Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa SECAM kwa Noeli 2020 na Mwaka Mpya 2021: Siasa safi kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha amani Barani Afrika. Ujumbe wa SECAM kwa Noeli 2020 na Mwaka Mpya 2021: Siasa safi kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha amani Barani Afrika. 

SECAM: Ujumbe wa Noeli 2020 Na Mwaka Mpya 2021: Siasa Safi!

SECAM: Mwaka 2020 ulitawaliwa pia na vita, kinzani na mashambulizi ya kigaidi sehemu mbalimbali za Bara la Afrika. Hali hii iligumishwa zaidi na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, kwa watu wengi kupoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na gonjwa hili. Mwaka 2021 uwe ni mwaka wa amani na utulivu, ili kuwarejeshea tena watu wa Mungu: imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; mazungumzo yanayowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani.  Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na maendeleo ya wengi. Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa!

Amani ya kweli inakita mizizi yake katika: Ukweli, haki, upendo na uhuru. Naye Mtakatifu Paulo VI anasema, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu haki msingi na uwajibikaji, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni katika muktadha huu, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, katika ujumbe wake kwa Sherehe za Noeli 2020 pamoja na Mwaka Mpya wa 2021, linasema, amani ni siasa safi hata kwa Bara la Afrika. SECAM kwa kusukumwa na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, linakazia kwa kusema kwamba: Upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita kutafuta mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu.

Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu; ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano ili watu waweze kuaminiana na kuthaminiana. Katika siasa kuna watu wanatafuta umaarufu si kwa ajili ya huduma kwa watu bali wanataka kuwanyonya na kujineemesha binafsi. Siasa safi inatengeneza fursa za ajira, inawalinda wafanyakazi na kupambana na umaskini wa hali na kipato. Inakuza na kudumisha umoja na mshikamano unaoratibiwa na kanuni ya auni.

Mwaka 2020 Bara la Afrika kama zilivyo sehemu nyingine za dunia, limeathirika sana kutokana na madhara makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. SECAM inapenda kutoa wito kwa viongozi wa Serikali na wanasiasa Barani Afrika kujizatiti zaidi katika kuwekeza na kuboresha mfumo wa huduma ya afya, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 zimethibitishwa kuwa ni salama na zenye ufanisi. Kardinali Philippe Nakellentuba Ouédraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, nchini Burkina Faso ambaye pia  ni Rais wa SECAM katika ujumbe wa Noeli na Mwaka Mpya wa 2021 anafanya rejea kwenye Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu “Utamaduni wa Utunzaji Kama Njia ya Amani”.

Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu madhara ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, majanga asilia, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani, hali ngumu ya uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Katika kipindi hiki kumeibuka pia utaifa, chuki dhidi ya wageni, vita na kinzani mambo ambayo yanapelekea maafa na uharibifu, kumbe, utamaduni wa utunzaji ni kama njia ya amani. Mungu Muumbaji ni kiini cha wito wa mwanadamu kutunza kama unavyofafanuliwa katika Maandiko Mtakatifu, yaani ulinzi wa Mungu kwa binadamu. Kuna uhusiano na mwilingiliano mkubwa kati ya maisha na mafungamano ya kibinadamu pamoja na mazingira. Haya ni mambo ambayo kimsingi  hayawezi kamwe kutenganishwa na udugu wa kibinadamu, haki na uaminifu kwa wengine.

SECAM inasikitika kusema kwamba, Mwaka 2020 ulitawaliwa pia na vita, kinzani na mashambulizi ya kigaidi sehemu mbalimbali za Bara la Afrika. Hali hii iligumishwa zaidi na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, kwa watu wengi kupoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na gonjwa hili hatari. Mwaka 2021 uwe ni mwaka wa amani na utulivu, ili kuwarejeshea tena watu wa Mungu: imani na matumaini. Bado gonjwa hatari la Corona, COVID-19 lipo na wataalam hawajui litakwisha lini na hivyo maisha kurejea katika hali yake ya kawaida. Bado kuna changamoto kubwa ya maambukizi Virusi vya Corona, COVID-19. Bila mshikamano wa Kimataifa, watu wengi wataendelea kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha, dawa na vifaa tiba. Bila mshikamano wa kidugu chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 itakuwa ni ndoto kwa nchi nyingi Barani Afrika. Mwishoni, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linapenda kutoa salam za rambirambi kwa watu wa Mungu Barani Afrika walioguswa na kutikiswa na Corona, COVID-19. SECAM inaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake, ili waweze kuimarika na kuendelea kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. SECAM inawaweka watoto wake wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa Afrika!

SECAM: Ujumbe Mwaka Mpya 2021

 

 

03 January 2021, 15:33