Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2021: Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu... " Zab. 95: 7-8. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2021: Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu... " Zab. 95: 7-8. 

Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Kwaresima 2021

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake unaonogeshwa na kauli mbiu “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu …” Zab 95: 7-8. Wanachambua kauli hii katika Maandiko Matakatifu; Wongofu kadiri ya Mababa wa Kanisa na Mamlaka Fundishi ya Kanisa; Madhara ya ugumu wa mioyo ya waamini na hatimaye, nini Wakristo wanapaswa kufanya!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar Es Salaam.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unaonogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake unaonogeshwa na kauli mbiu “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu …” Zab 95: 7-8. Katika sura ya kwanza, Maaskofu wanapembua kauli hii ya “Heri” katika Agano la Kale kwa kuangalia mandhari ya kihistoria; wajibu wa kuambizana na kuonyana kidugu na jinsi Manabii walivyotekeleza dhamana na wajibu wao kwa Waisraeli, kwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba, kwa Mungu kuna rehema na ghadhabu. Maaskofu pia wanaipembua kauli hii mintarafu Agano Jipya: Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji, Mafundisho ya Kristo Yesu pamoja na Mafundisho ya Mitume. Kwa ufupi maonyo yote hayo kutoka katika Maandiko Matakatifu, yaliwataka watu waondokane na mafundisho potofu, wajikite katika mafundisho ya kweli, wawe na busara, wataratibu, wawe timamu katika imani yao, upendo, uvumilivu, wenye kiasi na wenye mwenendo mwema na hatimaye, waweze kuurithi uzima wa milele.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Sura ya Pili linapembua wito wa wongofu kutoka kwa Mababa wa Kanisa na Mamlaka Fundishi ya Kanisa. Sehemu hii inachota amana na utajiri wa Mababa wa Kanisa kwa kukazia: Utakatifu wa maisha, ushuhuda wa imani katika matendo; toba, wongofu wa ndani na msamaha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza upendo kwa Mungu na jirani sanjari na huruma ya Mungu katika ujenzi wa amani. Mtakatifu Paulo VI anawahimiza Wakristo kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa upande wake, Mtakatifu Yohane Paulo II anawakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha kama chachu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Waamini wanahimizwa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, Kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kikamilifu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao katika matendo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Sura ya Tatu linagusia madhara ya ugumu wa mioyo katika maisha ya waamini. Ugumu wa moyo husababisha waamini kujitenga na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Ugumu wa mioyo hautowi nafasi ya wongofu na matokeo yake huzaa ukosefu wa shukrani na nafasi ya msamaha. Ugumu wa nyoyo ni kielelezo ukaidi kwa miongozo ya kiulimwengu. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Sura ya Nne wanagusia umuhimu wa toba, wongofu wa ndani na matendo ta huruma: kiroho na kijamii ndicho kiini cha Kipindi cha Kwaresima. Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaoteseka. Jamii inawahiji viongozi bora, siasa safi pamoja na kuongozwa na Mungu. Waamini wanahimizwa kuisikia sauti ya Mungu, kwa kutambua kwamba, wao ni wadhambi na wanahitaji kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu. Wale wanaoteseka kwa dhambi ya kuchambua dhambi kubwa za watu na wale wanaougua kwa kudekeza dhambi wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili waweze kutakaswa na kuwa weupe pe! “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu…” (Zab 95: 7-8).

UJUMBE KAMILI

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, “Ingekuwa heri msikie sauti yake leo,” ni kauli iliyojikita kwenye ukaidi na utukutu wa wanaoambiwa. Waisraeli walitakiwa walegeze mioyo yao na waambilike; na ndivyo tunavyotakiwa kuwa na sisi. Wao walikuwa Israeli ya zamani, sisi ndiyo Israeli mpya. Wao walikuwa vizazi vya Ibrahimu moja kwa moja (Yn 8:33-47), sisi ni kwa njia ya ubatizo wetu. (Rej. Rum 11:11-32, Efe 3:6). Walioambiwa kwanza wamepita, kumbe, sasa maneno hayo yanatuhusu mimi na wewe. Mwenyezi Mungu aliwatazamia watu wafanye mema ili wapate thawabu; na wala adhabu haikuwa lengo lake la kwanza. Badala yake alipenda watu waache njia zao mbaya wajiokoe na adhabu ya milele. Ndiyo maana hakuacha kuwakanya watu hasa wale aliowaona wanaelekea shimoni, akiwa na lengo la kuwaongoza wote kwenye ufalme wake wa milele. Sauti yake ilijikita katika kuwajenga kiroho, kuwafariji na kuwatia moyo. Kwaresima ni wakati wa kukua na kukomaa kiroho; ni kipindi ambacho mioyo yetu inatakiwa kumtamani Mungu zaidi na zaidi. Ndiyo maana, sisi wachungaji wenu tunawaleteeni ujumbe huu wa Kwaresima kama sehemu ya wajibu wetu wa msingi wa kuwafundisha watu na kuwafanya wamwongokee Mungu wao. Ni sala yetu kuwa katika kipindi hiki tutafanya bidii ya makusudi katika kufanya Mapinduzi ya kiroho, ili tuweze kuepuka nafasi za dhambi, tuondokane na chochote kile kinachoharibu urafiki wetu na Mungu, tukiendelea kuikuza na kuiishi imani yetu na hatimaye tuwe watu waliokomaa na kufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe. (Efe 4:13).

SURA YA KWANZA: Kauli ya Ingekuwa Heri katika Agano la Kale

1. Kusema “ingekuwa heri” inamaanisha kulikuwa bado na fursa ya kuweka mambo sawa. Ilikuwa na maana kuwa kulikuwa bado na fursa ya kusikia sauti ya Mungu na kubadilika. Ilikuwa na maana vile vile kwamba mambo hayakuwa yameharibika kwa kudumu. Kwa namna hiyo, mzaburi alitoa mwaliko kwa Waisraeli kughairi mwelekeo wao wa kutoambilika, mwelekeo wa kusahau ukuu wa Mungu na upendo wake kwao.

2. Shida ilikuwa kwamba, Waisraeli walikuwa na hatia katika dhambi za aina nyingi: wengi walikuwa watukutu, wanavunja Sabato, wengine walikuwa wanawafanyia ukatili wajane na yatima, wafanya biashara walikuwa wanapunja vipimo katika kuuza na kununua, wafalme walianzisha vita ovyo ovyo na kuua watu wasio na hatia, matajiri waliwadhulumu wafanyakazi ujira wao, makuhani walikuwa wananyamazia maovu, matajiri waliwanunua watu hata kwa jozi za makubasi (Amo 8:6), wazinzi walitamba, watu walikuwa wanaoa katika makabila waliyokatazwa, wengine walifanya dhambi za ushoga na ulawiti pasipo haya ya uso, makuhani na manabii walihubiri kwa malipo na tamaa ya pesa (Mika 3:11), wengine walikuwa wanapunja zaka (Mal 4:6-12) na kadhalika. Viongozi walikuwa wanapenda uovu kuliko wema. Wengine walikuwa wazembe katika kuwachunga watu ilivyowapasa; hawakuwajali wagonjwa wala wadhaifu, badala yake walikuwa wanawala wanono (Eze 34:1-31).

Mandhari ya Kihistoria

3. Mandhari ya kauli ya “ingekuwa heri msikie sauti yake” ni kukosekana kwa utambuzi kati ya Waisraeli wakiwa katika nchi ya ahadi. Walikosa utambuzi kwa kukosa kuyatafsiri matukio yaliyotukia kati yao tangu watoke Misri na kuingizwa katika nchi ya asali na maziwa. Kwa kutokujali au kutotafakari mambo yaliyotukia katika historia ya maisha yao; walitakiwa kutambua mambo matano: utawala wa Mungu, kazi za Mungu na nguvu ya Mungu (ndiyo inayoitwa mkono wa Mungu), uhusiano wao na Mungu, mambo aliyowatendea na mambo anayowatendea. Kumbe, walipaswa kuyatambua mambo haya na hivyo kuonesha mambo matano kwa Mungu: imani, matumaini, mapendo, utii na shukrani. Kuonesha mambo haya matano kungekuwa ndiko “kusikia” sauti ya Bwana katika leo yao.

4. Lakini kwa mkasa huo, Zaburi 95 inaorodhesha mambo ambayo Waisraeli walifurahi kuyatambua. Hawakutambua utawala wa Mungu jinsi vina vya dunia vilivyo mkononi mwake, vilele vya milima na bahari, aghalabu, jinsi alivyowaumba watu na kwa jinsi hiyo watu walivyo kundi lake mwenyewe. Hawakutambua kazi ya Mungu, yaani alivyoifanya bahari, alivyoumba nchi kavu na anavyowalisha watu kama kondoo wake. Hawakutambua nguvu ya Mungu, yaani jinsi Mungu alivyokuwa mwamba wa wokovu, Mungu mkuu na Mfalme wa miungu.

5. Mintarafu uhusiano wao na Mungu walipaswa watambue kwamba Mungu ndiye aliyewaumba na wao ndio viumbe wanaowajibika kwake. Walipaswa kutambua waliyotendewa na Mungu kwamba licha ya kuwaumba ndiye aliyewakomboa kwa wema na mkono wa nguvu. Mkono wa nguvu maana yake miujiza mikuu. Hatimaye, hawakuwa wanatambua anayoendelea kuwatendea siku kwa siku, yaani kuwatunza huku akiwalisha kama kondoo wake.

6. Kumbe, Zaburi 95:8 ni masikitiko yanayoelekea kwenye onyo dhidi ya kukosa imani kwa Mungu. Laiti Waisraeli wangelitambua uhusiano wao na Mungu wao, wakatilia maanani waliyotendewa na Mungu sawia na yale anayoendelea kuwatendea, imani yao isingelifanana na watu wa kizazi cha jangwani, kizazi kilichomjaribu Mungu pale jangwani kwenye maji ya Meriba na Masa.

Wajibu wa Kuambizana na Kuonyana

7. Wajibu wa kuambizana vitu na kutaka vifanyike kama ni vya kufanya au kutaka kujiepusha navyo kama vilikuwa vya kuepukwa, ulikuwa ni wa jamii pamoja na manabii (Eze 3:16-21). Jamii zisizosikilizana zilikuwa ni hatari na manabii wasioweza kuonya, kwa niaba ya Mungu walikuwa hasara kamili. Lakini Wayahudi walikuwa wanaonywa siku kwa siku. Mungu mwenyewe alikuwa anawaonya kwa kupitia maono na ndoto na pia alikuwa anawaonya kwa kupitia watumishi wake manabii na wafalme. Lakini bado walikuwa watukutu waliojivunia majaliwa yao ya kuwa taifa tukufu. Aidha, walikuwa na majivuno kwa sababu hekalu, lililokuwa makazi ya Mungu, lilikuwa kati yao. Hata hivyo, manabii hawakuacha kuwakataza wasijivunie uwapo wa hekalu kati yao, badala yake wazishike amri za Bwana kwa imani, matumaini na mapendo. Wayahudi walifanana sana na wanafunzi wanaojivunia kuwa na maktaba wakati hawajifunzi kwa dhati.

Manabii Walionya

8. Licha ya unafiki na utundu wa Waisraeli unaooneshwa mara kwa mara, Mungu hakuchoka kuwatuma manabii kuwaonya Wayahudi kabla ya kupelekwa uhamishoni Babeli, wakati wa uhamisho wenyewe na hata baada ya uhamisho huo (587-538 K.K.).

9. Isaya: Tukijipatia picha katika Isa 58:1-22 mahali ambapo Mungu anamtuma Isaya asiwaonee aibu Waisraeli bali awaambie kweli waachane na uovu wao, wajenge mahusiano mema na Mungu na kati yao wenyewe kwa wenyewe. Mahali hapa tunasoma ifuatavyo: “Mwenyezi Mungu asema: ‘Piga kelele, wala usijizuie, paaza sauti yako kama tarumbeta. Watangazie watu wangu makosa yao, waambie wazawa wa Yakobo dhambi zao. …” (Isa 58:1-22).

10. Yeremia: Nabii anapaza sauti ya kumwongokea Bwana, hasa kwa Taifa la kimasiya huko huko Sayuni, Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema BWANA; maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta Sayuni, nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu (Yer 3:14-15).

11. Baruku: Nabii alitolea sala ya “wahamishwa,” akasisitiza juu ya kuungama dhambi kusudi hekima na thawabu vionekane kwa watu wa Israeli. Tunamsikia akisema, Imekuwaje, ee Israeli, uko katika nchi ya adui zako, ukizeeka katika nchi ya kigeni? Umetiwa najisi na wafu, umehesabiwa nao washukao shimoni?(Bar 3:10-11). Anaendelea kuwaasa akisema, Jipeni moyo, wanangu, na kumlilia Mungu, kwani yeye aliyewaleteeni jambo hilo atawakumbukeni. Kama vile mlivyokusudia kwenda mbali na Mungu, vivyo hivyo rudini na kumtafuta kwa hamu mara kumi zaidi. Hivyo, huyo aliyewaleteeni balaa hizi, atawaokoeni na kuwaleteeni furaha ya kudumu milele(Bar 4:27-28).

12. Ezekieli: Maonyo ya Mwenyezi Mungu yanaendelea kutolewa kupitia kinywa cha nabii Ezekieli akisema, Mwanadamu nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu. Nimwambiapo mtu mbaya, hakika utakufa: wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache na kujiokoa roho yake; mtu yule atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mikononi mwako.”(Ezek 3:17-18).

13. Hosea: Hata kipindi cha Nabii Hosea dhambi ya Israeli iliendelea kushamiri. Hii ilikuwa pamoja na uovu wa makuhani, madhehebu ya Israeli wakawa ni maabudu ya miungu ya uwongo na ufasihi tu. Israeli akawa kama ndama mkaidi. Hapo ndipo maonyo yanatolewa: Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye nafasi! Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. Upepo umemfunikiza kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao”.(Hos 4:16-19).

Kwa Mungu kuna Rehema na Ghadhabu

14. Agano la Kale limeeleza kwa ufasaha kwamba Mungu alikuwa anaweza kusamehe watu walipokuwa watovu wa kumsikiliza na papo hapo alikuwa anawapa fursa ya kujirudi. Sote tunajua jinsi Waisraeli walivyopewa adhabu ya kupelekwa uhamishoni Babeli. (587-538 K.K.). Lakini kwa sababu ya rehema, manabii walikuwa wanatangaza mara kwa mara umuhimu wa kuachana na uovu kwa sababu ya kumpenda “anayewapenda” na hapo hapo kujiepusha na adhabu.

15. Kwa habari hiyo ya huruma, Mungu anayetangazwa kuwa mwingi wa huruma na asiye mwepesi wa hasira (Zab 145:8-13), huwahurumia wanaotubu na katika Agano Jipya ndiye atayeagiza tusameheane saba mara sabini, yaani pasipo kipimo (Mt 18:15-17; 21-35). Uwezo wa kuwasamehe wakosefu anao lakini anataka watu watambue makosa yao na waombe kusamehewa. Ndiyo maana alimsamehe Daudi dhambi ya kumchukua Bathsheba na kumuua Uria, mumewe, kwa sababu alitubu (2 Sam 11:1-27 na Zab 50:1-23) na pia aliwasamehe watu wa Ninawi walioamua kuisikia sauti ya Bwana katika leo yao (Yona 3:1-10)

Kauli ya “Ingekuwa Heri Leo” katika Agano Jipya

16. Kauli ya “Ingekuwa heri leo” haikomei katika Agano la Kale bali inavuka hadi Agano Jipya, lakini kwa mpangilio mwingine wa maneno. Kila aliyetumwa kati ya watu alichukulia suala la kumsikiliza Mungu na kuongoka kama agenda namba moja. Hakika ndivyo walivyofanya viongozi wa kiroho wa enzi za kale. Ushahidi wetu uko bayana kwa hawa wafuatao: Yohane Mbatizaji, Yesu Kristo, Mtume Petro (aliyetoa katekesi siku ya Pentekoste kwa niaba ya mitume na wanafunzi wote wa Yesu) na Mtume Paulo.

Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji

17. Kuhusu ushuhuda wa Yohane Mbatizaji tunasoma, “Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani” (Mk 1:4-5). Kwa namna hii aliwatangazia watu “ingekuwa heri waisikie sauti ya Bwana na kwa bahati njema aliwapata watu waliosikia. Hao walinyoosha njia zao, walifukia mabonde na wakasawazisha vilima vyao; watoto wakageuza mioyo yao kuwaelekea wazazi wao na wazazi wakageuza mioyo yao kuwaelekea watoto wao (Mal 3:23-24, Mt 17:10-13, Mk 1:1-4). Hao waliambilika wakajiokoa na mashoka yaliyowekwa shingoni mwao (Lk 3:1-18, Yn 10:41-42).

Mafundisho ya Yesu Kristo

18. Kuhusu mafundisho ya Yesu Kristo tunasoma, Yohane Mbatizaji alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu akisema, ‘Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema (Mk 1:14-15). Kwa kusema hivi, aliwaambia watu maneno yale yale ya Zab 95:8, “ingekuwa heri leo msikie sauti yake.”

19. Yesu aliyetumwa kuupatanisha ulimwengu na Baba yake alichukua miaka mitatu kupita huko na huko akiwafundisha watu kwa maneno na matendo yake. Kwa taabu hiyo alikusudia kuwaalika watu watubu. Alikusudia waovu waache uovu wao waongoke, lakini wema wadumu katika wema wao. Kwa mifano mingi aliyotoa alinuia wasikilize, wasikie; watazame waone; wafungue macho yao waone; watumie mioyo yao waelewe na kwa namna hiyo wapone (Isa 6:9-10, Mt 13:14-17). Ndipo katika malengo hayo alitamani watu wawe wenye kuambilika na wote walioambilika walimpendeza sana. Ni kwa sababu hiyo Yesu alisema, ndugu zake ni wale wanaolisikia neno lake na kulifanya (Mk 3:31-35).

20. Si hivyo tu, Yesu anamlinganisha mtu anayesikia na kulitenda neno lake, na mtu mwenye busara anayejenga nyumba yake kwenye mwamba; na kinyume chake, na mtu mpumbavu anayejenga nyumba yake kwenye mchanga (Mt 7:24-27). Na kabla ya kutoa mfano huo alisema wote ambao hawatatenda mapenzi yake wataishia pabaya kwani atawakataa ana kwa ana kwamba hakuwafahamu tokea mwanzo (Mt 7:21-23).

21. Tukiongezea, tunaweza kusema kwamba kuna mifano mingi ambayo Yesu aliitoa katika mafundisho yake akilenga watu waambilike wasiifanye mioyo yao migumu. Kwa mfano wa mpanzi, zile mbegu zilizoangukia njiani, mwambani au kwenye miiba ni mlinganisho na watu wasiomakinika na sauti ya Bwana kwa udumifu (Mt 13:1-9,18-30). Ule mfano wa watumishi waliowekeza talanta zao na yule asiyewekeza talanta aliyopewa ni mlinganisho na watu waliosikia na wasiosikia sauti ya bwana wao aliyewaagiza wafanyie biashara mafungu ya pesa aliyowapa (Mt 25:14-30, Lk 19:11-27). Hatimaye, ule mfano wa mtumishi aliyetapanya mali na kuwapiga wajoli wake pasipo kutilia maanani kurudi kwa bwana wake ni mlinganisho na watu wasiosikia na kujali waliyotahadharishwa na bwana wao (Lk 12:35-48).

22. Zile ole kwa miji isiyotubu, zinaashiria wazi kwamba tayari watu walikuwa na shingo ngumu na ugumu wa mioyo wakati wa Bwana wetu Yesu Kristo (Mt 11: 20-24; Lk 10: 13-16). Bwana wetu Yesu Kristo aliendelea kuwakaripia waliotaka miujiza akisema “…Waninawi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona!” (Mt 12:4; rejea pia Lk 11: 29-32). Yesu pia anaendelea kuwalaumu Wafarisayo na wanasheria kwa sababu ya kutoza ushuru kupita kiasi, kuwatwika watu mizigo isiyochukulika n.k. (Mt 23: 1-36; Mk 12: 38-40; Lk 11: 37-53).

23. Katika Injili ya Yohane, Yesu anatamani watu wote wa dunia wangeisikia sauti yake na hivyo kuwa kondoo wanaoisikia sauti yake kama mchungaji wao mwema (Yn 10:27-30). Kwa malengo hayo hayo anatamani sana awapate wote ambao hawajaingia katika kundi lake. Anatamani waisikie sauti yake na wamfuate (Yn 10:16).

Mafundisho ya Mitume

24. Katika Agano Jipya, kauli ya “Ingekuwa heri msikie” haiishii kwenye maneno na mifano ya Yesu bali imeendelezwa na mitume na wafuasi wake. Siku ile ya Pentekoste, Mtume Petro, kwa niaba ya mitume na wafuasi wote aliakisi kwa maneno na matendo yake kauli ya “ingekuwa heri leo”. Aliwaonya watu waigeukie toba na akafaulu kuwabatiza watu elfu tatu kwa mkupuo. Tunasoma ifuatavyo: “Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake, ‘Ndugu zetu, tufanye nini?’ Petro akajibu,’Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile ahadi ya Roho Mtakatifu. …Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao elfu tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo. Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali”. (Mdo 2:37-42).

25. Mtume Paulo naye anatoa maonyo kwa watu wenye mioyo migumu akisema, Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane (Rum 1:18). Kuhusu ukosefu wa uadilifu katika Kanisa, Paulo Mtume anawaasa watu wamfukuze mbali huyo mwovu (rej. 1Kor 5: 1-13). Vile vile tunamsikia Paulo akiwaonya na kuwakaripia Wagalatia waliokengeuka katika imani na sheria akisema, Enyi Wagalatia mmekuwa wajinga kweli!  Ni nani aliyewaloga? (Gal 3: 1).

26. Kwa ufupi maonyo yote hayo kutoka MAANDIKO MATAKATIFU, yaliwataka watu waondokane na mafundisho potofu, wajikite katika mafundisho ya kweli, wawe na busara, wataratibu, wawe timamu katika imani yao, upendo, uvumilivu, wenye kiasi na wenye mwenendo mwema na hatimaye waweze kuurithi uzima wa milele.

SURA YA PILI: Wito wa wongofu kutoka kwa Mababa wa Kanisa na Mamlaka Fundishi ya Kanisa

27. Mababa wa Kanisa tangu Kanisa la mwanzo hadi nyakati zetu, kwa nyakati mbali mbali katika historia ya Kanisa wanapaaza sauti kuwaalika waamini wasikie sauti ya Mungu na wasifanye migumu mioyo yao. Tukifuata mapokeo  hayo mazuri, nasi Maaskofu wenu wakati huu wa Mfungo Mtakatifu wa Kwaresima tunawaalika kusikia sauti ya Mungu, kwa kusoma na kutafakari mialiko hii hapo iliyotolewa na mababa wa Kanisa ambayo hata wakati wetu inafaa ili kumwongokea Mungu na kuenenda katika njia za Bwana.

Mababa wa Kanisa

28. Baba Mtakatifu Klementi I(88-97): Aliwaalika wakristo wamwongokee Mungu akisema “  Basi tuache kwa maumivu na tusihangaike na malimwengu bali tukaribie utukufu  na sheria ya Mungu inayotuita kwa utakatifu”  Aliongeza kuwa ….. “Tuyatafute yaliyo mazuri, yenye kupendeza na yanayokubalika mbele ya Yule aliyetuumba”. Pia aliwaonya Wakorintho akisema, “Muwe watu mnaotafuta amani kwa kumcha Mungu na siyo kutafuta amani kwa unafiki”.

29. Mtakatifu  Polycarpo wa Smyrna (69-155): Katika  barua yake kwa Wafilipi kuhusu uzushi wa  Docetis (fundisho la uzushi kuwa Yesu Kristo hakuwa na mwili wa kawaida bali alikuwa kama mzimu au kivuli) kuhusu kustahimili katika sala na kufunga alisema, “ ambaye haamini katika Kristo kuwa alikuwa na mwili wa binadamu huyu ni mpinga Kristo,  yule asiyekubaliana na ushuhuda wa msalaba ni shetani… Kwa hiyo tuachane na ubatili wa wengi na mafundisho yao potofu, hivyo turudie mafundisho ambayo tumeyapokea kutoka mwanzoni, tukazane kusali, tuwe na juhudi kufunga na kuomba kwa Mungu mweza yote ambaye atatuepusha na vishawishi. Tukumbuke kuwa Bwana alisema “ roho inapenda lakini mwili ni dhaifu”. Anaongeza kusema, “Simama imara kwa yote, fuata mifano ya Bwana, yaani kuwa na msimamo na kutobadilika katika imani, wapende ndugu zenu, shikamaneni nyote na kuunganika katika ukweli, kuweni na busara ndani ya Bwana katika mahusiano yenu na watu wengine na msiwadharau.”

30. Mtakatifu Ignatius wa Antiokia (35-110): Huyu Baba wa Kanisa aliwataka watu wasimame imara katika imani yao na wawasaidie wegine kuishi Ukristo wao. Kwa maneno yake alisema “ Sali pasipo kuchoka kwa niaba ya watu wote; kwa kuwa kuna matumaini ya kutubu na kumwongokea Mungu, kuweni waangalifu kwa kuwa watu wanapata ushuhuda kwenu, kuweni wapole mnapowajibu waliowakasirisha, wanyeyekevu katika kujibu majigambo yao,  jibuni unajisi kwa sala na uasi wao kwa imani;  simama imara katika imani.” Mtakatifu Ignatius anaendelea kusema “Ninawaonya mapema dhidi ya mbwa mwitu watakaokuja kwenye sura ya wanadamu. Inabidi muache kuwapokea na ikibidi msikutane nao. Hivyo waombeeni  ili watubu. Hata hivyo Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ndiye chimbuko la maisha yetu ana nguvu dhidi yao.

31. Mtakatifu Cyprian wa Carthage (Aliyefariki mwaka 258):  Kuhusu kuongoka na kumwelekea Mwenyezi Mungu na kusikia sauti ya Mungu na kutofanya moyo mgumu alisema “ Kwa hiyo  ikiwa mtu ataamua kujirekebisha kutokana na mambo haya na dhambi atajitakatifuza kwa  ajili ya heshima ya Mungu na atakuwa chombo maalum cha Mungu, atafanya kazi yo yote ya Mungu. Zaidi ya hayo akikimbia tamaa za ujana na kufuata njia nzuri, imani, upendo, amani, kwa hayo atasikia sauti ya Mungu katika moyo wake”

32. Mtakatifu Isidore wa Seville (560-636): Aliweka kwenye matendo yale aliyoyafundisha kuhusu kutubu kabla ya kifo chake. Aliwakusanya Wakristo wake akavaa nguo za magunia na akajipaka majivu akaungama dhambi zake na akawaomba msamaha kwa mabaya yote aliyowatendea.

 Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican

33. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya Kidogma juu ya Fumbo la Kanisa inatualika tusikie sauti ya Mungu na tutafute utakatifu wakati wetu, nayo inasema” Bwana Yesu, aliye mwalimu na mfano wa kimungu wa ukamilifu wote, aliwahubiria wanafunzi wake wote na kila mmoja peke yake mwenye hali yoyote, utakatifu wa maisha ambao Yeye mwenyewe ndiye mwanzishaji na mtimilizaji wake, “Ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mt 5:48). Akawapelekea wote Roho Mtakatifu ili awasukume kwa ndani kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa roho yote, kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote (Mk 12:30), na kupendana kama vile Kristo alivyowapenda (Yn 13:34; 15:12).  Sisi Wafuasi wa Kristo tuliitwa na Mungu na siyo tu kadiri ya matendo yetu, bali kadiri ya azimio na neema yake na kuhesabiwa haki katika Bwana Yesu. Katika ubatizo wa imani tulifanywa kweli watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na hivyo watakatifu halisi.

34. Kwa hiyo, yatupasa kwa msaada wa Mungu, kuushika na kuutimiliza katika maisha yetu utakatifu huu tuliopewa. Tunaonywa na mitume tuishi “kama iwastahilivyo watakatifu” (Efe 5:3), na “kwa kuwa tumekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, tujivike moyo wa rehema, utu, wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu” (Kol 3:12), na tuwe na matunda ya Roho ili tufanywe watakatifu (Gal 5:22; Rum 6:22). Kwa kuwa tukijikwaa sisi sote pia katika mambo mengi (Yak 3:2) tunahitaji daima huruma ya Mungu na tunapaswa kusali kila siku, “Utusamehe madeni yetu” (Mt 6:12.).

Mamlaka Fundishi ya Kanisa

35. Pamoja na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kutukumbusha kusikia sauti ya Mungu kwa kutafuta utakatifu, Baba Mtakatifu Paulo VI katika barua yake ya Kichungaji ya Evangelii Nuntiandi imetualika tusikie sauti ya Mungu kwa kutangaza Habari Njema, kushuhudia, kusikiliza na kukubali kubadili maisha kwa sababu ya Habari Njema tuliyoipokea. Baba Mtakatifu Paulo VI kwa maneno yake mwenyewe anasema, “Kanisa wajibu wake ni kuhubiri na kabla ya kuhubiri lazima kwanza lijihubirie lenyewe. Kanisa ni jumuiya ya wahubiri, pia ni jumuiya hai ya matumaini ambayo yanatangazwa, jumuiya ya ndugu wanaoishi kwa upendo. Kanisa linasikiliza bila kuchoka ujumbe ambao linapaswa kuuamini, kutoa sababu ya matumaini na amri mpya ya mapendo. Kanisa ni watu wa Mungu ambao wapo duniani lakini wanajaribiwa na kuamini miungu. Kwa njia hiyo linahitaji kusikiliza kutangazwa matendo makuu ya Mungu ili kumwongokea Mungu, linahitaji mara kwa mara kutiwa nguvu za kuunganika na kuhuishwa tena. Kwa njia hii Kanisa linabidi lihubiriwe tena ikiwa linataka kubakia na nguvu na uhai wa imani[1] “…. Baada ya kuhubiriwa Kanisa linatuma nje watu wa kuhubiri, wanatangaza na kueleza habari njema kutoka kwenye hazina iliyonayo…..”[2]; mwisho jumuiya inayopokea habari njema inakuwa alama ya mabadiliko na maisha mapya.[3]

36. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika barua yake ya Kitume ya Veritatis Spendor anawaita watu wamrudie Mwenyezi Mungu mwanga wa kweli kwa maneno yake mwenyewe anasema “Kristo ni mwanga unaomwangazia kila mtu, watu wote wanaitwa waokoke kupitia imani yao kwa Yesu Kristo, ambaye ni mwanga unaoangazia kila mtu , watu wanapata mwanga kwa Bwana na wanakuwa watoto wa Mwanga (Efe 5:8) na wanafanywa watakatifu kwa kutii ukweli (1Pet1:22). Lakini kutokana na matokeo ya dhambi ya kwanza iliyotendwa kwa sababu ya kudanganywa na shetani ambaye ni mwongo na baba wa uwongo , mwanadamu kila mara anajaribiwa na kuishi mbali na ukweli wa Mungu na kupelekwa kwenye uelekeo na miungu, na kubadilisha ukweli kuwa uongo (Rum1:25).

37. Hivyo, uwezo wa mwanadamu unapungua na kuwekewa giza, na kuanza kutoa tafsiri za kibinafsi na kimashaka. Hivyo anatafuta uhuru usio wa kweli.”[4]  Hata hivyo, Baba Mtakatifu anawaalika wasikie sauti ya Mungu kwa kutafuta ukweli wa Kristo na kwa maneno yake anasema, “Mwanga wa Mungu unang’aa katika uzuri wake katika Kristo, ambaye ni picha ya Mungu asiyeonekana’ (Kol 1:15), pia ni yeye anayeonesha Utukufu wa Mungu (Ebr 1:3), Yeye ni ukamilifu wa neema na ukweli (Yoh 1:14), Kristo ndiye njia, ukweli na uzima (Yoh 14:16). Yeye ndiye mwenye uwezo wa kujibu maswali yote ya mwanadamu ya kidini na kimaadili. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kuwa “Yesu Kristo ni mwanga wa mataifa ambao unaangaza kwenye Kanisa ambalo analituma duniani kutangaza Habari Njema kwa kila kiumbe (Mk 16:15).”[5]

38. Baba Mtakatifu Francisko anatualika kumwongokea Mungu na kuwa watakatifu; katika   barua yake ya Kitume ya   Gaudete et exsultate, anamwalika kila mmoja wetu kuweka juhudi ya kuwa mtakatifu. Anasema kuwa Mungu anamwita kila mmoja wetu kwa maneno haya “Iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu”[6]   (Law 11:44, I Pet 1:16). Baba Mtakatifu anaendelea kusema, “Kuwa mtakatifu siyo lazima uwe Askofu, Padre au Mtawa. Kila mara tunajaribiwa kufikiri kuwa utakatifu ni kutoka katika maisha ya kawaida na kwenda kushinda muda mwingi katika sala.

39. Sisi sote tunaalikwa kuwa watakatifu kwa kuishi maisha yetu kwa upendo na kutoa ushuhuda kwa kila kitu tunachofanya kila sehemu tunapokutwa. Kwa mfano,  kama wewe umeitwa kwenye maisha ya wakfu basi kuwa mtakatifu kwa kuishi maisha hayo kwa furaha na kujitoa zaidi. Kama wewe umeolewa au kuoa, kuwa mtakatifu kwa kumpenda na kumjali mme wako au mke wako kama Kristo alivyo kichwa cha Kanisa.  Kama wewe ni mfanyakazi, fanya kazi yako kwa uaminifu na weledi mkubwa kwa kutoa huduma kwa kaka na dada zako, kama wewe ni  mzazi au bibi, weka juhudi kuwa mtakatifu kwa kuishi na kuwafundisha kwa subira  watoto wadogo wamfuate Kristo, kama wewe  ni kiongozi, tafuta utakatifu kwa kutoa huduma iliyotukuka kwa jamii bila kutafuta mafao binafsi.[7]

40. Baba Mtakatifu Fransisko katika barua ya Kitume Gaudete et exsultate anasisitiza kwamba ili tuwe watakatifu na kupambana na shetani katika maisha yetu inabidi tuishi heri tisa za Mungu, kusali tukiwa na imani, kusoma na kutafakari Neno la Mungu, kushiriki Misa Takatifu, kuabudu Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kuungama, kufanya matendo ya upendo, kushiriki na kuishi maisha ya jumuiya na kushiriki utume wa kimisionari[8].

SURA YA TATU:

Madhara ya Ugumu wa Mioyo katika Maisha yetu

41. Katika Maandiko Matakatifu, moyo huwakilisha hali nzima ya ndani ya mtu – yaani fikira, hisia na utashi. Kama tunavyosoma katika kitabu cha Mithali 4:23 tunaonywa hivi: “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima”. Ni katika msingi huu huu hata katika Liturujia ya Kanisa Katoliki mkristo hujipigapiga kifua kama sehemu ya toba na pia watakaji wa Sakramenti ya Ubatizo hupakwa mafuta ya wakatekumeni kifuani kuashiria kuwa hapo ndipo ulipo moyo - unaomuwakilisha mtu kamili. Ndio maana Maandiko Matakatifu yanakaza kuwa Mungu hutazama moyo wa mtu kwani huko ndiko wema wake hudhihirika: “Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo” (1Sam 16:7); hali kadhalika na ubaya wa mtu: “Kwa maana ndani ya mtu, yaani moyoni mwake, hutoka: mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matusi, kiburi na upumbavu” (Mk 7:21-22). Hivyo, kiimani, mtu mwema huhesabiwa kuwa na moyo safi wakati mwenye moyo mgumu huhusianishwa na ubaya/dhambi na hivi kuleta madhara katika maisha ya mtu na ya wenzake kama tutakavyoainisha katika sehemu hii:

Ugumu wa Moyo husababisha kujitenga na Mwenyezi Mungu

42. Kadiri ya Maandiko Matakatifu, ugumu wa moyo humaanisha kuwa mbali na Mungu, hasa kwa kutolipa nafasi Neno lake. Kimsingi huu ndio wito mahsusi wa Ujumbe huu wa Kwaresima, yaani, hatualikwi tu kulisikia Neno la Mungu bali kulishika na kuliishi. Ugumu wa moyo hautoi nafasi kwa Mungu hata kidogo. Tunapomtazama Mama yetu Bikira Maria, Maandiko yanamshuhudia akiinua moyo wake kumsifu Mungu: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana” (Lk 1:46). Hii hudhihirisha kuwa ni moyo mnyofu tu unaoweza kumsifu Mungu na kusitawi katika maisha ya SALA na si vinginevyo. Kwao wenye moyo mnyofu kumsifu Mungu ni wajibu: “Mpigieni BWANA vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.” (Zab 33:1).

43. Katika nyakati zetu za sasa wako watu wengi ambao kwa ugumu wa mioyo yao wamemnyima Mwenyezi Mungu nafasi katika maisha yao na kujigeuza wao wenyewe na malimwengu kuwa watawala wa maisha yao. Ni hali kama hii ndiyo inazaa hali ya usekulari (secularism) katika jamii yetu, yaani, mfumo wa maisha ambapo Mungu hana nafasi tena. Tunashuhudia watu wengi ambao hawana nafasi tena ya kutega sikio kwa Mungu na Neno lake bali wamevurugwa na kelele nyingi zilizouzingira ulimwengu wa leo. Kwa bahati mbaya wako wengine wengi tu ambao kwa kisingizio cha kutafuta mkate wa kila siku kwa ajili yao na familia zao, wameshindwa kutenga nafasi kwa ajili ya Mungu. Mioyo yao imekuwa migumu na hata imefungwa hivi kwamba hata Mungu mwenyewe anakosa nafasi kwao. Wamesahau kuwa ni kupitia mioyo yetu ndipo tunakutana na Mungu. Tena, Mungu anaongea kwa njia ya Neno lake kwani kila Neno lina pumzi yake (2 Tim 3:16; 2 Pet 1:21). Laiti wangeisikia sauti ya Bwana: “…tazama nasimama mlangoni nabisha…” (Ufu 3:20).

Palipo na Ugumu wa Moyo hakuna Nafasi kwa ajili ya Jirani

44. Ni dhahiri kuwa mtu mwenye moyo mgumu hana kipimo kingine zaidi ya yeye mwenyewe, yaani ametawaliwa zaidi na ubinafsi (ego). Kwa maneno mengine tungeweza kusema moyo wake umefungwa! Kwa mtu wa aina hii shida za mwingine huziona kuwa ni kero kwake kiasi kwamba matendo ya huruma kwa wengine kwake hugeuka na kuwa msalaba usiobebeka. Vivyo hivyo, amri kuu ya upendo sio sehemu ya misamiati yake kwani moyo wake ni baridi.  Mtu wa namna hii, inapomlazimu kumkirimu mhitaji, hufanya hivyo kwa huzuni na manung’uniko kwani moyo wake ni mgumu na sio mkunjufu. Ni katika ukunjufu wa moyo ndipo huzaliwa ukarimu na kumpendeza Mungu kama Mtume Paulo anavyoshuhudia: “Maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2 Kor 9:7).

45. Katika jamii yetu watu wenye mioyo migumu sio haba! Wako watu wengi ambao kutokana na ugumu wa mioyo yao wameishia kujilimbikizia mali na kutowajali masikini na wahitaji. Kwao agizo la Bwana la kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavisha walio uchi kadhalika kuwatazama wagonjwa na wafungwa (Mt 25:31-46) halina nafasi. Dhamiri zao nazo zimekuwa ngumu mithili ya mioyo yao kiasi cha kutoguswa na kilio cha muhitaji. Mbaya zaidi, wako wengine wengi katika jamii zetu ambao si tu wameshindwa kuwa wakarimu kwa wahitaji bali wamefikia hatua ya kuwadhulumu wanyonge hata kile kidogo walicho nacho (rej. 1Fal 21:1-16). Watu wa namna hiyo, wanaalikwa katika Kwaresima hii kufanya mageuzi ya ndani.

Ugumu wa Moyo hautoi Nafasi ya Wongofu

46. Mwenyezi Mungu alimwumba mwanadamu katika hali ya utakatifu kwani vyote alivyokuwa ameviumba vilikuwa ni vyema sana (Mwa 1:31). Lakini kupitia wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva, dhambi iliingia duniani kwa kukosa kwao utii mbele ya Mungu na hivi kila mwanadamu hata leo kuathiriwa na dhambi hii. Mwenyezi Mungu kwa huruma yake alianzisha mpango mahususi wa kumrejesha tena mwanadamu kwake. Daima huo ndio umekuwa mpango wa Mungu kwamba mwanadamu yeyote asipotee (2Pet 3:9) na hata pale anapokengeuka kwa dhambi humpa fursa nyingi za kumuwezesha kurejea kwake. Pamoja na kuwa wongofu wa jumla ulikwishaletwa kwa njia ya mateso na kifo cha Kristo, bado ukombozi binafsi ni jukumu la kila mtu binafsi.

47. Katika jamii zetu za sasa wako watu wengi ambao wameshupaa katika dhambi na hata kuizoea, kiasi cha kupata ugumu sana kuondokana nayo. Mwenyezi Mungu kupitia wajumbe wake wa nyakati zetu hasa Makatekista, Watawa, Mapadre na Maaskofu amewatumia misaada mingi kwa ajili ya wongofu wao bila mafanikio. Ndio hao ambao wamehubiriwa sana juu ya ushiriki katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, kushinda vikwazo vya masakramenti na hasa kuepukana na uchumba sugu, kuhuisha moyo wa sala na kadhalika, lakini bila mafanikio. Mioyo yao ni migumu sana kiasi kwamba haiko tayari kubadilika na kumrudia Mungu. Aidha, wapo ambao japo hawajaasi dini rasmi ila wanaishi maisha ya vuguvugu na hushiriki maisha ya kiimani nusunusu (yaani, shingoni wamevaa rozari huku kiunoni wamevaa hirizi; asubuhi huenda kanisani na jioni huenda kwa waganga wa kienyeji na wapiga ramli). Kwa hawa wote, mwaliko huu wa kipindi hiki cha Kwaresima ni mahususi kwao. Wanaalikwa kugeuza mioyo yao iliyo migumu na kumrudia Bwana.

Ugumu wa Moyo huzaa Ukosefu wa Shukrani:

48. Mtu mwenye moyo mgumu hana shukrani katika maisha yake iwe ni kwa Mungu na hata kwa wanadamu wenzake. Hali hii ilijidhihirisha katika mahusiano baina ya wana wa Israeli na Mungu wao. Pamoja na mema mengi ambayo Mungu aliwafanyia wana wa Israeli katika historia ya maisha yao (mfano kuwapa maji na pia manna kama chakula jangwani (Kut 15:22-25; 16:1nk.) bado wanakosa shukrani na wanapokutana tena na shida ya aina hiyo hiyo wanakosa matumaini kwake na wanaishia kumlalamikia tena Mungu na Musa mtumishi wake (Kut17:18).

49. Hali hii hujitokeza sana katika jamii yetu ya leo. Baadhi yetu tunashindwa kutambua na kuthamini mema mengi ambayo Mwenyezi Mungu anatujalia katika kila siku ya maisha yetu na badala yake tunaishia kuwa watu wa manung’uniko na hata kutangatanga huku na kule kutafuta suluhu ya matatizo yetu nje ya Mungu. Ni vizuri tukakumbuka kuwa, “moyo usio na shukrani hukausha mema yote!” Udhaifu huu hujitokeza pia kati yetu hasa pale tunaposhindwa kuthamini na kuenzi ukarimu wa wengine kwetu na kushindwa kuridhika. Hali hii ndiyo imekuwa ikizaa tabia nyingine mbaya katika jamii zetu kama vile: kukimbilia nguvu za giza (kupiga bao, ramli na uchawi) na hata kuzua machafuko, dhuluma, rushwa, ufisadi, wizi na unyang’anyi kwa lengo tu la kujipatia mali kwa njia zisizofaa ili mradi tufanane na wengine walio na hali njema ya kipato. Wenye moyo wa aina hii wanahitaji tiba ya kiroho.

Palipo na Ugumu wa Moyo hakuna Nafasi kwa Msamaha:

50. Kwa kawaida msamaha ni tunda la upendo na huruma. Mtu mwenye moyo mgumu hana sifa hizi katu na hivyo hawezi kusamehe wala hana unyenyekevu wa kukiri makosa yake na kuomba msamaha, iwe ni kwa Mungu au kwa wanadamu wenzake. Moyo wake umesheheni kisasi, kinyongo, hila, majeraha ya maumivu ya zamani, uhasama, chuki, hasira, kelele, matusi na kila aina ya uovu. Kwa vile moyo wa mtu wa aina hii ni mgumu, ni vigumu kuwa na nafasi ya msamaha - kwani huruma na msamaha hububujika katika moyo mwema kama ambavyo Mtume Paulo anatukumbusha: “Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo” (Efe 4:32).

51. Katika jamii yetu ya leo, iwe ni hapa Tanzania na kokote ulimwenguni, tunu hii ya msamaha bado haijaweza kuota mizizi baina ya watu. Tunashuhudia matukio mengi ya kulipa kisasi na hata watu wengi kuharibu afya zao kwa kushindwa kusamehe. Sehemu nyingine hata amani imepotea kwa sababu ya watu kupenda kulipa kisasi. Kukaa katika meza ya mazungumzo na kumaliza tofauti zetu imekuwa mtihani mgumu kwa watu wengi. Machafuko mengi tunayoyashuhudia kati ya mtu na mtu, jamii na jamii au hata taifa na taifa, ni matokeo ya ugumu wa mioyo unaozaa ukosefu wa msamaha. Inatosha tu kutembelea wodi za majeruhi na hata magereza yaliyotuzunguka na kuushuhudia ukweli huu. Ni vizuri kujifunza kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu na kuchota huko upole, unyenyekevu na msamaha (Mt 11:29). Kadhalika tunaalikwa kuiiga huruma ya Mungu (Lk 6:36).

Katika Ugumu wa Moyo hushamiri pia Ukaidi kwa Miongozo ya kiulimwengu:

52. Mtu mwenye moyo mgumu si rahisi awe raia mwema. Mara nyingi kama sio mara zote, atakwenda kinyume na miongozo na maagizo halali yanayotolewa katika mifumo halali ya kiulimwengu kama vile serikali, uchumi, siasa, jamii na hata wajibu kwa mazingira. Utii kwa mifumo hii huwa kwake ni changamoto kubwa. Mtu mwenye moyo mgumu ni vigumu kwake kutii sheria za nchi na maagizo halali ya watawala; hawezi kutii kanuni zinazoongoza shughuli za kiuchumi badala yake angependa kujinufaisha binafsi kwa kuhujumu uchumi; hawezi kuendesha siasa safi na wala kuheshimu kanuni za kulinda mazingira asilia. Vile inavyokuwa vigumu kwake kumpa Mungu yaliyo yake, kadhalika hawezi kumpa Kaisari yaliyo yake pia (Mk 12:17).

53. Ni ukweli usiopingika kuwa wapo baadhi ya watu ambao kutokana na ugumu wao wa mioyo hufanya maisha ya hapa duniani kuwa magumu kwanza kwao wenyewe kadhalika na kwa wengine. Badala ya kuwa sababu ya furaha na hata kuufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri pa kuishi, wamekuwa chanzo cha mateso mengi. Tunashuhudia watu wengi wanaoenda kinyume na Katiba ya Nchi (sheria mama) na miongozo mingine, wengine wanachangia katika kudhoofisha mifumo ya kiuchumi kwa kuendesha biashara zao bila uadilifu, wapo wanaovuruga mifumo ya kisiasa na kuendesha siasa chafu (zinazofisha haki na kutoheshimu dhamiri na maamuzi ya wengi), kadhalika wapo wanaohatarisha sana usalama wa mazingira – ikiwemo kukata miti ovyo, kuchoma uoto wa asili, kuharibu vyanzo vya maji na hata kuharibu anga la ozoni (ozone layer) na mengineyo. Yote haya ni matokeo ya ugumu wa mioyo. Kwa watu wa aina hii tunawaalika wabadilike na wala wasifanye migumu mioyo yao!

54. Wito msingi wa kila mwanadamu ni kutafuta utakatifu (Mt 5:48). Ili tuweze kufikia lengo hili lazima tudumu katika bidii isiyokoma ya kupambana na dhambi na ubaya wote. Kwa vile dhambi nyingi ni matokeo ya ugumu wa mioyo, yatupasa kuweka jitihada za makusudi katika kuruhusu Sauti ya Mungu iweze kupata nafasi katika mioyo yetu na kutuunda upya. Ni lazima tuwe tayari kufanya mabadiliko ya ndani hasa kwa kubadili mioyo yetu migumu kuwa mioyo safi, kwani ni wale wenye moyo safi ndio watakaomuona Mungu (Mt 5:8).

SURA YA NNE: Tufanyeje basi?

55. Wapendwa Taifa la Mungu na wote wenye mapenzi mema, tafakari yetu hii iliyojikita katika ujumbe wa Mzaburi “Msifanye migumu mioyo yenu…” (Zab 95:8), imetuongoza kuona jinsi mwanadamu anavyofanya ugumu wa moyo katika kuelekea kutimiza mapenzi ya Mungu. Ugumu wa moyo husababisha kufunga milango kwa sauti ya Mungu; ugumu wa moyo vilevile husababisha kufunga milango kwa jirani na mahitaji yake. Ugumu wa moyo unasababisha kufunga milango katika njia ya kuelekea utakatifu. Ugumu wa moyo ni kuacha njia nyofu. Tukitafakari hayo, tunatambua kwamba ugumu wa moyo husababisha kumwacha Mungu kama vile Waisraeli walivyomwacha Mungu kule jangwani na kuanza kushika njia zao na kuabudu miungu ya uwongo. Katika hali hiyo, tunaalikwa kufanya kitu ili kurudisha mioyo yetu kwa Mungu; tunaalikwa kuchukua njia nyingine ya maisha: Njia hiyo ni toba.

56. Toba ndio msingi wa Kwaresima. Hata Jumatano ya Majivu tunakumbushwa hilo kwa kinywa cha Nabii Yoel akisema, “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote…” (Yoel 2:12). Kurarua mioyo ni kuingia ndani ili kujichunguza na kuruhusu moyo usikie sauti ya Mungu. Kurarua mioyo ni kuruhusu kubadilika. Lakini huku kurarua mioyo kunapaswa kuwa katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu: Kijamii, kiroho, kiuchumi, na kisiasa.

Kijamii

57. Mioyo migumu hufunga milango isione mahitaji ya jamii inayoizunguka. Katika jamii ya sasa ni jambo la kawaida kuona wengine wana kila kitu cha kuendesha maisha, mfano chakula, mavazi na malazi; huku tukishuhudia kundi kubwa la wana jamii wakikosa chakula na malazi. Katika Kwaresima hii tunaalikwa tuisikie sauti ya Mungu kwa kuwajali wale wenye mahitaji ambao ndani yao tunakutana na Kristo asemaye, “Nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia”(Mt 25: 35-36). Si rahisi kuisikia sauti hii ya Kristo tukiwa na mioyo migumu kwani mioyo migumu itatusababisha kutenda kile alichotenda tajiri kwa yule maskini Lazaro (Lk 16: 19-31).

58. Jamii inayosikia sauti ya Mungu ni jamii inayoguswa na mateso ya watu wengine, wawe karibu au mbali nao; ni jamii inayoguswa kutenda matendo ya huruma kwa walioachwa pembezoni na jamii. Jamii inayosikia sauti ya Mungu ni jamii inayoishi kwa mapendo na jirani; mapendo ambayo msingi wake ni Mungu mwenyewe. Kwaresima hii inatualika tusifanye migumu mioyo yetu; tuguswe na shida na matatizo ya jamii zinazotuzunguka kuwa kuwatendea kwa huruma na mapendo, ambayo lengo lake ni “Kupunguza kila aina ya dhiki za wanadamu… kama vile kukosa chakula, na kinywaji, mavazi, makao, madawa, kazi na elimu, na vifaa vinavyohitajika ili kuweza kuishi maisha ya kiutu.”[9]

59. Mfungo huu wa Kwaresima utupatie fursa ya kuushinda ubinafsi na uchoyo ambavyo hufanya mioyo yetu kuwa migumu. Mambo haya mawili: ubinafsi na uchoyo huathiri sana jamii yetu ya kitanzania kiasi cha kubadili hata mifumo yetu ya maisha ya kindugu tuliyoizoea. Ubinafsi na uchoyo huathiri hata utendaji wa taasisi zetu mbalimbali kiasi cha kusababisha watendaji kujifikiria wao zaidi ya ufanisi wa huduma walizokabidhiwa. Madhara ya haya yote ni kuzalisha watu wachache wenye nacho na kuacha jamii kubwa ya wasio nacho; na matokeo yake ni kuongezeka kwa umaskini na maskini/fukara katika jamii zetu. Kwa mfungo huu wa Kwaresima tunaalikwa kufanya toba ambayo itatusaidia kubadili hali na misimamo yetu mibovu: kama vile dhuluma na uonevu kwa wanyonge.

Kiuchumi

60. Kati ya matokeo tarajiwa ya Kwaresima ni kubadilika kwa mioyo yenu kuelekea mazingira mazuri ya kiuchumi yenye kujali watu wote. Utendaji mbaya umewafanya wachache kufaidi matunda ya kiuchumi na kuwaacha wengi wakiwa hawana fursa ya kujikwamua kiuchumi. Kwaresima hii inatualika kujiangalia ndani ya mioyo yetu kuona namna tunavyoweza kusikia kilio cha wanyonge wanaoteseka kiuchumi.

61. Kiuchumi, tunaalikwa kujiuliza maswali ya msingi yakiwemo haya: Je, tunazitumiaje mali na raslimali nyingine tulizokabidhiwa na Mwenyezi Mungu kama mawakili wake? Je, tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia huduma za jamii ambazo serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi? Je, wale ambao ni waajiri, tunawajali wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara halali? Je, wale ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali? Je, wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya kodi, ushuru na ada nyingine tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika? Tunaepukanaje na kishawishi cha rushwa, hongo, takrima, mulungula, magendo au aina nyingine yoyote ya ufisadi?

62. Jibu la changamoto zote hizi ni fadhila ya ukarimu ambao kimsingi “Ni tabia ya kiutu na asili yake ni upendo wa Mungu unaowavuta watu wote kwake bila ubaguzi.”[10] Ukarimu huu hutusukuma kuwakarimu majirani zetu wahitaji kama vile wagonjwa, wazee, watoto yatima, wajane, wageni na wakimbizi. Ni ukarimu ule wa Msamaria mwema (Lk 10: 29-37) unaoshinda tofauti za kiukoo, kikabila na hata kitaifa.

Kisiasa

63. Kati ya maeneo muhimu sana ya kipimo cha uongozi bora na siasa safi ni namna kiongozi anavyoishi uadilifu wake wa uongozi tukitambua kwamba “Hakuna mamlaka (halali) isiyotoka kwa Mungu” (Rum 13:1). Kutokana na hilo, uongozi, madaraka au mamlaka yoyote ile inapaswa kuwa ni dhamana kutoka kwa Mungu. Dhamana hii anapewa kiongozi kama mwakilishi wa Mungu katika uongozi tukitambua kwamba Mungu ndiye kiongozi na mtawala pekee. Dhamana hii inapaswa kumkumbusha kiongozi kwamba mamlaka aliyopewa si kwa ajili yake bali ni kwa ajili ya wote aliokabidhiwa.

64. Licha ya hayo yote mema ambayo wenye mamlaka hususani ya kisiasa wamekabidhiwa, nyakati zetu hizi dunia imeshuhudia manung’uniko na malalamiko kutoka kwa umma kwamba baadhi ya viongozi wanatumia dhamana hiyo kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe au kwa ajili ya manufaa ya kikundi fulani. Siasa za namna hiyo husababisha unyanyasaji wa baadhi ya watu au kikundi cha watu na hivyo kuondoa hali ya kuaminiana.

65. Mipasuko ya kisiasa ndani ya jamii huweza kutokea kwa sababu ya kikundi fulani kujiona bora kuliko kingine na wakati mwingine kujiona kiko juu ya Katiba na Sheria mbalimbali za nchi. Matokeo ya haya yote ni kufarakana kijamii, lawama zisizoisha na hivyo kuhatarisha amani na usalama wa jamii husika.

66. Ujumbe wa Kwaresima unatutaka kama jamii “Tusikie sauti yake, tusifanye migumu mioyo yetu.” Tutaisikia sauti ya Mungu kwa kuhakikisha kwamba haki inatendeka katika jamii, na hasa haki za kikatiba za kujiendesha kisiasa zikiwemo kuheshimu uhuru wa mawazo mbadala, kama sehemu ya kudumisha demokrasia na hasa katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Kiroho: Sote tunaalikwa tusikie Sauti ya Bwana Leo

67. Wapendwa wana familia ya Mungu, hakuna haja ya kusakamana kwa kuwa wote tu wagonjwa mintarafu maisha ya kiroho. Wanadamu tuna magonjwa matatu ya ajabu! Kuna watu wanaougua tatizo la kutojisikia wana dhambi. Kuna watu wanaougua ugonjwa wa kuchambua dhambi kubwa za wenzao na wao kujisikia salama kwa sababu wana dhambi ndogo ndogo. Na hatimaye kuna watu wanaougua ugonjwa wa kujadiliana na kudekeza dhambi zao.

68. Wanaougua ugonjwa wa kutojisikia wana dhambi, wanaishi maisha ya hatari na yasiyo ya ukweli. Ukweli ni kwamba kila mmoja anatenda dhambi na anayedhani hana dhambi anajidanganya mwenyewe na kumfanya Mungu mwongo (1Yoh 1:8-10). Ni heri sana kila mtu ajisikie ana dhambi na hivyo afanye jitihada ya kusikia sauti ya Bwana na kuungama. Waamini wote, makleri, watawa kwa walei, tuna dhambi zetu za maneno, matendo, mawazo na kutotimiza wajibu. Kama tukiwa watukanaji na wasema ovyo, tunakosea kwa maneno. Tukiwa wakatili, mafisadi, wauaji, waasherati na kadhalika, tunafanya dhambi kwa matendo. Tukiwa tunawaza mambo machafu tunatenda dhambi kimawazo. Kama hatutendi yaliyotupasa, tunatenda dhambi za kutotimiza wajibu. Kumbe, tukinyamazia maovu na eti “kupotezea” tunanaswa katika dhambi ya kutotimiza wajibu (Eze 3:16-21, 1Tim 4:11-16, 2Tim 4:1-5).

69. Dhambi zinatendeka duniani na sisi tunaishi na wenzetu duniani pia. Yesu hakuwatengenezea wafuasi wake ulimwengu wa peke yao. Kumbe, si kweli kwamba watenda dhambi ni watu wasio Wakristo au wasio Wakatoliki peke yao. Yakitangazwa majina ya majambazi au wahalifu, majina ya Wakristo huwapo pia. Kama tunalalamika kuhusu uovu duniani, inamaanisha na sisi Wakristo, na hata sisi Wakatoliki, tupo ndani. Katika nchi hii na dunia hii, wanazuia mimba kwa njia haramu, na sisi tumo ndani. Kama katika nchi hii na dunia hii, kuna watu wanawaua wenzao kwa ulimi na hata kwa Upanga nk., na sisi tumo ndani.

70. Kama katika nchi hii na dunia hii, vikongwe wanauawa kwa tuhuma za uchawi, watu wanahujumu mali za umma kwa ufisadi, kuna wanaosali ovyo ovyo, watu wasiomwabudu Mungu, watu waongo; viongozi wanaoacha kuhubiri neno la Mungu na badala yake kujitafutia pesa, umaarufu na vyeo kwa kufanya miujiza feki, si ajabu na sisi tumo ndani. Wahubiri wanapoacha “kuwajenga watu” na kuhangaikia miradi ya vitu, viongozi wanaofumbia macho maovu na dhuluma katika jamii wakitafuta kuwapendeza wakuu, si ajabu na sisi tunakumbwa na dhambi hiyo.

71. Kama kuna watu wanaoacha Sakramenti mbalimbali zikiwemo kati yake Ekaristi Takatifu na Kitubio, watu wanaoweka ahadi na nadhiri na kuzivunja, watu wadhalimu, viongozi wabaya wanaojali matumbo yao na ya ndugu na jamaa zao tu, si ajabu na sisi tumo ndani. Kama katika nchi hii na dunia hii, kuna watu wanaopeana vyeo kwa kupendeleana, kikabila, kikanda na kiitikadi, na sisi tumo ndani. Kama katika nchi hii na dunia hii, kuna watu hawatoi zaka na sadaka kwa uaminifu, na sisi tumo ndani. Kama katika nchi hii na dunia hii, kuna watu hawawapendi wenzao bali wanawachukia na kuwafanyia kisasi; kama kuna watu wanaomnung’unikia sana Mungu na watovu wa shukrani, si ajabu na sisi tumo ndani.

72. Ni kwa sababu hii, tukijitambua tulivyo wahanga wa dhambi, kila tunaposali sala ya Nakuungamia, kila mmoja wetu, toka aliye katika cheo kikubwa kanisani hadi mlei mdogo wetu, anapaswa kugonga kifua chake mwenyewe mara tatu. Ndiyo kisa Wakatoliki hatujiiti “tuliokoka” kwa vile hatujamalizana bado na dhambi. Hatujidanganyi dhidi ya ukweli kwamba tu wadhambi (1Yoh 1:8-10). Tunatambua tunapaswa kukabiliana na dhambi siku kwa siku mpaka tutakapokufa. Kwalo tunapaswa kujihimiza katika jitihada za kujiongoa kila uchao (metanoia) kusudi roho zetu zisilemewe na dhambi za anasa, ulevi na shughuli za maisha haya (Lk 21:34-36). Na hii ndiyo maana ya kukesha aliyolenga Kristo, yaani wala si suala la kukaa macho pasipo kulala usiku.

73. Ugonjwa wa pili ni ule wa wanaougua dhambi ya kuchambua dhambi kubwa za watu, wanaishi maisha ya kujisahau. Lakini, ukubwa wa dhambi ya fulani, haupunguzi makali ya dhambi ya mwingine. Kila mtu anapaswa kuziona na kuzichukulia hatua dhambi zake mwenyewe. Tunapitana katika kutenda dhambi kwa sababu moja tu, “Kila mbuzi anakula kwa kadiri ya urefu wa kamba yake.” Katika wizi, anayekutana na mafungu makubwa huiba mafungu makubwa. Katika ulevi, anayekutana na pombe nyingi, hulewa sana. Katika ufisadi, anayekutana na mitego mikubwa ya ufisadi, anafisadi makubwa. Katika uzinzi na uasherari, anayekutana akina mama au akina baba wengi kwa nafasi kubwa anazini zaidi. Kumbe, kwa namna hii, tupo wengine wenye utakatifu feki kwa vile tu hatujakutana na fursa zenyewe za kutenda dhambi. Yaani, kwa mfano, wengine tunaonekana si wezi kwa sababu tu, bali hatujakutana na vitu vyenyewe vya kuiba.

74. Ugonjwa wetu wa tatu unahusu wale wanaougua ugonjwa wa kudekeza dhambi. Yaani wao wameshagundua dhambi zao, lakini wanajihurumia. Wanasitasita kujibandua nazo kwa milele. Wapo wanaokaa uchumba sugu, wanaosita kujibandua. Wapo wezi wanaosita kuacha mchezo huo. Wapo waasherati na wazinzi wanaositasita kujitoa kwenye tatizo hilo. Lakini dawa ya dhambi ni moja tu, kutubu.

Tumeachiwa Sakramenti ya Upatanisho- itusaidie kiroho

75. Ikiwa kwa ujumbe huu wa Kwaresima tumegundua dhambi zetu, tusikate tamaa maana kuna habari njema kwetu. Yesu alisema hakuja duniani kutupoteza, bali kama tabibu, Yesu aliwajia hasa wagonjwa (Lk 15:1-32). Kazi ya kuwapoteza watu si yake bali ya adui Shetani. Yeye anaeleza anataka kutupatia uzima, tena uzima tele (Yn 10:10). Uzima tele si hasa kwa hapa duniani ila hasa mbinguni alikotutangulia.

76. Hapa duniani tunaweza kuwa tunaumwa na kuingizwa kwenye majaribu, masumbuko na mitihani mbalimbali. Tuhimili na wala tusivunjike moyo kwa sababu hayo yapo duniani na yeye alishayashinda maumivu na kifo kwa niaba yetu (Yn 16:33). Amesema furaha yake itakuwa na sisi tukiwapo pale alipo. Tunasoma alivyosema, “Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atamheshimu” (Yn 12:26).

77. Yesu aliiweka Sakramenti ya Kitubio au Upatanisho kusudi tunayoyakosea tuwe tunayafuta na kuanza upya kiasi hiki kwamba siku ya mwisho hata ikija ghafla isitukute tumesimamia mguu wa kushoto. Kwa maana hii, kati ya maneno ya Mungu tunayoalikwa kuyasikia leo ni kufanya toba pasipo kuvuta vuta miguu. Mzee Yoshua bin Sira anatuambia: “Usiseme, ‘Nimetenda dhambi lakini nimepata balaa gani? ’Usitegemee kupata msamaha hata kuongeza dhambi juu ya dhambi. Usiseme, ‘Huruma yake ni kubwa, yeye atanisamehe dhambi zangu nyingi’. Kumbuka, yeye ana huruma na ghadhabu na hasira yake huwakumba wenye dhambi. Usichelewe kumrudia Bwana wala usighairishe kurudi siku hata siku. Maana ghadhabu ya Bwana itakuwakia ghafla na wakati wa hukumu utaangamia” (YbS 5:4-7).

78. Na katika YbS 21:1-3 tunasoma, “Mwanangu, je, umetenda dhambi? Usitende tena. Lakini omba msamaha kwa yale uliyotenda. Ikimbie dhambi kama kumkimbia nyoka, maana ukimsogelea nyoka utaumwa. Meno ya dhambi ni kama simba. Dhambi hufisha maisha ya watu. Uvunjaji sheria ni kama panga kali kuwili, ukimjeruhi, mtu hawezi kutibiwa na kupona.”

79. Habari njema, kwetu sisi sote tulio wadhambi, ni kwamba dhambi zetu zote, isipokuwa ile ya kumkufuru Roho Mtakatifu zinaondoleka ilimradi tuuvae ushujaa wa kuziungama. Tunaambiwa, “Mwenyezi Mungu asema hivi: Njoni, basi, tuzungumzane, hata kama dhambi zenu ni nyekundu kama bendera, mtatakaswa na kuwa weupe kama theluji, madoa yenu yajapokuwa mekundu kama damu, mtakuwa weupe kama sufu. Mkiwa tayari kunitii, mtakula mazao mema ya nchi. Lakini mkikaidi na kuniasi, mtaangamizwa kwa upanga. Mimi, Mwenyezi Mungu nimesema” (Isa 1:18:20).

HITIMISHO

80. “Msikie Sauti yake, msifanye migumu Mioyo yenu” ni wito wa toba. Ni sauti ya toba inayomtaka kila mmoja amrudie Mungu kwa kuufanya moyo wake laini ili kupokea ujumbe wa Mungu. Ni toba inayotupelekea kukiri kwamba tu wakosefu; ni toba inayotupelekea kukiri kwamba tunahitaji kupatanishwa na Mungu. Ni toba ile waliyoambiwa makundi mbalimbali yaliyomwendea Yohane Mbatizaji wakiuliza: “Tufanye nini basi? Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.” Nao watoza ushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, “Mwalimu, tufanye nini?” Naye akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa. ”Nao askari wakamwuliza, “Na sisi tufanye nini?”Naye akawajibu, “Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uwongo.Toshekeni na mishahara yenu.” (Lk 3: 10-14).

81. Tunapoalikwa kutokufanya migumu mioyo yetu ni ishara kwamba tumeiacha sauti ya Mungu na hivyo tumeacha kufanya mapenzi yake. Wito wa toba unatualika kukiri kwamba tumekosa na hivyo kuahidi kubadili maisha na kuanza kuishi kadiri ya wito wa Kwaresima kwa kufunga, kusali na kutenda mema (moyo wa sadaka) kama sehemu ya kuisikia sauti ya Mungu. Toba hii itusaidie kuona wenzetu wanaohitaji msaada kama vile wagonjwa na makundi mengine ya wahitaji.

82. Ingekuwa heri leo tuisikie sauti ya Bwana tusifanye migumu mioyo yetu kama Mzaburi anavyotuasa (Zab 95:7-8). Kwa mazuri tuliyoambiana, tukawajibike; kwa maovu tuliyotahadharishana, tukaongoke. Kinyume cha hapo, kiburi chetu kitatufikisha pabaya sana. Kwa sababu ya ubatizo wetu, na fursa ya Maandiko Matakatifu tuliyopewa, na fursa ya mifano ya kimapokeo tuliyo nayo, na fursa ya masomo ya kihistoria tuliyo nayo, na uwezo wetu wa kuyasoma mazingira yanayotuzunguka, sisi Wakatoliki tukikosea tutapigwa zaidi kuliko watu wa dini na makanisa mengine.

83. Sababu ya kupigwa kwetu zaidi imeandikwa katika Lk 12:48 ifuatavyo: “Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana. Lakini yule ayafanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atadaiwa vingi, aliyepewa vingi zaidi atadaiwa vingi zaidi.”

84. Kwa vyovyote kufanya uzembe, kuzembea sauti ya Bwana katika leo yetu au kufanya kiburi kubishia sauti ya Bwana katika leo yetu ni HATIA kwa kila mmoja, kila mmoja kwa kadiri ya nafasi yake.   Hii ni Kwaresma na huu ni ujumbe wa Kwaresima, kwa hiyo mwito wa kuungama dhambi zetu ndio huo tena. Pamoja na kualikana kwetu kwenye kusali, kufunga na kuwasaidia maskini, tufanyeni toba. Tutubu na kuiamini Injili. Kwa sababu hiyo, INGEKUWA HERI LEO WOTE TUKIISIKIA SAUTI YA BWANA, TUSIFANYE MIGUMU MIOYO YETU (Zab 95:8)!

85. Tunawatakia Kwaresima njema. Ituzalie matunda ya kufufuka na Kristo na kutafuta yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu (Kol 3:1-4).

Ni sisi Maaskofu wenu,

1.     Mhashamu Askofu  Mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu, Mbeya

2.     Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Geita

3.     Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka,  Tabora

4.     Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi,  Ofm Cap, Dar es Salaam

5.     Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya,  Ofm Cap, Dodoma

6.     Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu, Songea

7.     Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, Arusha

8.     Mhashamu Askofu  Mkuu Renatus Nkwande, Mwanza

9.     Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Iringa

10. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani,  Lindi

11. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo,  Mahenge

12. Mhashamu Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar

13. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara

14. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma,  Bukoba

15. Mhashamu Askofu Method Kilaini,Bukoba (Askofu Msaidizi)

16. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS, Moshi

17. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe

18. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila,  Musoma

19. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga

20. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same

21. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Mpanda

22. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara

23. Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa

24. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga

25. Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Mtwara

26. Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS, Kigoma

27. Mhashamu Askofu Prosper Lyimo, (Askofu Msaidizi), Arusha

28. Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Shinyanga

29. Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Singida

30. Mhashamu Askofu Beatus Urassa, Sumbawanga

31. Mhashamu Askofu Antony Lagwen, Mbulu

32. Mhashamu Askofu Filbert Mhasi, Tunduru-Masasi

33. Mheshimiwa Msgr. Lazarus Msimbe, Msimamizi wa Kitume,  Morogoro

 

[1] Paul VI, Evangelii Nuntiandi,  Apostolic Exhortation  of His Holiness  Pope Paul VI no.15

[2] Ibid 15

[3] Ibid 23

[4]  Ioannes Paulus P. II,  Veritatis Splendor no.1

[5] Ibid no.2

[6]  Francis, Barua ya Kitume ya  “Gaudete et Exsultate” no.10

[7] Ibid,no.14

[8] Ibid, no162

[9] Hati za Mtaguso Mkuu wa Vatikano II: Utume wa Walei, 8.

[10]Hati za Mtaguso Mkuu wa Vatikano II: Mwanga wa Mataifa, 16.

Kwaresima 2021
25 February 2021, 11:11