Tafuta

Vatican News
Kwaresima ni safari ya toba na wongofu wa ndani inayofumbatwa katika maisha ya sala, mafungo na tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwaresima ni safari ya toba na wongofu wa ndani inayofumbatwa katika maisha ya sala, mafungo na tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Maana na Umuhimu wa Kipindi cha Kwaresima kwa Mkristo Mamboleo!

Papa Francisko anasema, Kwaresima ni safari inayofumbata maisha ya mtu mzima. Ni mchakato wa kutoka katika utumwa kuelekea katika uhuru wa kweli unaosimika mizizi yake kwa Mwenyezi Mungu. Ni safari ya kumrudia tena Kristo Yesu ili kumshukuru kwa zawadi ya wokovu. Ni safari ya kumrudia Roho Mtakatifu, ili kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, ili kuonja furaha ya kupendwa!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unaonogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Matumaini ni sawa kama na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini. Lengo na shabaha ya chapisho hili sio kusema kwa ukamilifu wake wa kitaalimngu au kihistoria juu ya Kwaresima na maana na umuhimu wake, bali itoshe tu kutupa mwanga kiasi juu ya sababu za kiteolojia na hata kihistoria juu ya siku hizi muhimu za neema za toba yaani Kwaresima. Sitatumia lugha au mifano migumu bali nitajitahidi kusema kwa lugha nyepesi na ya kueleweka na wengi ili tupate japo maana na historia na hata umuhimu wa kipindi hiki cha Kwaresima.

Ni safari ya siku 40 yenye lengo na shabaha ya kutuweka karibu zaidi na Kristo Mfufuka, hivyo kufanana naye zaidi. Kwa kurejea Injili ya Mathayo 28:1, kuhusu kutokea kwake kwa Kristo Mfufuka siku ile ya kwanza ya juma tunaona waamini wale wa mwanzo wanaanza kukusanyika na kusali siku hiyo iliyojulikana awali kama siku ya jua. Na waamini wale wakaanza kuitambua Dominika kama Siku ya Bwana. Ni siku ya Kuumega mkate na pia kuleta pamoja matoleo yao kwa ajili ya ndugu wenye uhitaji kati yao au katika jumuiya ile ya waamini wa Kanisa la Mwanzo. Matendo ya Mitume 20:6-12; 1Wakorintho 16:2; 2Wakorintho 8:9. Hivyo, pale mwanzoni hakukuwa na Sikukuu au sherehe nyingine yeyote zaidi ya makusanyiko yale ya siku ya kwanza ya juma, kama nilivyoeleza hapo juu. Ni baada ya miaka kadhaa kupita ndipo waamini wale wa mwanzo wakaanza kuona uhitaji wa kuwa na adhimisho moja kama kilele cha imani yao. Na hivyo ikaanza Dominika ile ya Pasaka iliyojulikana pia kama Dominika kati ya Dominika au Dominika Mama ya Dominika zote. Ilikuwa kama malkia ya Dominika na sikukuu nyingine zote walizoanza kuadhimisha kwa mwaka mzima.

Ni karne ya pili tunaona sikukuu hii ya Pasaka ikawa imeenea karibu katika jumuiya zote za waamini. Na kilele chake ilikuwa ni mkesha ule wa Pasaka walipokusanyika na kusali na kusikiliza Neno la Mungu usiku mzima, na kuhitimishwa na adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ilikuwa ni muhimu hivi hata tunaona Tertulliani anaandika juu ya ugumu kwa mwanamke mkristo aliyeolewa na mwanaume mpagani kama naye angeweza kupata ruhusa ya kushiriki katika adhimisho hilo adhimu katika maisha ya kanisa. Hivi waamini wale wakaona pia umuhimu wa kufanya maandalizi kabla ya sikukuu ile kubwa ya Pasaka na mwanzoni walitenga siku mbili au tatu kwa ajili ya kusali na kufunga na kuadhimisha pia mateso na kifo chake Mwokozi wetu Yesu Kristo. Ni katika karne ya tatu walianza kufanya matayarisho kwa juma moja na baadaye wakafanya majuma matatu na katika karne ya nne wakaanza kufanya matayarisho kwa siku arobaini. Tunalithibisha hili katika mtaguso wa kiekumene wa Nisea 325 kuwa ilikuwa ni matayarisho ya siku 40 kwa Kanisa zima.

Sherehe za Pasaka hazikupaswa tu kutayarishwa bali pia kuzidi kushiriki furaha ile na utajiri ule wa kiroho. Hivyo ndio ikaanza kusherehekewa siku tu kwa mkesha na mchana ule wa Pasaka bali kwa siku 50 na kuhitimishwa na sherehe ile ya Pentekoste. Mtakatifu Ireneo anatuambia kuwa siku zile 50 zilipaswa kuwa kama siku moja kwa maana furaha ile ya siku ya Pasaka iadhimishwe kwa kiwango kilekile kwa siku zote 50.  Kwa hiyo kwa muda wa siku zote 50 walisali wakisimama maana Kristo mfufuka ameyashinda mauti ni hai, ni mzima na hivyo walisali kwa furaha na katika siku hizi hawakuruhusiwa kufunga bali waliadhimisha sakramenti ya ubatizo, ilikuwa ni shauku yao kuona kuwa furaha ile ya Pasaka inabaki kwa siku hizo 50. Idadi au namba katika Biblia daima lazima kuwa nazo makini kwani zinabeba maana ya kitaalimungu.  Mfano ni ngumu kuamini kuwa Eliya aliweza kutembea kwa siku 40 usiku na mchana mpaka mlima wa Mungu yaani Horebu baada ya kuwa amekula kipande cha mkate na maji. 1Wafalme 19:6-8, au Musa aliyebaki mlima Sinai kwa siku 40 mchana na usiku bila kula wala kunywa, Kutoka 34:28 au Yesu aliyebaki jangwani kwa siku 40 akifunga na kusali. Mathayo 4:2.

Namba 40 inabeba maana ya kitaalimungu zaidi kuliko kuchukuliwa kama muda tunaoweza kuuhesabu kama tunavyoweza kufanya sasa kwa kuupima. Namba 40 inawakilisha kipindi kirefu au muda wote wa maisha. Pia ni muda wa matayarisho kwa ajili ya jambo muhimu na kubwa katika siku za usoni. Mfano mafuriko ya Nuhu yalidumu siku 40, miaka 40 Wanawaisraeli walisafiri jangwani kabla ya kuingia nchi ile ya ahadi, siku 40 watu wa Ninawi walifanya toba ya kufunga, na ndivyo kwa Eliya, Musa na Yesu kwa siku 40. Na ndio Kanisa la awali likaona pia umuhimu wa kutenga siku 40 kama siku za matayarisho kwa ajili ya kilele cha mama ya sikukuu zote yaani Pasaka. Na ndizo siku 40 za mfungo, sala na matendo mema kama matayarisho ya Pasaka yaani Kwaresima. Ni katika kipindi cha Kwaresima tangu awali tunaalikwa kufanya mambo makuu matatu yaani, sala, kufunga na kutenda mema, yote yakiwa na lengo na shabaha ya kufanya toba na mabadiliko ya kweli ya ndani, kubadili vichwa na namna zetu za kutenda na kufikiri, ni kipindi cha kufanya metanoia. Ni kipindi cha neema, cha mageuzi na mapinduzi ya kweli ndani mwetu, katika maisha yetu, katika safari yetu kumwelekea Mungu. Kusali kwa kweli sio tu kusema maneno, bali ni kuingia katika mdahalo na Mungu ili tuweze kufikiri kama Yeye na kutenda kama Yeye. Ni kutaka kufanana na Mungu ili ubinadamu wetu uakisi ukuu wake Mungu.  Chakula changu ni kufanya mapenzi ya yule aliyenituma. Yohana 4:34; 10:30 Yeye na baba ni umoja.

Ni kwa njia ya sala nasi tunaweza kusaidiwa kutoka katika hali zetu za kila siku ambazo mara nyingi zinatupelekea kupoteza kumwangalia Mungu mwenye, kuongea na Mungu mwenyewe. Hivyo kipindi hiki pamoja na kuwa tunasali kila siku na mwaka mzima bali kwa namna ya pekee sasa tutenge zaidi muda wa kuingia katika mdahalo na Mungu na hasa sala binafsi na hata zile za jumuiya. Ni kuingia ndani na kubaki na Mungu ili kuweza kujua hali zetu na hivyo kuomba neema za kufanana zaidi na Mungu na hapo ndipo tunaweza kufanya mabadiliko ya kweli maishani. Yesu alibaki jangwani kwa siku 40 akijaribiwa na yule Shetani, Ibilisi.  Marko 1:12-13. Kwa kweli sio tu anajaribiwa kwa siku 40 bali siku zote za maisha yake na ndicho kinachotokea kwangu mimi na weye. Yule mwovu anabaki kutushawishi kumuasi Mungu sio tu kwa kipindi hiki cha Kwaresma bali siku zote za maisha yetu. Ni mapambano na vita endelevu ila kwa msaada wa kipindi hiki cha neema kila mmoja anaalikwa kuchota nguvu za kupambana na huyo mwovu.

Na ya tatu ni kufunga, ni kwa kumfuasa Bwana na Mwalimu wetu tunaalikwa kujisahau sisi wenyewe na kuachana na ubinafsi wetu kwa ajili ya wengine wanaokuwa wahitaji. Kufunga kwetu hakuna maana bali inakuwa ni kushinda na njaa tu na kiu kama kile tunachojikatalia hakiendi kumsaidia mwingine anayekuwa mhitaji. Funga yetu ni mwaliko wa kuwaza na kutenda kama Mungu ni mwaliko wa kuwa wakarimu zaidi kwa wengine wanaokuwa katika uhitaji. Njaa na kiu haina faida yeyote wala mateso mengine tunayoweza kufanya katika maisha yetu kama hayatuleti karibu zaidi na Mungu kupitia wahitaji. Ni vema kuepuka kishawishi cha kufunga au kusali au kutenda mema kama Mafarisayo kwa kutaka kuonekana na watu au kusifiwa au kutaka kuweka dhamiri zetu kubaki na amani kwa kuwa tunafanya kadiri ya maagizo ya dini au imani. Na ndio tunaona Manabii Isaya na Zakaria wakituonya juu ya mfungo wa kweli. Isaya 58:4-7 na Zakaria 7:5-10

Pia Kanisa lile la mwanzo tunasoma katika Maandiko yajulikanayo kama ya Mchungaji wa Herma akielezea kuwa mfungo unaendana na upendo kwa jirani. Na pia Papa Leo Mkuu (440 – 461BK) anawaalika waamini wa Roma kama askofu wao kukumbuka kuwa kile chakula wanachojinyima na kujikatalia basi hawana budi kuwalisha wenye njaa na kiu. Ni katika karne ya 4 pia Kanisa linaanza kuandaa kwa umakini mkubwa wakatekumeni watakaobatizwa katika Mkesha ule wa Pasaka. Wakatekumeni walipaswa kufuata mafundisho kwa muda mrefu takribani miaka 2 au 3, na hata kuanza kuonesha jinsi ya kuishi na kuenenda kama wakristo, yaani watu wa mwanga. Kwa kweli jumuiya zile za mwanzo waliadhimisha sakramenti ya Ubatizo mara moja tu kwa mwaka yaani katika mkesha ule wa Pasaka. Ni katika mkesha ule waamini wapya walibatizwa na kusikiliza Neno la Mungu na kuhitimishwa na adhimisho la Ekaristi ambapo wale wabatizwa wapya nao walishiriki katika meza ile ya Ekaristi.

Kwa vile Mkesha wa Pasaka ulipambanuliwa pia na maadhimisho ya Sakramenti ya Ubatizo basi na wakatekumeni walifanya maandalizi ya mwisho wakati wa kipindi cha Kwaresima.  Hivi walipaswa kufanya katekesi kwa siku zote 40 na kipindi kile sio walifundiswa na katekista mwingine yeyote bali na Askofu aliye katekista mkuu katika jimbo. Hivi kilikuwa ni kipindi cha kuona kuwa wamekomaa kweli katika imani na katika mafundisho ya Kanisa. Jumatano ya juma la nne la Kwaresima waliweza kuwa na tukio muhimu sana kwa wakatekumeni yaani siku ya mtihani mkuu. Ndio siku waliyofunguliwa masikio, yaani walipokea Kanuni ya Imani na Sala ya Baba Yetu, ambazo zilichukuliwa kama ufupisho wa mafundisho yote ya imani. Wakatekumeni kama watoto wanaotarajiwa kuzaliwa hawana budi kuandaliwa chakula bora kwao na ndio Neno la Mungu. Mama Kanisa kwa namna ya pekee anachagua masomo ya kipindi hiki cha kwaresma kama chakula cha kiroho iwe kwa wakatekumeni na hata waamini wengine wote. Dominika ya kwanza ya Kwaresima daima Injili ni ile ya majaribu ya Yesu jangwani.

Ni mwaliko kutukumbusha kuwa maisha yetu yote hapa duniani tunakuwa majaribuni, hivyo hatuna budi kujifunza kwa Yesu mwenyewe katika kukabiliana na majaribu hayo kwa kwenda jangwani, kwa kusali na kufunga, ili kujiwekea sera na mikakati ya maisha ya kiroho. Dominika ya pili Injili ndio ile ya Kugeuka Yesu Sura pale Mlimani. Ndio maisha ya kumfuasa Yesu yanayotupekea nasi kugeuka na kufanana naye. Lengo la maisha ya kikristo ni kushiriki maisha ya utukufu na umilele mbinguni ambao umefunuliwa na Kristo Yesu katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wake. Utukufu, ukuu na utukufu wa Kristo Yesu vimetundikwa juu ya Msalaba! Dominika ya tatu na kuendelea tunaona wazo kuu linabadilika katika ya mwaka. Dominika ya nne tunaona ni wimbo wa wema wa Mungu na kujipatanisha naye. Dominika ya tano ni mwendelezo wa wazo la Dominika ya 4 juu ya huruma ya Mungu kwetu sote. Katika Dominika ya matawi tunasikia juu ya simulizi ya mateso ya Yesu. Hivyo kwa kumalizia tunaweza kusema kuwa Kwaresma ni kipindi cha toba, kipindi cha kufanya mageuzi au mapinduzi ya kiroho. Katika Kanisa lile la mwanzo wakristo walipofanya madhambi makubwa yaliyojulikana na jamii walitengwa na Kanisa.

Hivyo hawakuruhusiwa hata kuingia Kanisani bali walifika Dominika na kubaki katika malango ya Kanisa. Hivyo hata walipoungama walipaswa kufanya toba kwa muda mrefu na kwa adhabu ambazo zilijukana pia na wengine maana kwa mfano mmoja alipaswa kulima shamba la parokia au kushiriki kazi za ujenzi wa makanisa na mambo kama hayo na wengine walipita na kumuona akitumikia adhabu hizo kama kitubio kabla ya kuingizwa tena katika ushirika kamili wa Kanisa. Baada ya kutubu pia mbele ya Askofu muungamaji alipaswa kuvaa nguo za magunia na kujipaka majivu na kufunga na kusali sana. Ni siku ya Alhamisi Kuu mbele ya Askofu katika adhimisho, waliweza kurudishwa tena katika ushirika na Kanisa. Walifika wakiwa wamevaa nguo za gunia na kujipaka majivu. Ni baadaye katika historia ya Kanisa tunaona aina hii ya kufanya toba imepotea ila tunabaki na mwaliko wa kufanya toba kwa kuungama dhambi zetu kwa kasisi na kutimiza malipizi ya dhambi zetu na kuweka ahadi kama walivyofanya pia waamini wale wa mwanzo wa kubadili maisha yetu na kuenenda kadiri ya amri na maagizo ya Mungu. Nimeona japo kwa haraka haraka tu na kwa ufupi tuweze japo kufahamu historia fupi ya siku hizi za neema za mfungo wa Kwaresima. Tujenge utamaduni wa kuwashirikisha jirani zetu, amana na utajiri wa tafakari ya Neno la Mungu.

24 February 2021, 10:11