandao ya kijamii.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Ukandamizaji wa maandamano dhidi ya mapinduzi ya serikali ya tangu Februari 1, iliyopita umeendelea nchini Myanmar. Hata tarehe 3 Machi vikosi vya usalama viliwafukuza waandamanaji katika miji kadhaa nchini kote na kuua watu wasiopungua 8, kulingana na vyombo vya habari vya ndani na ripoti za mitandao ya ya kijamii. Na mshikamano wa maaskofu wa Marekani pia umewafikia watu wa Birmania. Katika barua iliyotolewa Jumanne tarehe 2 Machi 2021, Askofu David J. Malloy, rais wa Tume ya Haki ya Kimataifa na Amani ya Baraza la  Maaskofu (Usccb), inaungana hata na sauti ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewasilisha kwa mara nyingine tena wito wake tarehe 3 Machi mara baada ya katekesi yake ili kushinda ukandamizaji na maelewano juu ya mafarakano yaliyopo, pia akiwageukia  jumuiya ya kimataifa, ameomba wafanye kazi ili kuhakikisha kuwa matakwa ya watu wa Myanmar hasongwi na vurugu. Kwa niaba ya Kamati ya Haki na Amani ya Kimataifa barua hiyo inasomeka kuwa aliandika barua ya mshikamano kwa Baraza la Maaskofu wa Myanmar na kuomba Serikali ya Marekani  kuzingatia kwa uangalifu maoni ya Kanisa mahalia kufikia suluhisho la haki katika mgogoro. Askofu Malloy anawaalika Wakatoliki na watu wote wenye mapenzi mema kuwaombea watu na viongozi wa Birmania.

Hali nchini Myanmar:giza halishindi kamwe giza

Hali nchini Myanmar ilizidi kuwa mbaya  tangu Februari 28, wakati vikosi vya usalama vilipowafyatulia risasi waandamanaji katika miji kadhaa, na kuua watu 20 na kujeruhi wengine wengi. Wakati nchi iliharibiwa na vurugu, huko Yangon, siku hiyo hiyo Jumapili, Kardinali Charles Bo, rais wa Baraza la  Maaskofu wa Myanmar, alizungumza maneno mazito ya kuomba  damu isiyo na hatia simwagike  tena. “Sote ni watoto wa kike na kiume  wa nchi moja, wa mama mmoja, Myanmar. Giza halishindi kamwe giza; nuru tu ndio inayoweza kuondoa giza. Mantiki ya jicho kwa jicho hupofusha ulimwengu. Sote tunaamini katika nguvu ya upendo na upatanisho, alisisitiza  askofu mkuu wa Yangon katika mahubiri yake wakati wa Misa ya Jumapili ya pili ya Kwaresima, tarehe 28 Februari 2021, akionya kwamba chuki haishindi chochote. Amani inawezekana. Kardinali Bo, rais wa Baraza la Maaskofu nchini  kwa njia hiyo, amesema "Amani ndiyo njia pekee. Demokrasia ni nuru pekee."

Mtawa wa shirika la Mtakatifu Francis wa Saverio mbele ya polisi kutetea wanyonge

Hata hivyo Sista  Ann Nu Thawng wa Shirika la Wamisionari wa Mtakatifu Francis Saverio aliyepiga magoti kwa kusali huku akiwaomba Polisi wa kutuliza ghasia, ili waache kurusha risasi juu ya  waandamanaji nchini Myanmar, picha yake yake imetanda katika mitandao ya kijamii. Yote hayo ni kutokana na   mapinduzi ya kijeshi nchini humo, na  baadhi ya picha  zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na takwimu zinaonesha wazi kuwa vitendo vya kuwapiga na kuwajeruhi raia vinaongoza nchini humo, huku viokiongezeka vifo na majeraha kwa raia. Tuungane na wito wa  Baba Mtakatifu Francisco na viongozi wote wa kanisa kuwaombea watu wa Myanmar pia kuwaombea makuhani na Watawa wote wenye moyo wa ujasiri ambao wapo tayari kusimama kwa ajili ya kutetea wanyonge kama alivyofanya Sr Ann Nu Thawing. 

03 March 2021, 17:47