Tafuta

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanashirikishwa: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanashirikishwa: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. 

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Ukuhani, Ufalme na Unabii!

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana inatukumbusha Ubatizo wetu kiini cha Ukristo, zawadi kutoka kwa Mungu tunapozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na kufanywa kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa, na washiriki katika ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo. “Ee Mungu Utujalie sisi ulitufanya wanao tulipozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu tudumu siku zote katika upendo wako.”

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya neno la Mungu katika Sikukuu ya ubatizo wa Bwana kama maneno ya wimbo wa mwanzo yanavyotualika yakisema; “Bwana alipokwisha kubatizwa, mbingu zikamfunukia, Roho akashuka kwa mfano wa hua, na kukaa juu yake; na tazama, sauti ya Baba ikasema: Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Tunapoadhimisha sikukuu hii sisi nasi tunakumbuka ubatizo wetu ulio kiini cha Ukristo wetu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu Baba, tunapozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na kufanywa kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa, na kuwa washiriki katika ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo. Hivi ndivyo tunavyosali na kuomba katika sala mwanzo tukisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulimtangaza rasmi Kristo kuwa ndiye Mwanao mpenzi hapo alipobatizwa katika mto Yordani na kushukiwa na Roho Mtakatifu. Utujalie sisi ulitufanya wanao tulipozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu tudumu siku zote katika upendo wako.

Kwa sikukuu hii ya Ubatizo wa Bwana tunahitimisha kipindi cha Noeli na tunaanza kipindi cha kawaida cha mwaka B wa Kanisa ambapo jumapili tunapoadhimisha sikukuu ya ubatizo wa Bwana inachukua nafasi ya dominika ya kwanza ya mwaka wa kiliturujia. Kipindi hiki cha Noeli tunachokihitimisha kwa sikukuu ya ubatizo wa Bwana, kilitanguliwa na kipindi cha majilio ambapo; katika jumapili ya kwanza ya majilio ujumbe mkuu ulikuwa, Kesheni basi; kwa maana hamjui siku atakayokuja Mwana wa Adamu. Jumapili ya pili Yohane Mbatizaji alituhimiza kufanya toba kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Hivyo tuitengeneze njia ya Bwana na tuyanyoeshe mapito yake na katika Jumapili ya tatu, alitoa ushuhuda wa ukuu wa Masiha Bwana wetu Yesu Kristo kuwa yeye Yohane mbatizaji hastahili hata kulegeza kidamu ya viatu vyake. Jumapili ya Nne Malaika Gabrieli alimpasha habari Maria kuchukua mimba na kumzaa mkombozi wetu Yesu Krsito na akadokezwa habari za kutungwa mimba kwa Yohane mbatizaji. Huyu mkombozi ndiye tulisherehekea kuzaliwa kwake kwa wale waliokuwa wamejiandaa kumpokea.

Kwa wale ambao hawakujiandaa waliposikia kuzaliwa kwake pamoja na Herode walifadhaika, wakaungana na maaskari kumtafuta ili wamuue wakaishia kufanya mauaji ya kinyama ya watoto mashahidi tuliwakumbuka 28/12. Leo tunapohitimisha kipindi cha kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo kwa sikukuu ya Ubatizo wake, Mungu anajifunua kwetu katika nafsi zake Tatu, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Nabii Isaya katika somo la kwanza katika Sikukuu ya ubatizo wa Bwana anaorodhesha kazi za mtumishi mteule wa Bwana kwamba; hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatoa hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani. Kwanini? kwasababu Bwana aliyemuita katika haki na kumtoa awe agano la watu, na nuru ya mataifa; atamshika mkono na kumlinda. Kazi atakazofanya ni; kuyafungua macho ya vipofu, kuwatoa wafungwa gerezani na wale walio gizani kuwaonesha nuru. Katika Agano Jipya mtumishi huyo ni Yesu Kristo.

Katika somo la pili la Kitabu cha Matendo ya Mitume, Mtume Petro anakiri upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote akisema: Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Alimtuma Kristo kuwaponya watu wote walioonewa na Ibilisi kwa kumtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu baada ya ubatizo wa Yohane.Injili ilivyoandikwa na Marko inashuhudia maneno ya Mtume Petro kuwa; Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohane katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinafunguka, na Roho wa Mungu, kama hua akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni ikisema; Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Hapa utabiri wa Yohane Mbatiza tuliousikia katika jumapili ya tatu ya kipindi cha majilio unatimia. Maandiko Matakatifu yanatuambia kuwa; Ubatizo wa Yohane ulikuwa ni ubatizo wa toba kwa ajili ya utakaso na ondoleo la dhambi.

Maandiko Matakatifu pia yanatueleza kuwa: Yesu Kristo ni Mungu, hana dhambi, ni Mtakatifu, aliuchukua ubinadamu wetu kwa hiari yake ili apate kutukomboa sisi kutoka utumwa wa dhambi (Filp. 2:6-7). Huu ni ukweli usiopingika. Juu ya Ubatizo wa Yohane Biblia nayo iko wazi ya kwamba ulikuwa ni ubatizo wa toba, uletao ondoleo la dhambi na Yesu alibatizwa huo ubatizo. Sasa swali lakujiuliza; kama Yesu ni Mungu, Mtakatifu, hana dhambi kwanini alibatizwa ubatizo wa Yohane; ubatizo uliokuwa wa toba? Sababu na malengo ya kubatizwa kwa Yesu yako wazi. 1. kutuonesha kuwa ubatizo ni alama wazi ya kuupokea uzima wa Mungu rohoni mwetu. 2. Kutimiza haki yote na kutufundisha sisi unyenyekevu. 3. Kutufunulia ushirika wa Utatu Mtakatifu katika kazi ya ukombozi, ndiyo maana nafsi zote tatu pamoja, yaani, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu zilijifunua wazi, Mungu Baba anamtambulisha Mwanae wa pekee Yesu Kristo kuwa ndiye Masiha aliyengojewa; ndiye mtumishi mteule wa Mungu aliyetabiriwa na nabii Isaya (Isa 42:1).

Na Roho Mtakatifu akashuhudia kwa mfano wa hua akishuka toka juu mbinguni akianzisha kuumbwa upya kwa dunia kwa njia ya Yesu. 4. Yohane Mbatizaji aweze kumtambulisha Yesu kwa watu kuwa ndiye masiha na mkombozi aliyengojewa 5. Kuyatakatifuza maji kwa ajili ya ubatizo wetu. Na mwisho ni katika tukio hili la ubatizo wa Bwana Sakramenti ya Ubatizo imefungua mbingu na imewekwa kuwa mlango wa kuingilia mbinguni ndiyo maana katika mazungumzo ya Yesu na Nikodemo (Yoh 3:3); Yesu anamwambia Nikodemo kamwe usipozaliwa kwa mara ya pili kwa Maji na Roho Mtakatifu hutaingia kamwe katika uzima wa milele. Ubatizo wetu sisi ni moja ya maagizo mawili aliyoyatoa Yesu kwa Kanisa kabla ya Kupaa kwake mbinguni baada ya ufufuko. Yesu aliwaaambia wanafunzi wake; “Enendeni duniani kote mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu na kuwafundisha yote niliyowaamuru ninyi, natazama mimi nipo nanyi mpaka mwisho wa dahari (Mt. 28:19-20). Kumbe ubatizo ni wa muhimu na wa lazima kwa sababu ni agizo la Yesu Kristo mwenyewe. Kwa ubatizo tunapokolewa ndani ya Mwili wa Kristo ambao ndilo Kanisa (1Kor 12:13).

Ubatizo wetu ni njia ya kushuhudia hadharani na kukiri Imani yetu na ufuasi wetu kwa Kristo tukizaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu. Ubatizo wetu unaeleza na kuonesha waziwazi kifo, maziko na ufufuko ndani ya Kristo. Pia unaeleza kifo chetu juu ya dhambi na maisha mapya ndani ya Kristo, (Rom 6:4-11 Col. 2:12). Ubatizo ni alama ya nje tu ya mabadiliko yetu ya ndani kama waamini wa Kristo. Ni alama ya utii kwa Mungu. Kama ilivyotokea kwa Yesu siku ya ubatizo, sisi nasi wakati wa Ubatizo wetu tulimpokea Roho Mtakatifu na sauti iliyomshuhudia Yesu ikisema; huyu ni mwanangu mpendwa, nipendezwaye nawe, ilitushuhudia hata sisi. Mungu alipendezwa nasi, kwa sababu tuliamua kumkana na kumkataa shetani na fahari zake zote na tukaamua kujiunga katika familia ya watoto wa Mungu na ukoo wa kifalme, taifa teule la Mungu na kuwa hekalu la Roho Mtakatifu. Tunapoadhimisha sikukuu ya ubatizo wa Bwana na kukumbuka ubatizo wetu, tuchunguze dhamiri zetu tuone kama Mungu bado anapendezwa nasi, kama mbingu zilizotufungukia siku tulipobatizwa bado ziko wazi au tumezinga kwa dhambi zetu?

Mbingu ilishafunguliwa kwa ajili yetu sisi kwa mateso, kifo na ufufuko wake Kristo ili sisi tuweze kumfikia Baba yetu wa Mbinguni. Tusijifungie mbingu sisi wenyewe kwa dhambi zetu. Tupiganie kumpendeza Mungu daima kwa kuziishi ahadi zetu za ubatizo tukiongozwa na amri zake Mungu na za kanisa. Pale tunaposhindwa kuishi atakavyo Mungu, tuchukue hatua tufanye toba ya kweli naye Mungu atatusamehe na kutujaza neema zake. Basi tunapoadhimisha sikukuu hii ya ubatizo wa Bwana, tunakumbushwa kuziishi vema ahadi za ubatizo wetu na wajibu tulionao kwa jirani zetu, kuulinda, kuutetea, kuuthamini, na kuutunza uhai na utu wetu tukiwa wakristo taifa teule la Mungu watu tuliochaguliwa kuwa urithi wake Mungu. Imani yetu kwa Kristo iwe ya daima, wakati wa raha, taabu, dhiki, kiu, magonjwa, shida, taabu na katika afya njema. Kwa kuishi hivi Mungu atapendezwa nasi, na sala tunayosali baada ya komunyo tukisema kuwa: “Ee Bwana, sisi uliotushibisha mapaji matakatifu tunakuomba sana rehema yako, tupate kumsikiliza kwa imani Mwanao wa pekee, tuweze kweli kuitwa na kuwa wanao,” itakuwa na maana na matunda yake tutayaona.

08 January 2021, 07:33