Tafuta

Jimbo Katoliki la Tanga linaomboleza kifo cha Monsinyo Jacob Pesambili Maganga aliyejipambanua kwa huduma za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania! Jimbo Katoliki la Tanga linaomboleza kifo cha Monsinyo Jacob Pesambili Maganga aliyejipambanua kwa huduma za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa la Tanzania! 

Monsinyo Maganga: Maisha na Utume Wake Kwa Watanzania!

Familia ya Mungu nchini Tanzania na kwa namna ya pekee Jimbo Katoliki la Tanga litamkumbuka sana Monsinyo Jacob Pesambili Maganga aliyezaliwa kunako mwaka 1944 na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 25 Juni 1972. Katika maisha yake amejipambanua kama: Mwalimu, Mlezi na Gambera na kwa miaka 12 amekuwa ni Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Tanga. RIP Baba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mwana wa Mungu katika hali ya kibinadamu aliyofungamana nayo, aliposhinda mauti kwa kifo chake na ufufuko wake, alimkomboa mwanadamu akamgeuza kuwa kiumbe kipya. (Rej. Gal 6:15; 2Kor 5:17). Maana kwa kuwashirikisha Roho wake, anawafanya ndugu zake waitwao kutoka katika mataifa yote kuwa mwili wake katika fumbo. Kwa njia ya Ubatizo waamini wanashiriki mauti na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka la Kifo na Ufufuko wa Kristo ambaye ndani mwake waamini wana tumaini moja. Mkristo anayekufa katika Kristo “huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Bwana”. Mama Kanisa anafundisha kwamba, kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, “kufanana” kamili na “sura ya Mwana kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi hata kama analazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi. Mama Kanisa anapenda kumsindikiza mtoto wake hadi mwisho wa safari zake, ili kumweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu, hakimu mwenye haki, mwingi wa huruma na mapendo.

Kanisa linapenda kumtolea Baba katika Kristo mtoto wake Monsinyo Jacob Pesambili Maganga, aliyekuwa ni Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Tanga kwa muda wa miaka kumi na miwili. Amefariki dunia tarehe 13 Januari 2021 kwenye Hospitali ya Mawenzi, iliyoko mjini Moshi, Kilimanjaro. Katika tumaini, Kanisa linaikabidhi ardhi mbegu ya mwili wa Monsinyo Maganga utakaofufuliwa katika utukufu. Bila shaka wengi watakumbuka maneno yake ya shukrani wakati wa mazishi ya Askofu Anthony Mathias Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga, kilichotokea tarehe 20 Desemba 2020 kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu na kuzikwa Jumanne, tarehe 29 Desemba 2020 na kuongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Alisema: “Kamnyama kakishikwa na mtego, hakazuii wengine kula. Maana yake, kifo cha Askofu Anthony Banzi hakiwazuii wengine kuendelea na utume! Hata baada ya kifo cha Monsinyo Jacob Pesambili Maganga, maisha na utume wa Kanisa vinazidi kusonga mbele kwa imani na matumaini!

Monsinyo Maganga alizaliwa kunako mwaka 1944 huko Mwakijembe, Muheza, Tanga. Alianza masomo ya elimu ya msingi mwaka 1951 na kuhitimu mwaka 1959 huko Kwediboma Middle School. Kunako mwaka 1960 hadi mwaka 1961 alijiunga na Chuo cha Ualimu Singachini, kilichoko mjini Moshi. Kati ya mwaka 1962 hadi mwaka 1963 alifundisha shule ya msingi ya Kibaranga. Hapa mbegu ya wito wa Kipadre ikaanza kukua na hatimaye, akaamua kujiunga na masomo pamoja na malezi ya Kipadre. Haikuwa rahisi kuacha kazi ya mshahara na kuingia tena darasani, lakini penye nia pana njia. Monsinyo Jacob Pesambili Maganga kati ya mwaka 1964 hadi 1965 akajiunga na Seminari ndogo ya Mtakatifu Maria ya Nyegezi, Jimbo kuu la Mwanza. Mwaka 1966 ulikuwa ni mwaka wake wa kujitafakari kuhusu wito wake wa Kipadre, mang’amuzi aliyoyafanya akiwa Parokiani Kongoi. Kati ya mwaka 1967 hadi mwaka 1968 akajiunga na Masomo ya Falsafa, Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Mwaka 1969 hadi mwaka 1972 akajiunga na Seminari kuu ya Kipalapala kwa ajili ya masomo ya kitaalimungu.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi mwaka 1972 akapewa Daraja ya Ushemasi. Tarehe 25 Juni 1972 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Tanga. Akaendelea na maisha na utume wake wa Kipadre, hadi mwaka 1976 alipotumwa kuongeza ujuzi na maarifa kwenye Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Zamani kilijulikana kama Chuo Cha Ualimu Chang’ombe, Dar es Salaam) na huko akajipatia stashahada ya ualimu. Kati ya mwaka 1972 hadi mwaka 1976 akatumwa kwenda kufundisha na kulea seminari ya Mtakatifu Petro, Jimbo Katoliki la Morogoro. Kati ya mwaka 1977 hadi mwaka 1981 akateuliwa kuwa: Mwalimu na Mlezi Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yosefu, Soni, Jimbo Katoliki la Tanga.

Tangu mwaka 1979 hadi mwaka 1981 alikuwa ni Gambera wa Seminari Ndogo ya Soni, Jimbo Katoliki la Tanga. Kati ya mwaka 1985 hadi mwaka 1989 alikuwa ni Paroko wa Kanisa kuu la Mtakatifu Athony wa Padua, Jimbo Katoliki la Tanga. Kati ya Mwaka 1989 hadi mwaka 1998 aliteuliwa kuwa ni mlezi wa maisha ya kiroho, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Nyegezi, “Nyegezi Social Training Institute”. Kati ya Mwaka 1989 hadi mwaka 2006 aliteuliwa kuwa ni Baba na mlezi wa maisha ya kiroho Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, Jimbo kuu la Mwanza.  Kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2008 akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia Manungu, Korogwe, Jimbo Katoliki la Tanga. Tangu mwaka 2008 hadi mauti yanamfika tarehe 13 Januari 2021, Monsinyo Jacob Pesambili Maganga alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Theresa na Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Tanga.

Monsinyo Maganga

 

 

14 January 2021, 14:51