Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Noeli, Misa ya Mchana: Fumbo la Umwilisho. Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Noeli, Misa ya Mchana: Fumbo la Umwilisho. 

Sherehe ya Noeli: Misa ya Mchana: Fumbo la Umwilisho: Huruma na Upendo wa Mungu!

Fumbo la Umwilisho: Neno wa Mungu kutwaa mwili na kukaa kwetu. Ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa amani. Kazi ya mfalme ni kutawala na kuongoza. Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwa Mungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu hapa duniani; utawala wa haki, upendo, umoja na amani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Katika adhimisho la sherehe ya Noeli Mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana. Kila misa ina sala na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo ajili ya Misa ya mchana. Katika wimbo wa mwanzo tunaimba; Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu (Isa.9:6) na katika sala mwanzo tunasali; Ee Mungu, ulimweka mwanadamu katika cheo cha ajabu, na tena ukamtengeneza upya kwa namna ya ajabu zaidi. Tunakuomba utjalie kushiriki umungu wake, yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu. Noeli ni sherehe ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa binadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa amani. Kazi ya mfalme ni kutawala na kuongoza. Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwa Mungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu hapa duniani; utawala wa haki, upendo, umoja na amani. Ni Mungu aliyetwaa sura, umbo na mwili wa kibinadamu na kuzaliwa kati yetu kama mtoto mchanga.

Kwa kuzaliwa kwake ukombozi wetu umetimia, na nuru imeushukia ulimwengu kama alivyotuambia Nabii Isaya katika somo la kwanza la Misa ya usiku akisema; watu wale waliokwenda katika giza, wameona nuru kuu, wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza. Nuru hii inamwangazia kila anayeipokea ili aweze kuona njia ya kwenda Mbinguni kwa Mungu Baba, maana kila anayeipokea Nuru hii, kwake huondolewa giza la dhambi. Katika somo la kwanza la nabii ya Isaya; Mungu anatangaza ukombozi kwa Wayahudi kutoka utumwani Babeli. Kwa kinywa cha Nabii Isaya Mungu anawafariji na kuwapa moyo waisraeli akiwahakikishia kuwa ukombozi wao umefika, kwani kwa nguvu ya mkono wake watarudi tena Yerusalemu, “Yerusalemu mpya”. Ujumbe unaopelekwa ni huu, “ukombozi wenu umefika yaani amani imefika vita sasa vimekwisha, utumwa umekwisha. Utumwa wao ni mfano wa hali ya dhambi na ukombozi wao ni mfano wa ukombozi wa mataifa yote kutoka dhambini. Nabii Isaya anatoa wasifu wa mjumbe wa amani akisema; “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, aletaye habari njema ya mambo mema, yeye autangazaye wokovu, auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki.” Huyo ndiye Yesu mfalme wa amani, Emmanueli, Mungu pamoja nasi.

Somo la pili la Waraka kwa Waebrania linadhibitisha kuwa; “Utabiri wa kale umetimia katika Yesu Kristo. Katika yeye utukufu wa Mungu umefunuliwa na ni katika yeye tu Mungu anaongea nasi akisema; “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwanaye, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.” “Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu.” Kumbe mtoto Yesu ni chapa ya Mungu ambaye tangu kuanguka kwetu dhambini anatutafuta kutukomboa. Manabii walitabiri zamani na sasa waliyotabiri yanakamilishwa ndani yake. Injili ni mafundisho msingi ya imani yetu juu ya maisha ya Yesu Kristo alivyoishi katika nchi ya Uyahudi, aliyofundisha, alivyoteseka, akafa, akafufuka siku ya tatu na kupaa mbinguni baada ya siku arobaini.

Lakini kila Mwinjili ana namna yake ya kuanza na kuishia katika uandishi. Injili ya Marko haijishughulishi na habari ya kuzaliwa kwake Yesu, bali inaanza ikimuonesha Yesu akihubiri habari njema. Injili za Mathayo na Luka zinaanza kwa habari za fumbo la umwilisho; Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Injili ya Yohane mwanzo na asili ya Yesu Kristo ikisema; “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Mtume Paulo katika barua yake Flp. 2:6-7 anasema; “Yeye kwa asili alikuwa daima mungu, lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu, bali kwa hiyari yake mwenyewe aliachilia hayo yote akajitwalia hali ya mtumishi akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu”.

Lengo la kutwaa ubinadamu wetu ni kutaka kutuinua ili tuwe kweli watoto warithi wa Mungu. Neema hii ya kuwa watoto wa Mungu, hupewa wale wazishikazo amri za Mungu na kufanya mapenzi yake. Kwa kuamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu tutaamini pia kuwa yeye ni chanzo cha neema, ukweli na uzima.  Neno alitwaa mwili akakaa kwetu: Yesu Kristo kwa kuchukua ubinadamu wetu, hakupunguza Umungu wake, alikuwa Mungu, anaendelea kuwa Mungu. Alikaa kwetu kama binadamu, akaishi kama binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Mungu amejidhihirisha kwetu kwa njia yake na katika yeye tumepokea neema juu ya neema kwa mkono wake. Noeli ni sherehe ya matumaini kwa wale wote wanaokandamizwa na dhambi, na ibilisi na uovu; wagonjwa, masikini, wasiojua mema na mabaya, mafisadi, makahaba, wezi, wakimbizi, mateka wa vita, wanaoumia kwa unyanyapaa, watoto wanaofanyishwa kazi kubwa na za aibu, wenye kukandamizwa na janga la rushwa na hongo, wale wanaodhuluwa haki zao, yatima, wajane, maskini, walemavu na kadhalika.

Hawa ndio wanaokwenda katika giza na kukaa katika nchi ya uvuli wa mauti. Hawa ndio wanaotamani kuona nuru inawaangazia. Ni wajibu wa Kanisa likishirikiana na serikali na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha hawa watu wanapata ukombozi, na kurudishiwa hadhi yao. Kumbe Kanisa linaendeleza kazi ya Kristo katika kumwinua binadamu kiroho, kimaadili, kimwili, kiakili na kijamii ili awe karibu zaidi na Mungu aliye asili ya hadhi na heshima yake. Serikali za dunia zenye umakini na siasa safi kama anavyosisitiza Papa Francisko katika sura ya tano ya waraka wake wa kitume, “Fratelli tutti” yaani sisi sote ni ndugu zinapswa kushirikiana na Kanisa katika kuondoa, kutokomeza ujinga, umaskini, maradhi na kuleta maendeleo, ili kuhakikisha kuwa mwanadamu anatibiwa na kupona kimwili na kiroho kwa kuzingatia utu, haki msingi za binadamu na baada ya maisha yake hapa duniani aurithi uzima wa milele. Serikali inapaswa kuhakikisha nchi itiririke maziwa na asali ili watu wake wanaishi kwa furaha na amani. Kanisa linamhakikishia huyu mtu kuwa furaha hii itakamilishwa katika uzima wa milele. Na wakati mtu huyu duni akitibiwa na kuhudumiwa anaendelea kuheshimiwa: hata kama sasa hivi yu mchanga, mdogo, mgonjwa, masikini, mdhambi, kikongwe au tajiri: mjinga au msomi, anabaki na hadhi na heshima yake kubwa kuliko viumbe vingine vyote! Serikali inapaswa kumlinda kila mmoja kwa kuzingatia katiba, sheria na itikadi wakati huo Kanisa linaikumbusha serikali kuwa kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapaswa kuheshimiwa katika hali zote.

Kama tulivyokuwa tunaimba wakati wa majilio; Dondokeni enyi mbingu toka juu, na mawingu yammwage mwenye haki, nchi ifunguke na kumtoa mwokozi. Mawingu zimeshafunguka na mawingu yamemmwaga yule mwenye haki na nchi imekwishafunguka kumtuoa mwokozi ndiye Yesu Kristo aliyezaliwa kati yetu.  Basi, na sisi tuifungue mioyo yetu tumpokee ili yeye pamoja na sisi tulete ukombozi kwetu si wenyewe na kwa wengine. Leo tuna furaha, tunamshangilia Masiha kwa sababu kwa njia yake tumepata ukombozi. Katika shamrashamra, nderemo na vifijo vya kumshangia mkombozi aliyezaliwa, tusijiingize katika dhambi na kupoteza baraka na neema tulizojichotea katika kipindi cha majilio na hivyo kupoteza maana ya kusherekea noeli. Mtu atakayeendelea kuishi katika giza ni sawa na hao anawasema Yohone kuwa: “Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu. Kila mtu atendaye maovu anachukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe. Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu” (Yoh.3:19-21).

Tuipokee basi Nuru iliyokuja ulimwenguni, ituangazie tusiifanye Sherehe ya Noeli kuwa msimu wa kutenda maovu. Tukumbuke kwa majuma manne tulijiandaa kusherekea noeli kwa kufanya toba na malipizi kwa dhambi zetu. Tusisahau maazimio tuliyoweka. Kama tunavyosali katika sala baada ya komunyo tukisema; Ee Mungu mwenye huruma, tunaomba huyo Mwokozi wa dunia aliyezaliwa leo akatufanya watoto wako, atujalie pia uzima wa milele. Tumuenzi Masiha aliyezaliwa kati yetu kwa kutenda mema na kuepa dhambi na Mungu atatujaza baraka na neema zake. Mwisho tusali na kumwomba Mungu pamoja na Mtakatifu Francisko wa Asisi tukisema; “Ee Bwana unifamsanye kuwa chombo cha amani yako. Nieneze mapendo wanapochukiana, nilete msamaha wanapokosana, nipatanishe wanapogombana, nitumainishe wanapokata tamaa, niwashe taa panapoenea giza, nilete furaha panapo kaa huzuni. Ee Bwana mungu unijalie kufariji kuliko kufalijiwa, kufahamu kuliko kufahamika, kupenda kuliko kupendwa. Anayetoa atapokea, anaye samehe atasamehewa, anayekufa kwa ajili ya Kristo atazaliwa kwenye uzima wa milele”.

24 December 2020, 17:10