Tafuta

Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020: Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Tanzania kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020: Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Tanzania kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. 

Maadhimisho Siku ya Kimisionari Duniani 2020: Tanzania!

Askofu mkuu Damian Denis Dallu, Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, anawashukuru na kuwapongeza waamini kwa kuchangia kwa hali na mali katika maisha na utume wa Kanisa. Wamechangia pia Mfuko wa Dharura Dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 Ulioanzishwa na Papa Francisko pamoja na kuchangia Seminari kuu ya Nazareti, Kahama!

Na Askofu mkuu Damian Denis Dallu, Dar es Salaam.

Ndugu wapendwa, Tunayo furaha tena mwaka huu 2020 kuwaletea Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko alioutoa kwa ajili ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni. Katika Ujumbe huo Baba Mtakatifu anaanza kwa kulishukuru Kanisa lote la ulimwengu kwa kufanikisha maadhimisho ya Mwezi maalum wa Kimisionari Oktoba 2019. Ni matumaini yake kuwa ulileta uongofu wa kimisionari katika jumuiya nyingi ukiongozwa na kaulimbiu: “Umebatizwa na umetumwa kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika Utume ulimwenguni kote”. Baba Mtakatifu anakiri kuwa maradhi yaliyosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 yalileta mateso na changamoto nyingi. Anasema licha ya changamoto hizi umisionari wa Kanisa lote lazima uendelee ndani ya mwanga wa Kanisa kwa kufuata wito wa nabii Isaya: “Mimi hapa, nitume mimi” (Isa 6:8). Anatukumbusha kuwa Mungu aliye mwingi wa huruma yupo na binadamu kama alivyokuwa na mitume wakati wa dhoruba kali ambayo hawakuitarajia (Rejea Ujumbe wa Dominika ya Miito 2020).

Wakati wa janga hili la Corona, COVID-19 ni vema tutafakari ukweli huu kwamba hii ni changamoto ambayo inatufanya kutekeleza majukumu ya umisionari wetu kwa ajili ya Kanisa. Maradhi, mateso, hofu na kutengwa na jamii pia ni changamoto kwetu. Ufukara wa wale wanaoachwa kufa bila msaada wowote, wanaokimbiwa na ndugu zao, wale waliopoteza ajira pamoja na mapato, wasiokuwa na makazi wala chakula, yote ni changamoto kwetu. Kwa njia ya changamoto hizo Mungu anatuita akisema: “Nimtume nani”? Swali hilo linatujia tena sisi; tena linasubiri jibu la ukarimu na uhakika: “Mimi hapa, unitume mimi” (Is 6:8). Mungu anaendelea kuwatafuta wale atakaoweza kuwatuma duniani na kwa mataifa yote kuwa mashahidi wa upendo wake.

“Umisionari, ni ‘Kanisa katika kwenda mbele”. Na huo si mpango wa ujasiriamali, ambao unafanywa kwa nguvu za utashi tu. Ni Kristo mwenyewe anayeliwezesha Kanisa kwenda nje kwa utume. Baba Mtakatifu anamwalika kila mmoja wetu awe tayari kuwa mmisionari, yaani kupokea mwito wa Mwenyezi Mungu wa kufanya umisionari, iwe katika maisha ya wanandoa, ama ya watu wa Maisha ya wakfu, au walioitwa kwa ajili ya daraja takatifu, kwenye utume na katika majukumu ya kila siku ya maisha ya kawaida. Lengo ni kuwa tayari kutumwa wakati wowote na mahali popote na kutoa ushuhuda wa imani yetu juu ya Mungu, Baba mwenye wingi wa rehema, kuitangaza Injili ya ukombozi wa Yesu Kristo, kushiriki maisha kimungu ya Roho Mtakatifu katika ujenzi wa Kanisa. Tunaalikwa tuwe tayari, kama Bikira Maria Mama wa Yesu, kutoa huduma kikamilifu kadiri ya mapenzi ya Mungu (Rejea Lk 1:38). Maadhimisho ya Siku Umisionari Ulimwenguni pia ni muda muafaka wa kuboresha jinsi ya kusali. Mwaka huu Kanisa limetuwekea Novena kabla ya Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni. Tunaalikwa kusali novena hiyo kila mwaka. Novena hii ni tunda la maadhimisho ya Mwezi wa Pekee wa kimisionari, Oktoba 2019.

Katika novena hiyo tunamwombea Baba Mtakatifu na viongozi wote wa Kanisa. Tunaombea pia umoja wa Kanisa. Tunasali pia kwa ajili ya viongozi wa serikali. Tunaziombea familia, tunawaombea wagonjwa na wote wenye mahitaji mbalimbali. Tunaombea miito mitakatifu na utume wa uinjilishaji. Tunawaombea vijana, ili waitikie mwito wa Mungu wa kuwa vyombo vya Habari Njema. Pia tunafanya tafakari na matoleo ya sadaka kwa ajili ya wahitaji. Hizi ni njia za kushiriki kikamilifu Utume wa Yesu katika Kanisa lake. Matoleo yanayokusanywa wakati wa maadhimisho ya Kiliturujia ya Dominika ya tatu ya mwezi Oktoba yanalenga katika kutegemeza utume wa Uinjilishaji unaoendeshwa kwa jina la Baba Mtakatifu kupitia Mashirika ya Kipapa ili kufanikisha mahitaji ya kiroho na kimwili ya watu na Makanisa ulimwenguni kote. Tunaomba, Mama Bikira Maria wa Rozari takatifu, Nyota ya Uinjilishaji na Mtuliza wa Wenye Uchungu, Mfuasi wa umisionari wa Mwanae Yesu, azidi kutuombea na kutuimarisha.

MAISHA YA MTUMISHI WA MUNGU PAULINA MARIA JARICOT MWANZILISHI WA SHIRIKA LA UENEZAJI WA IMANI

Mtumishi wa Mungu Paulina Maria Jaricot (1799-1862), ndiye mwanzilishi wa Shirika la Uenezaji wa Imani. Tarehe 26 Mei 2020, Baba Mtakatifu Francisko aliruhusu uchapishwe ule waraka uliokubali muujiza uliopatikana kutokana na maombezi yake (Jaricot). Waraka huu ulifungua njia ya Paulina Maria Jaricot kutangazwa mwenyeheri. Paulina alizaliwa tarehe 22 Julai 1799 katika familia tajiri nchini Ufaransa, nchi ya viwanda, ambayo kwa wakati ule imani Katoliki ilistawi sana. Alikulia katika mji wa Lyons katika parokia ya Mtakatifu Nazier na Mtakatifu Polycarp. Maisha yake ya utotoni yalikuwa ya furaha, yakizungukwa na malezi ya imani ya Katoliki kutoka kwa wazazi, kaka na dada zake wakubwa. Akiwa mdogo alijifunza kusali mbele ya Ekaristi Takatifu, mazoea ambayo yalimfanya awe karibu zaidi na Mungu. Binti huyu alipokuwa na umri wa miaka 17, alitolea maisha yake kwa Mungu. Naye Mungu aligusa maisha yake kwa neema, akamwangazia moyo na kuyabadili maisha yake kwa ujumla. Paulina alimtolea Mungu maisha yake kama mlei.

Mwaka 1819, Paulina aliwasiliana na wamisionari ili kujua mahitaji yao. Alipotambua mateso na mahangaiko yao, aliamua kuwaombea zaidi na kuwasaidia katika mahitaji mbalimbali. Paulina alipata maono, na kwa kuyafuata maono hayo, alianzisha shirika la Uenezaji wa Imani. Shirika hilo lililenga kuwaunganisha watu wote kwa njia ya sala na upendo wa kimisionari. Shirika hili linatoa huduma kwa jina la Baba Mtakatifu katika Makanisa ya nchi za misioni. Paulina Maria Jaricot alikuwa na karama ya pekee ya kimisionari, na kwa karama hiyo alianzisha Rosari hai, iliyo chini ya Shirika la Uenezaji wa Imani. Kufuatana na juhudi zake za sala na ibada kwa Ekaristi Takatifu, yalizaliwa matendo ya upendo ndani ya kanisa zima, ambayo yalitoa msukumo wa uinjilishaji. Kati ya mwaka 1819 na mwaka 1820, akiwa na marafiki ambao walikuwa wafanyakazi, au wazazi, na akisukumwa na moyo wa upendo wa kimisionari Paulina alibuni utaratibu wa kuchangisha michango nyumba kwa nyumba. Michango hiyo ililenga kuwasaidia wamisionari ambao walikwenda kutangaza Habari Njema sehemu za pembezoni.

Alianzisha vikundi mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha uchangiaji: kila kikundi kilikuwa na watu kumi, na kila mtu kwenye kikundi alitafuta watu wengine kumi. Utaratibu huu ulisaidia kusisitiza kuwa kila mbatizwa ni mmisionari na anaitwa kushiriki katika kutangaza Injili kwa uwezo alio nao. Kwa njia hiyo, alisaidia katika kuhamasisha roho ya kimisionari, na lile wazo la wabatizwa wote kushiriki katika kutangaza Injili lilienea duniani kote. Habari juu ya upole wake na uwezo wake zilienea kwa haraka huko Ulaya na mataifa mengine ya dunia nzima. Tarehe 3 Mei 1922 chama chake cha kitume kiliinuliwa na kuwa Shirika la Kipapa. Paulina alianzisha Rozari hai ili iweze kukuza mambo ya kiroho chini ya Mama Maria Malkia wa misioni. Alianzisha kikundi cha watu kumi ambao walipaswa kusali rosari kila siku. Kikundi hiki kilienea katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu, hadi kifo chake Paulina, kikundi hiki kilikuwa na wanachama 2,250,000 ambao walikuwa wanasali Rosari hiyo hai. Paulina alifariki tarehe 9 Januari 1862 huko Lyons, Ufaransa. Shirika la Uenezaji Imani alilolianzisha linachangia kiuchungaji kwa majimbo yenye uhitaji, katika nchi za misioni. Kila mwaka shirika hili linasaidia miradi elfu tano ya uinjilishaji duniani kote.

SHUKRANI NA MWALIKO

Kwa niaba yangu mimi na Ofisi ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa ukarimu mlioutoa mwaka 2019 kwa ajili ya Mashirika ya Kipapa. Moyo wenu wa kujitoa kwa ajili ya utume wa uinjilishaji unazidi kuongezeka. Hivyo tunawashukuru na kuwatia moyo kuongeza ukarimu wetu kulingana na uhalisia wetu, kadiri Mungu anavyowajalia. “Mkijitajirisha katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu” (2Kor. 9:11). Mwaka 2019 kitaifa tulitoa Ukarimu mkubwa kupita miaka iliyotangulia (Rejea Takwimu za Ukarimu wetu Kitaifa zinavyoonyesha). Kwa namna ya pekee, tunatoa shukrani kwenu kwa kuendeleza moyo wa kimisionari wa kutoa ukarimu wenu kutoka kwenye Majimbo, Parokia, Mashirika ya kitawa na Maisha ya Wakfu, Taasisi, Seminari ndogo na kuu, Familia, Vyama vya kitume, Jumuiya ndogo ndogo, Marafiki wa Mashirika ya Kipapa, Watu binafsi na wenye mapenzi mema. Tunawaalika tena nyote, kuongeza juhudi za kuchangia kwa ukarimu zaidi katika Mfuko wa Pamoja kwa Kanisa lote la Mungu ili kutoa huduma zake katika nchi zetu za Misioni. Tunaambatanisha Ujumbe wa Baba Mtakatifu wa Dominika ya Misioni Duniani 2020 pamoja na taarifa za Ukarimu, ambao mwaka 2019 Kanisa la Tanzania, kupitia wewe na mimi, limechangia na kupeleka kwenye Ofisi za Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu lililoko mjini Roma.

Mshikamano na Baba Mtakatifu katika janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Napenda kutoa shukrani pia kwa ukarimu tuliouonesha kuchangia mfuko maalum wa Janga la Corona ulioanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko. Hadi sasa majimbo yaliyo mengi yamekwisha kuwasilisha michango hiyo, na tumeitanguliza huko Roma, tukiendelea kuwasubiri majimbo mengine ambayo wanamalizia ili kuipeleke mahali pake na hivi kushiriki kwa ukamilifu katika kuchangia mfuko huo. Mungu awabariki. Changamoto ya Baraka ya ongezeko la Idadi ya Waseminari wakubwa katika Seminari zetu. Tunamshukuru Mungu kwa ongezeko kubwa la miito mitakatifu. Tumekuwa na changamoto ya kutotosha kwa miundombinu yetu kwa ajili ya malezi ya waseminari wakubwa. Moja ya hatua zilizochukuliwa na Baraza la Maskofu Tanzania ni kuanzisha Seminari kuu nyingine, huko Mwendakulima, katika Jimbo la Kahama. Seminari hiyo inaitwa Seminari Kuu ya Nazareti. Tunashukuru sana kwa ukarimu wa majimbo yetu kuchangia gharama za mwanzo za ujenzi wa Seminari hiyo. Hatua nyingine imekuwa ni kuongeza majengo katika Seminari zetu nyingine. Na kwa hilo tunashukuru ukarimu wenu nyote na tunawaalika kuendelea kuchangia. Nawaalika sasa tuusome Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu katika Dominika ya Misioni ya mwaka huu 2020.

+ Damian Denis Dallu, Askofu Mkuu wa Songea na Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji Baraza la Maskofu Tanzania.

Askofu Mkuu Damian Dallu

 

19 October 2020, 08:07