Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu ni ufunuo wa utimilifu wote wa Unabii anaoutaka Mwenyezi Mungu: Anafundisha, anaganga na kuponya watu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu ni ufunuo wa utimilifu wote wa Unabii anaoutaka Mwenyezi Mungu: Anafundisha, anaganga na kuponya watu!  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili 4 Mwaka B: Kristo Yesu Ni Utimilifu wa Unabii!

Yesu kwa kuwa ameungana kabisa na Mungu Baba na tena kwa kuwa Yeye ndiye Neno lenyewe la Mungu Baba, basi anakuwa ni tafsiri kamili kabisa ya unabii anaoutaka Mungu Baba kwa ajili ya taifa lake. Muungano wa Kristo na Baba, Muungano wa Kristo na Neno lenyewe ndiyo chemchemi ya mamlaka ya kufundishia ya Yesu. Wakristo wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 4 ya mwaka B wa Kanisa.Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Kum 18:15-20). Somo la kwanza linazungumzia unabii ambao Waisraeli watakuwa nao watakapoingia katika nchi yao ya ahadi.  Tupo katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Musa amewaongoza waisraeli kutoka utumwani Misri na sasa wanakaribia kabisa kuingia katika nchi ya ahadi. Musa anajua kwamba yeye hataingia nao katika nchi ya ahadi. Anachokifanya sasa ni kuwapa mausia mbalimbali kuhusu namna wanavyopaswa kuishi wakishaingia huko, wakijua kabisa kwamba nchi hiyo ya ahadi ni nchi wanayopewa na Mungu. Anapouzungumzia unabii, Musa anawaambia: “Bwana atakuinulia nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivo mimi (yaani Musa), msikilizeni yeye”.

Unabii haukuwa ni kitu kilichoanza na waisraeli. Miungu ya makabila mbalimbali ambayo Waisraeli walikutana nayo huko njiani, ilikuwa na Manabii wake. Hao walikuwa ni watu waliokuwa wakiongea kwa niaba ya miungu hiyo. Walikuwa ni watu waliosikilizwa sana na waliogopwa pia kwa sababu kutokufuata anachosema nabii ilikuwa ni kuidharau miungu inayomtuma. Sasa, mausia ya Musa tunayosikia leo ilikuwa ni kuwaasa waisraeli wasimsikilize Nabii asiyekuwa mwenzao, yaani asiye Mwisraeli. Nabii ambaye Mungu atawapa waisraeli ni nabii atakayetoka miongoni mwa ndugu zao. Kuwaacha wamsikilize kila nabii watakayemkuta kutawapoteza kiimani na kutawafanya waanze kuabudu miungu wengine. Jambo la pili analosisitiza Musa katika somo hili ni kuwa Nabii huyo ni lazima apimwe kwa kile anachokisema. Kama ni Nabii wa kweli, basi kile anachokisema kitatendeka lakini kama si Nabii wa kweli, kile anachokisema kitabaki ni maneno matupu. Ni somo linaloalika imani kwa Mungu mmoja na imani kwa wajumbe ambao Mungu huyu mmoja anawatuma kwa watu wake.

Somo la Pili (1Kor 7:32-35): Katika somo la pili, Mtume Paulo anazungumzia kitu ambacho katika mafundisho ya kiroho kinaitwa “kuuishi upendo usiogawanyika”.  Tupo katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho katika sehemu ambayo Paulo anajaribu kuwarudisha katika mstari wale ambao walikuwa wamelowea katika malimwengu yaani katika maisha ya anasa.  Katika mwendelezo huo, leo anawaonesha aina mbili za maisha. Maisha ya ndoa (kuoa na kuolewa) na maisha ya useja (kujikatalia kuoa au kuolewa kwa ajili ya ufalme wa Mungu). Anasema yule aliye kwenye ndoa hujishugulisha zaidi na mambo ya mwenziwe lakini yule asiye oa wala kuolewa anajiweka huru na hivi hujishughulisha zaidi ya mambo ya Mungu. Swali linaloweza kuja kutokana na fundisho hili la Mtume Paulo ni, Je? Walio katika ndoa hawajishughulishi na mambo ya Mungu?

Katika kulielewa vizuri fundisho la Mtume Paulo, ni vizuri pia tukajua kuwa si Mtume Paulo pekee aliyekuwa akiyapinga maisha ya anasa ya Wakorintho. Lilikuwepo kundi la watu walioitwa Wastoa (Stoics). Hawa walikuwa na msimamo mkali sana. Walipinga anasa, burudani na hata kufikia kupinga maisha ya ndoa. Paulo sasa anapokuja anapinga anasa lakini pia anarekebisha msimamo mkali wa Wastoa. Anafundisha juu ya maisha ya ndoa ambamo anayeyaingia anayaingia katika upendo kamili kwa mwenzi wake na anafundisha juu ya maisha ya useja ambapo anayeyaingia anayaingia si kama mtu aliyeweka mgomo wa ndoa bali kama yule anayeingia kwa upendo kamili kwa mambo yamhusuyo Mungu. Msisitizo wa Mtume Paulo kwa Wakorintho na kwetu siku hii ya leo ni kuuishi upendo kamili; upendo usiogawanyika. Anayeuishi upendo usiogawanyika katika ndoa anayatimiza mapenzi ya Mungu, kadhalika na yule anayeuishi upendo usiogawanyika katika useja.

Injili (Mk 1:21-28): Katika Injili ya leo, Yesu anaingia kwa mara ya kwanza katika Sinagogi. Anaanza kufundisha. Katika hiki kitu ambacho kingeonekana cha kawaida, kwamba Yesu anaingia katika Sinagogi na anaanza kufundisha, mwinjili Marko anaonesha vitu viwili ambavyo si vya kawaida. Cha kwanza ni kwamba Yesu alifundisha kama mtu mwenye mamlaka. Na hii tukiitafsiri vizuri ni kwamba Yesu alifundisha akiwa na mamlaka. Kitu cha pili anachokionesha mwinjili Marko ni kuwa Yesu alipokuwa anafundisha, mtu aliyekuwa na pepo mchafu alianza kupaza sauti. Yesu akamtoa pepo huyo mchafu. Na kwa yote haya mawili, yaani Yesu kufundisha akiwa na mamlaka na kumtoa pepo mchafu, watu walishangaa. Yesu anafundisha akiwa na mamlaka kwa sababu Yeye ndiyo hiyo Habari Njema anayoitangaza. Yeye ndilo Neno lililoandikwa, linalosomwa na linalotangazwa. Anafundisha akiwa na mamlaka kwa sababu Yeye na Baba aliyemtuma ni kitu kimoja. Hii inawashangaza watu kwa sababu wale ma- rabbi waliokuwa wakifundisha katika Sinagogi hakuna hata mmoja aliyekuwa kama Yesu.

Ni hapa tunaona kuwa kile alichokieleza Musa katika somo la kwanza kinatimia. Musa alisema Mungu atamwinua Nabii kutoka miongoni mwenu. Nabii huyo wa kweli aliyekuja kuinuliwa na Mungu kutoka miongoni mwa waisraeli ndiye Yesu. Kama sasa Musa alivyowaagiza kumsikiliza nabii wa kweli, Mwinjili Marko anawaalika wote wanaoisoma injili yake kuyasikiliza mafudisho ya kweli ya Yesu. Kitendo cha kumtoa pepo mchafu ni kitendo kinachokuja kuonesha kwa nje mamlaka hayo aliyokuwa nayo Yesu. Ni muujiza. Na kama ilivyo katika miujiza ya Yesu, hafanyi muujiza kwa lengo tu la kufanya miujiza. Ni miujiza inayotokana na imani na ina lengo la kukuza imani. Yesu hajipambanui na miujiza, Yeye anatangaza Habari Njema. Mamlaka aliyonayo katika kutangaza Habari Njema ndiyo yanayojidhihirisha katika miujiza inayotendeka.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya 4 ya mwaka B yanatupatia mwaliko wa kuishi tumeungana na Mungu kwa kufuata mfano wa Kristo mwenyewe. Masomo ya leo yanatupatia mwaliko huu kwa kumuonesha Kristo Yesu kuwa ndiye ukamilifu wa ahadi ya Mungu, ahadi ambayo Mungu aliitoa kwa kinywa cha Musa kuwa atawainulia waisraeli nabii kutoka miongoni mwao, Nabii ambaye ukweli wa unabii wake utajionesha pale ambapo yale atakayofundisha na kuyaongea yatatimia kati yao. Naye Kristo, amekuwa kweli utimilifu wa ahadi hiyo ya Mungu kwa sababu alipoanza kufundisha amejitofautisha na wengine kwa kuwa yeye amefundisha kwa mamlaka. Katika jamii mamlaka au nguvu ya kufundisha jambo, iwe ni kuonya, kuelekeza au hata kusifia, yapo ya aina nyingi. Kuna mamlaka ya kimaadili ambapo anayekemea uovu fulani anatakiwa awe safi, asiwe amechafuliwa na uovu huo anaoukemea.

Yapo mamlaka ya kielimu yanayomtaka anayefundisha jambo awe amebobea katika jambo hilo. Lakini pia yapo mamlaka ya kiutawala n.k. Katika ufafanuzi wa masomo tumeonesha kuwa mamlaka aliyofundishia Yesu au kwa maneno mengine nguvu aliyokuwa nayo alipofundisha, awali ya yote kabisa ilitokana na muunganiko aliokuwa nao na Mungu Baba. Kazi ya kufundisha ni kazi ya kinabii. Na nabii hazungumzi maneno yake bali ya yule aliyemtuma. Kristo kwa kuwa ameungana kabisa na Mungu Baba na tena kwa kuwa Yeye ndiye Neno lenyewe la Mungu Baba, basi anakuwa ni tafsiri kamili kabisa ya unabii anaoutaka Mungu Baba kwa ajili ya taifa lake. Muungano wa Kristo na Baba, Muungano wa Kristo na Neno lenyewe ndiyo chemichemi ya mamlaka ya kufundishia ya Yesu.

Sisi sote wakristo, kwa Ubatizo tunashirikishwa unabii wa Kristo pamoja na ukuhani na ufalme wake. Kwa unabii tunaoshirikishwa, tunaitwa kuwa waalimu wa ukweli wa kimungu, yaani kuuishi ukweli wa kimungu katika maisha yetu lakini pia kuushuhudia ukweli wa kimungu katika mazingira tunayoishi. Leo basi tunakumbushwa kuwa nguvu ya kuuishi ukweli huo na mamlaka ya kuushuhudia na kuutetea, awali ya yote, vinategemea na muunganiko tulionao na Mungu. Neno analolitamka yule anayeishi katika muungano na Mungu lina nguvu ya kupenya mioyo ya watu; ushuhuda anaoutoa yule aliye karibu na Mungu unazungumza maradufu kwa watu na mafundisho yake yana uwezo wa kuiangaza zaidi mioyo yao kumuelekea Mungu. Tujitahidi basi kuukuza muunganiko wetu na Mungu ili yote tunayoyafanya kwa jina lake yabebe daima nguvu na mamlaka yake ya kimungu. Tuzisafishe dhamiri zetu zijazwe na hofu ya Mungu na tumkaribie Mungu sisi wenyewe kwa maisha ya sala na sakramenti pamoja na kujibidiisha katika upendo usiogawanyika kama anavyotufundisha Mtume Paulo.

Liturujia J4 ya Mwaka B

 

 

29 January 2021, 12:02