Tafuta

2019.07.20 Hati mpya ya Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM 2019.07.20 Hati mpya ya Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM 

Januari 21,inawasilishwa Hati ya Kampala ya SECAM kuhusu Jubilei yake!

Hatimaye Maaskofu barani Afrika wanawasilisha 'Hati ya Kampala' ya miaka 50 ya SECAM,tarehe 21 Januari 2021 kwa njia mtandao kuanzia saa 3.30 asubuhi huko Burkina Faso na Ghana na saa 5.30 nchini Afrika Kusini na Msumbiji.Hati hiyo ni tunda baada ya Jubilei iliyoadhimishwa kuanza julai 2018 hadi Julai 2019.Baadaye itakabidhiwa kwa maaskofu na mapadre wa Afrika ili waweze kueneza kwa waamini wao.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Inaitwa “Hati ya Kampala” ambayo ni maandishi ya kuhitimisha Jubilei ya  SECAM (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar), iliyoadhimishwa kuanzia Julai 2018 hadi Julai 2019, kwenye tukio la kumbukumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo. Kwa mujibu wa Shirika la habari ACI Afrika, wamebainisha kuwa Hati hiyo itawasilishwa hadharani kesho, tarehe 21 Januari 2021  kwa njia  mtandao kuanzia saa 3.30 asibuhi huko Burkina Faso na Ghana na saa 5.30 nchini Afrika Kusini na Msumbiji. Sababu ya kuitwa jina hilo la Kampala ni kutokana na kwamba ni katika  mji mkuu wa Uganda, ambapo sherehe za mwisho za Jubilei ya miaka 50 ilifanyika kuanzia tarehe 19 hadi 29 Julai 2019.  Katika fursa hiyo rais wa Secam wa wakati huo, Kardinali Philippe Ouédraogo alisema kuwa “Hati hiyo itasaidia kuweka kasi ya Jubilei hai na itasaidia watu wa Mungu barani Afrika kuongeza ujuzi wao kuhusu Kristo Mwokozi wetu na kumfanya ajulikane kama njia, ukweli na maisha”.

Hati inawalenga watoto wote wa Afrika na wenye mapenzi mema

Naye Katibu mkuu wa SECAM, Padri Terwase Henry Akaabiam, aliunga mkono na alisisitiza kuwa “Hati hiyo italenga watoto wote kike na kiume wa Afrika na visiwa vyake, pia kwa watu wenye mapenzi mema wanaoishi mahali pengine. Wajumbe wote wa Kanisa, Familia ya Mungu katika bara la Afrika watajivunia hilo.” Nchini Burkina Faso, nchi ambayo Kardinali Ouédraogo, Askofu Mkuu wa Ouagadougou, anapotoa huduma yake ya kichungaji, uwasilishaji wa maandishi hayo utaona watu wapatao 150 wanaohusiana, lakini kwa kufuata sheria kali za kupambana na Covid: wale wanaohusika na Mawasiliano ya Kijamii, Maaskofu wakuu wa majimbo, mapadri wa parokia na wajumbe wao, vyombo vya habari vya kitaifa na wale wa Kanisa. Mwaliko wa wawakilishi wa kiutawala na kisiasa, na vile vile madhehebu mengine na dini, kama vile Waprotestanti na Waislamu, pia wanatarajiwa.

Tukio hili litafunguliwa kwa sala ya kuombea umoja wa kikristo

Tukio hili kwa njia ya mtandao  tafunguliwa na wakati wa sala ya kuombea  umoja wa Kikristo, kwani ni katika fursa ya  utamaduni wa Wiki hiyo ya Kuombea Umoja wa Kiristo, hadi  tarehe 25 Januari. Baadaye Kardinali Ouédraogo atawasilisha  hati hiyo. Uwasilishaji huo utatangazwa moja kwa moja kwenye Radio Maria, kwenye mitandao ya kijamii na kwenye jukwaa la Zoom kwenye kiunga kifuatacho: https://us02web.zoom.us/j/5478392297?pwd=NTYvU25XMTFtWHdCWHJNTlY1MWlvZz09.

Baada ya uwasilishaji inakabidhiwa maaskofu na mapadre kwa ajili ya waamini wao

Baada ya uwasilishaji wake, “Hati ya Kampala" itakabidhiwa kwa maaskofu na mapadre wa Afrika ili waweze kueneza kwa waamini wao. Kwa kufiriwa na maaskofu wa Kiafrika tayari wakati wa Mtaguso wa Pili wa Vatican ambao ulifanyika kati ya  1962 na 1965, SECAM ilizinduliwa rasmi tarehe 29 Julai 1969 katika Kanisa Kuu la Lubaga, nchini Uganda, wakati wa mchakato wa Mkutano wa kwanza wa Baraza kuu la Maaskofu wa Bara Afrika. Mkutano huo ulihitimishwa na Papa Paulo wa VI, katika siku hizo akiwa ziarani nchini Uganda, na Papa wa kwanza kwenda barani Afrika. Jubilei ya miaka 50 ya Baraza la Maaskofu iliongozwa na kaulimbiu “Kanisa-Familia ya Mungu Barani Afrika, Sherehekea Jubile yako! Mtangaze Yesu Kristo, Mwokozi wako”.

Sinodi mbili kuhusu Afrika na wosia baada ya sinodi kutoka kwa Mapapa wawili

Kwa mujibu wa Sinodi za Afrika za Maaskofu, zilizofanyika jijini Roma mnamo 1994 na 2009, zilihitimishwa kwa kuchapisha Wosia wa kitume baada ya sinodi: “Kanisa barani Afrika” wa Mtakatifu Yohane Paulo II na “Africae Munus” wa  Papa Benedikto XVI. Ikumbukwe kwamba, katika tukio la Jubilei, mnamo Julai 2019, Baba Mtakatifu Francisko alituma ujumbe wake kwa SECAM, uliosainiwa na Kardinali  Pietro Parolin, Katibu Vatican, ambapo alikumbusha huduma ya thamani iliyofanywa na kiungo cha maaskofu kwa  ajili ya Makanisa ya Afrika katika kuleta msaada katika  Bara lote, huku akibainisha hata  muungano wa kidugu ambao umeoneshwa kwa miaka 50 ya shughuli yake.

20 January 2021, 17:00