Tafuta

Vatican News
Viongozi wa Kidini wasema: Kuvamiwa kwa Makao makuu ya Bunge la Marekani ni fedheha kubwa katika mchakato wa demokrasia na ushuhuda wa siasa na sera za kibaguzi zinazoipekenya Marekani. Viongozi wa Kidini wasema: Kuvamiwa kwa Makao makuu ya Bunge la Marekani ni fedheha kubwa katika mchakato wa demokrasia na ushuhuda wa siasa na sera za kibaguzi zinazoipekenya Marekani.  (ANSA)

Uvamizi wa Bunge la Marekani ni Fedheha kwa Demokrasia!

Wafuasi wa Rais Trump kuvamia Bunge ni fedheha kubwa katika mchakato mzima wa demokrasia, kwa kuzingatia kwamba, Marekani mara nyingi imekuwa ikijipambanua kuwa ni mlinzi wa haki, amani, demokrasia na utawala wa sheria sehemu mbalimbali za dunia. Lakini uvamizi huu umetia doa kubwa katika demokrasia ya Marekani katika ujumla wake. Ni matokeo ya sera za kibaguzi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linaungana na watu wote wenye mapenzi mema kulaani vikali, kitendo cha wafuasi wa Rais Donald Trump wa Marekani anayemaliza muda wake cha kuvamia Makao makuu ya Bunge la Marekani hapo tarehe 6 Januari 2021, ili kubadili matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika tarehe 3 Novemba 2020 na kumpatia ushindi Joe Biden, huku Rais Donald Trump akiwa amepigwa na butwaa kwa madai ya kuibiwa kura!  Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika ujumbe uliondikwa na Askofu mkuu Josè H. Gomez wa Jimbo kuu la Los Angeles, unabainisha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Marekani linaendelea kusali na kuwaombea wale wote waliojeruhiwa na kwamba, jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama, zifanikiwe kurejesha: amani, usalama na utulivu.

Takwimu zilizotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini Marekani zinaonesha kwamba, katika uvamizi huo, watu 4 wamepoteza maisha, Polisi 14 na wananchi kadhaa wamejeruhiwa vibaya na hivyo wamelazwa hospitalini. Kuna watu 52 ambao wanashikiliwa na Polisi katika tuhuma hizo! Hali ya hatari imetangazwa kwa muda wa siku 15 hadi Rais mteule Joe Biden atapokula kiapo na kuanza kutawala rasmi kama Rais wa Marekani. Rais Donald Trump anayemaliza muda wake wa uongozi amesema tarehe 20 Januari 2021 makabidhiano ya uongozi, yatakwenda kadiri ya taratibu za nchi, ingawa hakubaliani kamwe na matokeo ya uchaguzi. Huu ni mwanzo wa mapambano, ili kuiwezesha Marekani kuwa Taifa Kubwa Tena. “Make Amerika Great Again”.

Mchakato wa kubadilishana uongozi ni kati ya matukio makubwa nchini Marekani. Katika kipindi hiki cha machafuko makubwa ya kisiasa, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Marekani kujielekeza na kujikita katika kanuni, sheria na taratibu za nchi kama kielelezo makini cha demokrasia, ili kuendelea kuwa wamoja kama Taifa nchini ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Wafuasi wa Rais Trump kuvamia Bunge ni fedheha kubwa katika mchakato mzima wa demokrasia, kwa kuzingatia kwamba, Marekani mara nyingi imekuwa ikijipambanua kuwa ni mlinzi wa haki, amani, demokrasia na utawala wa sheria sehemu mbalimbali za dunia. Lakini uvamizi huu umetia doa kubwa katika demokrasia ya Marekani katika ujumla wake.

Makao makuu ya Bunge la Marekani anasema Kardinali Wilton Gregory, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington, DC., yamekuwa ni mahali muafaka wa kuwasilisha maoni mbalimbali ya wananchi; mahali pa kutungia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Kitendo hiki hakiwezi kuvumiliwa hata kidogo, kwa sababu kuna watu wamepoteza maisha, wengine kujeruhiwa na nyaraka mbalimbali kuharibiwa. Huu ni wakati wa kubadili lugha ya ubaguzi inayosababisha mipasuko ya kijamii, uvunjaji wa sheria na haki msingi za binadamu. Wamarekani wanahamasishwa kuwa ni watu wanaoheshimu na kuthamini tunu msingi za kidemokrasia, kwa kuheshimu mawazo ya watu wengine na hata kama hawakubaliani nayo! Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, badala ya kuendelea kujimwambafai kama walinzi wa demokrasia duniani!

Nalo Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., katika tamko lake kulaani vitendo vya wafuasi wa Rais Trump kuvamia Makao makuu ya Bunge la Marekani linasema, haya ni matokeo ya “siasa chafu” zinazolenga kuwagawa na kuwasambaratisha watu katika mambo msingi. Haya ni matokeo ya viongozi wanaotafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika miaka ya hivi karibuni, misingi ya haki, amani na demokrasia nchini Marekani imetikiswa, kiasi cha kuwa ni tishio la demokrasia kimataifa. Marekani kwa miaka mingi imekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha demokrasia na maridhiano kati ya watu wake, lakini sasa, demokrasia inaonekana kuanza kutoweka taratibu. Umefika wakati kwa wanasiasa, kuanza tena kujikita katika mambo msingi, kwa kujielekeza katika mchakato wa demokrasia ya kweli na kuachana na ubinafsi, uchu wa madaraka na tabia ya wanasiasa kutaka kujitafuta wenyewe. Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, Makanisa yatajaliwa hekima, nguvu na busara ya kuielekeza Marekani kutoka katika kipindi hiki kigumu kwa kujizatiti zaidi katika njia ya haki, amani na upatanisho!

Ghasia Marekani

 

07 January 2021, 16:34