Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Mkesha wa Sherehe ya Noeli: Fumbo la Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Tafakari ya Neno la Mungu, Mkesha wa Sherehe ya Noeli: Fumbo la Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. 

Tafakari ya Neno la Mungu: Mkesha wa Sherehe ya Noeli: Mkombozi!

“Mungu aliniambia: Wewe ni mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako”. Ni Antifona inayotualika kuadhimisha sherehe ya Umwilisho wa Mungu wa kuwa mwanadamu na kukaa kati yetu. Ni sherehe ya fumbo la Umwilisho wa Mungu, Mungu anayetwaa mwili wetu na kuwa sawa na sisi isipokuwa hakuwa na dhambi, ni Mungu anayefanyika mwanadamu katika historia ya watu wake.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! “Dominus dixit ad me: Filius meus es tu, ego hodie genui te” Ndio maneno ya lugha ya Kilatini ya Antifona ya mwanzo ya mkesha huu wa Noeli, kutoka Kitabu cha Zaburi 2:7. “Mungu aliniambia: Wewe ni mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako”. Ni Antifona inayotualika kuadhimisha sherehe hii kubwa ya Mungu kuzaliwa kati yetu, ya Mungu kutwaa Mwili na kukaa kati yetu, ni sherehe ya Umwilisho wa Mungu wa kuwa mwanadamu na kukaa kati yetu. Ni sherehe ya fumbo la Umwilisho wa Mungu, Mungu anayetwaa mwili wetu na kuwa sawa na sisi isipokuwa hakuwa na dhambi, ni Mungu anayefanyika mwanadamu katika historia ya mwanadamu. Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu.” Ni kwa kuanza na maneno hayo, Mwinjili Luka anaanza simulizi lake ya jinsi na wapi alizaliwa Yesu Kristo. Mwinjili anatueleza kwa nini Yesu alizaliwa Bethlehemu badala ya Nazareti. Kaisari hakuwa na habari yeyote juu ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, ila ni kutokana na amri yake Yesu anazaliwa katika mji ule uliotabiriwa kuwa kwao atazaliwa Masiha, yaani, mji wa Daudi.

Mwinjili Luka anaonesha tangu mwanzo kuwa kuzaliwa kwake Yesu kunaingia katika historia ya ulimwengu mzima. Na ndio tunaona agizo la Kaisari liligusa watu wote walioishi katika dola la Kirumi, ambayo nyakati zile ilionekana kuwa ni sawa na ulimwengu mzima. Ni wakati wa Kaisari Oktaviano Augusto, wanahistoria wanatuambia kulikuwa japo na amani katika dola zima la Kirumi na hivyo mtawala yule anatoa agizo la kuhesabiwa watu wote. Augusto kama mtawala alitaka tangu mwanzo kujitofautisha na watawale wengine wa Kirumi. Ni kutokana na kuzaliwa kwake, Augusto alitaka awe kweli “soter”, neno la Kigiriki lenye maana ya “mkombozi”, kwa kuwa mtawala anayeleta amani kwa dola zima la Kirumi. Siku ya kuzaliwa kwake Augusto ionekane kuwa ni siku ya mwanzo wa habari njema, yaani, “eungelion”, Lakini pia mtawala Augusto alipewa jina la Kigiriki la “sebastos”, yaani, “muabudiwa”, pia “soter”, likiwa na maana ya mkombozi kama nilivyotangulia kusema hapo juu. Majina haya ya Kimungu yalitumika pia kwa Augusto. Aliyejihesabu kama “mkombozi”, kwa kuwa kwa njia yake alileta amani katika utawala wake. (natus ad pacem – aliyezaliwa kwa ajili ya amani).

Mwanahistoria Virgilio anatuonesha kuwa siku ile ya kuzaliwa kwa Kaisari Augusto, tarehe 23 Septemba kuwa ni mwanzo mpya kwa wakazi wote wa dola ya Kirumi. Ni wakati wa utawala wake kumekuwa na amani baada ya vita vya miaka mingi vya watangulizi wake. Augusto alitaka pia kuhesabiwa na watu wake kama mungu, kwa kuwa mjumbe wa amani, alitaka aonekana na kuhesabiwa kama mkombozi, “soter”. Mwinjili Luka katika masimulizi ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, anatuonesha kuwa ni tukio la kihistoria, lililojiri katika muktadha wa kihistoria na pia kijiografia. Ni nia ya Mwinjili Luka kutuonesha jinsi kuzaliwa kwake Yesu ni kuingia katika historia ya ulimwengu mzima. Ni Mungu anayetwaa mwili na kuishi pamoja nasi katika mazingira yetu na hali zetu zote.

Yesu anazaliwa katika mji wa Daudi, Bethlehemu, kimsingi ni kijiji cha wachungaji au wafugaji. “Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba.” Ni Bethlehemu, Wayahudi walimsubiri Masiha. Yohane 7:40-43. Na pia tayari Nabii Mika alishatabiri juu ya Bethlehemu; “Lakini wewe Bethlehemu katika Efratha, wewe ni mdogo tu kati ya jamii za Yuda, lakini kwako kutatoka mtawala atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu.” Mika 5:1 Ndio kusema pia Mwinjili Luka anajaribu pia kutuonesha kuwa tukio la kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo, sio tukio la kubuniwa au kupikwa bali ni tukio la kweli lililojiri na kutokea katika historia ya mwanadamu, na ndio maana tangu mwanzoni anatuonesha hata wakati na pia jiografia nzima ya tukio lenyewe. “Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.”

Mwinjili Luka anatuonesha hata tukio la kuzaliwa kwake mtoto Yesu, ni tukio la kuzaliwa kama watoto wengine wote. Na mama yake anakuwa kama mama wengine wote wanapozaa kwa kumlinda na kumvisha mtoto nguo za kitoto ili kumkinga na baridi na hatari nyingine. Mwinjili Luka anazidi kutuonesha jinsi Yesu alivyozaliwa katika mazingira duni na ya kimaskini. Ni kutuonesha jinsi upendo wa Mungu ulivyo kwa mwanadamu aliye duni na dhaifu. Ni Mungu anayekubali kuzaliwa sio katika majumba ya kifahari bali katika hali duni kabisa. Ni Mungu anayezaliwa na binti mdogo wa Kiyahudi n asio katika familia za kifalme na watawala wa nyakati zile. Ni Mungu anayejifunua katika hali duni kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu. Noeli ya mwaka huu 2020 inatukuta pia katika mazingira magumu na tafakarishi hasa kutokana na janga la COVID19 linaloendelea kutikisa dunia nzima. Ni katika nyakati hizi, mwanadamu anagundua udogo na unyonge wake, anagundua pia maisha yeti hapa dunia ni ya mpito, ni ya muda mfupi tu, na hivyo tunazidi kumuomba Mungu atujalie hekima ya kuhesabu uchache wa siku zetu, kutujalia neema ya kupenda kutafakari umilele, maisha ya kweli, ndio maisha ya kweli ya kuungana na Mungu na kukubali kuongozwa naye.

Labda hata nasi leo mara kadhaa tunatarajia Mungu anayejifunua na kuongesha kuwa ni mwenye nguvu, anayeogofya kwa enzi na ukuu wake, lakini Yesu anazaliwa katika mazingira tofauti kabisa na hayo. Ni Mungu anayefanyika mwanadamu kweli, anakuwa mtoto mchanga asiyekuwa na uwezo sio tu wa kujitetea bali hata kuongea kwa niaba yake, ni mtoto mnyonge n aduni anayejikabidhi katika mikono ya binti mdogo Mariamu. “Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu.” 1Wakorintho 1:23. Ni Noeli inayotualika sisi sote kumwangalia kila mmoja anayekuwa duni na mnyonge katika ulimwengu wetu wa leo. Ni Yesu anatualika kuwakazia macho na kuwa wajumbe wa upendo wa Mungu kwa wale wote wanaokuwa wadogo n aduni, wanaokuwa maskini na wahitaji zaidi yetu. Na ndio maana ya Noeli, ni sisi kukubali kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, kukubali kuongozwa sio na mantiki za ulimwengu huu bali ule wa Mungu mwenyewe. Kuwa wajumbe wa upendo wa Mungu kwa kila mmoja tunayekutana naye, kuwa wajumbe wa habari njema, kwa njia yetu wengine waweze kukutana na Yesu Kristo, aliye kweli asili ya upendo, haki na amani ya kweli.

Sehemu ya pili ya Injili ya leo, tunajikuta tupo katika mazingira ya nje, ndio katika makonde, na hapo tunakutana na wachungaji na malaika. “Na katika nchi ile ile walikuwapo wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.” Ni wachungaji wanakuwa wa kwanza kupata habari njema ya kuzaliwa kwake mtoto Yesu. Swali ni kwa nini wao wanakuwa wa kwanza kupashwa habari hii kuu na njema? Wachungaji hawakuwa watu walioheshimika wala kuhesabika kuwa watu wa maana katika mazingira ya Kiyahudi. Wachungaji walihesabiwa kuwa ni watu najisi, kwani maisha yao ya kila siku hayakutofautiana sana na ya wanyama waliowachunga. Hivyo hawakuruhusiwa kuingia hekaluni kusali, hata pia hawakuweza kutoa ushahidi mahakamani, kwani walionekana kuwa ni watu waongo, wasio wakweli wala wanyofu, wezi na hata watu wa kutumia mabavu na fujo. Marabi waliona wachungaji ni kama watoza ushuru, kwao ilikuwa ni ngumu kuokoka kwani walitenda maovu mengi kiasi kwamba hata wao wenyewe wasingeweza kujua ni mara ngapi wametenda maovu hayo. Hivyo walikuwa ni watu wa kuangamia milele. “Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yetu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.”

Ndio kusema Mwinjili Luka anatuonesha kuwa mwanzo wa Habari Njema na Mkombozi na Mwokozi wa kweli sio Kaisari Oktaviano Augusto bali ni Yesu Kristo. Ni kwa kuzaliwa kwake Yesu, hapo kweli kunakuwa na mwanzo wa Habari Njema, Habari ya Furaha, “Euangelion”. Kuzaliwa kwake Yesu ni Habari Njema kwa wale wote waliokuwa bado gizani, mathalani wachungaji, wale walioonekana na kuhesabiwa kuwa wa mwisho n aduni kabisa. Ni Habari Njema kwa kila mmoja anayejiona kuwa duni na wa mwisho, Kristo anajifunua kwa nafasi ya kwanza sio kwa watawala wa kifalme, au viongozi wa dini bali kwa moja ya makundi duni kabisa katika ulimwengu ule. Yesu hata anapoanza kazi yake hadharani anabaki kuwa karibu zaidi na makundi ya wale waliohesabika kuwa waovu na wadhambi, kuwa duni na dhaifu katika jamii. Anatumia lugha yao, hata kula na kunywa pamoja nao, na kuwatembelea katika nyumba zao, anajipambanua kuwa pamoja nao, Yeye ni Emanuele, ni Mungu pamoja nasi. Ni Mungu anayekuja katika uduni na umaskini wetu iwe wa kimwili na hata kiroho ili nasi tuweze kupata hadhi ya kufanyika kuwa wana wa Mungu.

Na hata ishara wanayopewa wachungaji ni ya kustaajabisha, kwani hatusikii wakiambiwa kuwa watakuta kitu cha ajabu ili waweze kumtambua mtoto na badala yake; “Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.” Sifa moja kubwa ya mtoto huyu sio enzi na ufalme au utajiri bali ni mtoto anayezaliwa katika mazingira duni na fukara kabisa na hivyo anajipambanua kama fukara na duni kati ya fukara na duni. Na ndio Noeli pia ya mwaka huu tunaalikwa kutafakari tena tunapoalikwa kuisherehekea sio kwa sherehe za anasa, za kula na kunywa bali kwa kurudi na kuingia ndani mwetu na kuangalia upya mahusiano yetu na Mungu na jirani, hasa mahusiano na wale wote wanaokuwa katika duni na maskini kabisa. Katika baadhi ya mataifa duniani, Noeli inasherehekewa katika mazingira ya “Lockdown”, ni mwaliko wa kurejea katika hali ile ile aliyozaliwa naye Bwana wetu Yesu Kristo, katika pango la kulishia wanyama. Mateso na mahangaiko yetu yanapata umaana ikiwa tunakubali kumtafakari Yesu Kristo. Mtoto anayezaliwa ni mkombozi na mwokozi, anazaliwa ili kuwakomboa na kuwaokoa wale wote wanaokuwa katika hali duni iwe kiroho na hata kimwili.

Ni mtoto anayezaliwa kwa ajili yetu, ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu, hivyo hatuna budi kumpokea ili atukumboe, ili atutoe katika hali zetu duni, ndio giza la maovu na madhambi, hatuna budi kumpokea kwa kukubali kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, kwa kukubali kuongozwa naye aliye kweli Neno la Mungu, anayefanyika mwili na kukaa kati yetu. “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Hii ndio zawadi ya kweli ya Noeli, amani ya Mungu kwetu. Amani katika maisha ya kila mmoja wetu, lakini amani na watu wanaotuzunguka iwe katika familia, ndugu, jamaa na majirani, amani na watu wote pia. Noeli ni maadhimisho ya kuzaliwa kwake Mfalme wa amani, yaani, Kristo Bwana, hivyo hatuna budi nasi kuwapa wengine zawadi ya amani. Zawadi ya kweli ya Noeli, ni amani. Kila mmoja wetu hanabudi kuwa mjumbe na balozi wa amani, wengine wanapokutana nami wakutane na amani ya Mtoto Yesu. Ninawatakia maadhimisho mema ya Noeli, yawe ya baraka kwa kila mmoja wetu.

24 December 2020, 18:30