Tafuta

Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki Vya Biblia na BICAM wanasema, bado kuna umuhimu wa kunogesha utume wa Biblia kwa waamini wa Makanisa mahali, kwa kujikita katika majiundo na tafsiri makini. Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki Vya Biblia na BICAM wanasema, bado kuna umuhimu wa kunogesha utume wa Biblia kwa waamini wa Makanisa mahali, kwa kujikita katika majiundo na tafsiri makini. 

Utume wa Biblia Barani Afrika: Umuhimu wa Maandiko Matakatifu!

Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki vya Biblia Ulimwenguni pamoja na BICAM, wameendelea kukazia umuhimu wa Maandiko Matakatifu katika mchakato wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji haina budi kupata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na Biblia ipewe kipaumbele cha pekee katika maisha ya waamini Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki vya Biblia Ulimwenguni, “The Catholic Biblical Federation, CBF,” lilianzishwa kunako mwaka 1969. Hadi sasa lina wanachama 340 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 130. Na Kituo cha Utume wa Biblia Afrika Na Madagascar “The Catholic Biblical Centre for Africa and Madagascar” (BICAM) kilianzishwa na Mababa wa Kanisa Barani Afrika ili kusaidia mchakato wa kutafsiri Biblia katika lugha za waamini katika Makanisa mahalia ili kunogesha maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Maandiko Matakatifu ni chemchemi ya Liturujia ya Kanisa, kwani ni ushuhuda wa matendo makuu ya Mungu katika historia ya wokovu, iliyo fumbo la Kristo Yesu, fumbo ambalo daima lipo na linatenda kazi ndani ya waamini na hasa katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa.

BICAM ni chombo muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji wa kina Barani Afrika na hasa katika utekelezaji wa mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaokazia umuhimu wa Maandiko Matakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Tafsiri za Biblia lazima ziwe sahihi na aminifu, jambo ambalo linapaswa kutekelezwa kiaminifu na wataalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Maandiko Matakatifu ni muhimu sana kwa taalimungu. Hivyo, waamini wanahimizwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yao. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa Makanisa mahalia kuwa na Tafsiri sahihi na aminifu za Biblia Takatifu. Lengo ni kunogesha utamaduni wa kusoma na kulitafakari, kulimwilisha na kulitamadunisha Neno la Mungu katika maisha ya waamini.

Ni katika muktadha huu, Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki vya Biblia Ulimwenguni pamoja na BICAM, hivi karibuni, wameendelea kukazia umuhimu wa Maandiko Matakatifu katika mchakato wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji haina budi kupata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na kwamba, Biblia ipewe kipaumbele cha pekee katika maisha ya waamini Barani Afrika, ili waweze kujisomea, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Familia ya Mungu Barani Afrika isaidie pia mchakato wa kutafsiri Biblia katika lugha mbali mbali ili waamini wengi zaidi waweze kufikiwa na Neno la Mungu hasa kwa njia ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Pili, kuna haja ya kuendelea kuboresha utume wa Biblia Barani Afrika!

Viongozi wa Kanisa toka Barani Afrika walioshiriki katika mchakato wa maandalizi ya mkutano mkuu wa kumi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni wanasema kwamba, kumekuwepo na ufanisi mkubwa katika kutafsiri Maandiko Matakatifu katika lugha za waamini wa Makanisa mahalia. Ili kuweza kuwafikia waamini wengi zaidi, tafsiri ya Maandiko Matakatifu inapaswa kumwilishwa katika fasihi simulizi. Hadi kufikia mwaka 2021, zaidi ya Vitabu 500 vya Maandiko Matakatifu vimetafsiriwa kwa lugha za waamini wa Makanisa mahalia Barani Afrika. Licha ya hali ngumu ya fedha na uchumi, lakini takwimu zinaonesha kwamba, waamini wengi Barani Afrika wanapenda kununua Biblia, lakini pia wanapaswa kufundwa barabara kwa kuwapatia majiundo ya awali na endelevu ili hatimaye, waweze kukutana na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Majiundo makini ya Maandiko Matakatifu yaanzie kwenye familia, jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, parokia, jimbo na taifa katika ujumla wake. Wakristo wajenge utamaduni wa kumiliki Biblia Takatifu, ili waweze kujisomea kwa wakati muafaka. Utume wa Biblia Afrika na Magascar kwa wa waamini wanaozungumza lugha ya Kiingereza ulianzishwa kunako mwaka 1974 lakini utekelezaji wake ukaanza tarehe 5 Julai 1981.

Utume wa Biblia
23 January 2021, 15:38