Tafuta

Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima: Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2021: Ushuhuda wa imani katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima: Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2021: Ushuhuda wa imani katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19. 

Ujumbe wa Noeli 2021 kutoka kwa Patriaki Cyril wa Moscow na Urussi

Sherehe ya Noeli, iwe ni fursa ya kutafakari kuhusu: Noeli na hatima yake katika maisha. Kipindi cha janga la COVID-19 ni nafasi ya kuzingatia ushauri unaotolewa na madaktari na pia, waamini wajitahidi kupata “chanjo na kinga ya gonjwa hili linaloathiri maisha yao ya kiroho” kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Liturujia ya Kanisa na Injili ya upendo katika maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wa Kanisa la Kiorthodox wameadhimisha Sherehe ya Noeli ya Bwana hapo tarehe 7 Januari 2021 kadiri ya Kalenda ya Juliani. Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima, anawapongeza waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliojitokeza kuadhimisha Fumbo la Kuzaliwa kwa Mwana mpendwa wa Mungu, Kristo Yesu, Mkombozi wa walimwengu, katika kipindi hiki kigumu katika historia ya mwanadamu kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hiki kimekuwa ni kipindi cha majaribio makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu wa Mungu ndani na nje ya Urussi. Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu wanaoogelea katika shida na mahangaiko makubwa: kiroho na kimwili.

Fumbo la kuzaliwa kwa Kristo Yesu ni sherehe ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Sherehe ya Noeli, iwe ni fursa kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu maana yake katika maisha ya kiroho na hatima ya mwanadamu katika ujumla wake. Kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 ni nafasi ya kuzingatia ushauri unaotolewa na madaktari pamoja na wafanyakazi katika sekta ya afya, lakini pia, waamini wajitahidi kupata “chanjo na kinga ya gonjwa hili linaloathiri maisha yao ya kiroho” kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Liturujia ya Kanisa mambo yanayomwilishwa katika Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maisha ya sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu, yatawawezesha waamini kuzama katika mchakato wa uponyaji, ili hatimaye, waweze kurejea tena kwenye uzuri wao wa asili. Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima anasema, gonjwa la Corona, COVID-19 linaendelea kusababisha maafa makubwa sehemu mbalimbali za dunia. Watu wameshikwa hofu, woga na mashaka, kiasi hata cha kushindwa kutambua hatima ya maisha yao, kwa sasa na kwa siku za usoni. Ni katika muktadha huu wa watu kukata tamaa ya maisha, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kushikamana katika sala na Liturujia Takatifu, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwasaidia watoto wake wanaomlilia usiku na mchana wakiomba msaada wake wa daima.

Inaonkena kana kwamba, “gonjwa la Corona, COVID-19 linataka kutamalaki”. Mwenyezi Mungu, mwenye nguvu na uwezo wote, awakirimie watoto wake nguvu za kiroho na kimwili, ili kupambana na gonjwa hili “hadi kieleweke”. Awasaidie wagonjwa waweze kupona haraka na hivyo kurejea tena kwenye shughuli zao za kila siku. Awajalie nguvu, bidii, juhudi na maarifa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya, wanaoendelea kujisadaka usiku na mchana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Katika hali na mazingira kama haya, kuna haja kwa waamini kuendelea kujizatiti katika mchakato wa kuimarisha, kuitangaza na kuishuhudia imani yao inayomwilishwa katika matendo thabiti.

Waamini wajiaminishe na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Ni kwa njia hii, tu, waamini wataweza kumtukuza Mwenyezi Mungu na wao pia kutakaswa na kutakatifuzwa. Hii inatokana na imani kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu ametengeneza makao yake miongoni mwa waja wake, kwani kimsingi Yeye ni Emanueli, yaani “Mungu pamoja nasi”. Kristo Yesu, ni nuru ya ulimwengu inayouangazia umaskini na mapungufu ya binadamu kama ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa kwa Kristo Yesu katika pango la kulishia wanyama kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Waamini waendelee kumwabudu na kumsujudia Mungu kama ilivyokuwa kwa wachungaji na Mamajusi kutoka Mashariki ya Mbali. Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, yawe ni chemchemi ya furaha ya kweli, imani na matumaini yanayobubujika kutoka katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu.

Waamini wamtukuze Mwenyezi Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, kwa kumwilisha tunu msingi za Injili katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kuhakikisha kwamba, Injili ya upendo, inatangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa, kama kielelezo cha imani tendaji. Mwenyezi Mungu apende kuwaangazia walimwengu kwa mwanga utakaowawezesha kumtambua; awalinde na kuwabariki kwa amani pamoja na kuwawezesha watu wa Mataifa kutekeleza wajibu wao wa pamoja kwa ari na moyo mkuu. Mtoto Yesu aliyezaliwa Pangoni awe ni chemchemi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa; awalinde na kuwahifadhi vijana na waamini wote katika ujumla wao dhidi ya dhambi pamoja na kuwaepusha hatari zote za roho na za mwili.

Patriaki Cyrl

 

 

 

09 January 2021, 07:31