Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inatarajia kukutana huko Jimbo kuu la Torino, Italia kuanzia tarehe 28 Desemba 2021 hadi tarehe 1 Januari 2022. Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inatarajia kukutana huko Jimbo kuu la Torino, Italia kuanzia tarehe 28 Desemba 2021 hadi tarehe 1 Januari 2022. 

Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè: 28 Desemba 2021-2022 Ni Huko Torino

Maadhimisho ya Mwaka 2020-2021 yamefanyika kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Hiki kimekuwa ni kipindi cha: Sala, tafakari ya Neno la Mungu, ibada, shuhuda, semina pamoja na ujenzi wa madaraja ya vijana kukutana, ili kuaminiana na kuthaminiana katika maisha yao, licha ya tofauti zao msingi, lakini wakitambua kwamba wote wanaunda familia moja ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 44 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè Barani Ulaya, yatafanyika kuanzia Jumanne tarehe 28 Desemba 2021 hadi Jumamosi, tarehe 1 Januari 2022, Jimbo kuu la Torino, nchini Italia. Hii ni fursa kwa Jumuiya ya Vijana wa Kiekumene wa Taizè kujenga umoja, ushirikiano na mshikamano hasa katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Maadhimisho ya Mwaka 2020-2021 yamefanyika  kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Hiki kimekuwa ni kipindi cha: Sala, tafakari ya Neno la Mungu, ibada, shuhuda, semina pamoja na ujenzi wa madaraja ya vijana kukutana, ili kuaminiana na kuthaminiana katika maisha yao, licha ya tofauti zao msingi, lakini wakitambua kwamba wote wanaunda familia moja ya binadamu. Ni tukio linalowawezesha vijana kukutana na mashuhuda wa imani kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya. Vijana wametakiwa kusoma alama za matumaini katika maisha yao.

Wakati wa warsha mbalimbali, vijana wamejadili kuhusu changamoto kubwa ya wakimbizi na wahamiaji duniani, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa wakimbizi na wahamiaji. Vijana wametakiwa kugundua mtazamo mpya wa matumaini, huku wakishirikiana na baadhi ya wakimbizi na wahamiaji. Vijana wamejadili kuhusu vita, ukosefu wa haki msingi za binadamu, chuki na hasira pamoja na umuhimu wa kujikita katika wongofu dhidi ya kinzani mbalimbali duniani. Vijana wamepata nafasi ya kusikiliza shuhuda mbalimbali za vijana wenzao ambao wamezama katika siasa. Ili kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao, vijana wanahitaji wongofu katika siasa. Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inawashirikisha vijana kutoka katika Makanisa na madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Kumbe, imekuwa ni nafasi ya vijana hawa kutafakari kuhusu maana ya Kanisa sanjari na mchakato wa majadiliano ya kiekume kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Katika kipindi hiki ambamo kuna maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, vijana wametafakari pia kuhusu hija ya imani na mashaka na wakajifunza mbinu ya kusali vyema zaidi.

Tarehe 28 Desemba 2020 vijana wa Jumuiya ya Taizè kutoka nchini Senegal wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Tarehe 31 Desemba 2020, vijana wa Taizè wamefanya mkesha kwa ajili ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2021. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu “Utamaduni wa Utunzaji Kama Njia ya Amani”. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu madhara ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, majanga asilia, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani, hali ngumu ya uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Katika kipindi hiki kumeibuka pia utaifa, chuki dhidi ya wageni, vita na kinzani mambo ambayo yanapelekea maafa na uharibifu, kumbe, utamaduni wa utunzaji ni kama njia ya amani ni muhimu sana kwa mustakabali wa maisha ya binadamu. Mungu Muumbaji ni kiini cha wito wa mwanadamu kutunza kama unavyofafanuliwa katika Maandiko Mtakatifu, yaani ulinzi wa Mungu kwa binadamu. Kuna uhusiano na mwilingiliano mkubwa kati ya maisha na mafungamano ya kibinadamu pamoja na mazingira. Haya ni mambo ambayo kimsingi  hayawezi kamwe kutenganishwa na udugu wa kibinadamu, haki na uaminifu kwa wengine.

Itakumbukwa kwamba, Siku ya 43 ya Vijana wa Kiekumene Barani Ulaya ilizinduliwa rasmi Jumapili tarehe 27 Desemba 2020 na kuhitimishwa tarehe Mosi, Januari 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tumaini kwa wakati unaofaa na usiofaa”. Maadhimisho ya Mwaka 2020-2021 yanafanyika kwa njia ya mitandao ya kijamii kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa vijana wa kiekumene Barani Ulaya katika maadhimisho ya 43, amewahakikishia uwepo wake mwanana kwa njia ya sala. Haya ni maadhimisho ambayo yamekuwa yakifanyika kwenye miji mikuu Barani Ulaya mwaka hadi mwaka na hivyo kuwawezesha vijana kutoka ndani na nje ya Bara la Ulaya kuweza kushiriki. Lakini kutokana na janga la homa la Virusi vya Corona, COVID-19, mwaka huu, vijana wanashiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii. Ni wakati wa kuonesha na kushirikishana kipaji cha ugunduzi na uwezo wao wa kufikiri.

Hata katika umbali uliopo kati yao, lakini vijana bado wameunganishwa “kuna connection kati yao” kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Hiki ni kipindi cha kusali, kutafakari pamoja na katekesi ya kina miongoni mwa vijana. Kauli mbiu ya Mwaka huu: “Tumaini kwa wakati unaofaa na usiofaa” itawasindikiza katika hija ya maisha yao katika kipindi cha mwaka 2021. Mawasiliano kwa njia ya mitandao ya kijamii ni kielelezo cha matumaini kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyofafanua kwenye Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anakaza kusema, hakuna mtu anayeweza kupambana na matatizo pamoja na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo katika hali ya upweke. Watu wanahitaji Jumuiya itakayowajengea uwezo na kuwasaidiana, ili kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutokuwa kati ya wale wanaopandikiza mbegu ya kukata tamaa, kwa kujenga kinzani na mipasuko ya kijamii; na hali ya kutoelewana; kwani kwa mwelekeo huu, watakuwa wanafisha nguvu ya matumaini kutoka kwa Kristo Mfufuka kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kinyume chake, vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, wawe ni watu waliojazwa matumaini yanayowakirimia ari na mwamko wa kumfuasa Kristo Yesu, kwa kufanya kazi pamoja na maskini na wale wote wanaohitaji msaada zaidi, husasan wale wanaokabiliwa na changamoto mamboleo, kiasi cha kujikatia tamaa katika nyakati hizi. Fadhila ya matumaini ina mwelekeo mpana zaidi kwani inaweza kuwafungulia na hivyo wakawa na upeo mpana unaovuka fikara za mtu binafsi, usalama tenge na faraja zake zinazoweka mipaka ya mtazamo wao na hivyo kuwafungulia mawazo mapana zaidi yanayosaidia kuboresha maisha na kuwa ni bora na yenye thamani. Matumaini ndiyo njia pekee wanayopaswa kuifuata na kuiambata. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa kutembea na kuambatana kwa pamoja katika mwelekeo mpana wa matumaini kama yalivyofunuliwa na Kristo Mfufuka. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za Kitume.

Jumuiya ya Taizè

 

01 January 2021, 14:24