Tafuta

2020.11.21 Yesu Kristo ni Mfalme wa Ulimwengu. 2020.11.21 Yesu Kristo ni Mfalme wa Ulimwengu. 

Jumapili ya 34 ya mwaka A:Yesu Kristo ni Mfalme wa ulimwengu

Tujikabidhi basi kwa Kristo mchungaji mwema, mfalme wetu mtukufu,ili tuumalizie vyema mwaka huu A wa kiliturujia na kuanza vyema mwaka B wa kiliturujia kwa kipindi cha majilio tutakapojiandaa kuzaliwa kwake mkombozi wetu Yesu Kristo katika maisha yetu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vaticani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 34 ya mwaka A wa Kanisa kipindi cha kawaida. Hii ni Dominika ya mwisho wa mwaka wa kiliturjia. Kadiri ya utaratibu wa Mama Kanisa, Jumapili hii tunaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme, mfalme aliyetukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Sherehe hii iliidhinishwa na Baba Mtakatifu Pius wa XI mwaka 1925 akiuambia ulimwengu kwamba: Dunia haiwezi kuuepa utawala wa Kristo kama inataka kubaki salama. Kwa kuwa tangu mwanzo wakristo waliogopa kumwita Kristo Yesu Mfalme, kwa kuhofia kumfananisha na wafalme wa dunia hii, Baba Mtakatifu Pius XI alisisitiza kuwa; wakristo tusiogope wala tusione aibu juu ya kumkiri Kristo kuwa Mfalme, Mwokozi na Mkombozi wetu kwani Pilato alipomwambia; Wewe u Mfalme basi? Yesu alijibu; Wewe wasema, kwa kuwa mmi ni mfalme (Yn.18:37).

Kwa mwaka mzima Kanisa limetukumbusha ya kwamba: Kristo ni Mfalme na Mchungaji mwema wa wanadamu wote kwa maisha ya sasa hapa duniani na maisha yajayo mbinguni baada ya kufa kwani Yeye ndiye Mfalme, hakimu na Mwokozi wetu. Kumbe iwe tu hai au tumekufa, kama anavyotuambia Mtume Paulo tu mali yake Kristo. Tunapoadhimisha sherehe hii ya Kristo Mfalme tunapaswa kujiuliza kama kweli maisha yetu yanaakisi utawala wake ndani mwetu, kama kweli tunamtumikia, kama kweli tumejiweka chini ya utawala wake au tuko chini ya falme na tawala zingine ambazo kwazo kwa maisha yajayo zitatuangamiza milele yote. Kumbe leo tunahimizwa kumfuata Kristo mfalme wetu, kusudi mwishowe atukaribishe katika ufalme wake wa milele mbinguni.

Somo la kwanza la katika kitabu cha Nabii Ezekieli linaonyesha ukuu, ufalme na utawala wa Mungu kwa watu wake. Taifa la Israeli lilipochukuliwa mateka lilikuwa kama kundi lisilo na mchungaji kwa sababu viongozi nao waliwekwa chini ya utumwa na chini ya wafalme waovu huko Babeli. Nabii Ezekieli anatangaza kuondolewa kwa Wafalme hao waovu na Mungu mwenyewe kuliongoza taifa lake. Hii ilitokea kuwa baada ya maaskari wa Babiloni kuvamia nchi ya Israeli, mji wa Yerusalemu na Hekalu lake vilibomolewa na kufanywa kuwa magofu na watu walichukuliwa mateka. Huko uhamishoni waliteseka sana kwa utumwa kwa kufanyishwa kazi nzito. Viongozi wa dini na wazee wao hawakuwa tena na sauti ya kuwaelekeza wala kuwaongoza watu wao kwani wote pamoja walikata tamaa kabisa na kuona kuwa Mungu amewaacha waangamie kwa sababu ya dhambi zao. Lakini Mwenyezi Mungu anasikia kilio chao na kumtuma Nabii Ezekieli kuwatangazia ujio wa siku ya wokovu ambapo Mungu mwenyewe atakuwa Mfalme na mchungaji wa watu wake.

Ujumbe huu ulikuwa ni faraja kubwa sana kwa waliokuwa wanamsikiliza Nabii Ezekieli kwani Mungu mwenyewe aliahidi ya kuwa atawatafuta watu wake na kuwaulizia kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, atawatafuta waliopotea na kuwarudisha waliofukuzwa atawakusanya katika mahali pote walipotawanyika, atawalisha katika malisho bora, atawafunga waliovunjika na kuwatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu atawaharibu na kuwalisha hukumu. Unabii huu unakamilika katika Kristo aliye Mfalme na Mchungaji wa Kundi la Mungu. Yesu Kristo alikuja kuwakusanya wadhambi waliotawanyika na kuwaokoa wote wamwaminio kutoka utumwa wa dhambi na mauti, kuwakusanya wote katika familia ya Mungu yaani Kanisa ambapo anatulisha kwa Neno lake na Ekaristi Takatifu, anatuponya kutokana na majeraha ya dhambi kwa sakramenti ya Upatanisho kwa upendo wake mkuu, anatulaza chini ya mbawa zake yaani Msalaba mtakatifu ulio alama ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti, ili kutukinga na adui mwovu shetani. Anatuimarisha kuwa askari jasiri wa Imani katika nguvu ya Roho Mtakatifu, anatufanya wana na warithi wa uzima wa kimungu pamoja naye.

Katika somo la pili la waraka wake wa kwaza kwa Wakorintho, Mtume Paulo anatueleza wazi kuwa kwa kifo na ufufuko wake, Yesu alishinda dhambi na mauti; na kwa njia hiyo Mungu Baba amemtukuza. Mwishoni mwa dunia utawala wa shetani utashindwa kabisa, ndipo Mungu atamweka Yesu kuwa Mchungaji na Mfalme wa ulimwengu mzima. Ndiyo maana Paulo kwa msisitizo anasema; “Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake, limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.”

Katika Injili ilivyoandikwa na Matayo tunaona kuwa Mungu Baba amempa Mwanae Yesu Kristo mamlaka ya kutoa hukumu iliyo haki siku ya mwisho. Kristo aliye Mchungaji na Mfalme atahukumu kadiri tunavyoshuhudia imani yetu siku kwa siku na kadiri ya matendo yetu ya huruma kwa jirani. Kumbe hukumu yetu ya mwisho inatokana na jinsi tulivyoipokea na kuiishi amri ya mapendo kwa Mungu na Jirani. Upendo tunaouonesha kwa jirani ni kipimo cha upendo wetu kwa Mungu. Kadiri tunavyoyatendea makundi maalumu ya ndugu zetu kwa mahitaji yao kama wenye njaa, wenye kiu, maskini, wageni, wagonjwa, wafungwa, na walio uchi ndivyo hivyo tunavyomtendea Kristo na ndicho kipimo cha hukumu yetu. Tukumbuke kuwa kilio cha wahitaji hasa maskini, wajane na yatima kinasikika moja kwa moja maskioni mwa Mungu (Isa 53:6-7, 35-36, 42-43). Kristo aliambatana na makundi haya kwa ukaribu zaidi na ndiyo maana anaendelea kutufundisha kwamba: “Kadiri mlivyomtendea mmoja wa wadogo hawa mlinitendea Mimi.” Ikiwa tunawakirimia hawa, tuzo letu ni kubwa mbinguni. Tunachomtendea Jirani yetu kwa Upendo ni tendo la kukiri Imani kwamba Mungu ni Muumba na Baba Yetu sote. Tunapomtenda jeuri mwenzetu, kimsingi ni kumtenda jeuri Mungu, ni kumdharau Mungu. Ikiwa hatuwapendi wale walio wa Mungu, hatuwezi kudai kuwa tunampenda Mungu. Tutambue kwamba sisi ni wana wa Ufalme wa Mungu unaoanza hapa duniani na ukamilifu wake ni mbinguni. Hukumu tutakayoipata itatokana na matendo yetu wenyewe jinsi tulivyoishi hapa duniani na kuhusiana na wenzetu.

Tukumbuke methali hii; mdharau mwiba mguu huota tende. Kanisa daima linatukumbusha juu ya matendo haya ya huruma kila kukicha tukiyadharau na kutoyatendea kazi na kuyaishi mwisho wake ni kuangamia kwenye moto wa milele. Kumbe basi tutumie muda tulionao katika kuipokea huruma ya Mungu kwa kuwaonyesha wengine huruma hiyo ili nasi tukaipokee mda wetu ukifika. Tukumbuke kuwa amri ya mapendo ni sheria na ndio kipimo cha hukumu yetu. Kama Mtakatifu Augustino anavyotuambia “Mungu aliyetuumba pasipo sisi kupenda, hawezi kutukomboa pasipo sisi kupenda.” Agustino anasisitiza kuwa; “Mioyo yetu haiwezi kutulia mpaka imetulia katika Mungu.” Mungu ametupa uhuru, tuutumie uhuru huo kwa busara na kwa faida ya wokovu wetu. Hata kama Mungu wentu ni mwenye haki, huwaangazia jua lake wote, walio wema na wadhambi, huwanyeshea mvua walio waaminifu na wasiowaaminifu, anayaacha magugu na ngano vikue pamoja, lakini mwisho wa yote walioikataa huruma yake wakati uliokubaliki watahukumiwa pasipo huruma yake. Tujikabidhi basi kwa Kristo mchungaji mwema, mfalme wetu mtukufu,ili tuumalizie vyema mwaka huu A wa kiliturujia na kuanza vyema mwaka B wa kiliturujia kwa kipindi cha majilio tutakapojiandaa kuzaliwa kwake mkombozi wetu Yesu Kristo katika maisha yetu.

21 November 2020, 17:35