Tafuta

Vatican News
Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, amefungua ukurasa wa uelewa mpya wa maana ya fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, amefungua ukurasa wa uelewa mpya wa maana ya fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu! 

Tafakari Jumapili 4 Mwaka B: Ushuhuda wa Maisha ya Kikristo!

Fumbo la mateso na mahangaiko ya mwanadamu linapata maana mpya kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kristo Yesu ndiye yule Masiha aliyetabiriwa kwenye Maandiko Matakatifu, tangu Agano la Kale, ambaye sasa ametumwa na Baba yake wa mbinguni kuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwanzo mpya wa maisha!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 4 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika hii yanatuapa nafasi ya kutafakari matendo yetu tuone kama kweli yanadhihirisha ukristo wetu na imani yetu. Katika maisha yetu ya kila siku, watu hutambuliwa kwa matendo yao. Mtindo wa maisha na wakati mwingine hata mambo madogo-madogo ya kila siku huweza kutueleza sisi ni akina nani. Kumbe matendo na mtindo wa maisha yetu hutusema kuwa sisi ni akina nani? Ndivyo inavyopaswa kuwa kwetu sisi wakristo; maisha yetu yanapaswa kuonyeshe kwamba sisi kweli ni wabatizwa na wafuasi wa Yesu Kristo. Katika Somo letu la kwanza kutoka katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati linamwonesha Musa, katika nyakati za mwisho za maisha yake, baada ya safari ya miaka 40 katika jangwa kuelekea katika nchi ya ahadi. Musa alifahamu fika kuwa hataingia nchi ya ahadi amekaribia kufa. Hivyo anawafariji watu wake wasijekata tamaa kwa kifo chake. Hivyo kwa jina la Mungu, anawahakikishia kuwa atakuja Nabii wa pekee, ambaye ni mkuu kuliko yeye, ambaye atawaongoza kufahamu mpango wa Mungu kwa udhahiri zaidi na kuwaongoza katika Njia za kweli, na anawasihi wamsikilize. Ahadi hii ya Musa ilikuwa hai daima katika akili za Wayahudi ndiyo maana alipotokea Yohane Mbatizaji, walimuuliza: “Je, wewe ndiye Nabii yule ajaye?” (Jn. 1, 22).

Yohane Mbatizaji akajibu “Mimi siye.” Petro katika Mahubiri yake kwa Wayahudi baada ya kumponya mlemavu mbele ya mlango wa Hekalu anasema: Kwa maana Musa alisema; “Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu, itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia. Mtu ye yote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atakataliwa mbali kabisa na watu wake kwa kuwa Yesu ndiye Nabii na Masiha ambaye Musa alitabiri habari zake (Mdo 3:22-23).  Naye Stefano katika hotuba yake kwa Wayahudi kabla hawajamuua kwa kumpiga mawe anasema: Huyu ndiye yule ambaye Musa aliyewaambia Waisraeli: “Mungu atawainulia nabii kutoka miongoni mwa ndugu zenu” (Mdo 7:37). Kumbe Kristo Yesu ni yule Nabii ambaye Mungu kwa kinywa cha Musa aliwaahidi watu watu. Kama Musa alivyokuwa rafiki wa Mungu hata akafunuliwa kuja kwake Kristo, sisi nasi tunatakiwa kudumu katika urafiki na Mungu ili tuweze kumtambua Kristo Yesu Bwana wetu, tuweze kusema, kutenda na kuishi kadiri ya mapenzi yake. Matendo na maisha yetu yaonyeshe kuwa sisi tu rafiki zake Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

Katika somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho, Mtume Paulo anaeleza bayana kuwa katika Kanisa kuna mtindo wa maisha ya aina mbili. Maisha ya ndoa na maisha ya useja. Kila mtu anatakiwa kumtumikia Mungu kadiri ya maisha aliyochagua. Mseja ana nafasi kubwa ya kujitoa kwa ajili ya Mungu. Hivyo matendo yake yanatakiwa kumdhihirisha kuwa yeye ni mseja. Wakati mtu wa ndoa hushughulika zaidi na mambo yahusuyo ndoa yake ni lazima kutenda hayo yote ili kumpendeza Mungu katika maisha ya ndoa. Paulo anatoa angalisho juu ya uchaguzi wetu wa maisha, kuwa kila mtu achague vema mtindo wa maisha anayopenda na kuyaweza kuyaishi. Hivyo anatoa ushauri kwa kila mtu kujipima vema kabla ya kuchagua na kuingia katika mtindo wa maisha unayoyachagua yawe ya ndoa au ya useja. Kila mtu anatakiwa kuchagua mtindo ambao ataweza kumuwakilisha Kristo kwa maneno, matendo na tabia yake. Kumbe katika uchaguzi wa maisha tusiwe watu wa kufuata mkumbo na baadaye mtu anaishi kwa ubabaishaji na huzuni nyingi na mfadhaiko maisha yote.

Katika Injili, Marko anatueleza jinsi Yesu Kristo, baada ya kuwaita mitume wake wanne: Simon, Andrea, Yakobo na Yohane, anavyoanza utume wake. Yesu Kristo anajidhihirisha kwa watu wa Kapernaumu kuwa yeye ni Masiha aliyeahidiwa katika Agano la kale, kama somo la kwanza linavyosimulia. Yesu anadhihirisha hilo kwa kutekeleza wajibu wake kwa kufundisha, kuponya wagonjwa, kufukuza pepo wachafu na kuwa mtu wa sala (Mk 1:21&35). Maandiko Matakatifu katika Agano la Kale, yalieleza kuwa maradhi na kupagawa na pepo wabaya ni mapato ya dhambi na shetani. Hivyo Yesu kufanya miujiza ya kuponya maradhi, ni uthibitisho kwamba yeye ni Masiya aliyefika kuvunja utawala wa shetani na dhambi. Sisi tuliobatizwa na kumvaa Kristo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya nguvu tulizojaliwa za kupambana na mwovu shetani. Licha ya kuwa tunafahamu na tunafundishwa kuwa mkristo hana cha kuogopa kuhusu pepo wabaya, lakini kila majanga na mabalaa yanapotupata, tunaanza kuwa na mashaka kuhusiana na hali yetu na imani yetu inaanza kunywea, tunaanza kujihoji kama imani kwa Kristo inatosha kupambana na pepo wabaya.

Tutambue kuwa kila kilicho kiovu, na kilicho kibaya hakikuumbwa na Mungu bali ni matokeo ya dhambi. Kitabu cha Hekima ya Sulemani kinatufundisha kuwa: “Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi kuona watu wakipotea…ila ulimwengu uliingiliwa na mauti kwa husuda yake shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja” (Hek 1:13, 2:24). Kwa ubatizo tumetengwa na shetani na kuungana na Kristo kumbe, hatuna sababu ya kuogopa, bali kuwa na imani dhabiti kwa Yesu Kristo. Kwa maisha yake, Yesu Kristo anakuwa mwalimu wetu. Maisha na matendo yake yalimweleza kuwa yeye ni nani, hata mashetani walimtambua kuwa yeye ni Mtakatifu wa Mungu (Mk 1:25). Ndivyo tunavyopaswa kuwa sisi tuliobatizwa na kuwa wafuasi wake, maneno na matendo yetu yatutambulishe tulivyo. Sisi wabatizwa, tulioamua kumfuata Kristo aliyekioo cha Mungu Baba asiyeonekana, yatupasa kujiuliza: je matendo yetu yanadhihirisha ukristo na ufuasi wetu? Je mimi kama mkristo naishi Ukristo wangu? Au Ukristo wangu ni kama vazi ambalo jioni nalitoa na kulitundika? Kristo anatambuliwa kwa maneno na matendo yake. Je sisi tunatambuliwa kuwa wakristo kwa maisha yetu?

Maneno na matendo yetu ni utambulisho wetu? Wakati wa ubatizo wetu tuliweka ahadi. Je, kwa namna gani tunaziishi? Katika maisha yetu ya kila siku, hasa ratiba zetu, ni masaa mangapi tunatumia kwa kutafakari Neno la Mungu, kufundisha Neno la Mungu, tunapozungumza au kufundisha neno la Mungu, je watu wanaotusikiliza, wanaona kweli kama sisi tunasadiki na kuamini yale tunayofundisha? Tuombe basi neema na baraka za Mungu kama tunavyosali katika sala baada ya Komunio katika domenika hii tukisema; “Ee Bwana, sisi tuliokula sadaka ya ukombozi wetu, tunakuomba utuzidishie daima imani ya kweli kwa chakula hicho kiletacho uzima wa milele” tuwe kweli na Imani dhabiti ili kwa maneno na matendo yetu tumshuhudie Kristo katika maisha yetu na watu wamuone nao waweza kumwongokea wapate uzima wa milele.

Jumapili 4 ya Mwaka B

 

 

28 January 2021, 13:59