Tafuta

KARDINALI RANJITH WA SRI LANKA KARDINALI RANJITH WA SRI LANKA 

Sri Lanka:Kard.Malcolm Ranjith ashutumu ubinafsi wa ulimwengu

Haijalishi wewe ni dini gani,la muhimu ni kuishi kwa mujibu wa dini ambayo unaamini,katika ulimwengu huu ambao leo hii umejaa kizingiti cha uwiano mkubwa sana kati ya matajiri na masikini na ambao umezidi kuongezeka,wakati huo huo rasimali zake pia hazina usawa katika ugawaji na uchafuzi wa mazingira umesababishwa na ubinafsi wetu. Amesema hayo Kardinali Ranjith nchini Sri Lanka.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika Misa ya moja kwa moja iliyoongozwa na Kardinali Malcolm Ranjith, nchini Sri Lanka, misa iliyotangazwa na televisheni kwa mujibu wa habar za kanisa Asia UCA ameshauri waamini wa kila imani kujiomboa dhidi ya ubinafsi ili kuishi kwa mujibu wa misingi ya dini yao, ili kuzuia kwamba ulimwengu usiharibike. Kwa mujibu wake amesema “majanga yote haya ambayo tunajikuta tunakabiliana nayo katika jamii, kiukweli yamesababishwa na hisia zetu za ubinafsi”.

Kardinali Ranjith pia amezungumzia juu ya mashirika yenye nguvu na ambayo yanaendeleza kisiri siri, silaha za kibaiolojia kama vile silaha za maangamizi makubwa, aidha dini ambayo imesahauliwa katika nchi zenye uchumi mkubwa  na kuwa na  ukosefu wa kiroho na maadili. Kwa maana hiyo amesema “ haijalishi wewe ni dini gani, la muhimu ni kuishi kwa mujibu wa dini ambayo unaamini, katika ulimwengu huu ambao leo hii umejaa kizingiti cha uwiano mkubwa sana  kati ya matajiri na masikini  na ambao umezidi kuongezeka,   wakati  huo huo  rasimali zake pia hazina usawa katika ugawaji na  uchafuzi wa mazingira umesababishwa na ubinafsi wetu”. Amesisitiza Kardinali Ranjith.

Hata hivyo mbele ya kuongezeka kwa kesi za maambukizi ya covid-19, Serikali ya Sri Lanka imezuia mikutano ya umma hadi utaratibu mwingine utakapotolewa  kwa maana hiyo vijiji vingi vimetengwa kwa ajili ya kupambana na wimbi la pili la virusi vya corona ambavyo vinasambaratika kwa haraka sana. Nchini Sri Lanka hadi sasa imerekodi zaidi ya kesi 17.300 na vifo  58. Kabla ya kuanza kwa wimbi la pili la maambukizi, wiki ya kwanza ya mwezi wa Oktoba walikuwa wameorodhesha kesi 3.396  na vifo vya watu 13 tu.

17 November 2020, 14:44