Tafuta

Vatican News
Viongozi wa Makanisa nchini Siria wamemwandikia Rais wa Marekani barua kumsihi aiondolee Siria vikwazo vya kiuchumi vinavyoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu wa Mungu nchini humo! Viongozi wa Makanisa nchini Siria wamemwandikia Rais wa Marekani barua kumsihi aiondolee Siria vikwazo vya kiuchumi vinavyoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu wa Mungu nchini humo!  (AFP or licensors)

Barua ya Viongozi wa Kanisa kwa Rais Joe Biden wa Marekani

Vikwazo vya uchumi dhidi ya Siria ni kati ya changamoto zinazoendelea kugumisha maisha ya watu wa Mungu nchini Siria, hali inayoweza pia kuibua wimbi kubwa la machafuko ya kisiasa na kidini huko Mashariki ya Kati. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyomo kwenye Waraka wa Viongozi wa Makanisa nchini Siria, waliomwandikia Joe Biden ambaye sasa ni Rais wa 46 wa Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutokana na kuyumba kwa hali ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kimaadili, kiutu na kijamii huko Mashariki ya Kati, dunia imeendelea kushuhudia kuibuka na kuimarika kwa vikundi mbalimbali vya kigaidi. Makundi hayo ya kigaidi ni kama vile: Wapiganaji wa Dola ya Kiislam “Islamic State (IS”), Al- Shaabab, Boko Haram, “Al-Qaeda in the Gulf of Yemen and The Islamic Maghreb, Ansaru na “The Movement for the Oneness and Jihad in West Africa” (MOJWA). Makundi haya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa hali ya usalama, haki na amani duniani. Mateso na mahangaiko ya wananchi wasiokuwa na hatia huko Mashariki ya Kati, lakini kwa namna ya pekee nchini Siria, ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa, kuhakikisha kwamba, inajifunga kibwebwe ili kusitisha vita na hatimaye, kuanza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Ni wakati muafaka wa ujenzi wa umoja wa udugu wa kibinadamu na mshikamano wa kitaifa; kwa kukataa kumezwa na misimamo mikali ya kidini na kisiasa ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa wananchi wa Siria.

Uharibifu wa mazingira na kumbu kumbu za kihistoria ni jambo ambalo kamwe aliwezi kuvumiliwa na kuachwa liendelee kutokea kwani huu ni urithi mkubwa wa binadamu. Kuhusu hatima ya maisha ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, kuna haja ya kusimamia haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu kama chachu ya ujenzi wa mshikamano wa kidugu, umoja, amani na usalama huko Mashariki ya Kati. Wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria wanaohifadhiwa nchini Lebanon na Yordan, wataweza kurejea tena nchini mwao, ikiwa kama amani na utulivu vitarejeshwa tena huko nchini Siria na vijiji vyao kuanza kufanyiwa ukarabati mkubwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, Wakristo wanao mchango mkubwa sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi huko Mashariki ya Kati, kumbe, si Jumuiya inayopaswa kubezwa wala kudhalilishwa. Ni sementi inayounganisha jamii na kwamba, Wakristo wanapaswa kuwa ni sehemu ya maisha ya watu wa Mashariki ya Kati na kamwe wasionekane kama ni “watu wa kuja”. Siria inakabiliwa na vitendo vya kigaidi vinavyosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria kutokana na vita ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Kuna maambukizi makubwa ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Vikwazo vya uchumi dhidi ya Siria ni kati ya changamoto zinazoendelea kugumisha maisha ya watu wa Mungu nchini Siria, hali inayoweza pia kuibua wimbi kubwa la machafuko ya kisiasa na kidini huko Mashariki ya Kati. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyomo kwenye Waraka wa Viongozi wa Makanisa nchini Siria, waliomwandikia Rais Joe Biden ambaye amekula kiapo tarehe 20 Januari 2021 na hivyo kushika madaraka na kuwa ni Rais wa 46 wa Marekani. Viongozi wa Makanisa huko Mashariki ya Kati wanampongeza Rais Joe Biden kwa kuchaguliwa na wananchi wa Marekani ili kuwaongoza. Viongozi hawa wanatambua na kuthamini pia mchango wa Marekani katika Jumuiya ya Kimataifa. Wanasema, kati ya mambo yanayohitaji utekelezaji wa dharura ni pamoja na mateso ya watu wa Mungu nchini Siria kutokana na vikwazo vya kiuchumi.

Viongozi wa Makanisa wanasema, vikwazo hivi vinaendelea kuhatarisha maisha ya wananchi wa Siria ambao wamekwisha kutikiswa na kupepetwa na vita pamoja na changamoto mbalimbali za maisha. Kwa sasa Siria inashindwa kupata misaada ya kiutu, biashara imesitishwa na mchakato wa uwekezaji umekwamishwa kiasi kwamba, mfumo na miundo mbinu ya afya pamoja na vitega uchumi nchini Siria vinaendelea kufifia kila kukicha! Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, linabainisha kwamba, baa la njaa linaendelea kuwapekenya walau nusu ya wananchi wa Siria. Huduma ya afya imeendelea kuteteleka kila kukicha, kiasi kwamba, watu hawana tena uhakika wa maji safi na salama kutokana na vyanzo vya maji kuchafuliwa sana. Changamoto zote hizi zinagumisha jitihada za Siria za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni matumaini ya viongozi wa Makanisa kwamba, Serikali mpya ya Rais Joe Biden, itaweza kuingilia kati ili kuokoa maisha ya wananchi wa Siria, kwa kutekeleza kwa vitendo mapendekezo yaliyotolewa na Taarifa Alena Douhan, Mwakiishi Maalum wa Umoja wa Mataifa huko Siria. Mafao ya wananchi wa Marekani yanaweza kufikiwa pasi na kuwaadhibu watu wa Mungu nchini Siria.

Kilio Siria

 

27 March 2021, 14:42