Tafuta

Vatican News
Watanzania wanamlilia na kumwombolezea Hayati Dr. John Joseph Pombe Magufuli aliyeaga dunia hivi karibuni. Wana matumaini makubwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Watanzania wanamlilia na kumwombolezea Hayati Dr. John Joseph Pombe Magufuli aliyeaga dunia hivi karibuni. Wana matumaini makubwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.  (AFP or licensors)

Kilio kwa Dkt. Magufuli, Matumaini kwa Rais Samia Suluhu Hassan

Mama Esther Bhoke Madafa, anamwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli, anapenda kutuma salama za rambirambi kwa Mama Janet Magufuli na familia katika ujumla wake na zaidi anapenda kuonesha matumaini ya watanzania wengi kwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu wa Vikosi vya ulinzi na usalama. Umoja na Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S – Vatican.

Familia ya Mungu nchini Tanzania inaendelea kusali, kuomboleza na kumlilia Dr. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni kiongozi aliyesimama kidete kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Leo hii fedha ya walipa kodi inagharimia miradi mikubwa mikubwa iliyoanzishwa wakati wa uongozi wa JPM, kama wengi wanavyomkumbuka. Amesaidia kuimarisha nidhamu, uwajibikaji kazini. Kiongozi na mwanamapinduzi sasa ametangulia mbele ya haki Tarehe 29 Oktoba 1959 hadi tarehe 17 Machi 2021 ni kipindi kifupi sana, yaani ni umri wa miaka 61, lakini ndivyo ilivyo mpendeza Mwenyezi Mungu. Mtetezi wa wanyonge sasa “Pumzika kwa Amani, RIP”. Jumamosi tarehe 20 Machi 2021 wawakilishi wa watanzania kutoka sehemu mbalimbali za Italia, walishiriki katika Ibada ya Misa Takatifu na Dua ya kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli. Kilikuwa ni kipindi cha watanzania kutakiana faraja na kuombea amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha mpito wa majonzi.

Siku hii Ilikuwa ni nafasi kwa watanzania katika umoja wao, kulia na kuomboleza kama ndugu wamoja kwa kulipoteza “Jembe na Shujaa wa Afrika” ambaye amekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kuwapenda na kuwahudumia raia wake kwa ari na moyo mkuu. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Mama Esther Bhoke Madafa, mke wa Mheshimiwa George Kahema Madafa, Balozi wa Tanzania nchini Italia anamwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli, anapenda kutuma salamu za rambirambi kwa Mama Janet Magufuli na familia katika ujumla wake na zaidi anapenda kuonesha matumaini ya watanzania wengi kwa Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama. Mama Esther Bhoke Madafa anamwomba Mwenyezi Mungu awajalie watanzania: baraka, neema na nguvu ya kushikamana kama ndugu wamoja, huku wakimtanguliza Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kama alivyoshuhudia Hayati Dr. John Pombe Magufuli katika uhai wake.

Katika kipindi cha muda mfupi wa uongozi wake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya mambo makubwa na mazito ambayo hayatasahaulika kamwe katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni kiongozi aliyewaheshimu na kuwajali maskini na wanyonge na kwa watanzania wote alijipambanua kuwa ni Baba wa wote. Alifundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha, akakanya na kukaripia pale ilipobidi. Alikuwa ni kiongozi aliyesimamia ukweli na uwazi, akatamani kuona anawavusha watanzania kutoka katika umaskini na kuwaingiza katika uchumi wa kati! Mama Esther Bhoke Madafa anapenda kuchukua fursa hii, kutuma salam za rambirambi kwa Mama Janet Magufuli, Mjane wa Hayati Dr. John Pombe Magufuli kwa msiba huu mzito. Anamwomba afarijike kwa sala na dua njema zinazotolewa na watanzania pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo awe ni nguzo, faraja na mwanga angnavu katika safari ya maisha yake, apoanza sasa kuandika ukurasa mpya wa maisha bila ya uwepo wa “asali wake wa moyo”. Roho Mtakatifu Mfariji, awe ni ngome na kinga yake ya daima katika maisha.

Ni katika muktadha huu, Mama Esther Bhoke Madafa anakaza kusema, familia ya Hayati Dr. John Pombe Magufuli inaomboleza, lakini ndani ya familia kuna Mama Suzana Magufuli, Mama Mzazi wa Hayari Magufuli, ambaye kwa muda mrefu sasa yuko kitandani hajitambui. Lakini uchungu wa mwana anayeufahamu ni mama mzazi mwenyewe. Kama Mama mzazi katika hali na majonzi mazito kiasi hiki, atakuwa ameguswa katika hisia zake kwamba, kuna tukio kubwa limetendeka. Si haba kwamba, Hayati Dr. Magufuli aliwapenda na kuwathamini sana wagonjwa, akajitahidi kuboresha miundombinu ya afya, dawa na vifaa tiba kwa kutambua na kuguswa na mahangaiko ya wagonjwa na hasa maskini. Mwenyezi Mungu ampe nguvu ya kuweza kupokea msiba huu mzito, kwa imani na matumaini. Ni neema na faraja inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu inayoweza kuwa ni faraja yao ya daima.

Mzaburi anayetegemea ulinzi na tunza ya Mungu anasema: “Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi.  Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. BWANA ndiye mlinzi wako; BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele”. Zab 121. Mwenyezi Mungu awe ni msaada na kimbilio lao la daima. Hiki ni kipindi cha kuimarisha imani, matumaini na mapendo kwa Mwenyezi naye atawatendea kadiri ya utashi wake. Mama Esther Bhoke Madafa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulijalia Taifa la Tanzania kumpata Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama. Mwenyezi amkirimie nguvu, mwangaza, hekima ya mbinguni na uwezo katika kuwaongoza watanzania.

Rais Samia awe na ari na “kifua” cha kuyaendeleza yale mema aliyoyaacha Dr. John Pombe Magufuli kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mfao ya wengi. Kwa hakika, watanzania wanayo matumaini makubwa katika uongozi wake. Mwenyezi Mungu daima, awe ni nguzo na kimbilio lake la daima. Mama Samia Suluhu ni kioo cha wanawake. Kwa hakika atawashangaza wengi, kwa kuwafanyia mambo makubwa watanzania. Mwenyezi Mungu amlinde na kumwongoza katika maisha na utume wake huo mpya.

Mahojiano JPM
23 March 2021, 14:28