Tafuta

2020.04.10 Askofu Moses Hamungole wa jimbo la Monze,Zambia 2020.04.10 Askofu Moses Hamungole wa jimbo la Monze,Zambia 

Zambia:Askofu Moses Hamungole wa jimbo la Monze ameaga dunia

Kanisa nchini Zambia linaomboleza kifo cha Askofu Moses Hamungole wa Jimbo la Monze aliyeaga dunia tarehe 13 Januari 2021,baada ya kuambukizwa na Covid-19.Kabla ya kuchaguliwa kwake kuwa Askofu wa jimbo hilo alikuwa mkurugenzi wa Idhaa ya Kiingereza Afrika na Kiswahili,Radio Vatican.

Na Sr. Angela Rwezaula,-Vatican

Kanisa katoliki nchini Zambia wanasikitika na kuomboleza kuondokewa na Askofu Moses Hamungole, wa jimbo katoliki la Monze  nchini humo, ambaye amefariki tarehe 13 Januari 2021 kutokana na tatizo la maambukizi ya gonjwa la virusi vya Corona au Covid-19. Askofu alikuwa na umri wa miaka 53 na ambaye hivi karibuni alikuwa amelazwa katika Hospitali ya “Levy Mwanawasa” ya  Lusaka. Hivi karibuni Askofu Moses alikuwa ametangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook kuhusu maambukizi hayo akiwa na tumaini na imani ya kuweza kushinda gonjwa hili baya huku akiwashukuru waamini kwa sala zao na kuwashauri waendelea kufuata kanuni zote za kuzuia maambukizi.

Kwa ghafla hali yake ya afya ilizidi kuwa mbaya na kufariki. Ni Askofu wa kwanza mkatoliki kuambukizwa na virusi vya corona nchini Zambia, mahali ambapo hadi sasa, Covid-19 imekwisha ambukiza watu zaidi ya 31elfu na zaidi ya vifo 500. Hadi kumfikia mauti Askofu Hamungole alikuwa ni Rais wa Tume ya Mawasiliano kijamaii ya Baraza la Maaskofu nchini Zambia. Na kabla ya kuchaguliwa kuwa Askofu alikuwa ni mkurugenzi wa Idhaa ya Kiingereza- Afrika na Kiswahili ya Radio Vatican.

Askofu Hamungole alizaliwa tarehe Mei Mosi  1967 huko Kafue, karibu na Lusaka. Alijiunga na Sminari ndogo ya Mukasa na kuendelea na mchakato wa kawaida wa maandalizi ya ukuhani katika Seminari ya Kifalsafa ya Mtakatifu Augustine na Seminari ya Taalimungu ya Mtakatifu Dominiki ya Lusaka. Alipewa daraja la ukuhani tarehe 6 Agosti 1994 na kuwekwa katika Jimbo Kuu la Lusaka mahali ambapo pia alikuwa amepewa majukumu. Mingoni mwa hayo ni kama Mkurugenzi wa Radio Yatsani na Ofisi ya Mawasiliano ya Jimbo Kuu la Lusaka (1997-1999).

Kuanzia mwanzoni wa mwaka 2000 aliendelea na masomo ya juu kwa ajili ya Mawasiliano kijamii katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriana, Roma. Badaye kuanzia 2002 hadi 2008 alikuwa Katibu wa Mawasiliano ya AMECEA(Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki)yenye makao yake makuu Nairobi, Kenya, na wakati huo huo kuanzisha 2002 hadi 2009 alikuwa anaongoza pia SIGNIS-Africa katika nafasi ya urais. Mnamno mwaka 2010 alikuwa ni mkurugenzi wa Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatican. Kuteuliwa kwake kuwa Askofu wa Monze kuliwadia mnamo tarehe 10 Februari 2014 na tarehe 3 Mei mwaka huo huo aliwekwa wakfu wa kiaskofu.

14 January 2021, 10:47