Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Tafakari ya Neno la Mungu, Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. 

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Nazareti: Chombo Cha Uinjilishaji

Mwaka wa Upendo ndani ya Familia, "Famiglia Amoris Laetitia" utazinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu na kuhitimishwa tarehe 26 Juni 2022 katika maadhimisho ya Siku ya Kumi ya Familia Duniani, itakayoongozwa na kauli mbu "Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu. Familia za Kikristo zinapaswa kuwa ni kitovu cha uinjilishaji wa kina.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, hapo tarehe 19 Machi 2021 ametangaza kwamba, itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani itakayoadhimishwa mjini Roma tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Baba Mtakatifu Francisko ametoa tamko hili wakati wa kuadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, tarehe 27 Desemba 2020. Neno la Mungu katika Dominika ya leo ya ndani ya Oktava ya Noeli bado ni mwaliko ya kutafakari fumbo la Mungu kutwaa mwili, na kukaa katikati yetu, yaani Fumbo la Umwilisho. Ni fumbo la upendo wa Mungu kwa mwanadamu, Mungu kuutwaa mwili wetu na kuwa sawa na sisi isipokuwa dhambi, ni upendo wa Mungu kwako na kwangu, ni ukombozi wako na wangu.Ni Mungu anayezaliwa na kuwa mwanafamilia kama ambavyo sisi sote tumezaliwa na kuingia katika familia ya wanadamu. Yesu Kristo pamoja na kuwa mwanafamilia wa familia kubwa ya wanadamu wote ila pia ni mwana na mtoto wa familia ile ya Yusufu na Mariamu.

Kadiri ya sheria ya Kiyahudi, kila mzaliwa wa kwanza iwe wa mwanadamu au mnyama alipaswa kutolewa sadaka kwa Mungu. Rejelea Kutoka 13: 1-16. Badala ya kuwatolea sadaka watoto, basi kwa nafasi yao walipaswa kutoa sadaka ya wanyama au njiwa kadiri ya uwezo wa wazazi. Na hapo wazazi walipaswa kutolea sadaka mnyama asiye na mawaa, yaani aliye mchanga bado. Kwa Wayahudi mtoto mchanga pia alipaswa kutakaswa mara baada ya kuzaliwa, na hivyo wazazi walipaswa kwenda hekaluni kwa kuhani na kutolea mnyama asiye na mawaa badala ya mtoto mwenyewe. Kwa matajiri walitoa sadaka ya mwanakondoo na kwa maskini ilitosha kutoa njiwa na ndio Mwinjili Luka kwa kusema walileta njiwa hekaluni ni kutuonesha kuwa familia ya Yusufu na Mariamu ilikuwa ni maskini. Mwinjili Luka anatuambia kuwa familia hii Takatifu ya Nazareti ilikuwa inashika sheria na taratibu za kidini na kiimani na hivyo kumkuza mtoto Yesu katika imani ile ya kiyahudi.

Hivyo nasi katika sherehe hii ya familia takatifu ni ujumbe tosha kwa familia zetu za kikristo wazazi kukumbuka kuwa wanao wajibu wa kuwarithisha watoto wao imani na kuwalea siku zote katika kumpenda Mungu na jirani. Tunawapowapeleka watoto kanisani kwa ubatizo pia tunachukua jukumu la kuwasaidia siku zote watoto kukua katika imani na hasa upendo na urafiki na Mwenyezi Mungu katika maisha ya kila siku. Je, ni familia ngapi leo hii zinachukua muda wao japo jioni na kukaa pamoja kusali na kutafakari Habari Njema ya Wokovu? Je, ni wangapi kila Dominika wanaongozana kwenda kanisani na kuitakatifuza siku ya Bwana, au kwenda Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo pamoja kama familia? Na huu si wa wajibu wa mama peke yake, bali wote kama familia yaani baba, mama na watoto. Hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka

Mwinjili Luka pamoja na kutuelezea juu ya familia takatifu ya Nazareti ilivyoenda hekaluni kumtolea mtoto Yesu, pia anatutatajia wahusika wengine wawili nao ni Mzee Simeoni na Mama mjane mzee Ana. Ni Mzee Simeoni na Ana wanamtambua mtoto Yesu kuwa ni Masiha na Mkombozi. Mzee Simeoni pamoja na kutokuwa na kazi maaumu hekaluni, alikuwa mtu mwenye haki na mchaji, na hivi kuweza kuona na kutambua kile ambacho wengine hawakioni. Alikubali na kupokea maongozi ya Roho Mtakatifu na hivi kumpokea mtoto Yesu mikononi mwake na kumwimbia Mungu wimbo wa kumshukuru. Simeoni baada ya kuiona nuru anamshukuru Mungu na kujiweka mikononi mwake kuwa sasa yu tayari kufa maana sasa amemwona Mwokozi aliye nuru ya ulimwengu. Mzee Simeoni pia anazungumzia juu ya unabii mwingine kumhusu Mariamu, mama wa Yesu na mama yetu pia. Upanga unaozungumziwa na Mzee Simeoni kwa kweli sio mateso atakayopata ua kupitia Mama Bikira Maria katika safari na historia ya ukombozi.

Mama wa Yesu hapa anasimama kama ishara ya Taifa la Israeli, na hivyo ujio wa Yesu utakuwa ni mwanzo wa mgawanyiko kwa Taifa lile kwani wapo watakaompokea na kufanyika wana na pia wale wasiokuwa tayari kumpokea mtoto Yesu kama Masiha au Kristo. Rejea Luka 12:51-53 Mwinjili Luka anaandika juu ya unabii huu pia akirejea hali halisi ya jumuiya za waamini waliokuwa tayari wanapitia kipindi kigumu cha kutengwa na hata kuteswa kwa sababu ya imani yao kwa Yesu Kristo. Nabii Ana, binti Fanueli wa Kabila dogo kabisa la Asheri. Ambaye naye tunasikia kuwa alibaki daima hekaluni siku zote baada ya kifo cha mume wake. Kama mjane alikuwa na haki bado ya kuolewa na mwanaume mwingine, ila alibaki kuwa mwaminifu kwa mume wake mmoja na hivyo kwake alibaki siku zote akimtumkia Mungu kwa kufunga na kusali. Anna alibaki daima hekaluni kwenye nyumba ya Mchumba wake wa daima yaani Mungu mwenyewe anayebaki daiama mwaminifu kwa watu wake. Katika Biblia mahusiano ya Mungu na watu wake yalifananishwa kama mahusiano ya wana ndoa yaani Bibi harusi na Bwana Harusi.

Pia Anna aliye mjane kwa miaka 84, mwinjili Luka anatutajia na miaka ya ujane wake sio kwa bahati mbaya ila namba katika Biblia pia zina ujumbe na maana yake. 84 = 7 x 12. Namba 7 maana yake ni ukamilifu na 12 ni ukamilifu pia kwa maana makabila 12 ya wanawaisraeli; Na hivyo miaka 84 ni kuonesha Anna ni Ndiye Binti Israeli aliyekamilisha misheni yake na sasa anafurahi anapokutana na Mchumba wake wa milele ambaye ni Yesu Kristo. Hivyo ni mwaliko wa furaha kwa wote wawili iwe Mzee Simeoni pamoja na Anna baada ya kukutana na Mtoto Yesu, zaidi sana ni fundisho la uaminifu wao kwa Mungu na hivi kutualika nasi kuwa waaminifu daima kwa Mungu. Wazee hawa ni ishara pia kuwa uzee mtakatifu ni urithi mkubwa wa imani na kumjua Mungu. Yusufu na Mariamu hawakuelewa yote haya pale mwanzoni isipokuwa walibaki na mshangao mkubwa kuhusu mambo yote yaliyokuwa yananenwa kumhusu mtoto Yesu. Sehemu ya Injili tuliyoisikia inamalizia na wao baada ya kumaliza kufanya kadiri ya sheria ya Bwana walirejea kijijini kwao Nazareti na huko mtoto Yesu alikuwa kama watoto wengine katika familia ya Yusufu na Mariamu ila jambo moja mwinjili Luka anatujuza kuwa kwa mtoto Yesu alikuwa pia katika hekima na neema. Hekima katika kujua siri za Mungu na neema katika utakatifu na urafiki na Mungu.

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Yoshua Bin Sira aliyekuwa mtu mzee na mwenye hekima na hivi kuwaandikia vijana waliokuwa wanaishia katika diaspora jinsi ya kuenenda kwa hekima na busara. Bin Sira anatukumbusha wajibu wa watoto kwa wazazi wao na hasa katika uzee wao. Kuheshimu baba na mama sio tu kuwapa heshima wao ila zaidi ya kuenenda ya uadilifu ili wao wasipate aibu na fedheha. Kuwapa uzito wanaostahili maana mara nyinyi wazee wanaonekana kudhaurika na kusahaulika bali watoto wanapaswa kuwapa bado uzito na umuhimu ule ule waliokuwa wanawapa wangali wana nguvu zao. Mwandishi pia anaelezea mafao yatokanayo na kuwaheshimu wazazi kama kujiwekea hazina mbinguni, kuja kuheshimia pia na watoto wako, sala yako kusikiwa na Mungu na kuwa na maisha marefu. Somo la pili Mtume Paolo anatukumbusha si tu wajibu wa watoto kwa wazazi bali pia wazazi kwa watoto. Na pia Mtume Paolo anaalika watu wa ndoa mume na mume kutendeana kwa upendo na uchaji; na ndio kuvaa maisha mapya yaani kumvaa Yesu Kristo kama vazi letu la kiroho linaloongoza maisha yetu. Mwaka mpya wenye kila neema na baraka zake Mtoto Yesu.


 

28 December 2020, 10:31