Tafuta

Vatican News
Prof. Mario Draghi, Waziri Mkuu Mpya wa Italia, amepongezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI na kwamba, ataendelea kupokea ushirikiano wa dhati kutoka kwa Kanisa katika kutekeleza majukumu yake mapya. Prof. Mario Draghi, Waziri Mkuu Mpya wa Italia, amepongezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI na kwamba, ataendelea kupokea ushirikiano wa dhati kutoka kwa Kanisa katika kutekeleza majukumu yake mapya.  (ANSA)

Prof. Mario Draghi, Waziri Mkuu Mpya wa Italia! Salam za CEI

Profesa Mario Draghi anashika wadhifa huu wakati ambapo nchi ya Italia inakabiliana na changamoto pevu, kama inavyojionesha hata kwa Bara la Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake. Maaskofu wamekuwa wakifuatilia kwa wasiwasi na mashaka makubwa machafuko ya kisiasa baada ya Matteo Renzi “kupindua” meza ya uongozi wa Waziri mkuu wa zamani Giuseppe Conte.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, limemtumia salam na matashi mema Profesa Mario Draghi aliyeapa na kusimikwa rasmi tarehe 13 Februari 2021 kuwa Waziri mkuu mpya wa Italia. Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, Profesa Mario Draghi anashika wadhifa huu kama Waziri mkuu wakati ambapo nchi ya Italia inakabiliana na changamoto pevu, kama inavyojionesha hata kwa Bara la Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, limekuwa likifuatilia kwa wasiwasi na mashaka makubwa machafuko ya kisiasa yaliyopelekea Chama cha “Italia Viva” kinachoongozwa na Matteo Renzi “kupindua” meza ya uongozi wa Waziri mkuu wa zamani Giuseppe Conte.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linatambua kwamba, kuna umuhimu kwa familia ya Mungu nchini Italia kuunganisha nguvu zake, ili kukabiliana na maafa makubwa yaliyosababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hili ni janga ambalo athari zake zimeonekana na kukita mizizi yake katika medani mbalimbali za maisha ya watu wa Mungu nchini Italia. Janga hili limesababisha madhara makubwa katika sekta ya afya, uchumi, elimu na maisha ya kijamii. Limesababisha kuibuka kwa makundi makubwa ya maskini nchini Italia. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwamba, Waziri mkuu Profesa Mario Draghi ataweza kuzivalia njuga na kuzishughulikia kikamilifu changamoto hizi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia zinazoendelea kuteseka; ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa. Maaskofu wanampongeza pia kwa utekelezaji maridhawa wa nyadhifa mbalimbali alizotunukiwa na Jumuiya ya Kimataifa kiasi cha kudhihirisha weledi, nidhamu na uwajibikaji mkubwa.

Maaskofu wanampongeza kwa kuwa na mwelekeo mpana kuhusu siasa za Umoja wa nchi za Ulaya, EU., unaofumbatwa katika misingi ya mshikamano kati ya Mataifa, amani, maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na haki jamii. Kanisa Katoliki nchini Italia, litaendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa pamoja na kutoa ushirikiano wa dhati kama kawaida yake, kwa kuheshimu na kuthamini dhamana na wajibu wa kila upande! Waziri mkuu Profesa Mario Draghi pamoja na Mawaziri wake, wamekula kiapo cha utii mbele ya Rais Sergio Mattarella wa Italia. Itakumbukwa kwamba, Profesa Mario Draghi alizaliwa tarehe 3 Septemba 1947 mjini Roma. Ni mchumi na mwanasiasa mbobezi. Kati ya Mwaka 2011 hadi mwaka 2019 alikuwa ni Rais Benki Kuu ya Ulaya “European Central Bank”. Amewahi pia kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Italia. Tarehe 3 Februari 2021 Rais Sergio Mattarella akampatia dhamana ya kuunda Serikali mpya baada ya Serikali ya Waziri mkuu wa wakati huo Giuseppe Conte kushindwa kuwa na wajumbe waliokuwa wanaunga mkono Serikali yake. Tarehe 13 Februari 2021 akala kiapo cha utii mbele ya Rais Sergio Mattarella wa Italia.

Prof. Mario Draghi

 

 

14 February 2021, 14:42