Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 6 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Waamini wamwendee Kristo Yesu kwa imani na ujasiri ili awaondolee dhambi na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao wa kimwili. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 6 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Waamini wamwendee Kristo Yesu kwa imani na ujasiri ili awaondolee dhambi na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao wa kimwili. 

Tafakari Jumapili 6 Mwaka B: Nendeni kwa Yesu kwa Imani na Ujasiri

Ni imani katika Kristo Yesu na ujasiri wa mkoma vilivyomponya. Alitambua kuwa Imani kwa Kristo itamponya ndiyo maana anasema: “Bwana ukitaka waweza kunitakasa.” Huu ni mwaliko kwetu sote kuwa tukipatwa na matatizo tumwendee Kristo tumshirikishe tukimwambia; “Bwana, ukitaka waweza kutuponya.” Yesu atatuhurumia, atanyoosha mkono wake, atatugusa, na kutuponya.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 6 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ya 6 ni mwendeleo wa tafakari fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu. Masomo ya domenika ya 5, yalitupa faraja na matumaini kuwa uaminifu wetu kwa Mungu utatuponya na taabu zote kama ilivyokuwa kwa Ayubu na Yesu Kristo, ni tabibu magonjwa na udhaifu wa kila namna. Masomo haya yalitukumbushwa pia wajibu wetu wa kuwahudumia walio wagonjwa kwa kuwapeleka kwa Yesu ili aweze kuwaponya. Swali, Je, tumafanya hivyo? Masomo ya domenika ya 6 yanatueleza ubaya wa kutengwa kwasababu ya dhambi na kuishi katika hali ya upweke kama wakoma katika somo la kwanza na katika injili. Upweke ndicho kitu cha kwanza Mungu alikiita “si vizuri.” “Si vizuri huyu mwanaume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye” (Mwanzo 2:18). Maisha bila rafiki ni kama kufa bila mtu yeyote kushuhudia. Wakoma walikuwa hawana rafiki hawana mtu wa karibu, walikuwa wapweke. Upweke ni ukiwa, unyonge, huzuni, msiba na majonzi. Upweke ni kujihisi kuwa hauhitajiki, haustahili na kwamba haujakamilika.

Somo la kwanza la Kitabu cha Walawi (13:1-2, 44-46), linatupa picha halisi jinsi Wayahudi walivyokuwa wanawaona watu wenye ukoma. Ukoma ni ugonjwa unaoharibu na kukata baadhi ya viungo vya mwili wa mwanadamu na kuufanya uwe na madoa au mistari katika ngozi. Ugonjwa huu upo katika makundi matatu: Kundi la kwanza ni madoa madoa mwilini (Nodular leprosy). Kundi la pili ni ule ambao unaua hisia katika mwili wa binadamu, wakati mwingine bila mhusika kujua (anesthetic leprosy). Kundi la tatu ni mchanganyiko wa aina ya 1 na 2 (mixed leprosy). Kadiri ya Wayahudi ukoma ulijumlisha magonjwa yote ya ngozi, wakati mwingine hata yale yaliyosababisha ngozi kuwa nyeupe (2Fal. 5:27). Ukoma ulihusishwa na unajisi, hivyo mkoma alitengwa na Jamii (Heb. 5:2, 2Fal 15:2), ndiyo maana alipopita sehemu yenye watu ilimbidi kupiga kelele kwa sauti; “mimi najisi, mimi najisi, mimi najisi” ili wasio najisi wampishe wasije wakanajisika na wao. Ukoma ulikuwa ugonjwa usio na kinga wala tiba hivyo ulifanya maisha ya wenye ukoma enzi za Agano la Kale kuwa magumu mno. Walionekana kama ni wafu wanaoishi, hawakuruhusiwa kujumuika pamoja na watu. Wakipelekewa chakula kengele inagongwa wanajificha kwanza kikishawekwa na waliopeleka wakiondoka wao ndipo wanachukua na kula wakimaliza wanagonga kengele ili watu waje kuchukua vyombo vya chakula. Waliishi maisha ya mateso makali mno.

Katika somo la pili la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 10:31-33, 11:1), Mtume Paulo anatuambia tuwe na juhudi katika kufuata mapenzi ya Mungu. Ni lazima katika maisha yetu, tuungane na Kristo na kufanya mambo yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Paulo anatuasa tujihadhari sana na mambo yanayoweza kuwakwaza wenzetu kwa matendo yetu. Hasa kuwatenga wenye matatizo kama walivyofanya Wayahudi kwa Watu wenye ukoma. Mtume Paulo anatuhimiza kumwiga yeye jinsi alivyoishi katika kumfuata Kristo. Na anasema: tuiishi Injili iliyo dira ya maisha yetu, tuwe mfano mzuri wa maisha ya Kikristo kwa wakristo wenzetu na wale wasio wakristo. Imani yetu idhihirike kwa matendo mema yenye upendo. Injili kama ilivyoandikwa na Marko inasimulia jinsi Yesu alivyomponya mkoma. Ukoma ulichukuliwa kuwa ni ugonjwa usiotibika. Yesu kwa kumponya mkoma anaonyesha kuwa ameushinda utawala wa shetani na kuleta ufalme wa Mungu.

Kisha pata uhai mpya, yule mkoma alitangaza habari za Kristo; kadhalika nasi tutangaze habari za ufalme wa Mungu. Ni imani katika Kristo Yesu na ujasiri wa mkoma wa kumkimbilia Yesu ndivyo vilivyomponya.  Mkoma huyu alitambua kuwa Imani kwa Kristo itamponya ndiyo maana anasema: “Bwana ukitaka waweza kunitakasa.” Huu ni mwaliko kwetu sote kuwa tukipatwa na matatizo au magonjwa tumwendee Kristo tumshirikishe tukimwambia; “Bwana, ukitaka waweza kutuponya.” Yesu atatuhurumia, atanyosha mkono wake, atatugusa, na kutuponya. Wagonjwa wa ukoma walitengwa na jamii kwa sababu walionekana najisi sura zao zilitisha na kuwafanya ndugu, jamaa na familia zao kuwatenga. Huenda sisi nasi tukawa wakoma. Tumepoteza sura na mfano wa Mungu ndani mwetu kwa njia ya dhambi. Katika hili hakuna aliye salama kwani Yohane anatuambia kuwa; “Tukisema kwamba hatuna dhambi twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani mwetu. Tukiziungama dhambi zetu yeye ni mwaminifu, atatuondolea dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote.

Kama vile wenye ukoma walivyotengwa na jamii na kuwekwa mbali na watu sisi nasi tukitenda dhambi tunajitenga na Mungu, tunajitenga na wale tunaowakosea, tunajitenga sisi wenyewe na nafsi zetu. Kama mkoma nasi tumwendee Yesu mara moja bila kusita tena kwa haraka tutamkuta katika sakramenti ya utakaso, sakramenti ya upatanisho, sakramenti ya msamaha na uponyaji, upatanisho na kutuondolea dhambi zetu au tunangojea ratiba wakati mwingine mpaka tuwe hata kama tukiwa mahututi yeye atatuponya. Hii ni habari njema kwetu; Kanisa haliwatengi wenye dhambi. Hata hivyo wapo wanaojitenga na Kanisa kwa kuogopa kupokea Sakramenti ya Upatanisho wakiona kuwa kuishi katika dhambi ni ufahari. Tukumbuke kuwa kuishi katika hali ya dhambi ni chukizo kwa Mungu, kwa Kanisa, kwa jamii, jumuiya na familia, ni makwazo kwa walio wadogo. Tukumbuke kuwa; Imani yetu kwa Mungu ndiyo itakayotuponya na si Mungu kuwa na Imani nasi. Ndiyo maana Mtakatifu Agustino anatuambia Mungu ametuumba sisi bila sisi kutaka lakini hatatukomboa pasipo sisi kutaka. Tukiwa na Imani kwake yeye atatuponya na dhambi zetu zote na kututakasa. Daima Mungu hutaka kutuponya, lakini atafanya hivyo punde tutakapoonyesha nia yetu ya kutaka kuponywa. Lazima shauku ile ya kutaka kuponywa iwepo mioyoni mwetu kwanza. Yesu halazimishi tiba kwani anaheshimu uhuru wa kila mtu.

Magonjwa na mateso yaliyo na suluhisho tuyatafutie ufumbuzi. Yasiyo na suluhisho la kibinadamu tuyaweke mikononi mwa Mungu. Tumwombe Mungu vitu vitatu. Kwanza kutambua na kukubali mambo ambayo hatuwezi kuyatatua tumwachie yeye. Pili tuombe ujasiri wa kudhubutu kushughulikia matatizo tunayoyaweza. Tatu, tuombe hekima ya kutambua tofauti ya mambo tunayoyaweza na tusiyoyaweza. Tumwangalie Kristo katika safari ya ukombozi katika njia ya msalaba, kwani maumivu aliyoyapata, yalileta ukombozi kwetu sisi. Daima tuombe kuimarika katika imani, matumaini na mapendo yetu katika kuyachukulia magumu yote yanayotupata. Tuombe neema ya uvumilivu, busara na utii katika kutimiza mpango wa Mungu katika amaisha yetu. Katika nyakati za hofu, kutengwa na machungu, tumkumbuke mkoma aliyemlilia Yesu katika machungu yake naye akamponya. Tusiwe watu wa kukata tamaa. Tumkumbuke Ayubu, aliyeteseka lakini hakuthubutu kumwacha Mungu. Ukiunganisha mateso yako na ya Kristo utafarijika. Tuko mbioni kuanza kipindi cha Kwaresima, tujitafiti nafsi zetu ili tuweze kujirekebisha tulipojitenga na Mungu, na wenzetu, na familia zetu ili tuishi kwa umoja na upendo. Tuuvae basi ujasiri katika imani kama wa mkoma tumwendee Yesu kwa moyo wa majuto na kumwomba atutakase na kutuponya na udhaifu wetu naye atatukasa na kutuponya.

Jumapili ya 6 ya Mwaka B

 

10 February 2021, 15:50