Tafuta

Mamajusi wakamtolea Mtoto Yesu zawadi zao: Dhahabu Ufalme wa Yesu: Ubani ni kielezo cha Umungu na Ukuhani wake na Manemane ikionesha ubinadamu wake, mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Mamajusi wakamtolea Mtoto Yesu zawadi zao: Dhahabu Ufalme wa Yesu: Ubani ni kielezo cha Umungu na Ukuhani wake na Manemane ikionesha ubinadamu wake, mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. 

Sherehe ya Epifania: Ufunuo wa Mungu Mkombozi wa Mataifa Yote

Mamajusi ni wawakilishi wa watu wa mataifa mengine, waliokuwa wapagani ila nao nyota ile imewaangaza na kuwaalika kufika kumwabudia huyu mtoto aliyezaliwa. Na ndio wanamtambua huyu mtoto kama Mfalme na Mungu kweli na ndio wanamsujudu na kumtolea zawadi za: Dhahabu alama ya Ufalme wake; Ubani alama ya Umungu wa Kristo na Manemane.: Ubinadamu na kifo.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Leo ni sherehe ya Epifania, ni sherehe ya mwanga. Ni Yesu anayejifunua na kujidhihirisha kwa watu wa mataifa yote, maana yeye ni Mkombozi wa ulimwengu mzima. Epifania linatokana na neno la lugha ya Kigiriki επιφαινω (epifaino) maana yake ni kitendo cha kujidhihirisha au kujifunua. Mamajusi, tunaposoma Maandiko Matakatifu hatusikii sana juu ya habari zao kuwa walitoka wapi na walikuwa watu wa namna gani, walikuwa wangapi kwa hakika na hata baada ya kumwona mtoto Yesu na kurejea makwao walifanya nini baada ya hapo. Haya yalikuwa ni maswali yaliyosumbua sana pia zile jumuiya za waamini za mwanzo na labda hata sasa tunaposoma sehemu hii ya Injili tunabaki na maswali kadha wa kadha.

Ni kutokana na maswali hayo basi Mapokeo yanasema walikuwa wafalme watatu kutokana na zile zawadi tatu, na majina yao ni: Gaspari aliyekuwa kijana, Melkiori (mzee kiumri) na Baltasari (mtu wa makamu). Injili haisemi kuwa walikuwa wangapi au walikuwa wafalme ila wanatambulishwa kama wataalamu wa nyota au mamajusi. Hawa wataalamu wa nyota au mamajusi, kwa nyakati zile za kuzaliwa Yesu walikuwa ni watu wenye hekima na uwezo wa kutafsiri njozi ili kujua mambo yajayo na kusoma mapenzi ya Mungu katika matukio ya kawaida na yasiyo ya kawaida katika maisha. Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hawa Mamajusi ni wawakilishi wa watu wa mataifa mengine zaidi ya Wanawaisraeli waliopata kumwona Mtoto Yesu.  Mwinjili anaiandikia jumuiya ya wanakanisa ambayo tayari imekuwa na waamini hata watu kutoka mataifa mengine zaidi ya Israeli.  Ni lengo la Mwinjili Mathayo kutuonesha kuwa Yesu Kristo tangu mwanzoni amezaliwa kama Mwokozi na Mkombozi wa Mataifa yote.

Nyota anayozungumzia Mwinjili Mathayo ni zaidi ya ile ya angani, anatualika kuitafuta pia katika Maandiko Matakatifu, maana hadhira yake ilikuwa inaelewa vema Agano la Kale na kuhusiana na unabii wa nyota itakayowaangazia kutoka gizani.  Na ndio maana Herode pia aliwaarika wakuu wa makuhani na waandishi ili wamweleze Maandiko yanasemaje. Rejea Kitabu cha Hesabu 22-24, Balaam anatabiri juu ya nyota itakayochipuka kutoka uzao wa Yakobo, Anaagua Balaamu miaka 1200 kabla ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. (Hesabu 24:17,19). Nyota hii ni Yesu Kristo anayemwangazia kila mwanadamu. Hivyo simulizi hili la Mamajusi ni mfano anaotumia mwinjili Mathayo kwa Kanisa lile la Karne ya kwanza ambapo watu wa Mataifa mengine nao walimwongokea Kristo na kupokea imani na kuwa wafuasi wake Yesu Kristo. Ni kupitia Taifa la Israeli, watu wa Mataifa nao wameweza kuifikia hii Nyota iliyotabiliwa na manabii miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Mwinjili Mathayo anawaandikia wale wakristo wa mwanzo waliojua vema kabisa Maandiko Matakatifu hasa Agano la Kale, hivyo adhira yake ilimwelewa vema kabisa kuwa nyota anayoiongelea ni Masiya au Kristo anayekuja kutuangazia kutoka katika maisha ya giza.

Mamajusi ni wawakilishi wa watu wa Mataifa mengine, waliokuwa wapagani ila nao nyota ile imewaangaza na kuwaalika kufika kumwabudia huyu mtoto aliyezaliwa. Na ndio wanamtambua huyu mtoto kama Mfalme na Mungu kweli na ndio wanamsujudu na kumtolea zawadi za dhahabu, ubani na manemane. Mamajusi wanasafiri kutoka katika nchi zao na wananyanyua macho yao juu kuongozwa na nyota ile ya haki, wakati Herode na waandishi na wakuu wa makuhani wanabaki katika hali zao za awali, maana hawapo tayari kuongozwa na Mungu mwenyewe katika maisha yao. Mfalme Herode alibaki akisumbuliwa na habari hizo. Neno la Kigiriki linalotumika ni ταρασειν (tarasein) likimaanisha ile hali ya kuchafuka kwa bahari, ndio hali ya chuki kali na mbaya aliyojaa nayo Herode na kinyume chake ni Mamajusi waliojawa furaha na shauku kubwa walipomwona Mtoto Yesu akiwa na Mama yake Maria pale Bethlehemu.

Somo la kwanza linatueleza kuwa mwanga ule ulioiangaza Yerusalemu ukawaongoza watu wote kwenda katika mji ule mtakatifu na zawadi zao. Na ndio unabii huu unakamilika katika somo la Injili ya leo ambapo Mamajusi ndio watu wa Mataifa wanaokuja na zawadi zao kwa Mtoto Yesu aliye nyota ile ya haki. Wakiongozwa na mwanga au nyota ile ya Masiha, Mamajusi wanakuja Yerusalemu na dhahabu, ubani na manemane. Zawadi hizi baadaye zinaelezwa kuwa na maana pia ya kitaalimungu kadiri ya Mapokeo ya waamini wa kwanza, dhahabu ikimtambua kuwa Yesu ni mfalme, ubani ukionesha Umungu wake na ukuhani wake wa milele na manemane ikionesha ubinadamu wake na hasa fumbo lile la kifo chake. (Mk15:23; Yoh 19:39) Ni Taifa la Israeli pia lilijulikana kama Taifa lenye Mungu kama Mfalme wao, Taifa la kikuhani na pia mchumba mwaminifu wa Mungu. Ni dhahabu inayoashiria Ufalme wa Israeli, ubani kuwa ni Taifa la Mungu na manukato ya manemane yenye harufu nzuri kama harufi nzuri ya bibi harusi au mchumba mwaminifu wa Mungu.

Watu wa Mataifa wanamsujudia mtoto Yesu na hivyo kumtambua kama Mungu wao na Mfalme wao. Mamajusi wanabaki kuwa ni ishara ya Kanisa zima kama jumuiya ya waamini kutoka watu wa rangi zote, kabila zote, lugha zote na mataifa yote. Kuwa mwanakanisa haimaanishi kukataa utambulisho wetu, ila ni utajiri wa Kanisa kwani ni moja, takatifu, katoliki na la mitume na lenye watu kutoka mataifa yote bila kubagua. Kila mwanakanisa anaalikwa kubaki na utambulisho wake uwe wa lugha au utamaduni na hivyo kila mmoja wetu kuwa mchango na msaada katika kulijenga Kanisa la Kristo. Mamajusi ni kielelezo na mfano wa maisha ya kila mwanakanisa, ndio maisha ya ya kutoka na kuanza safari ya kuifuata nyota ile ya ukweli, ndio Kristo Mwenyewe. Ni kama mwaliko wa Kristo mwenyewe kwetu, kama alivyowaalika wanafunzi wake pembeni mwa ziwa la Galilaya, Njoo unifuate. Mt. 4:18-22.

Ni mwaliko wa kuachana na yote yanayokuwa kinyume iwe ni vitu au tabia zetu zisizoakisi ufuasi wetu. Kinyume chake ni kuwa sawa na makuhani wa Yerusalemu waliodhani kuwa wao wana ukweli wote na hivyo kukosa kujishusha na kutoka na kwenda Bethlehemu kumsujudia mtoto Yesu. Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Isaya ni mwaliko wa kuvaa nuru maana utukufu wa Bwana utakuwa juu ya watu wale waliokata tamaa na kuwa katika giza la utumwa kwa miaka mingi kwani saa yao ya wokovu sasa imefika. Na ndio siri anayozungumzia Paolo Mtume katika waraka wake kwa Waefeso na siri hiyo ndio ukombozi wa watu wote. Katika Kristo na kwa njia ya damu yake, Mwenyezi Mungu anatufanya watu wa mataifa yote, kuwa warithi pamoja na Mwanae wa pekee. Ndugu zangu, Mamajusi mara baada ya kumwona mtoto Yesu walirejea nyumbani kwako kwa njia nyingine.

Ni mwaliko kwetu nasi pia mara baada ya kukutana na Yesu Kristo hatuna budi kubadili njia na kuanza njia mpya nayo ndio ile ya Yesu Kristo mwenyewe, njia ya uzima na ukombozi. Epifania ni mwaliko wa kuanza kuishi maisha ya mwanga maana nuru yake mtoto Yesu imetufikia na hivyo hatuna budi kutembea katika nuru na mwanga wa kimungu. Ni mwaliko wa kuyabadili maisha yetu na kutembea katika mwanga. Kinyume chake ni Herode anayesema anataka kumwabudu mtoto Yesu ila akiwa na nia ovu ndani mwake. Wapendwa tumwombe Mungu atukinge na roho ile ya wivu na kisasi katika maisha yetu ili daima tuwe wajumbe wa Upendo wa kimungu kwa watu wote. Ninawatakia sherehe njema ya Epifania na mwaka mpya wenye kila neema na baraka zake Mtoto Yesu!

04 January 2021, 08:12