Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania: Waraka Kuhusu Gonjwa la Corona, COVID-19 na umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kulinda maisha. Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania: Waraka Kuhusu Gonjwa la Corona, COVID-19 na umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kulinda maisha.  (AFP or licensors)

Waraka wa Kichungaji: Gonjwa la COVID-19 Jimbo Kuu la Arusha

Askofu mkuu Amani anasema: Ushirikiano ulikuwa mkubwa na Mwenyezi Mungu akabariki juhudi zetu. Kutokana na watu wengi kuitikia mwaliko wa kuzingatia kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni pamoja na vitakasa mikono pamoja na tahadhari nyingine tulifaulu kuzuia maambukizi kwa sehemu kubwa. Yatupasa tumshukuru Mungu. Hata hivyo tuliambiwa ugonjwa bado upo.

Na Askofu mkuu Isaac Amani Massawe, Jimbo Kuu la Arusha, - Tanzania.

Awali natumia fursa hii kuwatakieni nyote heri na baraka kwa mwaka mpya 2021. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na kutupatia natasi ya kuendelea kumtumikia katika jamii. Nimesukumwa na dhamiri njema kuwapelekea Waraka huu Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Arusha, nikirejea hasa waraka wangu wa tarehe 25.04.2020. Waraka huo uliweka bayana mambo ya kufanya binafsi na kijumuiya ili kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ushirikiano ulikuwa mkubwa na Mwenyezi Mungu akabariki juhudi zetu. Kutokana na watu wengi kuitikia mwaliko wa kuzingatia kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni pamoja na vitakasa mikono pamoja na tahadhari nyingine tulifaulu kuzuia maambukizi kwa sehemu kubwa. Yatupasa tumshukuru Mungu. Hata hivyo tuliambiwa ugonjwa bado upo.

Baadaye baadhi ya masharti yalilegezwa tukaweza kusali Misa, kurejesha mikutano ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na mafundisho ya Komunyo ya kwanza na Kipaimara. Tulihimizwa kuendelea na matendo ya kuzuia maambukizi hasa kuzingatia usafi mpaka ugonjwa utakapoondoka kabisa. Kwa hiyo safari bado ipo. Hali inavyoonekana sasa ni kwamba mahali pengi watu wamejitangazia kwamba hakuna Corona, COVID-19 na hivyo hakuna haja ya tahadhari. Maji ya kunawa mikono Makanisani yameondolewa na mahali pengine yapo lakini watu hawanawi tena kwa imani kwamba hakuna Corona, COVID-19. Ile tahadhari ya kujizuia kushikana mikono watu wamejiondolea wao wenyewe kwa imani kwamba hakuna Corona, COVID-19.

Ule utaratibu wa kutoa sadaka baada ya Komunyo na kukomunika mikononi, watu wamejiondolea kwa imani kwamba maambukizi hayapo tena. Mapadre na watawa walihimizwa kuwa waangalifu zaidi ili wasisababishe maambukizi kati yao wenyewe au kwa watu wanaowahudumia. llihimizwa pia kuvaa barakoa kwenye vyombo vya usafiri wa watu wengi, sokoni, kwenye ibada na hospitalini kwa sababu barakoa ni kinga bora ya maambukizi hata ya mafua ya kawaida. Kwa kifupi, kutokana na hali halisi ya kuwepo na ugonjwa wa Corona, COVID-19 katika jamii, inatupasa kujenga utamaduni na tabia mpya za kujinusuru kwa vingine kwa hakika tunatembea sasa pekupeku juu ya mbigili! Tutafakari hali halisi kwani mwenye macho haambiwi tazama!

Lengo la Waraka huu ni kumwalika kila mtu ajisimamie kwa usalama wake binafsi na kujali usalama wa wengine. Corona, COVID-19 inatikisa ulimwengu wote na sisi tusijidanganye kiasi cha kutokuchukua tahadhari. Tusimjaribu Mungu kwa kufanya uzembe na afya zetu. Turejee tahadhari za kuzuia maambukizi bila kuwa na hofu: Hakuna haja ya kufungiwa. Tuendelee kusali na kuchukua tahadhari, tunawe mikono, tuvae barakoa ikibidi na kuepa mkusanyiko wa watu wengi. Ukiona unawashwa kwenye koo, kukauka koo, kuwa na kikohozi kikavu, joto kubwa na kupumua kwa taabu haraka mwone daktari ili usaidiwe.

Mimi sio daktari ila ni mchungaji. Tunapoendelea na Mwaka huu wa Mtakatifu Yosefu aliyelisha na kulinda Familia Takatifu, natoa tahadhari hii ili mwenye kujali ajue Waraka umeandikwa kwa ajili ya kuhimiza kuwajibika na kushirikiana katika Kristo kwa jambo linalohusu uhai kwa kusoma alama za nyakati. Natumaini mtaupokea ujumbe kwa dhamiri njema na kuuzingatia mara moja ili tuendelee kutumikia Taifa na Kanisa. Nawatakieni baraka na fanaka tele kwa Mwaka Mpya wa 2021. Wenu Katika Kristo, Mhashamu lsaac Amani, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha.

Jimbo Kuu Arusha
28 January 2021, 14:33