Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Ufunuo wa Umungu wa Kristo Yesu uliofichwa katika Fumbo la Umwilisho! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Ufunuo wa Umungu wa Kristo Yesu uliofichwa katika Fumbo la Umwilisho! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 2 ya Kwaresima: Ufunuo wa Mungu

Kugeuka sura kwa Yesu na kumetameta kwa mavazi yake ni alama ya utukufu, utukufu ambao kimsingi ni sifa ya kimungu. Yesu anapogeuka sura anaudhihirisha utukufu wake wa kimungu, anaionesha hadhi yake ya kimungu ambayo ilijificha pale alipotwaa mwili wa kibinadamu. Musa na Eliya wanaomtokea ni wawakilishi wa ufunuo mzima wa kimungu katika Agano la Kale.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 2 ya Kwaresima mwaka B wa Kanisa. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Mwa 22:1-2, 9a,15-18). Somo la kwanza la dominika hii ya pili ya Kwaresima linatoka katika kitabu cha Mwanzo. Ni somo linalotupatia simulizi kuhusu sadaka ya Isaka. Katika somo hili tunaona Mungu anamwambia Abrahamu amtwae mwanae Isaka akamtoe sadaka ya kuteketezwa. Agano la Kale linaeleza uwepo wa aina nyingi za sadaka ambazo watu walimtolea Mungu. Sadaka ya kuteketezwa ilikuwa ndiyo ya juu kabisa. Na kwa Isaka ilimaanisha kumchinja na kisha kumchoma moto hadi ateketee kabisa. Hili halikuwa jambo dogo. Sisi tunaosoma simulizi hili leo tunajua kwamba hilo lilikuwa ni jaribu ambalo Mungu alikuwa anampa Abrahamu, na imeandikwa hivyo. Lakini Abrahamu mwenyewe hakujua kama hilo lilikuwa ni jaribu. Yeye alilipokea kama agizo kutoka kwa Mungu. Mungu anayemwamini, Mungu aliyempatia mtoto Isaka kama zawadi na Mungu huyo huyo ambaye sasa anataka kumchukua. Abrahamu anatii na akakuwa tayari kutimiza.

Simulizi hili ambalo ni la kipekee kabisa katika Agano la Kale, limekuwa na mafundisho mengi sana katika maisha ya Wakristo. Kubwa tunaloliona kati ya hayo ni imani. Mwitikio wa Abrahamu unawekwa kama mfano wa mwitikio anaopaswa kuwa nao mwamini. Abrahamu anaonesha imani kubwa sana kwa neno la Mwenyezi Mungu. Anajua kwamba Isaka ni mwana wa ahadi na kuwa ahadi zote ambazo Mungu alikuwa amempa zilikuwa zinapitia kwa Isaka – uzao mwingi, nchi ya ahadi na kuwa taifa teule la Mungu. Hata hivyo Abrahamu hakusita hata kidogo kumtoa Isaka sadaka.  Ni kama imani yake Abrahamu ilikuwa inamwambia na kumhakikishia kuwa ahadi za Mungu hazipotei, akiahidi ameahidi, atazitimiza tu, iwe ni kwa njia ya Isaka au kwa njia nyingine. Ni kwa imani hiyo, Abrahamu haoni kama anakwenda kumpoteza mtoto bali anaona anakwenda kutekeleza mpango mkubwa zaidi wa Mungu katika maisha yake. Liturujia imetupatia somo hili katika dominika hii ya kwaresima kwa lengo hilo hilo la kuamsha imani yetu. Abrahamu anawekwa kwetu kama mfano wa imani thabiti kwa Mungu, imani inayotusaidia kuyaona maisha yetu na yote tunayopitia katika mpango mpana zaidi wa Mwenyezi Mungu kwetu.

Somo la Pili (Rum 8:31b-34): Mafundisho anayoyatoa Mtume Paulo katika somo la pili, tunaweza kuyaeleza kwa maneno machache kabisa kuwa ni mwaliko wa kujiaminisha kwa Mungu. Dhana ni ile ile ya imani ambayo Abrahamu ametuonesha katika somo la kwanza. Hapa Mtume Paulo anaizungumzia lakini kutoka katika upande mwingine. Anawaandikia wakristo wa Roma, wakristo ambao walikuwa wanapitia kipindi kigumu cha mateso kutoka kwa watawala wa dola ya kirumi. Mtume Paulo anawataka wakristo hao wa Rumi wasiiache imani yao kwa kuogopa vitisho au manyanyaso kutoka kwa watawala. Anawaambia “Mungu akiwa upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” Mtume Paulo anachowakumbusha Warumi ni kuwa wakiendelea kuishika imani yao na wasipokubali kuyumbishwa na vitisho hivyo, basi watumainie ushindi kwa jina lake Mungu wanayemwamini.

Kwa Mtume Paulo imani sio kitu cha mzaha, sio nadharia na wala sio kanuni tu ya maisha. Imani inamuunganisha mwamini na Mungu mwenyewe na inamjalia mwamini nguvu na ulinzi wa pekee kutoka kwa Mungu mwenyewe. Imani haiwezi kumwangusha mtu hata mara moja. Anapoendelea sasa Mtume Paulo kujenga juu ya fundisho lake hilo kuhusu Imani, anatoa mfano wa kitu kama kile kilichotokea kwa Abrahamu. Abrahamu alikuwa tayari kumtoa sadaka mwanae kwa kulishika neno la Mungu. Waisraeli wote walimsifu Abraham una kumuona kuwa ndio mfano wa uaminifu. Sasa Mtume Paulo anarejea hilo na kusema Mungu mwenyewe hakumkatalia mwanaye Yesu. Alikuwa tayari kumtoa afe kwa ajili yetu sote. Kwa maneno mengine hapa Paulo anaonesha kuwa Mungu ni mwaminifu. Neno lake ni la uhakika. Kumbe anapowaambia washike imani kwa Mungu na wasihofu chochote basi waishike kweli kweli na Mungu kwa uaminifu wake atawajalia salama.

Injili (Mk 9:1-9): Somo la Injili ya dominika hii linaeleza tukio la Yesu kugeuka sura. Tukio hili linatokea mlimani ambapo Yesu aliwatwaa wafuasi wake watatu Mtume Petro, Yakobo na Yohane na kwenda nao. Katika injili hii kuna vitu ambavyo mwinjili Marko ameviandika na tunapovisoma vinatusaidia kuelewa ni nini maana au fundisho la tukio hili zima la Yesu kugeuka sura. Somo linaanza kwa kusema “hata baada ya siku sita”. Ni siku sita zipi? Ni siku sita baada ya tukio la Petro kumkiri Yesu kuwa ndiye Kristo. Petro akiwa anajibu lile swali la Yesu “watu huninena mimi kuwa ni nani?” Kwa maneno hayo “baada ya siku sita”, msomaji anadokezwa kwamba hiki kinachokwenda kuelezwa kina uhusiano na kilichotokea siku sita kabla. Nacho ni nini? Ni ufunuo au utambulisho wa Yesu kuwa ni nani. Kugeuka sura kwa Yesu pamoja na kumetameta kwa mavazi yake ni alama ya utukufu, utukufu ambao kimsingi ni sifa ya kimungu. Kumbe, Yesu anapogeuka sura anaudhihirisha utukufu wake wa kimungu, anaionesha hadhi yake ya kimungu ambayo ilijificha pale alipotwaa mwili wa kibinadamu. Musa na Eliya wanaomtokea ni wawakilishi wa ufunuo mzima wa kimungu katika Agano la Kale. Musa anawakilisha Torati na Eliya Manabii, vitu ambavyo vilisimama badala ya ufunuo huo wa kimungu.

Swali sasa analouliza Mtume Petro au ombi analolitoa ya kuwa wajenge vibanda vitatu ni tafsiri ya wafuasi kuhusu hicho wanachokiona. Tunaweza kusema pia kuwa ni tafsiri ya kibinadamu kuhusu tukio hilo zima. Mtume Petro anawaona Musa na Eliya katika mstari mmoja wa usawa lakini pia anavutiwa na utukufu huo kiasi cha kuomba wasishuke kutoka mlimani. Wajenge vibanda, yaani wajenge makazi huko na wabaki huko huko. Kutoka katika tafsiri hiyo ya kibinadamu, sauti inashuka kutoka mbinguni. Ni sauti tunayoweza kusema inakuja kutoa tafsiri ya kimungu ya tukio zima. Nayo inasema “huyu ni mwanangu mpendwa, msikieni Yeye”. Musa na Eliya wanatoweka anabaki Yesu peke yake. Yesu anabaki peke yake kuonesha kuwa sio Musa na Eliya wanaobeba ukamilifu wa ufunuo wa kimungu, bali ni Yeye. Ni Yesu. Kumsikiliza Yeye ni kuusikiliza au kuushika ufunuo wote wa kimungu.

Pili neno hilo Mwana mpendwa linaonesha uhusiano wa pekee wa upendo kati ya Baba na Mwana. Zaidi ya hayo lakini ni sifa ya yule mtumishi wa Bwana aliyemtabiri Nabii Isaya (Rej. Is 42:1). Ni mtumishi ambaye alililetea taifa ukombozi kwa njia ya mateso. Hapa, ombi la Petro la kujenga vibanda vitatu linapata jibu. Yeye alitamani wabaki huko juu katika utukufu. Sauti ya Mungu lakini inasema utukufu huo Yesu ataupata. Lakini njia yake ya kuupata utukufu ni ile ya kupitia mateso kama ya mtumishi wa Isaya, yule mwana mpendwa wa Mungu. Kugeuka sura kwa Yesu ni tukio la ufunuo wa juu kabisa wa Yesu katika umungu wake na katika njia yake ya mateso na kifo ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhamni na mauti!

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu ya dominika hii ya pili ya Kwaresima yanatupatia tafakari juu ya imani. Somo la kwanza limemweka mbele yetu Abrahamu, babu yetu wa imani, kwa kile ambacho ni imani tu ingeweza kumsukuma mtu kukifanya: kuwa tayari kumtoa sadaka mwanaye kwa agizo la Mungu. Katika somo la pili, Mtume Paulo ametuonesha kuwa imani sio kitu kinachobaki tu ndani ya yule anayeamini. Imani sio fikra. Imani humuunganisha mtu na Mungu na humjalia anayeamini mafaa yake. Injili sasa imetuonesha kuwa Yesu ndio ufunuo kamili wa yote tunayoamini kuhusu Mungu Baba. Yeye ndio umwilisho wa hazina yetu ya imani. Kumsikiliza Yeye ndio hatua ya kwanza ya kuishika imani. Kwaresima ni kipindi cha kukuza imani. Ametukumbusha pia Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu wa 2021. Ni kipindi cha kujitahidi kuyashinda mashaka ya kiimani. Wakati mwingine sio kwamba hatuna imani. Imani tunayo. Ila inakuwa ni imani inayosongwa na mashaka. Kwa mashaka mashaka ya imani hatuwezi kujiweka moja kwa moja mikononi mwa Mungu ili tuongozwe naye. Tuamini kuwa Mungu akiwa upande wetu hakuna aliye juu yetu. Na huyu ni Mungu ambaye daima yu upande wa wale wanaomwamini na kumtumainia.

Liturujia J2 Kwaresima
26 February 2021, 16:21