Tafuta

Vatican News
Dominika ya Pili ya Majilio Dominika ya Pili ya Majilio  

Neno la Mungu Domenika ya pili ya majilio mwaka B:Itengenezeni njia ya Bwana!

Dhambi zetu ni kama vichaka,milima,mabonde na miinuko inayotuzuia kumuona Bwana na mwokozi wa maisha yetu.Ujumbe huu wa Nabii Isaya katika somo la kwanza,wa Petro katika somo la pili na wa Yohane Mbatizaji katika Injili uwashe ndani mwetu tamaa ya kufanya toba ya kweli na hivi kila mmoja wetu ajiulize ni vichaka na visiki gani vimejaa moyoni,lini utaanza kuvikata na kuving’oa?

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatikani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya majilio mwaka B wa Kanisa. Masomo ya domenika hii yana ujumbe wa faraja na matumaini, ujumbe unaoambatanishwa na wajibu wetu wa kuitengeneze njia ya Bwana, kuyanyoosha mapito yake ndani ya mioyo yetu ili aweze kuingia na kukaa nasi. Ni ujumbe wa maandalizi ya kuzaliwa upya Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu. Mungu kwa kinywa cha nabii Isaya katika somo la kwanza anawatuliza na kuwafariji Waisraeli wakiwa utumwani Babeli kwa kuwatangazia kuwa utumwa wao umekwisha hivyo wajiweke tayari kwa ujio wa Mkombozi na mchungaji wao mwema atakaowarejesha katika nchi yao. Ujumbe huu umebebwa na maneno ya faraja yasemayo;watulizeni mioyo, watulizeni mioyo watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote.

Ujumbe huu unawapa wajibu wa kuitengeneza nyikani njia ya Bwana, kuyanyoosha jangwani mapito yake, kuinua kila bonde na kushusha kila milima na vilima, kupanyoosha palipopotoka, na palipoparuza kupasawazisha ili utukufu wa Bwana utakapofunuliwa, wote wenye mwili wauone. Nabii Isaya anapaswa asiogope bali apande mlimani, apaze sauti kwa nguvu ili watu wote wapate kusikia ujumbe huu wa Mungu. Tukumbuke kuwa wayahudi wanapewa ujumbe huu wakiwa uhamishoni Babiloni, na njia ya kutoka Babiloni hadi Palestina ilipita jangwani. Kwa namna nyingine watu hawa wanakumbushwa magumu waliyoyapata walipotoka utumwa Misri waliposafiri na kukaa jagwani kwa miaka 40 na sasa safari ni ileile ya kupita jangwani kurudi katika nchi yao. Kumbe haikuwa kazi rahisi ya kuitengeneza njia hii kwa ajili ya Mkombozi anayekuja. Lakini ujumbe huu sio wa kutengeneza barabara juu ya ardhi, bali ni matayarisho ya kiroho ya wayahudi ambao kwa wakati ule mioyo yao ilikuwa kama jangwa kwa sababu ya dhambi zao.

Ndiyo maana Mungu anasema adhabu walioyoipokea kwa dhambi zao imeisha kwa kuwa walitambua makosa yao na dhambi zao, wakatubu kwa kumlilia Mungu awasamahe naye akawasamehe dhambi zao na sasa anawaandaa tayari kwa kurudi katika nchi yao. Ujumbe huu kwetu sisi unatukumbusha wajibu wetu wa kuiandaa mioyo yetu ili Kristo aweze kupita na kuingia ndani ya mioyo yetu kwa kufanya toba ya kweli. Ujumbe huu ni wetu sote tulio katika utumwa wa dhambi. Tunaalikwa tuuvae moyo wa unyenyekevu na kufanya toba ili Mungu aingii ndani mwetu na kukaa nasi kwa njia ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Mda uliokubalika ndio sasa na wakati ndio huu wa kujipatanisha na Mungu maana hatuji siku wala saa Bwana amtumapo mjumbe wake kutuita kwake; anaweza kukawi au kufika mapema hivyo tujiandae mda wote. Mtume Petro katika somo la pili la waraka wake wa pili kwa watu wote anasisitiza umuhimu wa kujiandaa na kutukumbusha kuwa Mungu anatupa nafasi na Muda ili tujipatanishe naye ili siku atakapotuita tusiwe na lawama mbele zake. Mtume Petro anasema; Bwana yu aja hata kama anakawia lakini yu aja.

Sababu ya kukawia kwa Bwana kuja iko wazi; ili sote tuokoke, Mungu anatupa muda wa toba kama anavyosititiza mtume Petro; Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, bali huvumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi, hivyo tufanye bidii ili tuonekane katika amani kuwa hatuna aibu mbele za Mungu. Tutambue kuwa kwa Mungu hakuna haraka, kwake miaka 1000 ni sawa na siku moja. Mungu ni mvumilivu, yeye ana nguvu, uwezo na huruma. Hivyo kuchelewa kuja kwa Kristo ni upendeleo kwetu. Kama Petro alivyowaasa wakristo wa nyakati zake watumie muda wao vizuri wangali wanamsubiri Kristo akisema; Nawasihi ndugu zangu ishini katika mwenendo wa utakatifu na utauwa, mwonekane mbele ya Bwana kwa amani na pasipo doa…waa wala aibu (1Pet 3:14). Hivyo basi; msubirini Bwana kwa furaha mkitenda yawapasayo kwa busara na upendo. Basi nasi tunaousikia ujumbe huu nyakati zetu kila mmoja wetu ajitafakari na kujiuliza moyoni mwake kama yuko tayari kuikabili siku ya mwisho wakati na mda wowote Bwana amtumapo mjumbe wake.

Injili kama ilivyoandikwa na Marko jinsi inavyoanza ni tofauti kabisa na Injili zingine. Marko anaanza kuandika akimnukuu Nabii Isaya akisema; Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu kama ilivyoandikwa na Nabii Isaya; Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Sauti hii iliayo nyikani ni ya Yohane Mbatizaji. Ujumbe wa Marko unatuambia kuwa habari njema ni hii; Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, Mkombozi wetu, ataunda taifa jipya. Manabii walitabiri juu ya kuja kwake Kristo; na Yahane Mbatizaji alitayarisha ujio wake kwa ubatizo wa toba, wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu, wakabatizwa katika mto Yordani, wakiziungama dhambi zao. Nasi leo tunaitwa kufanya toba ya kweli mioyoni mwetu kwa kuzitubu na kuziungama dhambi zetu.

Ujumbe wa Yohani Mbatizaji katika injili ni mwangwi wa ujumbe wa Nabii Isaya katika somo la kwanza. Nabii Isaya alitangaza kutengeneza njia ya Bwana jangwani akiwa Babiloni kwa ajili ya wana wa Israeli wakiwa utumwani. Yohani Mbatizaji anatangaza ujio wa Yesu Kristo yeye mwenyewe akiwa jangwani amevalia vazi la singa ya ngamia na kula asali na nzige nao watu wakamwendea na kubatizwa ubatizo wa toba. Sisi tumebatizwa kwa maji na roho Mtakatifu tumepokea wokovu. Wokovu huu tulioupokea kwa njia ya Yesu Kristo ni mtimilifu wa yote kwani yeye amekuja si kwa wokovu wa taifa moja bali kwa ulimwengu wote. Kristo anamkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi na mauti akitupatia uzima wa milele. Anakuja kama mchungaji mwema wa kundi lote la wanadamu. Anawapenda kondoo wote hasa waliopotea na walio wagonjwa. Wote anawakusanya, anawalisha na kuwaongoza. Wenye moyo mnyenyekevu ndiyo watakaokoka.

Dhambi zetu ni kama vichaka, milima, mabonde na miinuko inayotuzuia kumuona Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Ujumbe huu wa Nabii Isaya tuliousikia katika somo la kwanza, wa Petro katika somo la pili na wa Yohane Mbatizaji katika Injili uwashe ndani mwetu tamaa ya kufanya toba ya kweli na hivi kila mmoja wetu ajiulize ni vichaka na visiki gani vimejaa moyoni, lini utaanza kuvikata na kuving’oa? Una vilema gani? Mda uliokubalika ndio sasa. Kristo ni mshindi anataka azaliwe moyoni mwako. Jipange sawasawa. Tumwongokee yu aja kwetu. Tusichelewe. Tufanye hima kujipatanisha naye.

TAFAKARI NENO LA MUNGU
04 December 2020, 09:09