Tafuta

Domenika ya Neno la Mungu: Neno la Mungu linalosomwa, kutafakariwa na kumwilishwa katika maisha ya kila siku, kama kielelezo cha imani tendaji! Domenika ya Neno la Mungu: Neno la Mungu linalosomwa, kutafakariwa na kumwilishwa katika maisha ya kila siku, kama kielelezo cha imani tendaji! 

Dominika ya Neno la Mungu: Neno la Mungu Katika Sala za Waamini

Dominika ya Neno la Mungu ni adhimisho la kutambua na kuonesha umuhimu wa Biblia katika maisha ya waamini na maisha ya Kanisa kwa ujumla. Kwa ajili ya umuhimu huo, dominika hii inatoa mwaliko kwa waamini kuchota kwa ajili ya Maisha yao yote hazina ya ufunuo wa Mungu iliyomo katika Biblia Takatifu na Zaidi ya hayo kuwa Hodari kuifundisha na kuitangaza hazina hiyo.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Kanisa limeweka dominika ya 3 ya Mwaka kuwa ni dominika ya Neno la Mungu. Mwaka 2020 lilikuwa ni adhimisho lake la kwanza na mwaka huu, 2021 ni la pili. Tunapozungumza juu ya Neno la Mungu, tunazungumza juu ya Biblia Takatifu. Kumbe adhimisho la dominika ya Neno la Mungu ni adhimisho la kutambua na kuonesha umuhimu wa Biblia Takatifu katika maisha ya waamini na katika maisha ya Kanisa kwa ujumla. Kwa ajili ya umuhimu huo, dominika hii inatoa mwaliko kwa waamini kuzidi kutamani kuchota kwa ajili ya Maisha yao yote hazina ya ufunuo wa Mungu iliyomo katika Biblia Takatifu na Zaidi ya hayo kuwa Hodari kuifundisha na kuitangaza hazina hiyo. Karibu ndugu mzikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya masomo ya dominika hii, masomo ambayo ni Neno lile lile la Mungu linalozungumza kwetu.

Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Yon 3:1-5,10) Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Yona. Tukikiangalia kitabu hiki katika ujumla wake tunaona kuwa ni kitabu ambacho kinabeba unabii kwa waisraeli katika kipindi ambacho walikuwa wametoka utumwani Babeli na wamerudi katika nchi yao. Kilikuwa ni kipindi ambacho wanajaribu kujenga upya taifa lao na hasa zaidi kujenga upya imani yao kwa Mungu aliyewaokoa kutoka huko utumwani walikokuwa. Ni kipindi ambacho pia tunaweza kusema, kilikuwa ni cha kuwakumbusha waisraeli yale mafundisho ya msingi ambayo tayari walikuwa wamekwishafundishwa na Torati ya Musa lakini pia na manabii wengine awali. Sasa, kitabu cha Yona – kati ya mafundisho yake mengi – kinakuja kukazia sifa kuu ya Mungu: amejaa huruma na neema. Hii ni sifa ambayo Mungu aliifunua kwa Musa na Musa akawafundisa waisraeli katika kitabu cha Kutoka 34:6 “Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli.” Tunaliona fundisho hili kwa sababu katika kitabu cha Yona, nabii mwenyewe ni kama vile alikuwa hataki watu wa Ninawi wasikie maonyo ya Mungu na watubu. Alipotumwa mara ya kwanza alikataa kwenda hadi akatumwa mara ya pili. Na hata alipofika hakuzungumza kama manabii tuliowazoea. Ni kama alikuwa anatoa ujumbe nusu nusu. Katika somo la leo anasema tu “baada ya siku 40 Ninawi utaangamizwa”. 

Lakini hata hivyo ujumbe huo huo ulitosha kabisa. Watu wa Ninawi wakatubu na Mungu akawasamehe. Kumbe somo hili la leo linamwonesha Mungu kuwa ni mwenye huruma na msamaha hata kuchukua yeye nafasi ya kwanza kuwasaidia watu kufikia kuomba toba. Ni somo linalotuonesha kuwa katika kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu sehemu kubwa anaifanya Mungu mwenyewe. Sehemu ya mwanadamu ni kuupokea ujumbe wa Mungu na kuufungua moyo wake kwa toba ya kweli. Somo la Pili (1Kor 7:29-31): Somo la pili la dominika hii ya Neno la Mungu, linatoka katika waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho.  Mojawapo ya mambo ambayo Paulo ameyazungumzia katika waraka huu ni mmomonyoko wa maadili uliokuwa umewakumba wakristo wa Korintho. Mmong’onyoko huu ulisababishwa kwa kiasi kikubwa na watu kupenda starehe na anasa. Katika somo hili la pili la leo, Mtume Paulo anawapa wakorintho kanuni ya maisha ambayo mkristo anapaswa kuifuata. Paulo hapendi kuwa ni mtu yule anayeonya tu, au anayelaumu au kulaani peke yake. Anatoa pia na suluhisho au njia ya kufuata ili kuepuka mtindo wa maisha anaoulaani.

Katika kutoa suluhisho, Mtume Paulo anawakumbusha wakorintho kuwa dunia na mambo yake yanapita. Na kwa Mtume Paulo, huu ni uhalisia ambao anaona utawasaidia wakorintho kutokujishikamanisha sana na dunia na mambo yake. Paulo hataki watu wajitenge na dunia. Anachotaka ni kwamba wawe na picha hiyo daima, picha ya uhalisia wa maisha ya duniani pale wanapohusiana na dunia na mambo yake. Huu ndio msingi wa maneno hayo anayoyarudia rudia katika somo hili: walio na wake wawe kama hawana, waliao kama hawalii, wafurahiao kama hawafurahi. Hayo maneno “kama…kama… kama…” ni maneno yanayomrudisha mtu kwenye fahamu zake pale anapotaka kuzama sana katika malimwengu, iwe ni kwa uzuri au kwa ubaya Somo hili, ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, linarejea fundisho lile lile la Yesu kwa mitume wake kuwa wao ni wakaaji wa ulimwenguni lakini sio wa ulimwengu huu.

Injili (Mk 1:14-20): Injili ya Marko tunayoisikia leo inamtangaza Yesu kuwa ndiye Habari Njema. Yesu amezunguka maeneo na maeneo kuhubiri Habari Njema ya Wokovu, lakini kimsingi Yeye ndiyo hiyo Habari Njema aliyokuwa anaihubiri. Yeye ndiyo ile habari ya wokovu ambayo Mungu aliwaahidi watu wake na Yeye ndio huo wokovu wenyewe. Ndiyo maana kama tunavyosikia katika injili ya leo, anapoanza tu kuhubiri anasema “wakati umetimia, ufalme wa Mungu umekaribia: tubuni na kuiamini Injili”. Hapa tunaona wazi utofauti kati ya Yesu na manabii wa Agano la Kale. Yesu anapotangaza Habari Njema hazungumzi kama walivyofanya manabii. Wao walikuwa wanasema “wakati unakuja…  ambapo Mungu atatenda hivi na hivi…” Yesu mwenyewe anasema “wakati umetimia”: kuonesha kuwa ni Yeye aliyesubiriwa na ni Yeye aliye wokovu wa watu. Mwinjili Marko anazidi kuionesha sura ya wokovu wa Yesu pale Yesu anapowaita wanafunzi wake wa kwanza na kuwaambia “Njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” Kumbe kazi anayoifanya Yesu ni ya uvuvi wa watu na anawaita wanafunzi wake ili nao waje awafanye wavuvi wa watu.

Katika Uyahudi, bahari au kwa ujumla maji mengi, yalionekana kama ni mojawapo ya makao ya Shetani, Ibilisi na hivi ni maeneo hatarishi kwa usalama wa watu. Mara kadhaa injili zimemuonesha Yesu akituliza dhoruba baharini ili tu kuonesha kuwa Yesu anazo nguvu za kuzinda nguvu za shetani anayetawala baharini. Katika taswira hiyo watu walio baharini ni watu walio chini ya nguvu za shetani, ni watu walio mateka. Kuwavua watu hao kutoka baharini ni kuwaokoa. Kumbe Yesu anapowaambia wafuasi wake kuwa atawanya wawe wavuvi wa watu maana yake ni kwamba anawaita ili awahusishe katika kazi yake ya kuwaokoa watu. Na wa kwanza kuokolewa ni wafuasi wenyewe kwa maana wao nao walikuwa baharini wakivua samaki. Kwa upande wa watu wenyewe sasa, kuanzia na wafuasi wenyewe, wokovu huu unahitaji utayari: “wakaziacha nyavu zao wakamfuata…wakamwacha baba yao pamoja na watu wa mshahara wakamfuata.” Inarudi katika injili hii dhamira ya toba na utayari wa watu wa Ninawi na inarudi tena dhamira ya mafundisho ya Mtume Paulo kwa wakorintho – kutokujishikamanisha na dunia na mambo yake.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tumepata ufafanuzi wa masomo ya dominika hii ya 3 ya mwaka ambayo pia ni dominika ya Neno la Mungu. Ni dominika ambayo kama tulivyokwisha eleza hapo awali, inatualika kuutambua na pia kuudhihirisha umuhimu wa Biblia Takatifu katika maisha ya mkristo na katika maisha ya Kanisa kwa ujumla. Baba Mtakatifu Francisko, wakati akitangaza kuanza kuadhimishwa dominika ya Neno la Mungu, aliandika waraka wa kitume (Aperuit illis). Katika waraka huo alieleza mambo mengi kuhusu dominika hii na akatoa pia dondoo za tafakari katika kuwasaidia waamini kuiishi vema roho ya dominika ya Neno la Mungu. Katika tafakari ya leo, ninawaalika kuchota kipengele kimoja tu kati ya vingi alivyovizungumzia. Kipengele hicho ni kile anachokiita “kusali pamoja na Biblia”.

Biblia Takatifu ni mkusanyo wa ufunuo wa Neno la Mungu. Mkusanyiko huu umewekwa katika vitabu mbalimbali kulingana na historia kadiri ambavyo Mungu alivyojifunua kwa watu wake na kadiri ambavyo watu wenyewe walivyoupokea ufunuo huo. Mwingiliano huo kati ya Mungu na watu wake ni sala. Kwa maana sala ni nini – ni mazungumzo kati ya mtu na Mungu, ni mawasiliano kati ya mtu na Mungu na ni mahusiano kati ya mtu na Mungu. Ufunuo huo wa Mwenyezi Mungu ni hai. Mungu anaendelea kuzungumza katika Neno lake. Kumbe kulisoma tu Neno la Mungu katika moyo huu wa kuingia katika mazungumzo na Mungu, ni sala. Papa anapotualika kusali pamoja na Biblia hamaanishi kufanya kitu cha pekee. Anatualika kujua kuwa tunapoishika Biblia na kuisoma hatuisomi kama kitabu cha historia au kama kitabu cha matukio, tunaingia katika mahusiano na Mungu – tunaingia katika uwepo wa Mungu kwa maana Mungu mwenyewe anazungumza pale Neno lake linaposomwa au kusikilizwa.

Mara nyingi sana tumesikia watu wanasema “mimi sijui kusali au siwezi kusali” au mara nyingine tunapohitaji kusali basi tunabaki tu katika zile sala rasmi zilizoandaliwa na Kanisa. Hiyo ni sawa lakini pia mtu anaweza tu kufunua Biblia na akasoma kifungu kidogo katika moyo wa sala na akapata mastahili yale yale ya sala. Vipo vitabu katika Biblia ambavyo moja kwa moja ni vya sala, kama vile Zaburi na pia vipo vifungu vingine ambavyo katika Agano la Kale na Agano Jipya ambavyo pia ni sala. Mwaliko wa Papa ni mwaliko wa kuviendea vifungu hivyo pale tunapokuwa hatuoni maneno mazuri zaidi ya kusali tukavitumia hivyo kama sala zetu. Kusoma Biblia kwa namna hii kumewaongoa wengi, kumewasaidia wengi kuwa karibu na Mungu na kumewajaza wengi na ufahamu wa ufunuo wa kimungu, ufunuo ambao daima umekuwa ni taa na mwanga katika njia za maisha. Tusali pamoja na Biblia tuongozwe nayo katika maisha yetu.

Liturujia J3

 

 

 

22 January 2021, 16:24