Tafuta

2020.11.26 Mshumaa wa Dominika ya kwanza  ya Majilio Mwaka B. 2020.11.26 Mshumaa wa Dominika ya kwanza ya Majilio Mwaka B. 

Dominika ya I ya majilio mwaka B:Angalieni,kesheni&ombeni

Lazima kuomba.Ndiyo maana Kristo anasema:“angalieni,kesheni, ombeni.Tabia zingine na mazoea ya dhambi flani flani ni ngumu kuziacha,yahitaji msaada wa Roho Mtakatifu, kwa maana hiyo ni katika sala na maombi tunajipatia nguvu ya kushindana na tabia na mazoea ya dhambi zetu.Tuwe wasikivu kwa neno la Mungu ambalo ni kama kengele inayotuamsha ili tusali,tuombe na kukesha,tubaki macho tukimsubiria ndugu yetu kifo.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatikani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya majilio mwaka B wa Kanisa. Leo tunaanza kipindi cha majilio. Domenika iliyopita tulimaliza mwaka A wa kiliturjia katika Kanisa kwa sherehe ya Kristo Mfalme na kwa Domenika hii ya kwanza ya majilio tunaanza mwaka mpya wa kiliturujia ambao ni mwaka B. Katika Kalenda ya liturujia, Kanisa limetenga sehemu kuu sita ambazo ni majilio, noeli, kwaresma, Pasaka, Pentekoste na kipindi cha kawaida cha mwaka. Majilio ni kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa Kristo siku ya kuzaliwa kwake mioyoni mwetu. Noeli ni kipindi ambapo Kristo anazaliwa upya mioyoni mwetu. Kwaresma ni kipindi cha kukubali kuteseka na kufa kuhusu dhambi. Pasaka ni kipindi cha kufufuka pamoja na Kristo katika upya wa maisha. Pentekoste ni kipindi cha kumpokea Roho Mtakatifu, mfariji na kiongozi wetu katika kweli na uzima. Kipindi cha kawaida cha mwaka kinatualika kuishi ndani ya Roho Mtakatifu tukiwajibika kuusimika Ufalme wa Mungu na kumsubiri Kristo ajapo katika hukumu ya mwisho.

Kumbe kipindi hiki cha majilio ni kwa ajili ya maandalizi ya kumpokea Mungu anayekuja kwetu katika hali ya kibinadamu yaani Yesu Kristo, Mkombozi wetu. Kipindi hiki cha Majilio kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza huanza na Dominika ya kwanza ya Majilio na huishia tarehe 16 Desemba. Katika sehemu hii Kanisa linatualika kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Sehemu ya pili huanza tarehe 17 hadi 24 Desemba. Masomo ya sehemu hii yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo. Liturjia na masomo ya sehemu hii yanatukumbusha zile siku Wasraeli walipokuwa wakimsubiri mkombozi. Ni wakati wa matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo.

Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya linatusimulia kuwa Wayahudi, baada ya kurudi toka utumwani Babeli, kwa mara ya kwanza walitambua kuwa wanaye Baba mmoja, naye ni Mungu aliyewakomboa toka utumwa na hivyo kwake wanaomba msamaha na wanatumaini msaada toka kwake wakisema; Wewe, Bwana, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako. Urudi kwa ajili ya watumishi wako, kabila za urithi wako. Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo. Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu. Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako (Isaya 63:16-17).

Hii ni kiri nzito ya dhambi ya Israeli, ni toba ya kweli isiyo na waa lolote. Sisi nasi tunapoanza kipindi hiki cha majilio tunaitwa kuifanya toba ya kweli ndani kabisa mwa mtima wa mioyo yetu, bila kusita ili tuweze kujiandaa vyema kumpokea Masiha, Bwana wetu Yesu Kristo, atakapozaliwa upya ndani ya mioyo yetu na kutufanya upya watoto wa Mungu na wa Kanisa. Tujichunguze ni wapi tumekosea, ni wapi tumeanguka, ni wapi kuna mapungufu ili tupate kumuomba mwenyezi Mungu msamaha na atupokee tena kama wanawe wapendwa na pale tulipofanya vizuri tuombe neema na baraka zake ili tuendelee kudumu katika kutenda mema.

Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho anamshukuru Mungu kwa neema zote walizopewa Wakorintho katika kupokea imani ya Kristo. Pia anawahakikishia kuwa Kristo atawaimarisha mpaka siku ya mwisho, akisema; Ndugu zangu, neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu; kwa kuwa katika kila jambo mlitajirika katika yeye, katika maneno yote, na maarifa yote; kama ushuhuda wa Kristo ulivyothibitika kwenu; hata hamkupungukiwa na karama yoyote, mkikutazamia sana kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye atawathibitishia hata mwisho, ili msilaumiwe siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanae, Yesu Kristo Bwana wetu (1Kor. 1:3-9).

Maneno haya ya Mtume Paulo kwa wakorinto yanasikika tena masikioni mwetu yakitukumbusha kuwa sisi nasi pia kwa ubatizo tumepewa kila aina ya neema kutoka kwa Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu tuliyempokea, na hivyo tukafanya upya wana wa Mungu na wa Kanisa. Aidha tunapewa nafasi kama hizi za kipindi cha majilio ili tujikumbushe tena na tena wajibu wetu wa kujirekebisha na kujiandaa kila mara tukiwa tayari ili Kristo atakapofunuliwa kwetu pale tutakapokufa tusilaumiwe kwa kutotumia vema nafasi tulizopewa bali tuingie katika ushirika wa Yesu Kristo Bwana wetu katika ufalme wake huko mbinguni. Huu ni ujumbe wa faraja kubwa kwetu ambao uko wazi kwa kila mmoja wetu. Kwa kuwa Mungu wetu ni mwaminifu ambaye kwaye sisi tuliitwa ili tuingie katika ushirika na Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo sisi nasi tunaitwa kuwa waaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo ambazo kwazo ndizo sinatustahilisha kuingia katika ufalme wa Mungu Mbinguni.

Katika Injili ilivyoandikwa na Marko Yesu anatuhadharisha kuwa hatujui siku wala saa ya kifo chetu ambayo ndiyo siku na saa ya hukumu yetu kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi hivyo tukeshe daima asije akawasili ghafla akatukuta tumelala. Huu ni ukweli na uhalisia wa maisha ya mwanadamu kuwa hakuna anayejua siku wala saa ya kufa kwake. Katika nyakati zetu ambapo kuna magonjwa mengi ya ajabu na yasiyo na tiba ni vyema kujiweka sawa mda wote kwa kuzishika na kuziishi amri za Mungu kwa furaha na amani tele ili siku hii isitukute ghafla bali itukute tumejiandaa kuingia katika ufalme wa mbinguni. Lakini tutambue kuwa kufanya haya maandalizi si jambo rahisi. Lazima kuomba. Ndiyo maana Kristo anaongeza kusema; “angalieni, kesheni, ombeni.

Tabia zingine na mazoea ya dhambi flani flani ni ngumu kuziacha, yahitaji msaada wa Roho Mtakatifu, kumbe ni katika sala na maombi tunajipatia nguvu ya kushindana na tabia na mazoea ya dhambi zetu. Tuwe wasikivu kwa neno la Mungu ambalo ni kama kengele inayotuamsha ili tusali, tuombe na kukesha, tubaki macho tukimsubiria ndugu yetu kifo. Tuige mfano wa Waisraeli kama walivyomlilia Mungu awasamehe na kuwaponya. Nasi pia tumlilie Mungu ili atusamehe na kutuponya na uovu wetu wote aweze kutustahilisha kuingia katika ufalme wake.

TAFAKARI MAJILIO
27 November 2020, 16:03