Tafuta

Seminari kuu ya Nazareth, Mwendakulima, Jimbo Katoliki la Kahama imebarikiwa na kuzinduliwa rasmi tarehe 5 Desemba 2020 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Seminari kuu ya Nazareth, Mwendakulima, Jimbo Katoliki la Kahama imebarikiwa na kuzinduliwa rasmi tarehe 5 Desemba 2020 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. 

Seminari Kuu ya Nazareth, Mwendakulima, Jimbo Katoliki Kahama! Chimbuko Lake!

Seminari kuu ya Nazareth ni mahali ambapo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapania kutoa elimu ili kulea wito, kukuza na kuimarisha imani ya Majandokasisi wanaoandaliwa kwa ajili ya maisha na utume Kipadre. Kanisa linawaombea amani na usalama. Majaalimu na walezi wajaliwe neema na baraka za mbinguni ili wawe na hekima, akili na uchaji wa Mungu, wawe mashuhuda!

Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS. – Kahama, Tanzania.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri hivi karibuni lilichapisha Mwongozo wa Malezi ya Kipadre  unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Utangulizi wa mwongozo huu unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia! Tarehe 5 Desemba 2020, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., limezindua Seminari kuu ya Nazareth, Mwendakulima. Seminari hii imeanza na Majandokasisi 106 kwa masomo ya falsafa chini ya uongozi wa Monsinyo Pius Rutechura, Gambera wa mpito!

Seminari hii imebarikiwa na kuzinduliwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu  mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Askofu Mkuu Marek Solczynski – Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Maaskofu pamoja na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Kahama! Matendo makuu ya Mungu. Hapa ni mahali ambapo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapania kutoa elimu ili kulea, kukuza na kuimarisha imani ya Majandokasisi wanaoandaliwa kwa ajili ya maisha na utume Kipadre. Kanisa linawaombea amani na usalama chini ya ulinzi wa Malaika. Majaalimu na walezi wajaliwe neema na baraka za mbinguni ili wawe na hekima, akili na uchaji wa Mungu. Wafahamu kwa akili yale watakayofundisha, wayatunze na kuyatimiza kwa matendo. Wale wote watakaopitia Seminarini hapo wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Kwa upande wake, Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania, kuendeleza moyo wa upendo na mshikamano wa dhati katika kuitegemeza Seminari kuu ya Mwendakulima. Bado wema na ukarimu wao unahitajika ili kuiendeleza Seminari hii ambayo ni sehemu ya sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Ifuatayo ni hotuba Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS, wa Jimbo Katoliki Kigoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Seminari-RBS/KKNSM na Mlezi wa Mapadre na Seminari Kuu.

UTANGULIZI/SALAMU: Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo – Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga – Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mhashamu Askofu Mkuu Marek Solczynski – Balozi wa Baba Mtakatifu Nchini Tanzania, Wahashamu Maaskofu Wakuu, Wahashamu Maaskofu, Waheshimiwa Viongozi wa Serikali, Mheshimiwa Msimamizi wa Kitume, Waheshimiwa Mapadre, Watawa (wa kike na wa kiume), Waseminaristi, Waamini Walei na watu wote wenye mapenzi mema, TUMSIFU YESU KRISTO.

HISTORIA FUPI / KWA NINI TUWE NA SEMINARI MPYA? Wapendwa familia ya Mungu, katika Neno langu hili fupi, ningependa kwanza kabisa kuwashirikisha kwa ufupi sana historia tuliyopitia hadi kufikia hatua hii muhimu ya Uzinduzi Rasmi wa Seminari hii Kuu mpya ya Nazareth – Mwendakulima (yaani, ni kwanini tumeamua kuanzisha Seminari hii?): Ni ukweli usiopingika kuwa kwa miaka ya hivi karibuni Kanisa letu la Tanzania limeshuhudia ongezeko kubwa la miito ya upadre, hadi kupelekea Seminari zetu Kuu zilizopo kuelemewa na idadi ya waseminaristi, hali ambayo imefanya baadhi yao kupata changamoto za malazi na hata malezi yao kwa ujumla kuwa magumu. Kwa mfano, kwa mwaka mpya wa masomo 2020/2021 zaidi ya waseminaristi 200 walikuwa wanaelekea kukosa nafasi katika Seminari Kuu zetu.

Hali hii ilitufanya tufikirie namna ya kuikabili changamoto hii. Ndipo hapo tulianza jitihada mbalimbali kama vile kujenga mabweni ya nyongeza katika seminari zetu, kuomba nafasi katika seminari za Mashirika ya Kitawa, kufungua Kituo cha Malezi ya Kijimbo pale Morogoro na hata kwa baadhi ya majimbo kulazimika kupeleka waseminaristi wao nje ya nchi. Jitihada hizi hazikuweza kukidhi hitaji letu. Hivyo, likazaliwa wazo la kuwa na Seminari Kuu Mpya. Katika maeneo yote yaliyopendekezwa kujengwa Seminari Kuu Mpya, eneo lililoonekana kufaa zaidi ni hapa Mwendakulima, jimbo la Kahama.

Baada ya mchakato wa muda mrefu, tunamshukuru Mungu kwamba siku ya leo tunashuhudia rasmi ufunguzi wa Seminari hii. Kila mmoja wetu anayo kila sababu ya kumshukuru Mungu na kufurahi kuwa anashuhudia historia ikijirudia tena – kwani katika ukanda huu huu wa Magharibi katika miaka ya nyuma sana hitaji kama hili hili limewahi kujitokeza na hatimaye kuzaliwa Seminari ya Ushirombo – mwaka 1918, baadaye kuhamia Utinta – mwaka 1921 na hatimaye kuhamia Kipalapala – mwaka 1925 hadi sasa. Leo inazaliwa tena Nazareth – Mwendakulima. Hakika jambo hili ni Neema ya Mungu kweli na tunayo kila sababu ya kumshukuru.

SHUKRANI NA PONGEZI: Kwa niaba ya Bodi ya Seminari Kuu, kwa nafasi ya kwanza kabisa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha haya yote. Tunamshukuru Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Askofu Mkuu Marek Solczynski kwa misaada na miongozo yake mbalimbali kuelekea uanzishwaji wa Seminari hii hadi hii leo anapoungana nasi kushuhudia tukio hili la baraka. Tunamshukuru Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye tarehe 26.04.2004 alifika eneo hili kuweka jiwe la msingi kwa wakati huo kikiwa ni kituo cha kijimbo, pasipo kutarajia kuwa leo hii atafungua rasmi Seminari Kuu Mpya mahali hapa. Vile vile, tunamshukuru sana kwa kutuongozea adhimisho hili la Misa Takatifu ya Ufunguzi rasmi wa seminari hii na kubariki Makanzu ya waseminaristi wetu. Aidha, tunawashukuru kwa dhati wanajimbo la Kahama kwa ukarimu wao kwa Kanisa letu la Tanzania hata kutupatia miundombinu ya awali ya kuanzisha Seminari hii, tukimshukuru kwa namna ya pekee kabisa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Kahama, Askofu Ludovick Joseph Minde (ALCP/OSS).

Shukrani zetu nyingi tunazitoa kwa Maaskofu wote kwa majitoleo yao makubwa sana hadi kufikia hatua hii ya leo. Tunaishukuru timu maalumu ya mapadre walioteuliwa kusimamia maandalizi ya uanzishwaji wa Seminari hii chini ya Uongozi wa Monsinyo Pius Rutechura akisaidiana kwa ukaribu zaidi na Padre Justine Msaiye. Tunawashukuru na kuwapongeza Mapadre-Walezi ambao tayari wamekwishaanza kazi hii muhimu ya kuwalea vijana wetu. Tunawashukuru pia ndugu zetu wa Redio Maria ambao mara nyingi wamekuwa wadau muhimu sana katika kuhamasisha miito kwa njia ya matangazo yao na hata leo hii wamekuja kushiriki nasi ili kuupasha habari ulimwengu mzima juu ya matukio haya ya leo. Vile vile tunaishukuru Kurugenzi yetu ya Mawasiliano - TEC kwa kushiriki katika tukio hili. Kadhalika, tunawashukuru watu wote wenye mapenzi mema kwa majitoleo yao.

Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, tunawashukuru na kuwapongeza sana waseminaristi wetu walioko hapa. Hakika wanayo kila sababu ya kumshukuru Mungu na kujivunia wito wao kwani wao wamepata bahati hii ya kuwa waasisi wa Seminari yetu hii mpya. Tunawasihi muendelee kuupokea wito wenu huu kwa shukrani, mkidumu katika kuwa watii kwa malezi mfungamano (Integral Formation) mnayopewa na zaidi sana kuzitunza na kuziishi tunu za Familia Takatifu ambazo ndizo utambulisho (identity) wa seminari yenu. Kwa kuthamini majitoleo ya kila mmoja wetu ninasema tena Ahsanteni Sana.

WITO/MWALIKO: Wapendwa familia ya Mungu, pamoja na ongezeko hili kubwa la miito tunalolishuhudia nyakati hizi, bado kilio cha Kanisa kitaendelea kubakia kuwa kile kile: “Mavuno ni mengi wavunaji ni wachache” (Lk.10:2) na wala Injili haitabadiilika na kuwa kinyume chake. Katika msingi huu, ninapenda kumualika kila mmoja wetu kuendelea kusali kwa ajili ya kupata miito mingi zaidi na pia kushiriki katika kazi ya malezi ya waseminaristi wetu waliopo hapa na katika seminari nyingine zote. Daima tuendelee kukumbuka kuwa majitoleo yetu endelevu katika kutegemeza miito bado yanahitajika sana. Kama mnavyoona, leo tumefungua seminari hii mpya lakini bado mahitaji yako mengi ambayo yanadai ukarimu wa kila mmoja wetu. Kwa kuzingatia kuwa kwa siku zijazo seminari hii itakuwa kwa ajili ya masomo ya Falsafa na Taalimungu, mwaka hadi mwaka waseminaristi watazidi kuongezeka. Hivyo, bado liko hitaji kubwa zaidi la kuongeza miundombinu wezeshi kwa kazi ya malezi. Hili ni jukumu letu sote, karibuni tuungane pamoja!

Aidha, kwenu walezi na walelewa katika Seminari hii ya Nazareth - Mwendakulima, ni vema mkakumbuka siku zote ya kuwa upendo hujibiwa kwa upendo. Hivyo, ninapenda kuwaasa na kuwahimiza kudumisha mahusiano mazuri na wenyeji wenu, yaani wanajimbo Katoliki la Kahama kama ishara ya shukrani yetu kwao. Kwa upande wenu mapadre - walezi, pale inapowezekana, ninawaomba muwe tayari kutoa huduma za kiroho kwa parokia za jirani za Jimbo la Kahama (hasa kwa siku za Jumapili) lakini pasipo kuathiri wajibu wenu msingi wa malezi kwa waseminaristi wetu. HITIMISHO: Ahsanteni sana nyote na Mungu awabariki sana. Wenu katika utumishi,

Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS. Askofu wa Kigoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Seminari-RBS/KKNSM na Mlezi wa Mapadre na Seminari Kuu

15 December 2020, 13:33