Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC: Tahadhari juu ya maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19 na Ugonjwa wa Uviko, COVID-19. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC: Tahadhari juu ya maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19 na Ugonjwa wa Uviko, COVID-19.  (©Romolo Tavani - stock.adobe.com)

Maaskofu Katoliki Tanzania: Tahadhari Dhidi ya Virusi vya Corona

TEC: Tusiache kuwashauri na kuwaongoza taifa la Mungu katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona. Tuhimize mapambano dhidi ya Virusi vya COVID-19 kwa kutumia silaza zote za kiroho, kimwili, kisayansi na za kijamii. Tusikome kuhimiza sala, kuepuka kugusana, kunawa na kujitakasa kila wakati, kuchukua hatua tuonapo dalili za ugonjwa na kuepuka misongamano hatarishi.

Na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, - Dar Es Salaam.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tunapenda kukushirikisha waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuhusu tahadhari juu ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Itakumbumbwa kwamba, Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Kuu la Arusha katika Waraka wake wa kichungaji kuhusu gonjwa la Corona, COVID, -19 kwa kifupi, amesema kwamba kutokana na hali halisi ya kuwepo na ugonjwa wa Corona, COVID-19 katika jamii, inatupasa kujenga utamaduni na tabia mpya za kujinusuru kwa vingine kwa hakika tunatembea sasa pekupeku juu ya mbigili!Tutafakari hali halisi kwani mwenye macho haambiwi tazama! Lengo la Waraka huu ni kumwalika kila mtu ajisimamie kwa usalama wake binafsi na kujali usalama wa wengine.

Corona, COVID-19 inatikisa ulimwengu wote na sisi tusijidanganye kiasi cha kutokuchukua tahadhari. Tusimjaribu Mungu kwa kufanya uzembe na afya zetu. Turejee tahadhari za kuzuia maambukizi bila kuwa na hofu: Hakuna haja ya kufungiwa. Tuendelee kusali na kuchukua tahadhari, tunawe mikono, tuvae barakoa ikibidi na kuepa mkusanyiko wa watu wengi. Ukiona unawashwa kwenye koo, kukauka koo, kuwa na kikohozi kikavu, joto kubwa na kupumua kwa taabu haraka mwone daktari ili usaidiwe.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema: Ninayo heshima kuwaandikia barua hii yenye somo la “Tahadhari juu ya Maambukizi Mapya ya Virusi wa Corona, COVID-19 na ugonjwa wa uviko-19 (COVID-19)”. Tangu Mwaka 2020, tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha tunazuia kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Baadhi ya hatua hizo zilikuwa za kufanya sala, kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotutaka tunawe mikono kila wakati, tutumie vitakasa mikono, tuzingatie kanuni za afya katika kukohoa ua kipiga chafya na kuepuka kusogeleana, kugusana na kusongamana. Kwa mwaka 2020 nchi yetu ilifanikiwa katika mapambano haya dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Visa vya maambukizi ya Corona, COVID-19 vilipungua na baadae tukaamini tumeshinda. Bila shaka mafanikio hayo yalitokana na tumaini letu la dhati kwa Mwenyezi Mungu, heshima yetu kwa miongozo ya kitaalamu na kujali kwetu. Tunamshukuru Mungu na wote waliotusaidia.

Mwaka huu wa 2021 kuna wimbi jipya la maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Nchi kadhaa zimethibitisha kuwa zinapitia kwenye kipindi kigumu cha kuenea kwa Corona, na kutokea kwa vifo vya watu. Nchi yetu sio kisiwa. Hatuna budi kuzingatia hekima ya wahenga kuwa "mwenzio akinyolewa wewe tia maji." Hatuna budi kujihami, kuchukua tahadhari, na kumlilia Mungu kwa nguvu zaidi ili janga hili lisitukumbe. Kwa uhalisia huo, tusiache kuwashauri, kuwahimiza na kuwaongoza taifa la Mungu katika mapambano haya dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Tuhimize mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kutumia silaza zote za kiroho, kimwili, kisayansi na za kijamii. Tusikome kuhimiza sala, kuepuka kugusana, kunawa na kujitakasa kila wakati, kuchukua hatua tuonapo dalili za ugonjwa na kuepuka misongamano hatarishi. Ninamwomba Mungu atulinde na kutuwezesha kubaki salama katika vita hii dhidi ya janga la kiafya.

Tahadhari ya Corona

 

29 January 2021, 13:05