Tafuta

Vatican News
2021.01.28 kimbunga nchini Msumbiji kiliathiri pakubwa. 2021.01.28 kimbunga nchini Msumbiji kiliathiri pakubwa. 

Msumbiji:Mgogoro wa kibinadamu umezidi kuwa mbaya huko Cabo Delgado!

Askofu Luiz Fernando Lisboa wa Pemba,ambaye,katika mahojiano na shirika Katoliki Ureno liitwalo “Ecclesia”,ameelezea hali mbaya ya wakazi wa eneo hilo.”Kukosekana kwa misaada na msimu wa mvua kunazidisha mzozo wa kibinadamu katika Jimbo la Cabo Delgado,nchini Msumbiji, ambayo tayari imeharibiwa na mzozo mzito ulioanza mnamo 2017.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Kukosekana kwa misaada na msimu wa mvua kunazidisha mzozo wa kibinadamu katika Jimbo la Cabo Delgado, nchini Msumbiji, ambayo tayari imeharibiwa na mzozo mzito ulioanza mnamo 2017 ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu 2,000 na wakimbizi 600,000. Kwa kuongezea, tangu 23 Januari, nchi hiyo ya Afrika imekumbwa na kimbunga Eloise ambacho kimesababisha zaidi ya wakimbizi elfu 260 na karibu waathiriwa 21.

Hayo ni kwa mujibu wa Askofu Luiz Fernando Lisboa wa Pemba, ambaye, katika mahojiano na shirika Katoliki Ureno liitwalo “Ecclesia”, ameelezea hali mbaya ya wakazi wa eneo hilo. “Watu waliokusanyika katika kambi za wakimbizi katika mkoa wa Metuje, karibu kilomita 40 kutoka Pemba, wanaishi katika mahema hatari sana, wakipigwa na mvua na kinapatikana chakula kidogo”. Wakati huo huo, mzozo unaendelea: “Katika siku chache zilizopita amesisitiza Askofu huyo  kumekuwa na mashambulio katika miji ya Palma, Macomia na Nangade”. Kama matokeo, “watu wanaendelea kukimbia kutafuta hifadhi mahali pengine”, na kuifanya  kuzidi kuwa ngumu kupata misaada ya kutosha kwa wote”.

Aidha Askofu huyo amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ukaribu wake na wakazi wa eneo hilo mara kadhaa, na siyo  tu mara ya mwisho ya mkutano na Askofu Lisboa kunako tarehe 18 Desemba ambapo Askofu wa Pemba amebainisha juu ya jitihada za kuwa “sauti inayotumika katika kutetea watu wa Msumbiji”, kwa sababu utume wa Kanisa ni ule wa kutoa sauti kwa wale ambao hawana sauti”. Wakati huo huo, kiongozi huyo ameonesha kwamba hali ya sasa ya mgogoro imelilazimisha Kanisa mahali hapo kujibadilisha ili kutoa matumaini mapya kwa waliokimbia makazi yao, zaidi ya yote kwa sababu, mara tu mzozo utakapoisha, ujenzi wa jumuiya ya wenyeji utahitaji miaka mingi”.

Onyo lalilotoa Askofu Lisboa pia linahusu shida ya kiafya inayosababishwa na janga la Covid-19 na ambayo, hadi sasa, imesababisha visa zaidi ya 38,000 kwa jumla na vifo 367 nchini Msumbiji. Lakini idadi, kwa bahati mbaya, inaongezeka kwa kasi na ni kwa sababu hiyo askofu wa Pemba ametoa wito kwa “usambazaji sawa wa chanjo”, ili kuepusha kwamba isifike barani Afrika tu katika dakika ya mwisho, baada ya kufikia nchi zingine za ulimwengu. Hii haitakuwa sawa” , amehitimisha askofu huyo.

02 February 2021, 15:38